Friday, December 9, 2011

MIAKA 50 YA UHURUNa Baraka Mfunguo,


Leo Tanzania inaadhimisha miaka 50 tangu ilipojitwalia Uhuru wake mikononi mwa Mwingereza. Mengi yanaongelewa lakini kikubwa hatuna cha kujivunia cha maana zaidi ya kujivunia miaka 50 yenye mateso na laana kwa kigezo cha amani, utulivu na umoja wetu kauli za viongozi wetu zilizojaa ghilba, jeuri, ulaghai na kebehi. Hakuna asiyejua kwamba kiwango cha maisha sasa hivi kimepanda tofauti na miak
a iliyopita. Wao wanachoweza kudai ni fursa wanazopeana wao na wake zao kwa ajili ya kujiendeleza katika dhana ya uwekezaji.

Cha msingi mwananchi wa kawaida amekuwa akichezewa shere kama mchezo ule wa karata tatu wa cheusi na chekundu. Hakuna jipya zaidi ya Rushwa, Ubadhirifu, Ukosefu wa maadili, Uchu wa Madaraka, Huduma duni za jamii , Uongozi mbovu pamoja na maendeleo duni. Sina cha kueleza zaidi ya kujipa matumaini na huwezi jua vizazi vijavyo watachukuliaje. Mimi nimeshuhudua miaka 50 ya UHURU isiyokuwa na lolote zaidi ya propaganda za tumethubutu, tumeweza na tunasonga mbele. Ni kiongozi gani (Ukimwacha Mwl Nyerere, Bibi Titi Mohamed na wengineo) wanaweza wakainuka wakaongea kauli hiyo. Kauli (tumethubutu,tumeweza na tunasonga mbele) iliyojaa kejeli na ghilba ambayo inaweza kuamsha hisia kwa mwananchi dhidi ya serikali yake.

Miaka ya enzi za Mwalimu watu walikuwa wakijivunia utumishi uliotukuka leo hii watu wanajivunia wizi uliotukuka kwa kuhakikishiwa usalama wao na mashirika makubwa ya kimataifa pamoja na yale ya kijasusi ili watunyonye vizuri. Ni ukweli usiopingika sasa Afrika na nchi zingine zinazoendelea hazina kauli dhidi ya mabeberu na viongozi tulionao ni matokeo yao na hata mifumo tuliyo nayo ni matokeo yake. Miaka ile tuliambiwa tuishushe shilingi yetu thamani, tubinafsishe njia kuu za uchumi, tuwe na uchumi huria, tubane matumizi, tupunguze matumizi ya serikali na tuwe na mfumo wa vyama vingi. Leo hii tunaambiwa tuwe mashoga yote kwa kigezo cha misaada. Leo hii asilimia ya 30-40 ya bajeti ya Tanzania inategemea misaada kutoka nje huko ni kuthubutu na kuweza na kusonga mbele? Tuacheni unafiki bwana. Sasa hivi ukijaribu kuangalia hayo mapendekezo ya IMF na Benki ya Dunia ni kama tumefanya mara kinyume chake na zaidi yake. Tumerudi nyuma hakuna lolote la kujivunia kwa mwananchi wa kawaida zaidi ya tabaka la juu pamoja na mfumo unaowalinda wawe madarakani wafaidi mvinyo wa damu ya Watanzania.

Waswahili husema mwamba ngozi siku zote huvutia kwake. Na uongo hujitenga na ukweli kujulikana na Wajinga ndio waliwao. Sisi Watanzania tumeshapumbazwa na sumu ya amani, umoja na utulivu na hata pale unapohoji suala la msingi unaambiwa wewe ni mhaini na unataka kuvuruga amani ya nchi. Leo ni miaka 50 ya UHURU tuwaulize hao CCM wameshafanya nini kipya ambacho wananchi wamekiona na kusema eeeh! kweli kazi imeonekana sana sana Mkapa alijaribu kuonyesha uelekeo. Sina nia ya kukashifu viongozi walio madarakani kwani dhamira inanieleza kwamba wananchi waliowengi wamewachagua kwa kipande cha kura. Isipokuwa dalili zinajidhihirisha dhahiri hivi sasa hakuna jipya lolote la maana.

Miaka 50 ya UHURU italeta mateso pale wezi, wauaji pamoja na wanyang'anyi watakapo ingia uraiani kwa msamaha wa rais. Ni kweli wanastahili msamaha kwa upande mmoja lakini kwa upande mwingine sina uhakika sana kama watakuwa wamebadilika tabia zao. Hii ndio miaka 50 ya UHURU tutakayoishuhudia kwa gwaride, michezo ya hailaiki, ngoma za jadi , michezo ya kuigiza, kwaya na sarakasi. Aghalabu wapo wale watakaojipendekeza waonekane kana kwamba wao ni watanzania sana kupita wengine na wanaoipenda nchi yao kwa kudai nyongeza za posho huku muuguzi na mkunga akipata posho ambayo haitoshi nauli ya basi kutoka mkoa mmoja kwenda mwingine. Hii ndio Tanzania Bwana inayotimiza miaka 50 ya UHURU. Vipo vyombo vya habari ambavyo vilikuwa ndio vichocheo vya vuguvugu la UHURU lakini leo ndo mashine ya propaganda ya kueneza upotoshaji uliowazi kwa wananchi.

HONGERA KWA MIAKA 50 YA MATESO TANGANYIKA NA WADANGANYIKA

No comments: