Friday, November 4, 2011

UTAIFISHAJI WA MASHIRIKA KISIASA ULIVYOATHIRI UCHUMI
Lawrence Kilimwiko


MOJA ya azma ya Azimio la Arusha ilikuwa ni kuziweka njia kuu zote za uchumi mikononi mwa umma ili kuondokana na unyonyaji.

Haikushangaza kuwa mara baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha, Februari 7, 1967, Serikali ilitangaza kutaifishwa kwa mabenki yote ya kigeni nchini. Benki pekee zilizoachwa ni zile za Washirika (yaani, Co-operative Bank) pamoja na Benki ya Watu wa Zanzibar (yaani, Zanzibar People’s Bank).

Makampuni nane ya uagizaji na usafirishaji bidhaa nje pia yalikumbwa na kumba kumba hiyo. Haya yalikuwa ni pamoja na: Smith Mackenzie and Co. Ltd; Delgety (E.A.) Ltd; International Trading and Credit Co.Ltd; Twentsche Overseas Trading Co. Ltd; Co-operative Supply of Tanganyika Ltd; A. Bauman and Co.(Tanganyika)Ltd na vile vile Wigglesworth and Company (Africa)Ltd.

Makampuni yapatayo nane ya usagishaji ambayo yalikuwapo wakati huo, nayo yalitaifishwa na Serikali kuwa mali ya umma chini ya Shirika la Usagishaji la Taifa.

Shirika la Bima la Taifa (The National Insurance Corporation) liliwekwa chini ya mamlaka ya umma na kupewa hodhi ya mambo yote ya bima nchini.

Unyakuaji wa mali binafsi na kuziweka mikononi mwa umma haukuishia hapo. Serikali ilinyakua asimilia 60 ya hisa katika viwanda kadhaa. Hali kadhalika, asilimia 60 ya biashara ya mkonge ilitaifishwa na kuwekwa chini ya umma kwa kuundiwa Mamlaka ya Mkonge Tanzania.

Kati ya mwaka 1967 hadi 1980 mashirika ya umma yaliyotafishwa yaligusa karibu kila sehemu ya uchumi, na kwa maana hiyo Serikali ikajiingiza katika kufanya biashara.

Takwimu zilizopo zaonyesha ya kuwa hadi kufika mwaka 1990, kulikuwa na Mashirika ya Umma zaidi ya 400, yaliyokuwa yamelimbikiza hasara ya zaidi ya Dola za Marekani milioni 100.

Moja ya tatizo la awali lililoikabili serikali ni ule ukweli kwamba haikuwa na watumishi wa kutosha wenye weledi wa kuendesha mashirika yote hayo na hasa yale ya biashara kwa wakati moja.

Lakini tatizo kubwa ni jinsi uteuzi wa mameneja na ajira ya watumishi ilivyofanywa. Uteuzi wa mameneja ulifanywa na Rais kwa kuzingatia zaidi uzalendo badala ya weledi wa kibiashara wa shirika husika.

Na kwa kuwa serikali ilikuwa na mashirika mengi kuliko watumishi wenye weledi, mengi ya mashirika haya yaliendeshwa kisiasa zaidi kuliko biashara.

Isitoshe kila meneja aliposhindwa kuendesha shirika kutokana udhaifu, ubadhirifu au vinginevyo, mtindo uliokuwepo ulikuwa ni kumhamishia kwenye shirika jingine badala ya kumfukuza. Matokeo yake uwajibikaji kikawa ni kitu adimu sana.

Kwa upande wa wafanyakazi wa kawaida, hawa walipangiwa kwenda kwenye mashirika bila kujali matakwa yao. Hiyo nayo ikachangia kuua ari ya kuyaendesha mashirika haya kwa ufanisi.

Kama hiyo haitoshi , kulikuwa na uingiliaji wa kisiasa ambao haukuzingitia tija kiasi kwamba mashirika haya yakageuzwa kuwa vyombo vya kukidhi matakwa ya kisiasa badala ya kudumia umma na kuleta maendeleo na ustwi wa watu.

Haikushangaza basi kwamba, lilipoibuka wazo la ubinafsishaji, mashirika 78 yalikwisha kufungwa kwa kushindwa kujiendesha. Mengine mengi yalikuwa yamewaachisha kazi wafanyakazi au kuwapa likizo bila malipo huko mengi ya yaliyosalia yakizalisha chini ya uwezo.

Kwa hakika, tatizo la kuyaendesha mashirika kulichangiwa na siasa zaidi kuliko ujuzi. Ni kweli kwamba kuna mashirika ambayo ni lazima yamilikiwe na kuendeshwa na umma kutokana na unyeti wake. Eneo hili linagusa mashirika ambayo huzalisha faida kidogo na ambayo si rahisi kwa kampuni binafsi kuyaendesha.

Ujenzi wa miundo mbinu hasa barabara, njia za reli, viwanja vya ndege, bandari, mamlaka za maji, ujenzi wa njia za umeme na huduma kwa umma hasa elimu na afya ni jukumu ambalo duniani kote kubebwa na umma.

Lakini badala ya serikali ya TANU kusimamia maeneo haya, yenyewe ilijiingiza hata biashara iliyopaswa kuendeshwa ba mtu mmoja mmoja, mathalani, kuendesha biashara ya bucha, mikate ya siha au vinywaji.Matokeo yake ikawa kusambaza uwezo, mtaji hadi watumishi na hivyo kushindwa usimamiaji.

Na kwa kuwa kusudio jingine lilikuwa kutoa ajira, mengi ya mashirika haya yalijikuta yakiwa na watumishi wengi kuliko ilivyohitajika. Na kama hiyo haitoshi, hata mishahara ya watumishi wa mashirika ya umma ilikuwa inafanana kwa vile ilikuwa ikipangwa na Kamati ya Mashirika ya Umma, maarufu kama SCOPO.

Kwa maneno mengine, mashirika yaliyokuwa yanapata hasara yalikuwa yanafidiwa na yale yaliyokuwa yanazalisha ziada. Mwisho wa siku kukawa na hakuna ushindani wala ufanisi.

Lakini pia kulikuwa na uingiliaji mkubwa sana wa kisiasa katika uendeshaji wa mashirika hayo. Kulikuwa na michango isiyoisha kwa ajili ya uendeshaji wa chama tawala licha ya ukweli kwamba uzalishaji ulikuwa unazorota.
Matokeo ya jumla ikiwa kushindwa kwa mashirika ya umma kuhimili ushindani wa kibiashara kutokana na urasimu, ukiritimba pamoja na mfumo mbaya wa uongozi na usambazaji bidhaa au utoaji wa huduma.

Kuzorota kwa huduma na bidhaa kulizababisha kuibuka kwa biashara ya magendo, foleni, vibali, rushwa na hata maduka ya kaaya.

Haikushangaza kwamba, mwisho wa siku serikali ililazimika kufanya mageuzi kwa kurudi kule kule ilikotoka, yaani kubinafsisha mashirika yale yale yaliyokuwa yametaifishwa kwa makampuni yale yale yaliyokuwa yamenyakuliwa mali zake.


MWANANCHI

No comments: