Wednesday, November 30, 2011

OPERESHENI BARAKUDA YARUDI AFRIKA
Na Marie Shaba,

“Hillary Clinton alipotembelea Jamhuri ya Kidemokrasia ya watu Kongo (DRC) Agosti, 2009 aliwashangaza raia wa Kongo alipowaambia wasahau yaliyopita wasonge mbele. Swali ni je, Marekani iko tayari kusahau Septemba 11, na kusonga mbele?” Ndivyo alivyoandika Prof. Georges Nzongola –Ntalaja kwenye Jarida la The Africa Report la Aprili-Mei, 2010.

Waafrika tumesamehe mengi, lakini kamwe hatutasahau madhila na madhara ya biashara ya Utumwa na Ukoloni. Kila kukicha tunakumbushwa utumwa wa kisiasa, kiuchumi na kijamii. Bw. Yesu alisema; “Akupigae shavu la kulia, mgeuzie na la kushoto”. Huwa najiuliza ukisha mpa yote mawili inakuaje?

Waafrika ni taifa moja kwa hiyo yanayotokea kote Afrika yanatuhusu sote. Kwa nini hatushangai Marekani yenye nchi /majimbo zaidi ya 50 au Umoja wa Ulaya nchi zaidi ya 20, zinaongea kwa pamoja na nchi zetu mmoja mmoja.

Hivi hatuoni hili peke yake ni tatizo, hata kama Gaddafi “asingewaswaga” kama baadhi ya viongozi wa Afrika wanavyodai? Mpaka lini kiongozi wa Afrika ataendelea kuvumilia unyonge wakusimama peke yake mbele ya nchi za Marekani au Ulaya katika masuala ambayo yanatuumiza waafrika wote? Je, tunasubiri idhini yao na kibaraka wao ndio tuzinduke?

Tuna changamoto ya kuchanganya “ kusamehe na kusahau”. Kusamehe ni rahisi kwani mtu anaweza kukutia kovu kwa kukusudia au kwa bahati mbaya, ukamsamehe. Lakini itakuwa ni unafiki ukisema utasahau, kwani kovu litakukumbusha. Je mtu huyo akikuumiza tena utafanyaje?

Historia inatabia ya kujirudia ndio maana matukio yote yanaandikwa ili kila kizazi kielewe na kisibweteke. Inaelekea Waafrika tu ndio mabingwa wakusamehe na kusahau. Viongozi wetu wengi wameuawa kikatili na kwa njama; Patrice Emery Lumumba wa Kongo mpaka leo damu yake haijakauka.

Oparesheni Barakuda ya kumuua Patrice Lumumba ni mfano hai kuwa wajukuu wa wakoloni hawabweteki. Udhalimu na dhuluma vipo, kusahau na kusonga mbele bila kujihami ni usaliti.

Marekani wanakumbuka 11.09.2001 na kuhakikisha haitokei tena, Wayahudi wanakumbuka, ili kila kizazi chao kiape yasitokee tena. Iweje sisi na kwa utakatifu gani, tusahau? Kwa nini tunawaandalia watoto na wajukuu wetu utumwa wa hiyari ?

Raoul Peck alitoa maoni yake kuhusu kitabu cha “Mauaji ya Lumumba” kilicho andikwa na Ludo de Witte “…ni hadithi isiyo isha, yenye kujaa dharau, uroho na utemi. Wauaji bado wako kati yetu.” Kila Mwafrika ni lazima akumbuke, yaliyotokea kwa Lumumba ni ushahidi dunia imejaa wanywadamu. Miaka 50 ya Uhuru itukumbushe ufashisti wa kiuchumi uliosababisha Lumumba auwawe Januari 17, mwaka 1961 na Gaddafi Oktoba 20, mwaka 2011. Ludo de Witte anatueleza kwa ufasaha mambo yalivyokuwa Kongo Juni 30, mwaka 1960.

Anasema wageni kutoka nje na ndani ya Kongo na waandishi wa habari walikusanyika Ikulu mjini Leopoldville. Katika lango kuu la kuingilia Ikulu ilikuwapo sanamu ya Leopold 11, “muasisi “ wa nchi ya Kongo, ikikejeli kwamba uhuru huu hautabadilisha chochote.

Mfalme Baudouin wa Ubelgiji alikuwa wa kwanza kuhutubia, na akaonyesha mazuri yaliyofanywa wakati wa ukoloni. “Uhuru wa Kongo ni matokeo ya juhudi za Mfalme Leopold 11 kwa hiyo, mjihadhari msije mkabadili mifumo ambayo tunawakabidhi leo mpaka mkiwa na uhakika kuwa mtafanya vizuri zaidi kuliko sisi… msihofu tuko pamoja na tutajenga uwezo wenu wakujitawala…”

Baada ya Mfalme ikawa zamu ya Joseph Kasa -Vubu, Rais wa kwanza wa Kongo naye aliwafurahisha wakoloni aliposema hata kama wao Waafrika watashika madaraka lakini nyuma ya pazia wazungu wataendelea kuongoza ili mambo yasiharibike. Baada ya Rais Kasa -Vubu kuongea, Spika Joseph Kasongo alimkaribisha Waziri Mkuu Patrice Lumumba, akiwa na umri wa miaka 35 atoe hotuba yake.

Mfalme na waziri wake mkuu Gaston Eyskens wakashikwa na butwaa kwa kuwa Lumumba hakuwepo kwenye ratiba na wala hawakupata nakala ya hotuba yake, japo waandishi wa habari waligawiwa. Maneno yaliyokuwa kwenye hotuba yake yalifanya damu zao zigande. Hotuba ya Lumumba ilikuwa kwa ajili ya Wakongo waliopigana kupata uhuru na kushinda. Sherehe ikahamia katika kuwaenzi Wakongo badala ya wakoloni.

Wakongo waliambiwa kwamba uhuru walioupata si fadhila za Brussels kama Mfalme anavyotaka waamini na si matokeo ya makubaliano kati yao na Ubelgiji. Lumumba alisema “Hakuna Mkongo mwenye heshima yake anaweza kusahau kwamba ni harakati zetu ndio zimetufikisha hapa. Tumepambana kila siku, harakati za dhati…na kila tone la damu lilikuwa ni sehemu ya mapambano.”

Lumumba aliukashifu ukoloni uliosifiwa na Baudouin, kwamba ni utumwa uliosokomezwa kwa Wakongo. Aliendelea kusema; “Tulichoambulia katika ukoloni ni kejeli na matusi, tumevumilia ngumi tangu machweo mpaka kuchwa kwa kuwa sisi ‘nyani’. Nani atasahau kwamba mtu mweusi alikua anaitwa “wee” kwa dharau. Tumeshuhudia jinsi ardhi yetu ilivyonajisiwa na sheria dhalimu ambazo zimewapendelea wazungu wachache.

Tumeshuhudia wazalendo wanaopigania haki na utu wakiwa wakimbizi ndani ya nchi yao, adhabu ambayo ni kubwa kuliko kifo…nani atasahau milio ya bunduki na kaka zetu waliouwawa na jela zilizojaa wanamapinduzi waliokataa utawala wa dhuluma wa wakoloni. Wabelgiji wasingeweza kuzuia uhuru wetu.”

Lumumba alishangiliwa sana na hotuba yake ilikatishwa mara kwa mara; Kongo nzima ilipata habari ya namna Lumumba alivyotema cheche mbele ya Wabelgiji. Kaongea lugha ambayo Wakongo hawakuamini inawezekana mbele ya wazungu. Kwa Wakongo ilikuwa kama zawadi kwa miaka 80 ya utawala wa wabelgiji. Kwa mara ya kwanza Mkongo kazungumza kuashiria ujenzi wa historia ya Kongo mpya na kutia ragba kwa Wakongo kwamba wanastahili kujithamini, kujiamini na kujitawala.

Wakoloni walibaki na mshangao na Brussels ghafla ikajikuta ana kwa ana na mapinduzi iliyokua inayahofia. Ukoloni ulionadiwa na Mfalme kama biashara nzuri, ukanyambuliwa na Lumumba kuwa ni utumwa mbele ya wakoloni wenyewe. Majuma machache kabla, wakoloni walimnanga Lumumba kwamba ni ngumbalo, limbukene, nyani aliepaishwa juu kama jiwe kwenye manati.

Wakati Lumumba anaendelea kutema cheche kulikua na kanali Frederic Vandewalle kiongozi wa upelelezi, ambaye alikuwa anamsikiliza kwa makini. Japo hakupenda maudhui ya hotuba ya Lumumba, alielewa kuwa hayo ndiyo maoni ya wa Kongo wanataka kusikia kutoka kwa viongozi wao. Vandewalle ameandika katika kitabu chake “Siku 1004” jinsi umma wa Kongo ulivyotaka uhuru wao uwe wa dhati na ujidhihirishe katika maisha bora.

Je, Vandewalle alikua ni nani Kongo baada ya Uhuru na kwa nini Moise Tshombe na msafara wake walivutiwa nae? Ni kwa vipi alikua adui hatari wa uhuru wa Kongo? Kwa nini baada ya kustaafu na Kongo kuingia katika machafuko Vandewalle alihitajika tena Kongo?

Sehemu ya pili ya muendelezo wa makala haya tutaona jinsi mwaka 1960 ulivyokuwa wa mafanikio kwa Lumumba lakini pia wenye maafa makubwa. Mwaka 1959 alikuwa jela Katanga, Mei akashinda uchaguzi, Juni Waziri Mkuu. Septemba, akapinduliwa na kuwa chini ya ulinzi, aliuwawa17 Januari 1961.


RAIA MWEMA

No comments: