Sunday, December 11, 2011

MBEGU YA UDINI IMEANZA KUPANDIKIZWA NA KUMEA. IKIIVA TUTAANZA KUKATANA MAPANGA


Naomba kulitumia jamvi hili kuelezea hisia zangu na uchungu nilio nao kwa taifa hili kwa jinsi mbegu ya udini ilivyopandwa na kutishia uhai wa nchi yangu niipendayo sana ya Tanzania. Labda nianze kwa kusema kwamba binadamu wote tumezaliwa ama kuumbwa na sura ya mfano wa Mungu lakini sisi tumeongeza sura za ziada juu ya wanadamu wenzetu. Matokeo yake ni kwamba mbali na sisi sote kuumbwa na Mungu mmoja na wote kuwa sawa mbele zake, kwa bahati mbaya dini tulizo nazo zimetufanya tuweke sura za ziada kwa wanadamu wenzetu na kuwahukumu na kuwachukia kwa vigezo vya dini zetu na kwa bahati mbaya sijawahi kusikia kuwa katika hizi dini zetu kuna vyeti maalumu toka kwa Mungu vinavyotuambia dini zetu ni bora kuliko nyingine na hivyo zina haki ya kuhukumu wengine. Ni viongozi wetu wa dini ndio wanaotulisha chuki dhidi ya wengine na sisi tunayapokea mafundisho yao bila kuhoji.

Hebu niende kwenye hoja yangu ya leo. Nimesoma Mwananchi leo kuwa Shule ya sekondari ya Ndanda imefungwa kwasababu ya mgomo baridi wa wanafunzi wa kiislamu wanaodai kuwa wanabaguliwa, wanataka udahili ulio sawa kati ya wakristo na waislamu na wanataka wajengewe msikiti hapo shuleni. Habari hii imenikumbusha vuguvugu hili ambalo limeibuka sana tangu wakati wa uchaguzi mwaka jana na vuguvugu hili la waumini wa kiislamu limekuwa likichochewa pia na magazeti ya kiislamu, vyuo na shule za kiislamu na kwa upande wa dini ya kikristo nako lipo vuguvugu la kuwaambia waumini wao wajipange dhidi ya wenzao.

Yapo matukio kadhaa yaliyotokea nchini ambayo yanaashiria kukua kwa chuki hizi za kidini nchini. Nikikumbuka machache, ni nyaraka za kidini wakati wa uchaguzi hususani zile za kuwahimiza waislamu kutomchagua mkristo, kauli mbiu za vyombo vya habari vya kidini kuwahimiza waumini wao kupambana na mfumo kristo nchini, vurugu za kidini chuo kikuu cha Dodoma, mihadhara ya kidini huko Arusha na vurugu za kidini huko Mwanza nk. Inasikitisha sana kuona sisi watanzania wa leo tunafanywa maadui kwa njia ya dini za kigeni. Naionea huruma Tanzania yangu inakoenda si kuzuri.

Kamwe sitasita kupaaza kilio changu kuwalaumu wanaisasa wanaotumia dini kwa maslahi ya matumbo yao na si taifa hili. Nakilaumu chama cha mapinduzi, tena nakilaumu kwa wazi kabisa kwa kubeba bango la udini kama mtaji wa kisiasa na kuliacha taifa likichakaa. Taifa lililosimikwa katika misingi ya uzalendo leo linasimikwa katika misingi ya ubaguzi. Ninashindwa kuelewa kwanini ndugu zangu waislamu wanawaona wakristo kama maadui hapa nchini na siku zote wameaminishwa hivyo, kwanini?

Nataka tujiulize kwa uwazi kabisa, hivi ni wakristo waliowazuia Zanzibar kusiwe na shule na vyuo? Hivi ni wakristo wamewazuia kujenga vyuo au kukosa pesa za kusimamia misikiti na taasisi zao? Hivi ni wakristo ndo wanaoenda kwenye shule kuwaachisha watoto wao masomo? Hivi ni wakristo ndio wanaoandika majibu ya watoto wao kwenye mitihani? Hivi ni wakristo ndo wanaowatuma wawe na migogoro kwenye misikiti? Mbona hata wakristo wanayo migogoro yao na wanaimaliza? Hivi, nataka kujua, hawa wakristu ndo wanaowazuia wao kuswali? Wakristo wanaingiaje kwenye mfumo wa maadili kwenye misikiti na madrasa ya waislamu? Hivi watanzania tumefikia katika hali ya kuchukiana kiasi hiki kwa misingi ya dini zisizo zetu?

Kama kuna jambo ambalo sitasita kulisema wazi ni hili la CCM kutumia dini kama mtaji wa siasa kila kinapofika kipindi cha uchaguzi. Lakini chuki zilizojengwa sasa ni hatari zaidi na ninasikitika kuwa taifa litaangamia. Najiuliza, mwaka jana walidai Chadema ni chama cha kidini, lakini sijawahi kumwona wala kumsikia mgombea wa Chadema wa urais akitumia makanisa kwa kampeni. Hakuwahi kuomba achangishe harambee za makanisa, sherehe za kidini nk, lakini hawa viongozi wa CCM wanatumia makanisa na misikiti kujinadi. Nani mdini hapa? Naipenda Tanzania, nalipenda taifa langu, nawachukia sana wanaoligawa taifa hili kwa misingi ya ukabila, udini na rangi. Sote tuungane kulitetea taifa letu.

Asanteni sana kwa kusoma waraka wangu huu mrefu.


KUTOKA SWAHILI TIME/BLOG

My Take:

Kila mtu ana uhuru wa kuabudu na kila mtu anatakiwa kuheshimu dini ya mwenzake. Hata hivyo dini ikitumika vibaya huweza kuvuruga amani na utulivu kwani ndani ya dini mna imani ambayo hubeba hisia za maisha ya binadamu pamoja na fikra zake. Kulitatua suala hili haitakiwi jazba bali busara na hekima. Hata hivyo ni lazima vitafutwe vyanzo na hao wapotoshaji ili sheria iweze chukua mkondo wake.

No comments: