Friday, December 16, 2011

HALI SI SHWARI CUF NA NCCR

WAKATI uongozi wa CUF, ukiwa bado haujamwita kwenye Kamati ya Maadili, Mbunge wa Wawi, Hamad Rashid Mohamed, Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, amesema hatishwi na kikao cha dharura cha Halmashauri Kuu ya chama chake cha NCCR-Mageuzi, kinachotarajiwa kuketi kesho kumjadili kama inavyodaiwa.

CUF na NCCR- Mageuzi vimekuwa katika migogoro ya ndani kwa muda mrefu na kadiri siku zinavyosonga mbele, migogoro hiyo inaonekana kuendelea kukua kiasi cha kutishia uhai wa vyama hivyo vya upanzani.

Upande wa CUF
Wakati uongozi wa chama hicho ukiwa bado unasuasua kumpa barua ya wito Hamad kama ilivyoahidiwa na Naibu Katibu Mkuu wake Bara, Julius Mtatiro, wanachama 4,000 wa chama hicho Kata ya Manzese, jijini Dar es Salaam wameonya kwamba kitendo cha kumzuia mbunge huyo kufanya mikutano, kinaweza kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya chama.

Mtatiro jana aliliambia gazeti hili kuwa chama hicho bado hakijampekelea barua Hamad kumwita kwenye kikao hicho cha maadili, lakini mpango wake huo, haujabadilika.

"Bado tutampelekea tu na tutamuita katika Kamati ya Maadili ya chama muda wowote kuanzia sasa,”alisema Mtatiro.
Akieleza sababu za kumwita mbunge huyo pekee na sio Maalim Seif Sharif Hamad, Mtatiro alisema Hamad Rashid, ndiye aliyeanza kuzungumza na waandishi wa habari na kueleza matatizo yake aliyonayo ndiyo maana uongozi ukabaini kwamba kuna kila sababu za kumuita na kuzungumza naye.

Alisema baada ya kumwandikia barua, vikao vya ndani vya chama vitakaa na kumhoji na maamuzi yatakayotafanyika kikatiba ndio yatakayoamua hatima yake. “Vikao vya ndani ndivyo hasa vitakavyojua hatma ya Hamad Rashid na sio mimi. Kwa kweli siwezi kukueleza chochote kile sasa hivi,”alisema
Wakati chama kikipanga kumwita, Hamadi mwenyewe amezungumzia hatua hiyo kuwa ni ukiukwaji mkubwa wa katiba akieleza kuwa kimsingi alipaswa kuitwa katika vikao vya chama na sio kuhukumiwa na kushutumiwa kupitia vyombo vya habari.

Kauli ya mbunge huyo wa Wawi ilikuja baada ya Mtatiro kutoa kauli kwenye mkutano na wanahabari akidai kuwa kitendo cha Hamad kufanya mkutano na wanachama wa Tawi la Chechinya, Manzese bila kibali cha chama ni kwenda kinyume na taratibu.

Wananchama 4,000
Wakati uongozi huo wa CUF ukisuasua kumpa barua Hamad wanachama 4,000 wa Kata ya Manzese jijini Dar es Salaam, wameonya kuhusu kitendo cha kumzuia mbunge huyo kuendelea na mikutano yake.

Wanachama hao waliyasema hayo jana kufuatia mbunge huyo kushindwa kukabidhi msaada wa samani za ofisi ya kata hiyo alizopaswa kuzikabidhi Desemba 11 mwaka huu, lakini akazuiwa na ulinzi wa chama hicho wanaojulikana kama Blue Guard.

Katibu wa Kata hiyo, Hamdan Kulangwa alisema kitendo cha mbunge huyo kuzuiwa na walinzi wa chama hicho kinakiuka taratibu za chama na hivyo kuwasikitisha sana wapenzi na wanachama wake katika kata hiyo.

“Sisi tulimwalika Hamad Rashid aje atukabidhi msaada wa samani za ofisi ambazo tulimwomba atusaidie, lakini siku ya tarehe 11 Disemba, alipofika kabla hajaanza kufanya lolote lilikuja kundi la Blue Guard na kumzuia kuzungumza na sisi,” alisema Kulangwa

Kafulila: Sina hofu kikao cha NEC

Wakati upepo ukivuma vibaya ndani ya CUF, NCCR nako mambo bado magumu baada ya mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, kusema kuwa hana hofu na kikao cha NEC ya chama hicho inayoketi kesho.

Kafulila ambaye anadaiwa kuzungumza mambo ya ndani ya chama katika vyombo vya habari pamoja na kupingana wazi wazi na mwenyekiti wake, James Mbatia kinyume alisema hana wasiwasi kwa kuwa mpaka sasa hakuna ajenda zilizowekwa wazi juu ya mambo yatakayojadiliwa katika kikao hicho.

Kafulila alisema, “Mimi ni mjumbe wa kikao hicho na nitakuwepo, ila mpaka sasa sijaelezwa ajenda…, hili ni jambo dogo na kila kitu kitajulikana katika kikao, nadhani kikao kitajadili mambo mbalimbali,” alisema Kafulila.

Alipoulizwa hoja atakazoziwasilisha iwapo atajadiliwa katika kikao hicho, Kafulila alisisitiza kwamba hawezi kulizungumzia suala hilo kwa kuwa mpaka sasa hajui nini kitakachojadiliwa.

Imeandaliwa Fidelis Butahe, Hussein Issa na Aidan Mhando


LinkMWANANCHI

No comments: