Thursday, December 22, 2011

MAONI YANGU KUHUSU ZOEZI LA UOKOZI WA MAFURIKO DAR.

 1. Watendaji wa mitaa watoe idadi kamili ya watu walio katika vitongoji vyao haswa vilivyoathirika na mafuriko
 2. Iandaliwe orodha maalum ya wahusika ambao wamepotea kutokana na mafuriko na ipelekwe katika vyombo husika mfano. Polisi, vikosi vya uokozi vya zimamoto na JWTZ pamoja na vyombo mbalimbali vya habari
 3. Kampuni mbalimbali za mawasiliano zijipange kuhusiana kuchangia upatikanaji wa taarifa mbalimbali sanjari na mawasiliano juu ya matukio na maendeleo ya uokozi yanavyoendelea
 4. Wananchi waondoe tofauti zao za kisiasa, jinsia, dini, rangi na vyeo wajitolee kusaidia katika kuokoa maisha ya wananchi
 5. Kamati ya maafa kutoka ofisi ya Waziri Mkuu ihusishe wataalam wa kada mbalimbali na kuweka siasa na maslahi kando ili kuweza kuokoa maisha ya wananchi kwa kushirikisha mashirika ya Msalaba/Mwezi mwekundu, Asasi zisizokuwa za kiserikali, Mashirika pamoja na idara za serikali.
 6. Kwa kuweka uzalendo mbele watendaji wote wa serikali wanaosheherekea likizo ya Krismas warejee kazini ili kuweza kushirikiana bega kwa bega katika uokozi. Pongezi za dhati kwa Mh. Abdulkarim Shah (MB-Mafia) kwa kuweza kujitoa bega kwa bega katika janga hili na wengine muige mfano.
 7. Ni wakati muafaka sasa kwa kufuatilia hadidu za rejea za Tume iliyoundwa na aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam ndugu William Lukuvi kuhusiana na suala zima la ujenzi holela jiji la Dar es Salaam na kusimamia mapendekezo yake
 8. Serikali itafute namna ya kuweza kuwapatia maeneo mbadala wakazi wa mabondeni na pia urasimu usitumike katika kufanikisha zoezii hilo kuwe na " FAST TRACK SYSTEM" pamoja na uwazi wa zoezi lenyewe.
 9. Nchi rafiki kama CUBA, CHINA na nchi zingine za jirani ziombwe ili ziweza kushiriki kusaidia katika uokozi huu na iwe fursa muhimu kwa Watanzania kujifunza
 10. Wizara ya Elimu iweke mitaala maalum ambayo itatumika kuwafundisha wanafunzi mbinu na njia mbalimbali za kujiokoa pindi janga linapotokea
 11. Idara ya Mipango miji, Wizara ya Ujenzi pamoja na wakala wa bara bara kwa kushirikiana na wataalam waliobobea wa ndani na nje watathmini athari zilizojitokeza na wabuni mbinu mbadala ya kuweza kukabiliana na tatizo la ujenzi holela unaotokana na ongezeko la watu mijini kwa kuweka taratibu na sheria kali zitakazodhibiti ujenzi holela kwa kuzingatia taaluma zao .
 12. Mwisho, waheshimiwa Wabunge wakatwe posho zao kwa muda wa miezi sita pamoja na wale wanaopata posho nono nono serikalini ili kuweza kuwasaidia wananchi walioathirika na mafuriko kwani hicho wanachotumia wao kinatokana na kodi ya mwananchi mnyonge

No comments: