Wednesday, December 28, 2011

MAMBO YA "NDUMBA NANGAI "MKOANI MTWARA

Na Baraka Mfunguo,

Wahenga wanasema kua uyaone, wengine wanasema kuishi kwingi ni kuona mengi na wengine wanasema ukimwona nyani amezeeka
ujue amekwepa mishale mingi na wengine wanasema kama wewe unajua hivi na wenzio vile. Hiyo sio misemo yangu, ni misemo ambayo nimekua nikiisikia na nimekuwa nikionywa na kufunzwa nayo toka nikiwa mdogo.
Pichani Mtaalam wa kuzingua "mang'opo akiwa amefukua mauchawi katika eneo mojawapo mjini Mtwara/Mikindani hivi karibuni.


Pia ukiingia kwa watu kama wewe ni mgeni usionyeshe tofauti kwa wenyeji shurti uishi kama wanavyoishi wao. Huku Mtwara kuna mambo ambayo yanasifika sana na mojawapo ni hili la "ndumba nangai-yaani uchawi" Uchawi unatofautiana na pia unazidiana. Lakini ambao ni almaarufu sana ni ule unaotumika kuwaibia watu fedha zao bila wao kujijua kwa huku wanaita "Mang'opo".


Unaweza ukawa unafanya biashara yako kuanzia January mpaka Disemba usione fedha iliyoingia wewe kila siku ni kutoa fedha kwa ajili ya kuendesha biashara na mtaji hauonekani.

Ukiona hivyo ujue wapo wataalam tayari wanakula fedha yako. Wapo wale ambao wanajifanya ombaomba ole wako umpatie fedha na aone kwenye pochi yako kuna kiasi gani unakuja kushangaa hakuna fedha, ama kuna ile ya kutoa pesa dukani ambayo itahitaji chenji ole wako ile chenji uchanganye na fedha zako nyingine katika pochi , Utalia.

Ama kuna wafanyabiashara ndogo ndogo ambao wanauza vitu kama matunda, nguo za watoto na waakina mama wakishakukamata tu wewe utajikuta pesa yako huelewi umeitumia vipi. Lakini kuna wale wafanyabiashara wa Sokoni, utamkuta mtu kazi yake ni kuuza viberiti tu ama majani ya tumbaku kwa ajili ya kutengeneza ugoro ama sigara za goso na kwa siku aweza kuwa na wateja wasiozidi 5. Lakini jioni fedha anayokuhesabia ni mabulungutu kwa mabulungutu. Hapo ni lazima mtu ujiulize.

Hivi sasa amejitokeza mtu ambaye anafanya kazi hiyo ya kufukua hayo "mang'opo" pamoja na mauchawi mengine na anazunguka kijiji kwa kijiji mtaa hadi mtaa. Na inasemekana wapo watu wamechimbia "mang'opo yao sehemu za biashara na mikusanyiko ya watu ambapo mzunguko wa hela unakuwa mkubwa ambapo kila mtu anayepita sehemu hiyo ni lazima alipie lakini bila ya yeye kujijua .

Changamoto ni kwa wale ambao wanagundulika kuhusika na mang'opo hayo kutishia kwenda polisi. Kutokana na serikali kutotambua uchawi , mara nyingi kesi hizi huishia kimya kimya.
Iko haja kubwa ya kupambana na hawa watu wanaofanya haya "mang'opo" kwani kwa kiasi kikubwa wanarudisha maendeleo ya watu wengi nyuma. Hii ndio hali halisi ya Mtwara kama wewe ni mpenda maendeleo katika maisha yako unatakiwa uwe makini kwa mtu unayepeana naye mkono kwa kusalimiana, makini kwenye fedha zako za matumizi na makini unapokutana na mtu unayemtilia mashaka. Hivi vitu ni vya kweli huku umakondeni.

No comments: