Wednesday, November 16, 2011

WADOGO ZETU WA KIKE HAWAKO SALAMA FACEBOOKAbigail, mdada ambaye tuko jengo moja la ofisi alisafiri kikazi kwenda nje ya nchi mwezi uliopita. Laptop yake alimuachia mdogo wake wa kike ambaye anasoma O-level na kwa wakati huo alikuwa likizo. Abby anasema aliporudi siku ya pili yake wakati anatumia laptop aliamua kuingia Facebook, bahati mbaya mdogo wake akawa amesahau ku-sign out kwenye account ya Facebook. Ile kufunguka tu chat windwos kibao zikaja toka kwa watu ambao ni rafiki zake mwenye ile account. Si unajua mambo ya u-dada, udaku ukamuingia akaamua kuzama inbox kuona mdogo wake anawasiliana na kina nani. Alichokikuta huko ndo kimenifanya niandike hii article. Message alizokuta anatumiwa na majamaa ambao hata wengine hajawahi kuonana nao zilimtia wazimu hadi akaniomba ushauri endapo amwambie mdogo wake aifunge account.

Sitaki kuongelea sana ishu ya mdogo wake Abby, ila nataka nigusie huu ugonjwa wa Facebook ambao naona watanzania wengi miaka mitatu iliyopita ndo umewakamata. Siku hizi kila mtu anaijua facebook, anataka kuwa nayo.. hata siku hizi mambo ya kuwa na photo album nyumbani kuna baadhi wameacha, wakipiga picha wanatengeneza album facebook zote zinakuwa uploaded kule.

Kwa watu wazima, nikimaanisha hawa wa kuanzia umri wa vyuo mimi sioni tatizo anapofanya mambo ya ajabu Facebook, wanajua wanachokifanya. Tatizo ni kwa hawa wadogo zetu ambao wachache ni wa shule za msingi na wengi sana wa sekondari (O-level na A-level). Siku hizi utongozaji umekuwa rahisi sana kupitia Facebook, Enzi zetu (Miaka ile nikiwa Sekondari) ilikuwa ishu kuwapata watoto wa geti kali hasa wale ambao unakuta asubuhi anapelekwa shule na school bus jioni anarudishwa nyumbani na gari la mzazi wake. Ilikuwa inahitaji moyo na kung’atwa sana na mbu nje mtaani kwao hadi uanzishe mashambulizi. Nakumbuka kuna jamaa ilikuwa inabidi waende kuwinda sleepway weekend manake ndo siku ndege wanatolewa viotani. Lakini siku hizi wala huitaji kuhangaika sana, umempenda mtoto wa kike? Tafuta jina lake la Kwanza na la Ukoo alaf unaingia kwenye “facebook search” unaliandika lile jina.. kama yupo lazima utamuona. Au kama ukishindwa kumpata inawezekana ametumia nickname, wewe tafuta rafiki yake ambaye yupo Facebook alaf nenda kwenye friend list alaf scroll down taratiiiibu hadi utampata. Kisha bonyeza “send a friend request”, bahati nzuri hawakatai. Akikubali nenda kwenye profile yake, anza ku-comment kwenye picha zake. Hata kama hajapendeza press ile “Like” button, akiandika kwenye wall fanya hivo hivo yaani hakikisha anakuzoea, kifuatacho mvute kwenye inbox anza slow slow nakuhakikishia kama una maneno matamu haichukui mda kabla haujaangusha mbuyu kwa shoka moja.

Watoto wa sekondari asilimia kubwa bado hawajajua aina za marafiki wao walio nao Facebook, ni wepesi kukuamini na kukupa info zao binafsi. Ni rahisi kukutana na mtoto wa kike facebook mkaongea kwa siku chache alaf ukamuomba mkutane Mlimani City au sehem yoyote ya starehe akaja bila kukataa. Wengi wanadanganywa na picha wanazoziona kule jamaa wakiwa wamepiga kwenye sehemu nzuri za starehe au kwenye majumba na magari makali bila kujua kuwa siku hizi ni rahisi kwenda kwa jirani au ndugu yako na simu ukapiga picha kwa mapozi yoyote unayotaka na kuiweka Facebook na kila mtu akaamini kuwa ni ya kwako. Wengine tamaa baada ya kutumiwa vocha kwa ajili ya ku-top up simu zao ili waendelee kutumia Internet siku nzima wanajikuta wameingia kwenye huu mtego wa kuvutwa na majamaa ambao kazi yao kubwa ni kucheza na watoto wa shule.

Lakini mwisho wa siku tunarudi kwetu sisi ambao ni watu wazima na tumeona mabadiliko kwenye huu ulimwengu wa mawasiliano. Tumechukua hatua gani kuwalinda watoto wa kizazi hiki kwenye janga la hawa wanaoitumia teknolojia vibaya? Au tunasubiri siku tusikie binti mmoja kaitwa na mwanaume aliekutana nae Facebook kisha akabakwa na kuuwawa ndo tuanze kukemea? Nadhani tunatakiwa kuwaelewesha wadogo au wanetu ambao ndio kwanza wanaingia Facebook matatizo yake. Huwezi kusema utamzuia asitumie Facebook, utamzuia kutumia simu yenye Internet, atapata jamaa wa kumhonga simu nyingine na ataitumia usiku wakati mmelala. Au anaweza kuingia Internet Cafe akafanya analolitaka bila hata wewe kujua na saa nyingine wanapokuwa shule ni rahisi kuazima simu ya rafiki yake akaingia. La muhimu hapa ni kuwa muwazi.

Mfano mimi wakati mdogo wangu anajiunga wakati huo akiwa Form 5 nilimweleza A-Z ya watu anaoenda kukutana nao, nilimpiga mkwara kuhusu picha atakazoweka kule na hata vitu atakavyoviandika kwenye wall yake kwa kumwambia akifanya kitu chochote cha aibu, haitakuwa ya kwake ila ya familia nzima. Nashukuru alinielewa. Vile vile kama upo facebook, jaribu kuhakikisha umemuweka mwanao au mdogo wako kwenye marafiki zako na uwe unafatilia vitu anavyoviandika au picha gani anatumia. Itakuwa rahisi kwako kujua aina ya marafiki zake na pale utakapohisi kuna kitu ambacho sio cha kawaida kinaendelea basi muulize.

Sijui kama mamlaka ya mawasilianio Tanzania TCRA zaidi ya kuvuta mkwanja kwenye makampuni ya simu na wadau wengine kama wana utaratibu wa kutoa elimu kwa mlaji wa mwisho. Wenzetu wana utaratibu wa kuwafundisha watu matumizi ya internet kwa usalama zaidi mfano ni United States Computer Emergency Readiness Team (Marekani) kazi yao ni kuhakikisha usalama wa watumiaji wote wa mtandao kwa kutoa dondoo za matumizi bora. Nchi nyingine pia kama Uingereza, afrika Kusini, Australia, Saudi Arabia wote wanavyo hivi vitengo.

Hii tabia ya yetu ya kulea matatizo iliwahi kututokea puani mwaka 2010 wakati Uchaguzi. Nakumbuka kabla ya hapo alikuwa anatokea mjinga mmoja anaandika message ya matusi anaituma kwa watu wengi baada ya hapo inasambaa kwa karibu nusu ya watumiaji wa simu hasa wakati ule wa extreme SMS. Kwa kutumia mwanya huo huo wa watu kuwa vilaza wa matumizi ya simu, mtu mmoja akatuma message ya kumkashifu Doctor Slaa kuwa analeta ukabila na matusi mengi mengi ikasambazwa kwa watu wengi sana. Baada ya hapo ndio TCRA wakapiga mkwara.

Nadhani wakati wa kutafakari Umefika.

Ni hayo tu.


BEEN THERE DONE THAT

No comments: