Tuesday, November 8, 2011

VUTA NIKUVUTE ARUSHA


MAHAKAMA YAMNYIMA DHAMANA LEMAMussa Juma , Arusha.
MBALI ya jitihada kubwa kufanywa na maofisa wa juu wa Jeshi la Polisi nchini sambamba na Mwenyekiti wa Chadema taifa , mwishoni mwa wiki iliyopita kumshawishi Mbunge wa Arusha Mjini, Gobless Lema, kulegeza msimamo wake ili atoke mahabusu jana na mwanasiasa huyo kuafiki, suala hilo liligonga mwamba baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha, kukataa kutoa hati maalumu ya kumtoa rumande.

Jumamosi iliyopita ujumbe mzito wa Jeshi la Polisi ukiwa na makamishna wawili, kutoka Makao Makuu ya Polisi Dar es Salaam ulimtembelea Lema gerezani na kuzungumza naye kuwasilisha maombi maalumu ya kumtaka akubali kutoka mahabusu ili kurejesha amani na utulivu mjini Arusha.

Maofisa waliomtembelea mbunge huyo ni Peter Kivuyo, Simoni Siro na Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Arusha, Leonard Paul.

Mbali na maofisa hao Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na viongozi wenzake alimtembelea Lema gerezani hapo na kumsihi akubali kutoka kwa dhamana ili apate nafasi ya kwenda bungeni kuueleza umma wa Watanzania na jamii ya kimataifa, adha anazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake.

Hatua ya mahakama hiyo kukataa kutoa hati ya kumwachia Lema ilifanya sakata la mbunge huyo kugeuka kuwa kama sinema au mchezo wa kuigiza, huku Jiji la Arusha na viunga vyake likiingia kwenye taharuki baada ya mamia ya wafuasi wa Chadema walioamini kuwa ataachiwa leo, kuamua kupiga kambi Viwanja vya Unga Limited wakishinikiza mwanasiasa huyo aachiwe huku viongozi wao wakitoa hotuba kali.

Wakati wafuasi hao wakishinikiza Lema afikishwe mahakamani kisha achiwe huru kwa dhamana, mahabusu waliokuwa wakifikishwa katika Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Arusha, nao waligoma kushuka kwenye karandinga na kusababisha shughuli zote za mahakama hiyo kusimama.

Licha ya shinikizo la wafuasi hao kutaka kuachiwa Lema kuwa juu, mahakama hiyo jana mchana ilipasua machungu kwa wanachama na wapenzi hao baada ya kutangaza kwamba mbunge huyo atatoka kwa dhamana Novemba 14 mwaka huu saa 2:30 asubuhi.

Hali mahakamani
Kuanzia jana saa 2:30 asubuhi, mamia ya wafuasi hao wa Chadema walikuwa wamefurika viwanja vya Mahakama kuu, wakiimba nyimbo mbalimbali za kuhamasisha umoja na mshikamano hali iliyosababisha adha kubwa katika eneo hilo la mahakama lenye Mahakama ya Mkoa, Mahakama Kuu na Mahakama ya Biashara.

Kadri muda ulivyokuwa ukisogea watu walizidi kuongezeka. Saa 3:30, lilifika Karandika la mahabusu na washtakiwa wengine lakini wote waligoma kushuka wakitaka kwanza Mbunge Lema afikishwe mahakamani na kupewa dhamana.

Hali hiyo, ilizua kelele katika viwanja vya mahakama na baada ya majadiliano kati ya maofisa wa mahakama na polisi, iliamuliwa karandika lirejeshwe gerezani na kesi zote za jana zitapangiwa siku nyingine.

Hata hivyo, kadri muda ulivyozidi kujongea harakati za kumtoa Lema zilionekana kukwama, ndipo viongozi wa Chadema, walimwita Mwenyekiti wa chama hicho mahakamani ambaye alikwama kufanikisha kumtoa Lema.

Saa 10 jioni, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa na Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki, Tundu Lissu, walifika viwanja vya mahakama kufuatilia sakata hilo lakini waligonga mwamba.

Wakati wafuasi na viongozi hao wa Chadema wakihaha kumtoa Lema, mahakimu na watendaji wa mahakama walifanya kikao ofisini kwa Jaji Aisha Nyerere hali ambayo iliongeza jazba kutoka kwa wafuasi na wapenzi wa Chadema waliokuwa eneo hilo.

"Sisi tunamtaka mbunge wetu wao wanafanya kikao," walisikika walalamika wafuasi hao na baadaye walianza kuimba:, "Tunamtaka mbunge wetu..., tunamtaka mbunge wetu!"

Hata hivyo, baadaye kikao hicho kilimalizika na kupatikana barua rasmi iliyokuwa imetolewa mapema mchana kuwa mahakama imekataa kutoa dhamana kwa Lema hadi Novemba 14, mwaka huu saa 2:30 asubuhi atakapofika mahakamani na wadhamini wake.


Awali, Mahakama hiyo ya Hakimu Mkazi Arusha iligoma kutoa hati maalumu ya kumtoa Lema mahabusu anayeshikiliwa katika Gereza kuu la Kisongo lililopo nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Barua ya kuomba hati hiyo iliyoandikwa na Wakili wa Lema, Method Kimomogoro, kwenda mahakamani kuomba mteja wake aletwe kwa ajili ya taratibu za dhamana, ilikumbana na kigingi hicho cha mahakama baada ya Hakimu, Judith Kamara, anayesikiliza shauri hilo, kuagiza wenye nia ya kumdhamini mbunge huyo kufika siku kesi itakapotajwa.

“Wadhamini wamshtakiwa wafike mahakamani siku ya kutajwa kesi tarehe 14/11/2011 Saa 2:30, asubuhi kwa ajili ya utaratibu wa dhamana kwa mujibu wa masharti ya dhamana iliyowekwa na mahakama,” imeeleza barua ya mahakama kujibu ombi la wakili wa Lema.

Katika barua hiyo ya Novemba7, mwaka huu yenye kumb. namba RM/GC/Vol. 111/50, mahakama haikutoa sababu za kukataa kutoa hati hiyo ambayo ingefanikisha Lema kuwekewa dhamana na kuungana na viongozi wa kitaifa wa chama hicho kwenye mkutano mkubwa wa hadhara uliofanyika viwanja vya NMC.

Wadhamini waliojitokeza kumdhamini mbunge huyo aliyeamua kwenda mahabusu kwa hiari yake kupinga uonevu, manyanyaso na ukandamizaji wa Jeshi la Polisi dhidi yake, wanachama na wapenzi wa Chadema walitambuliwa kwa majina ya Sarah Mohamed na Halfani Rashid ambao walilazimika kuondoka mahakamani hapo Saa 9:30 alasiri baada ya kusubiri kutekeleza jukumu hilo tangu saa 2:30 asubuhi.

Akizungumzia suala hilo ofisini kwake jana, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Mkoa Arusha, Charles Magessa, alisema kisheria hakimu habanwi na kifungu chochote kutoa hati ya kumtoa mahabusu gereza bali kinachozingatiwa ni mazingira ya kesi na ulazima unaojitokeza.

“Kwa mfano, iwapo kuna ushahidi muhimu unatakiwa kutolewa na shahidi ana dharura ya safari nje ya nchi itakayomnyima kufika mbele ya mahakama siku iliyopangwa, hakimu anaweza kutoa hati ya kumtoa mtuhumiwa mahabusu ili ushahidi huo usikilizwe. Mengine yanayobaki ni busara ya mahakama ambayo haifungwi na jambo au nguvu yoyote kisheria,” alisema Magessa.

Hakimu Magessa alisema kiutaratibu, maombi ya hati hiyo huwasilishwa kwake kama kiongozi kiutawala, naye huifikisha kwa hakimu anayehusika na kesi na ndivyo alivyofanya katika suala la maombi ya wakili wa Lema.

Gari la Mbowe chupuchupu
Katika tukio jingine, jana gari lililokuwa limebeba Mwenyekiti wa Chadema, Mbowe lilinusurika kugongwa na gari la polisi lililokuwa likimzuia kiongozi huyo asikaribie eneo la majengo ya mahakama alipokwenda kuzungumza na uongozi wa muhimili huo wa dola, kujua kinachokwamisha hati hiyo ya kumtoa Lema gerezani .

Gari lilikimbizwa na kuzuiwa njia likiwa tayari limeingia ndani ya
uzio la mahakama baada ya Mkuu wa Idara ya Upelelezi Mkoa wa Arusha (RCO), Leonard Paul, kumwagiza dereva wa gari la polisi lenye namba za usajili PT 1178 kuzuia njia ili Mbowe asipite.

“Zuia hiyo gari...zuia hiyo gari, likimbize lisipite, fanya haraka
linapita,” alisikika akitoa amri RCO Paul, amri iliyotekelezwa kwa
gari la polisi kulikimbiza gari la Mbowe ambalo tayari lilikuwa
imepita, hivyo kumlazimisha dereva wa gari hilo kusimama na kutishia kuligonga ubavuni upande wa dereva.

Hali tete iliyokuwepo mahakamani hapo jana ililazimisha uongozi wa polisi kuimarisha ulinzi ulioongozwa na RCO Paul, huku Kaimu Kamanda wa Mkoa, Akili Mpwapwa, akifanya doria ya kukagua hali ya usalama.

Uongozi wa polisi ulilazimika kuwaomba viongozi wa Chadema wakiongozwa na Mbowe, Katibu Mkuu, Dk Slaa, Mbunge wa Singida Mashariki, Lissu na Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Ephata Nanyaro kufika mahakamani hapo kuwaomba wafuasi wa chama hicho kuondoka ili kuwawezesha majaji, mahakimu, mawakili na makarani waondoke.

Viongozi hao walifika na baada ya majadiliano na polisi na uongozi wa mahakama, ndipo Mbowe na Dk Slaa waliwaomba wananchi waliokuwa wamefurika eneo la mahakama kuondoka kuelekea uwanja wa NMC ambako kulikuwa na mkutano mkubwa wa hadhara.

Hatimaye, msafara wa wanachama hao ulioongozwa na Mbowe na Dk Slaa uliondoka mahakamani hapo manmo saa 9:30 alasiri hadi Uwanja wa NMC ambako licha ya mvua kubwa iliyokuwa ikinyesha, watu waliendelea kusikiliza hotuba za viongozi hao kwa utulivu huku wakipaza sauti kuomba ruhusa ya kuchukua uamuzi mgumu wa kwenda kumtoa gerezani Lema kwa nguvu ya umma.

Dereva wa Lema adaiwa si raia
Dereva wa Lema, Rashid Shubeti ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema Kata ya Kati, jana alifikishwa mahakamani kujibu mashtaka matatu ya kuchochea vurugu, kuharibu mali na kufanya vurugu.

Shubeti ambaye alikamatwa tangu Ijumaa, pia awali analihojiwa na maofisa wa Uhamiaji Arusha kuhusu na uraia wake na jalada lake la uchunguzi linaendelea.

Akizungumza mara baada ya kupata dhamana jana, Shubeti ambaye tangu Jumatano wiki iliyopita alikuwa akilalamika kufuatwa na polisi nyumbani kwake kabla ya kukamatwa ,alisema maofisa wa polisi walimfuata nyumbani na kumpekua kisha kumfungulia kesi hizo.


Polisi wataka amani.
Idadi kubwa ya polisi ambao jana walikuwa wamefurika katika viwanja vya mahakama, waliomba vyombo vya habari visaidie kuweka wazi mgogoro wa Arusha ili amani ipatikane.

"Jamani tusaidieni leo tumekaa siku nzima hapa na jambo hili litaendelea sasa hali hii itaendelea hadi lini, Arusha ni mji wa kimataifa unataka amani andikeni kila kitu msimuogope mtu ili amani irejee Arusha," alisema polisi mmoja kwa sharti la kutoandikwa jina gazetini.
MWANANCHI

No comments: