Wednesday, November 9, 2011

POLISI AMFYATULIA RISASI MREMBO: KISA ANATAKA PENZI KWA KUTUMIA NGUVUNa Joseph Ngilisho, Arusha


NI akili yake au nguvu ya Shetani? Ni kiburi cha silaha ya moto au ubabe kwa sababu anavaa magwanda? Tukio la askari polisi aliyefahamika kwa jina moja la Sengerema kumfyatulia risasi mrembo aliyemnyima penzi limeacha mshtuko mkubwa.

Sengerema, anadaiwa kumfyatulia risasi mrembo, Brenda Mrema, 25, baada ya kutoleana lugha chafu ambazo chanzo chake ni kushindwa kuelewana kwenye somo la mapenzi.

Tukio hilo lilichukua nafasi Oktoba 2, 2011 eneo la Benki ya NBC, Tawi la Unga Limited. Sengerema na wenzake, walikuwa wakilinda usalama kwenye kituo hicho cha fedha.

Mashuhuda wa tukio hilo walieleza kuwa Brenda akiwa na rafiki yake anayeitwa Brenda Mike, 24, waliegesha gari lao aina ya Toyota Alteeza Gift kwenye eneo la maegesho kwenye benki hiyo.

SHARI ILIPOANZA

Vyanzo vyetu vilidai kuwa Sengerema aliwafuata warembo hao na kuwauliza ni kwa nini waliacha gari linawaka eneo la benki, swali ambalo Brenda (Mrema) alilijibu kwamba wameacha hivyo kwa sababu kiyoyozi kinawaka ndani.

Brenda (Mrema) aliliambia Uwazi: “Nilipomjibu hivyo, akaanza kuongea mambo ya mapenzi kuonesha kuwa ananitaka, mwenzangu alimjibu tofauti kumuonesha kuwa anachotaka hakiwezekani. Tukashangaa yule askari anaanza kutoa maneno ya kashfa.

“Alituambia tunaringia ngozi ya kichina, sura zetu zimekomaa, tulipomjibu ndipo alikasirika na kutulenga bunduki na kuikoki. Bahati nzuri alitokea mwenzake, akaishika bunduki kwa nyuma, hiyo ikasaidia kuikwepesha risasi na kwenda kupiga ukuta wa benki.”

Mmoja wa wafanyakazi wa benki hiyo (jina tunalo), alilithibitishia Uwazi kuwa aliona tukio hilo na jinsi askari wa pili (jina halijapatikana) alivyomdhibiti Sengerema kwa kuishika bunduki kwa nyuma, hivyo kusaidia risasi imkose Brenda (Mrema).
“Kama siyo yule askari yangekuwa mengine, alikuwa amemlenga kifuani yule dada,” alisema mfanyakazi huyo wa benki.

SAKATA LATINGA KWA WAKUBWA

Baada ya shambulio hilo, taarifa zilifika Makao Makuu ya Polisi Arusha, kabla ya Mkuu wa Kituo cha Polisi Kati (central) Arusha, OCS Philip Mziray kufika eneo la tukio akiwa ameongozana na ofisa upelelezi (Inspekta) anayeitwa Elikana na kumuweka chini ya ulinzi Sengerema.

Habari zinadai kuwa OCS Mziray na Inspekta Elikana, walimnyang’anya Sengerema bunduki yake, wakaikagua na kubaini kuna ganda moja la risasi limebaki, hivyo kuthibitisha kuwa risasi moja ilifyatuliwa.

OCS Mziray alimueleza mwandishi wetu kuwa tukio la Sengerema kudaiwa kumfyatulia risasi Brenda lipo lakini alikataa kutoa ufafanuzi kuhusu hatua ambazo zitachukuliwa dhidi ya askari huyo.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Arusha Mjini, OCD Zuberi Mombeji aliliambia Uwazi kuwa uchunguzi unaendelea kisha akaomba atafutwe Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Akili Mpwapwa aweze kutoa ufafanuzi zaidi.

Kamanda Mpwapwa alipoulizwa alisema: “Ngoja nilifuatilie nipate ukweli unajua tukio kama hilo si la kawaida kutokea.”


UWAZI

No comments: