Monday, November 7, 2011

WANAJESHI WA DRC WATINGA KIGOMA KUSAKA WAASI


Anthony Kayanda, Kigoma


KIKUNDI cha askari wa Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasi ya kongo Congo DRC wakiwa na silaha nzito za kivita wametia nanga katika Bandari ya Kigoma kwa madai ya kuwasaka waasi wanaopigana na Serikali ya nchi hiyo waliokimbilia hapa kutafuta matibabu.

Askari hao waliowasili hapa juzi jioni wakiwa katika boti ya kijeshi, walipenya bila kikwazo chochote na kuegesha jirani na boti ya polisi na ndipo Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) lilipopewa taarifa ya uvamizi huo na mara moja liliwasili katika eneo hilo na kuwaweka wanajeshi hao chini ya ulinzi.

Akizungumzia na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Kikosi cha 24 KJ, Luteni Kanali Emmanuel Mcheri alisema wanajeshi hao wa DRC wapatao 20 waliingia Kigoma kinyume cha utaratibu jambo ambalo ni kosa kwa vile kitendo hicho kinaweza kusababisha vita baina ya nchi hizi mbili.

Alisema askari hao wa DRC walikuwa wakiongozwa na Luteni Kanali Mohamed Mustafa wa Kikosi cha Askari wa Miguu cha 42 chenye makazi yake Mashariki ya DRC ambaye alisema walikuja kufanya operesheni maalumu kuwasaka waasi wa nchi hiyo waliokimbilia Kigoma kutafuta huduma ya matibabu.

“Hawa Askari 20 kutoka DRC wamevuka mpaka kinyume cha sheria na kuvamia mkoani kwetu. Wameingia hadi kwenye bandari yetu ya Kigoma. Askari wetu wamewapekua na kuwanyang’anya silaha zote walizokuwa. Tunawashikilia hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine," alisema Luteni Kanali Mcheri.
Askari hao walipelekwa katika Gereza la Bangwe.

Alitaja aina ya silaha walizokuja nazo ni bunduki 17 aina ya SMG, bunduki moja aina ya LMG, pistol moja ya, RPG moja, bomu moja la kutupwa kwa mkono na makombora matatu ya milimita 12 na milimita 16 yenye uwezo wa kutungua ndege.

“Lakini pia wamekuja na shehena kubwa ya risasi na tulipowapekua tumekamata magazini 32 za SMG zikiwa na jumla ya risasi 960, risasi tano za pistol, risasi za LMG zilikuwapo 360, lakini walikuja na boksi lililojaa risasi. Kwa kweli wamekiuka taratibu za kuingia nchini hata kama wanadai walikuwa katika operesheni yao kuwasaka waasi wanaopigana na Serikali yao” alisema.

Kuhusu kuingia bila ya kupata kikwazo chochote hadi bandarini, Luteni Kanali Mcheri alisema licha ya tukio hilo, askari wa JWTZ wapo imara kukabiliana na tishio lolote la uvamizi kutoka mahali popote.

“Mpaka wa mkoa wetu na nchi jirani ni mkubwa sana hivyo suala la ulinzi wa mipaka wakati mwingine linakuwa gumu sana, lakini bado nawahakikishia kwamba vijana wetu wapo imara kwa lolote na wala jambo hili lisiwatie hofu hata kidogo,” alisema.
Katika kikosi hicho cha askari wa DRC walikuwapo maofisa wanane wa jeshi, askari wa kawaida kumi na mmoja na raia mmoja anayedaiwa kuwa ni fundi wa boti hiyo la kijeshi.

Habari za ndani zinasema kuwa kutokana na tukio hilo, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Kigoma ilikutana kwa dharura katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa, hata hivyo, haikufahamika mara moja kilichojitokeza katika kikao hicho.

Mnamo Novemba 3, mwaka huu, kundi la watu tisa waliodaiwa kuwa ni waasi wa DRC wakiwa na majeraha yanayoaminika kuwa ni kutokana na kushambuliwa kwa risasi, waliingia mkoani Kigoma kupitia Kijiji cha Mtanga ambako kuna Kituo kidogo cha JWTZ na hivyo kujikuta wakitiwa mbaroni kirahisi.

Baada ya kukamatwa, waasi hao walipelekwa katika Hospitali ya Mkoa wa Kigoma, Maweni kupata matibabu kutokana na majeraha hayo. Inadaiwa kuwa mmoja wao ameshafariki dunia.


MWANANCHI

No comments: