Friday, December 9, 2011

MIAKA 50 YA UHURU TUIFURAHIE AU TUILILIE NCHI YETU?


Na Johnson Mbwambo

KARIBU wiki nzima hii, gumzo linalotawala mazungumzo ya Watanzania popote pale walipo; ni sherehe za miaka 50 ya uhuru ambazo zitahitimishwa Ijumaa, Desemba 9, na ambazo tumeelezwa kuwa zitahudhuriwa na marais saba wa nje.

Maadhimisho haya ya miaka 50 ya uhuru (au tuseme nusu karne ya uhuru) yamepokewa kwa hisia tofauti na Watanzania. Wako wanaoona mantiki na busara ya kufanya sherehe kabambe na wako wanaoona kuwa sherehe hizo ni kisingizio kingine cha kutafuna fedha za umma katika kipindi ambacho serikali yenyewe inakabiliwa na ukata mkubwa.

Sina hakika, mpenzi msomaji, hisia zako wewe ni zipi kuhusu maadhimisho haya; lakini niseme tu kwamba sote tumekuwa tukitumia maadhimisho haya kujadili zile “t” tatu maarufu nilizopata kuzizungumzia huko nyuma; yaani tulikotoka, tulipo na tunakokwenda.

Katika kuzijadili “t” hizo, vyombo vya propaganda vya Serikali ya CCM vimekuwa vikijitahidi katika wiki hii ya mwisho ya maadhimisho kutuaminisha kwamba maendeleo makubwa yamepatikana katika kipindi hicho cha miaka 50 ya uhuru.

Na katika kuzifanya hoja zao ziaminike, vyombo hivyo vimekuwa vikitulisha takwimu kwa kasi ya kutisha; tena takwimu ambazo hazina mchanganuo wowote.

Kwa kasi yao hiyo, unaweza kabisa kuiita wiki hii kuwa ni ‘wiki ya takwimu’ – takwimu za “maendeleo” yetu ya miaka 50!

Wiki nzima hii tumetajiwa na tutatajiwa idadi ya hospitali tulizokuwanazo mwaka 1961 na tulizonazo sasa (2011). Tutatajiwa pia idadi ya barabara za lami zilizokuwepo nchini mwaka 1961 na zilizopo sasa, mwaka 2011.

Bila kujali suala la viwango, hawatasahau pia kututajia idadi ya vyuo vikuu, shule za sekondari na shule za msingi zilizokuwepo wakati tunapata uhuru na zilizopo sasa.

Ukiwa si mvumilivu, takwimu hizo zinaweza kukuchefua kwa sababu zinamwagwa kwako bila hata kuzingatia vigezo muhimu; kama vile wingi wa miaka ya uhuru tunayosherehekea, na pia wingi wa idadi ya sasa ya Watanzania.

Katika hali ya kawaida, ili zisikuchefue, takwimu hizo zilipaswa kupambanishwa na takwimu nyingine za idadi ya sasa ya watu katika Tanzania ikilinganishwa na ile ya mwaka 1961 na pia idadi ya miaka ya uhuru tunayoadhimisha; maana, hakika, miaka 50 si haba kwa maendeleo haya madogo tunayotakiwa kujivunia kupita kiasi.

Natujiulize: Wingi wa barabara hizi za lami tunazopaswa kujivunia inaendana na wingi wa watu na inaendana na ukweli kwamba miaka ya uhuru tunayozungumzia ni 50; yaani nusu karne?

Ukijiuliza hivyo, unaweza kugundua kwamba idadi hiyo ya barabara za lami tunazotajiwa si kitu kikubwa cha kufurahia mno kwa nchi yenye Kilomita za mraba 945,090 na idadi ya watu inayofikia karibu milioni 45!

Tunawezaje kujivunia idadi hiyo ya barabara za lami kama kuna nchi nyingine duniani zenye ukubwa wa chini ya Kilomita za mraba 300,000 na watu wasiofikia milioni 10, lakini zina wingi wa barabara za lami kuliko tulizonazo sisi?

Kwa hakika, unaweza kujiuliza na kujihoji hivyo hivyo kwa mambo mengine yote tunayoaminishwa na watawala wetu kwamba ni “maendeleo makubwa” tuliyoyapata katika kipindi hicho cha miaka 50 ya uhuru.

Ukilinganisha na baadhi ya nchi tulizopatanazo uhuru miaka ile (kama Malaysia mwaka 1957, Singapore mwaka 1963 au hata Botswana mwaka 1966 nk), utagundua kuwa hicho tunachokiita ‘maendeleo makubwa’ si chochote wala lolote!

Wakati tunapata uhuru, Desemba 9, 1961, tuliambiwa kuwa wakati mataifa tajiri duniani yanatembea, sisi tunapaswa kukimbia. Lakini kilichojitokeza miaka 50 ya uhuru ni kwamba tumeshindwa kukimbia, tumeshindwa kutembea na tumebaki tunatambaa.

Kwa kusuasua kwetu huku, mtu unajiuliza; itatuchukua miaka milioni ngapi kuweza kufikia viwango vya maendeleo vya sasa vya mataifa tajiri? Lakini ukiwauliza wenyewe (watawala) watakujibu haraka; tumeweza, tumethubutu na tunasonga mbele!

Ukweli ni kwamba kama tungekuwa tumeongozwa vyema na watawala wetu kuchapakazi, pengine leo tusingezungumzia kujivunia barabara za lami; bali treni za chini ya ardhi!

Pengine leo tusingezungumzia idadi ya vyuo vikuu; bali uwezo wa kujitengenezea wenyewe vitu muhimu katika maisha yetu kama vile matrekta, malori, barabara za juu, madaraja makubwa, njia mpya za reli nk.

Tungekuwa tumeongozwa vyema na viongozi wetu (na si watawala) kuchapa kazi kweli kweli, pengine miaka 50 ya Uhuru tusingekuwa tunazungumzia nchi ambayo hata vidonoa mabaki ya nyama mdomoni au leso za kujifutia jasho, ni ‘made in China’.

Ndugu zangu, sipingi kwamba hatujapiga hatua yoyote katika miaka hiyo 50 ya Uhuru. La hasha. Nitakuwa mwendawazimu kuamini kwamba hatujapiga hatua yoyote katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Na wala sikumbuki kama kuna nchi yoyote duniani ambayo haijapiga hatua yoyote ya maendeleo katika kipindi cha miaka 50 iliyopita.

Hata Vanuatu (moja ya nchi masikini kabisa duniani) nayo imepiga hatua katika miaka 50 iliyopita! Kama ambavyo Vanuatu ya sasa si sawa na Vanuatu ya miaka 50 iliyopita, vivyo hivyo Tanzania ya sasa si sawa na Tanganyika ya miaka 50 iliyopita!

Lakini ninachojaribu kueleza hapa, ndugu zangu, ni kwamba tumepiga hatua; lakini hatua tuliyopiga si kubwa na ya kujivunia kwa kipindi kirefu kama cha nusu karne! Tulipaswa tuwe mbali zaidi. Kwa miaka 50, tulitakiwa tumefanya vyema zaidi; hasa ukizingatia utajiri wa maliasili ambao Mungu ameijalia nchi yetu.

Labda tukumbushane: Pamoja na miaka yetu hii 50 ya Uhuru, bado tu nchi ambayo tunategemea misaada ya kigeni kujiendesha. Bado tu nchi ambayo tunaagiza karibu kila kitu ugenini. Bado tu nchi ambayo, kama ilivyokuwa enzi za ukoloni, ni eneo la Wazungu la kupata malighafi za viwanda vyao Ughaibuni.

Kwa ufupi; pamoja na miaka yetu 50 ya Uhuru, bado tumo katika orodha ya nchi masikini duniani – Least Developing Countries (LDC). Bado tumeganda katika orodha hiyo wakati wenzetu wengine wameshajinasua na kuingia orodha ya Nchi Zinazoendelea (Developing Countries – DC).

Nazungumzia nchi ambazo katika kipindi cha miaka hiyo 50 iliyopita zimefanikiwa kujinasua kutoka kundi la LDC na kuingia kundi la DC. Nazungumzia nchi kama vile Botswana iliyoingia kundi hilo mwaka 1994, nchi kama vile Cape Verde - 2007 au nchi kama vile Maldives (2011) nk.

Ni kwa sababu hizo chache nilizozitaja miongoni mwa nyingi, nasita, ninapozijadili zile “t” tatu, kuamua iwapo ninapaswa kuifurahia miaka hii 50 ya uhuru wetu au ninapaswa kuililia nchi yangu Tanzania!

Hisia za kuililia zaidi Tanzania zinanijia kwa kasi; hasa nikikumbuka kwamba migodi yetu tumeibinafsisha yote kwa wawekezaji wa kigeni na inakaribia kukauka; huku ikiwa bado haijatuletea maendeleo yoyote makubwa; achilia mbali hata kule tu kuijenga miji yetu ambako migodi hiyo ipo!

Hisia za kuililia Tanzania zinanijia zaidi ninapokumbuka kwamba hata chuma cha Liganga ambacho kingekuwa muhimu katika mapinduzi yetu ya baadaye ya viwanda, sasa nacho tumewakabidhi wawekezaji wa Kichina kwa ajili ya viwanda vyao vya Beijing!

Hisia za kuililia zaidi nchi yangu Tanzania zinanijia nikikumbuka pia kwamba hata maliasili tulizobarikiwa na Mungu nazo zinateketea kwa kasi na miaka si mingi zitakuwa historia; huku bado tukiwa nchi masikini.

Naililia zaidi nchi yangu Tanzania nikikumbuka kwamba katika miaka hii 50 ya uhuru wetu, vyanzo vya maji vimeteketezwa kwa kasi, mabonde makuu ya mito yamevamiwa na wafugaji kiasi kwamba iliyokuwa mito mikuu sasa imegeuka kuwa mifereji, na miaka si mingi itakauka kabisa.

Naililia nchi yangu ambayo miaka 50 mingine ijayo, sehemu kubwa ya ardhi yake itakuwa na hali ya ujangwa kutokana na ukame.

Ndugu zangu, wakati Watanzania wenzangu wanasherehekea na kuifurahia miaka hii 50 ya Uhuru wetu, mimi machozi yananilengalenga kwa sababu mbele naona giza kwa wanetu na wajukuu wetu!

Naona mbele giza, kwa sababu hata misingi ya amani na umoja aliyotujengea Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, tumeanza kuibomoa kwa kasi, tukianzia na ujengaji matabaka ya kutisha nchini.

Ni wazi pengo kati ya walionacho na wasionacho linaongezeka kwa kasi nchini, na hali hii haiwezi kuweka mazingira ya kujenga amani na utulivu. Bob Marley alisema: Mwenye njaa huwa na hasira; na kwa maana hiyo kwenye njaa hapawezi kuwa na amani.

Nihitimishe safu yangu kwa nukuu ya Mwalimu Nyerere. Mwalimu alipata kusema hivi: Bila Azimio la Arusha, wananchi wanyonge wa Tanzania watakuwa hawana matumaini ya kupata haki na heshima katika nchi yao. Na bila matumaini hayo, kazi ya serikali ya kujaribu kufufua uchumi itakuwa ngumu sana. Itakuwa vigumu zaidi kuwafanya Watanzania wanyonge, ambao ndio wengi, wakubali kujitolea na kufanya kazi kwa bidii, kazi ambazo hazina matumaini kwao.”

Hivyo ndivyo alivyonena Mwalimu. Labda tujiulize: Tanzania hii ya miaka 50 ya uhuru ina matumaini gani kwa mamilioni ya wanyonge nchini?

Ni muhimu tujiulize swali hilo; maana jibu lake ndilo linaloweza kutusaidia kuamua iwapo tunapaswa kuifurahia miaka hii 50 ya uhuru wetu au tunapaswa kuitumia kuililia nchi yetu Tanzania!

Tafakari.


RAIA MWEMA

No comments: