Monday, November 14, 2011

NANI ALICHOCHEA JESHI KUASI MWAKA 1964


Na Joseph Mihangwa
,


USIKU wa kuamkia Januari 21, 1964, Jeshi la Tanzania liliasi na kushikilia serikali kwa muda, tukio ambalo Baba wa taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alilielezea kuwa ni “siku ya aibu sana kwa Taifa” .

Wakati jeshi hilo likiasi; siku hiyo hiyo, na saa hiyo hiyo, majeshi ya Kenya na Uganda nayo yaliasi kwa staili hiyo hiyo. Maasi yote ya nchi tatu hizo yalizimwa na majeshi ya Uingereza siku moja na wakati huo huo.

Kwa Tanzania, maasi haya yalitokea wiki moja tu baada ya mapinduzi ya umwagaji damu ya Zanzibar, Januari 12, 1964; na usiku huo wa maasi hayo, Kiongozi wa Mapinduzi ya Zanzibar “Field Marshal” John Gidion Okello, alikuwa na mazungumzo na Mwalimu Nyerere Ikulu, Dar es Salaam, katika hali ya kubadilishana mawazo juu ya hali ya Zanzibar ambapo Mwalimu, alimshauri Okello afanye kazi kwa imani na Rais Abeid Amani Karume.

Karume aliteuliwa na Okello, Januari 13, 1964 kuwa Rais asiye Mtendaji kutokana na mapinduzi hayo; na yeye Okello akajiteua Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Maasi hayo yalitulizwa kwa juhudi kubwa za Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, Oscar Satiel Kambona, kabla ya kudhibitiwa na hatimaye kuzimwa kabisa na wanajeshi wa Kiingereza siku moja baadaye.

Mpaka leo, haijafahamika vizuri aliyepanga na kutekeleza maasi hayo; lakini swali kuu linaloulizwa bila kupata jibu ni je, ilikuwaje majeshi ya nchi tatu za Afrika Mashariki kuasi siku na wakati ule ule, juma moja tu baada ya Mapinduzi ya Zanzibar?

Dhana moja inajitokeza kwamba, kwa kuwa John Okello, mzaliwa wa Lang’o, Uganda, ndiye aliyeongoza Mapinduzi ya Zanzibar, na pia kwamba aliwahi kuishi nchini Kenya kabla ya kwenda Zanzibar miezi michache kabla ya Mapinduzi; huenda alikuwa na mkono wake katika maasi hayo. Okello alijitapa pia kushiriki vita vya Mau Mau nchini Kenya, miaka ya 1950.

Lakini, kwa vipi maasi hayo nchini yaanze usiku huo huo Okello alipokuwa mgeni wa Mwalimu, Ikulu? Alitorokaje yalipoanza?

Ipo dhana nyingine kwamba, huenda Oscar Kambona alikuwa na mkono wake. Kwa nini wanajeshi walimsikiliza yeye, wakati huo huo askari hao wakimtafuta Mwalimu hadi viwanja vya Ikulu, kwa shari au vinginevyo?

Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kuangalia kwa ufupi matukio kadhaa yaliyotangulia maasi ya nchi hizo tatu, kuona kama yana uhusiano wowote.

Tanzania bara ilirithi Jeshi kutoka kwa Wakoloni wa Kiingereza baada ya uhuru, Desemba 9, 1961, likijulikana kama “Kings African Rifles” – (K. A. R) na baadaye kuitwa “Tanganyika Rifles” (TR) na kutokana na maasi hayo ya Januari, 1964 likaitwa “Jeshi la Wananchi wa Tanzania” (JWTZ).

Katika kipindi kufuatia uhuru, ili kukidhi matarajio ya Watanganyika, zilitakiwa hatua za haraka kuhakikisha nafasi zote za juu serikalini na taasisi zake, zinashikwa na Wazalendo. Huu ni utamaduni uliokuwa umejengeka kwa nchi zote za Kiafrika zilizokuwa zikipata uhuru

Nyerere hakuwa na ujasiri wa kuchukua hatua haraka hivyo, kama pia ambavyo Waziri wake wa Mambo ya Ndani wa wakati huo, Clement George Kahama, hakuwa na ujasiri wa kuwatimua Waingereza katika nafasi za juu ndani ya Jeshi la Polisi.

Yakaanza malumbano ndani ya Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Tawala, Tanganyika African National Union (TANU), kwamba Nyerere alikuwa anairudisha Tanganyika katika enzi za Ukoloni, na hivyo kwamba “uhuru” haukuwa na maana kwa Watanganyika kwa kushindwa kwake kuwapa vyeo Waafrika.

Ili kuepusha shari, na ili Chama kisifarakane, Mwalimu akaachia ngazi Januari 16, 1962 na kurejea kijijini kuimarisha Chama kama Mwenyekiti wa Taifa wa TANU; na Rashid Kawawa akachukua Uwaziri Mkuu. Naye Oscar Kambona, ambaye wakati huo alikuwa Waziri wa Elimu, akawa Waziri wa Mambo ya Ndani badala ya George Kahama. Wote wawili hao wakaachiwa kazi ya kuwaondoa Wazungu katika vyeo walivyokuwa bado wanashikilia haraka bila visingizio.

Kazi ya kwanza ya Kambona ilikuwa ni kumtimua Kamishna wa Polisi Mwingereza, na kumteua Elangwa Shaidi kuchukua nafasi hiyo, lakini hakufanya mabadiliko kwa Jeshi (T. R.). Zoezi hili la “Africanisation” lilifanywa kwa kasi ya kutisha kiasi cha kuishitua jamii ya Kimataifa.

Desemba 1962, ulifanyika Uchaguzi Mkuu ambapo Mwalimu Nyerere alichaguliwa kuwa Rais Mtendaji wa kwanza. Kwa hiyo, Januari 1963, Mwalimu alirejea madarakani kama Rais wa kwanza wa Tanganyika na kusitisha mara moja zoezi la “Africanisation” na kuchochea hasira ya viongozi wa Vyama vya Wafanyakazi nchini, ambao waliapa kutolala usingizi, wala kuupa nafasi uamuzi wa Mwalimu wa kusisitiza zoezi la kuwapa madaraka Watanganyika.

Kwa wiki nzima baada ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwalimu alijishughulisha zaidi na mambo ya hali ya kisiasa nchini Zanzibar, ambapo Jumapili ya Januari 13, 1964; alikutana na Karume (aliyeondoka Zanzibar usiku saa chache kabla ya Mapinduzi kuanza), akamshauri arudi Zanzibar mara moja isije kutafsiriwa kwamba alikimbia mapinduzi kwa woga.

Siku hiyo ndiyo Okello alitangaza Serikali yake mpya, ambapo alijiteua kuwa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi na akamteua Karume Rais asiye Mtendaji; kisha akamwita arudi haraka kutoka popote alikokuwa (amejificha?) ili ashike nafasi yake.

Jumatatu, Januari 14, Kambona, wakati huo Waziri wa Mambo ya Nje na Ulinzi, akiwa Nairobi, alimpigia simu Nyerere kumtaarifu kwamba Kenya na Uganda tayari zilikuwa zimeitambua Serikali mpya ya mapinduzi Zanzibar na kumwomba naye aitambue. Nyerere alikataa akisema hakuwa na hakika kama kweli Karume alikuwa ameshika madaraka.

Jumanne, Januari 15; Mwalimu alikwenda Nairobi kukutana na Waziri Mkuu wa Kenya, Jomo Kenyatta, kuzungumzia Shirikisho la Afrika Mashariki, ambako alibaini kuwa Kenyatta na Milton Obote (Uganda) walikuwa wamefuta kabisa wazo hilo, baada ya kubaini kuwa shirikisho hilo lilikuwa mbinu za mkoloni kuzitia nchi hizo ndani ya kikapu kimoja ziweze kudhibitiwa kwa urahisi chini ya “uhuru wa bendera”.

Jumatano, Januari 16, Sultani wa Zanzibar, aliyetimuliwa na Okello Zanzibar, alitia nanga Dar s Salaam, baada ya kukataliwa kutia nanga wala kupewa hifadhi na Serikali ya Kenya. Mwalimu alimpokea na kumpa hifadhi hadi aweze kukamilisha mipango ya kukimbilia uhamishoni nchini Uingereza.

Alhamis, Januari 17, Mabwana Karume, Abdulrahman Babu na Kassim Hanga, walikutana na Mwalimu, Ikulu, kuelezea hali ya kisiasa ilivyokuwa Visiwani, na kuomba wapelekwe askari Dar es Salaam wa kutuliza Ghasia (FFU) ili kurejesha hali ya utulivu na amani. Siku hiyo, Okello akafuta uteuzi wa Karume, wa nafasi ya Rais, badala yake akampa Umakamu wa Rais kwa kile alichodai kuwa “hakushiriki hata kidogo katika mapambano wakati wa mapindizu” kasha akajiteua yeye mwenyewe kuwa Rais na Kiongozi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi, Zanzibar.

Ijumaa, Januari 18 na Jumamosi, Januari 19, zilikuwa tulivu kwa Mwalimu, ambapo Jumamosi hiyo, askari wa FFU 300 waliwasili Zanzibar kuitika ombi la Karume. Hata hivyo, kwa kupeleka askari hao 300, Mwalimu hakujua kwamba alikuwa anajipunguzia nguvu ya ulinzi wa nchi yake kwa siku ya maasi ambayo hakuitarajia.

Matata yalianza usiku wa Januari 20, kuamkia 21 usiku huo, siku ambayo Okello alikuwa na mazungumzo na Mwalimu, Ikulu usiku. Lakini ilipofika saa 7:50 alfajiri, Januari 21, Mkuu wa Kikosi cha kwanza cha TR, Brigedia Patrick Sholto Douglas, aliamshwa nyumbani kwake na sauti ya baruji (buggle) na ving’ora, karibu na kambi ya Jeshi ya Colito (sasa Lugalo Barracks).

Alipotoka nje, aliona askari wake 12 wakikamatwa na wenzao wenye silaha na kutiwa mahabusu. Ndipo alipofahamu kwamba, nusu ya askari 800 wa Kikosi hicho walikuwa wameasi. Aliweza kutoroka yeye na familia yake hadi katikati ya jiji, akaiacha familia kwa Balozi wa Australia, kisha akakakimbilia kwa Afisa mwenzake, eneo la Oyster Bay.

Akiwa huko, akampigia simu Oscar Kambona, akamwomba, naye akakubali, kupeleka ndege tatu Kikosi cha Pili huko Tabora, kuleta askari waliokuwa bado waaminifu kwa Serikali.

Douglas na Kambona hawakujua kwamba, tayari waasi walikuwa wamefunga barabara iendayo uwanja wa ndege; kwa hiyo, marubani walirudi mbio; naye Douglas akakimbilia kwenye Ubalozi wa Uingereza, akajificha kwa siku tano hadi Januari 25.

Douglas alikuwa amempigia simu Mkuu wa Polisi, ambaye alikwenda moja kwa moja nyumbani kwa Makamu wa Rais, Rashidi Kawawa, eneo la Ikulu na kumwamsha, kisha hao wawili kwa pamoja, wakaenda kumpa habari Mwalimu.

Mwalimu alipoelezwa juu ya maasi hayo, alilipuka kwa hasira na ghadhabu kubwa papo hapo; akataka kwenda yeye mwenyewe kukutana na Waasi hao ili wamweleze sababu za kitendo hicho cha aibu. Mama Maria Nyerere, kwa machozi na kwa kupiga magoti, alimsihi mumewe asitoke kwenda kukutana na watu wenye silaha, lakini hakufanikiwa kumgeuza nia.

Ndipo watu wa Usalama walipojenga hoja nzito kumzuia, na hoja hiyo ikamwingia; akakubali kuteremka dari ya chini, kisha yeye, Kawawa na Mama Maria Nyerere, wakatorokea mahali kusikojulikana. Wakati huo, tayari waasi walikuwa kwenye lango kuu la Ikulu wakimtafuta.

Bado ni kitendawili kuhusu mahali Mwalimu na wenzake walikokuwa wamejificha. Wapo wanaodai alijificha Misheni au Kanisani; wapo pia wanaosema alijificha kwenye nyumba ya Balozi mmojawapo Jijini.

Wengine wanasema alijificha kwenye kibanda kidogo sana (Kigamboni?) karibu na Pwani; na baadhi wanadai alikwenda Arusha au Nairobi. Lakini wapo pia wanaosema alijificha kwenye meli. Wala haielezwi kama John Okello aliondokaje Ikulu usiku huo baada ya mazungumzo au kama maasi yalimkuta Ikulu usiku huo.

Kufikia saa 9:00 alfajiri, waasi walikuwa wamekamata kambi ya Colito, kisha wakajigawa vikundi vitatu na kuingia mjini. Kikundi kimoja kilibakia kulinda kambi ya Colito, kikundi cha pili, kikiongozwa na Sajini Francis Higo Ilogi, ndicho kilichokwenda Ikulu kumtafuta Rais; wakati kikundi cha tatu kililinda barabara kuu zote mjini.

Kikundi cha Sajini Ilogi kilipofika Ikulu, kilishauriwa na mmoja wa Maafisa Usalama wa Taifa, wamwone kwanza Waziri wao wa Ulinzi, Oscar Kambona; nao wakakubali kufanya hivyo. Wakaenda hadi kwa Kambona na kumleta Ikulu, na kumweleza kwamba walikuwa wamewakamata na kuwaweka mahabusu maafisa wake (Wanajeshi) 16; na kwamba, kama (Kambona) alikuwa tayari kusikiliza malalamiko yao, afuatane nao hadi Colito. Kambona alikubali.

Ni ujasiri gani huo; ni kujiamini vipi kwa Kambona, kwamba bila ulinzi wala woga, tena akiwa amepanda gari la Mkuu wa Polisi tu, aliweza kukubali kuandamana na askari wenye silaha, na hasira kali, kwenda Colito Barracks?

Ukimwondoa Nyerere na Kawawa, ambao walikuwa na kila sababu ya kujificha, kulikuwa na Waziri wa Mambo ya Ndani, Job Malecela Lusinde; kwa nini Kambona hakumshirikisha, kama aliona mambo yalikuwa salama kiasi hicho? Hapo ndipo baadhi ya watu wanakwenda mbali zaidi kusema kwamba, huenda Kambona alihusika na maasi hayo.

Huko Colito Barracks, walimweka Kambona “kiti moto”, wakimtaka aamue papo hapo, pamoja na mambo mengine, kuondolewa mara moja kwa Maafisa wa Kiingereza Jeshini, na nafasi zao zishikwe na Wazalendo. Walitaka pia mishahara iongezwe, kutoka 105/= hadi 260/= kwa mwezi.

Bila kuonyesha kwamba ameyakubali au kuyakataa madai yao, Kambona aliomba wateue wawakilishi wachache ili wafuatane naye hadi Ikulu kwa mashauriano na Mwalimu Nyerere. Ndipo Kiongozi wa waasi, Francis Higo Ilogi, alipokataa na kusema, “Tunataka kila kitu leo hii”, Yowe zikasikika, “Apigwe risasi, apigwe” (Kambona) huyo!”.

Pengine kwa kuingiwa na hofu, kwamba lolote lingeweza kumtokea, Kambona akauliza: “Mnataka nani awaongoze?” Lilitajwa jina la Alex Nyirenda; lakini likakataliwa kwamba alikuwa na majivuno. Akatajwa Luteni Elisha Kavana, akapitishwa kwa kauli moja na kuvishwa kofia ya Brigedia Douglas.

Kambona alikataa kutia sahihi makubaliano, kwa madai kwamba mpaka ashauriane kwanza na Rais. Ndipo kikundi chote cha Ilogi kikafuatana naye kwenda Ikulu.

Walipofika huko, askari hao walijipanga barabara yote iingiayo Ikulu, lakini Sgt Ilogi aliwakataza wasiingie ndani, wakamruhusu Kambona pekee. Wakati huo Nyerere alikuwa ametoroka zaidi ya saa mbili zilizopita.

Baada ya mashauriano kwa muda na wasaidizi wa Rais pamoja na mama mzazi wa Mwalimu, Kambona alitoka nje na kuwatangazia waasi hao kuwa Rais ameyakubali madai yao. Lakini askari hao wakapiga kelele “mwongo huyo! Rais hayumo ndani; mpige risasi, mwongo huyo!”

Hata hivyo, waliondoka wameridhika, wakarejea kambini siku hiyo. Hima, Kambona aliwaondoa maafisa wa Kiingereza na kuwasafirisha kwao kupitia Nairobi.

Akiwatangazia wananchi kupitia Redio “Tanganyika Broadcasting Corporation” (TCB), Kambona alisema: “Huyu ni Waziri wenu wa Mambo ya Nje na Ulinzi; Serikali ingalipo… Kumekuwa na kutoelewana baina ya askari Waafrika na maafisa wa Kiingereza katika Jeshi. Baada ya kuingilia kati shauri hili, sasa askari wamerudi kambini”. Hata hivyo, hakusema lolote juu ya Nyerere, wala mahali alikokuwa.

Je, ni kweli mambo yalikuwa yamekwisha? Kwa nini Nyerere hakutokea hadi siku mbili baada ya askari kurejea kambini? Kwa nini askari hao waliasi tena siku nne baadaye na Nyerere kulazimika kuita majeshi ya Uingereza kuja kuzima maasi?


RAIA MWEMA

No comments: