Sunday, November 20, 2011

MADARAKA YA RAIS ASIYEAMBILIKA YANAZAA UDIKTETAMOJA ya mambo yanayolalamikiwa na baadhi ya wanaharakati wa demokrasia na utawala bora nchini, ya wanasiasa na wanasheria kuhusu Katiba ya 1977 inayotumika sasa, ni madaraka makubwa aliyopewa Rais chini ya Katiba hiyo, yanayoonekana kufifisha au kuuwa kabisa dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka (Separation of powers), kati ya mihimili mikuu ya nchi, ambayo ni Bunge, Utawala na Mahakama.

Hoja ya madaraka makubwa ya Rais imeanza kutema cheche pia kwa kadiri tunavyozidi kuelekea kwenye mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya, kwa kundi la wanaharakati nchini kupinga muswada wa Bunge wenye madhumuni ya kumpa Rais mamlaka ya kuteua tume itakayosimamia mchakato huo.

Je, ni kweli kwamba Rais amepewa madaraka makubwa chini ya Katiba ya sasa? Je, madaraka hayo yanashabihiana na zama hizi za siasa na uchumi huria, utawala bora, utawala wa sheria na haki za binadamu?

Kupata majibu ya maswali haya, hatuna budi kwanza kufahamu chimbuko la madaraka hayo kwa (Tanganyika) Tanzania huru.

Akiandikia gazeti la “The London Observer” mwaka 1963, mwaka mmoja tu tangu kuanzishwa kwa nafasi ya “Rais Mtendaji” nchini, Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, aliwahi kukiri jambo hili kwa kusema: “Katiba yetu inatofautiana na ile ya Amerika kwa sababu inamwezesha Rais kutenda kazi bila kuulizwa ulizwa [wala kuwajibishwa] mara kwa mara...Matakwa yetu si kudhibiti mwendo wa mabadiliko ya kijamii …Tunataka kiongeza mwendo (Rais) chenye nguvu kuweza kuvunja umasikini na vizuizi vilivyo ndani ya jamii…kusema kweli, Katiba (hii) inanifanya dikteta kwa kigezo chochote kile cha kidemokrasia”.

Katika zama hizi za demokrasia, utawala bora na utawala wa sheria, bila shaka Serikali imeanza kuliona hili kwamba Novemba 2007, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Ghasia, aliliambia Bunge kuwa, Serikali inaangalia uwezekano wa kumpunguzia kazi, madaraka na majukumu Rais “kwani, kazi na majukumu aliyonayo kusema kweli ni makubwa na magumu sana”.

Japo Waziri Ghasia hakutaja kazi na majukumu yanayolengwa kupunguzwa, lakini ni jambo lililo dhahiri kwamba, madaraka ya Rais ni ya Kikatiba, kwa hiyo ili hatua hiyo itekelezwe, itahitaji marekebisho ya Katiba na sasa ni wakati mwafaka tunapoelekea kwenye mchakato wa kuandika Katiba mpya.

Tanganyika (sasa Tanzania) ilipata uhuru wake Desemba 9, 1961 na kujiunga na Jumuiya ya Madola ili kuweza kurithishwa mfumo wa demokrasia na Serikali kwa mfumo aina ya “Westminster” wa Uingereza.

Katiba ya Uhuru (the Independence Constitution) ya 1961 ndiyo iliyoanzisha mfumo huo kuashiria tamati ya ukoloni mkongwe nchini kwa kuhamishia madaraka ya nchi na utawala kwa viongozi wazalendo.

Kama ilivyokuwa kwa nchi nyingine za kiafrika ambazo ni wanachama wa Jumuiya ya Madola, Katiba ya Tanganyika ilitolewa kwenye ofisi ya kikoloni, lakini tofauti na za nchi nyingine za Jumuiya hiyo, Katiba ya Tanganyika haikuwa na ibara inayozungumzia haki za binadamu (Bill of Rights). Inadhaniwa kuwa, kutowekwa kwa ibara hiyo ama kulikuwa na lengo la makusudi la wakoloni au ilisahauliwa kwa bahati mbaya.

Katiba hii kwa mfumo wa Westminster, ilitambua mihimili mitatu huru ya Serikali – Utawala, Bunge na Mahakama; au kwa lugha nyingine, “Mgawanyo wa Madaraka”.

Chini ya mfumo huo, Bunge lina ukuu juu ya Utawala (Rais na wasaidizi wake) kwa misingi ya dhana kwamba mawaziri wanawajibika kwa Bunge kwa uamuzi wao kama Baraza la Mawaziri na kwa waziri mmoja mmoja juu ya utendaji kazi wa wizara yake.

Kwa dhana ya demokrasia huru chini ya mfumo wa “Westminster”, mihimili ya Bunge na Mahakama huchukuliwa kama kidhibiti mwendo kwa matendo ya watawala.

Katiba ya Uhuru hata hivyo, haikuiachia Serikali ya wakati huo ilale usingizi au kwenda likizo. Miswada ya Serikali ilipita baada ya majadiliano marefu, makali na kwa uwazi, makini na bila ya woga wala vitisho miongoni mwa wabunge.

Waziri Mkuu na mawaziri wake waliwekwa kiti moto kwa majibu “rojorojo” bungeni, tofauti na siku hizi ambapo mawaziri wameota mapembe kiasi cha kuwakejeli au kuwafokea wabunge wanaowakilisha hoja za wananchi zenye ukakasi kwa Serikali.

Ilikuwa hivi: Novemba 23, 1962, Bunge la Katiba lilipitisha Sheria ya kuanzishwa kwa Katiba ya Tanganyika (the Constituent Assembly Act) Namba 1 (Cap. 499) iliyozaa “Katiba ya Jamhuri” (the Republic Constitution) ya 1962 na kuiweka nchi kwenye madaraka makubwa ya Rais asiyeambilika (imperial Presidency), na kuengua kabisa haki za kidemokrasia za wananchi kupitia Bunge lao.

Chini ya Katiba hii, Rais sasa alifanywa kuwa mkuu wa nchi na Mkuu wa Serikali. Rais ndiye alikuwa (na hadi sasa) Amiri Jeshi Mkuu na sehemu ya Bunge kwa sababu bila yeye kutia sahihi, muswada wa Bunge hauwezi kuwa Sheria.

Rais pia alipewa mamlaka ya kuteua mawaziri kutoka miongoni mwa wabunge na ni Mwenyekiti wa Baraza la Mawaziri. Inapokuwa kwamba mbunge ameteuliwa kuwa waziri, mara nyingi utii wake huhamia kwa Rais, hawezi kuihoji Serikali bungeni, badala yake kazi yake inakuwa kuitetea Serikali dhidi ya hoja za wabunge hata kama ni kwa jambo lenye adha na kero kubwa kwa wananchi wa Jimbo la Uchaguzi analowakilisha.

Kwa sababu hii, kitendo cha mbunge kuteuliwa kuwa waziri, kinawapokonya wananchi wa jimbo husika la uchaguzi uwakilishi wa kweli bungeni. Ni sawa na jimbo hilo kutokuwa na mwakilishi kwa sababu “mbunge – waziri” hawezi kutumikia mabwana wawili kwa wakati mmoja.

Uwajibikaji wa Baraza la Mawaziri na wa Waziri mmoja mmoja haukuwa tena kwa Bunge bali ulihamia kwa Rais asiyeambilika au kushaurika, ambaye kwa mujibu wa Ibara ya 3 (3) ya Katiba hiyo ya 1962, alipewa uwezo wa kuongoza nchi atakavyo; wala hakulazimika kusikiliza au kupokea ushauri wa mtu yeyote kuhusu masuala ya uongozi wa nchi.

Hii ilikuwa kinyume cha mfumo wa “Westminster”, unaotaka watawala kutekeleza majukumu yao kwa ushauri wa mawaziri.

Ingawa wakati wa kupitisha Katiba hii ilielezwa kuwa kuongezewa kwa madaraka ya Rais kusingeathiri kwa vyovyote vile wajibu na ukuu wa Bunge (Taarifa ya Serikali Na. 1 ya 1962), ukweli kilichofuata kilikuwa kinyume kabisa na ahadi hiyo, kwani Katiba hiyo ilimpa Rais uwezo wa kuvunja Bunge wakati wowote (Katiba ya Jamhuri, ibara 44 kifungu cha pili), uwezo ambao wakati wa Katiba ya Uhuru ulikuwa wa Gavana, ambao aliweza kuutumia tu kama Bunge lingepitisha kura ya kutokuwa na imani na Serikali, na kama Waziri Mkuu hakuweza kujiuzulu ndani ya siku tatu kuepusha shari (Katiba ya Uhuru, ibara 40 kifungu cha tatu).

Kama vile hiyo haikutosha juu ya kulimaliza nguvu Bunge, Katiba ya Jamhuri ililiondolea Bunge uwezo wa kupiga kura ya kutokuwa na imani na Serikali, wala kuhoji kama Rais ataamua “kuukalia” kwa muda mrefu muswada wa Sheria uliopitishwa na Bunge bila kuutia sahihi. Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya 1977 haina tofauti na Katiba ya Jamhuri ya 1962 kuhusu madaraka makubwa ya Rais.

Misingi ya Katiba ya 1977 inasimama juu ya mafiga matatu: figa la kwanza ni Rais mwenye imla, asiyeambilika wala kushaurika ikiwa ni masalia ya Katiba ya 1962; figa la pili ni Serikali mbili – Tanzania Bara na Zanzibar; tatu, ni utawala wa chama kimoja na siasa ya ujamaa na kujitegemea. Ingawa tumeingia mfumo wa vyama vingi, Katiba inanuka harufu ya chama kimoja kiasi cha watu wengine kukiita chama kilichoshinda “chama dola”, wakati dola si ya chama, bali ni ya wananchi.

Mhimili wa chama na ujamaa kati ya mitatu umekwishavunjika; sera za ujamaa na kujitegemea zimevunjwa na Azimio la Zanzibar mwaka 1992; nao mfumo wa chama kimoja umeuawa na mfumo wa vyama vingi vya siasa tangu mwaka 1992. Mfumo huu na ule wa uchumi huria, havikuwa katika mawazo ya watunga Katiba ya 1977. Ndiyo maana, Katiba ya sasa inakinzana kwa kiasi kikubwa na mengi yanayotokea nchini.

Tunachosema hapa ni kwamba, madaraka makubwa ya Rais asiyeambilika yalidumu na kuweza kufanya kazi tu kwa msaada wa mafiga mawili yaliyovunjika – (ujamaa na chama kimoja) na kwamba, maadam sasa msaada huo haupo tena, madaraka makubwa ya Rais yataendelea kuelea na kupwaya kwa vigezo vyovyote vya utawala wa sheria, demokrasia na utawala bora.

Tunaambiwa, nchi yetu inafuata mfumo wa Utawala wa “Westminster”, unaozingatia mgawanyo wa madaraka. Chini ya mfumo huo, muhimili mmoja wa Serikali unakatazwa kuingilia kazi za muhimili mwingine ili kwamba kila muhimili uchunge mwenendo wa muhimili mwingine. Dhana hii sasa ipo kwa jina tu kama tutakavyoona baadaye.

Marekebisho ya hapa na pale yaliyofanyika baadaye hayakugusa madaraka ya Rais, lakini badala yake, kadri sekta ya umma ilivyozidi kupanuka na ukuu wa mfumo wa chama kimoja kujiimarisha, ndivyo jinsi madaraka ya Rais yalivyozidi kuwa makubwa.

Aliweza kutumia nyundo ya chama wakati huo huo kama Rais wa nchi, na aliweza kutumia pia ngao ya Rais kama mwenyekiti wa chama. Rais wa nchi na mwenyekiti wa chama taifa kilikuwa kitu kimoja. Na ndivyo ilivyo leo kwa dhana potofu ya “chama dola”. Kwa sababu hii, madaraka ya Rais yalipanuka kinyemela kuanzia na Katiba ya nchi hadi kwenye Katiba ya chama tawala.

Kwa sababu hii, Rais asiyeambilika (the imperial presidency), anachukuliwa kama moja ya nguzo au misingi mikuu mitatu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 inayoendelea kutumika sasa.

Uhalali wa madaraka makubwa ya Rais, kwa mtazamo wa watawala wa enzi hizo, ulikuwa ni kuharakisha maendeleo kwa njia ya “udikteta” wa mkuu wa nchi ili asiulizwe ulizwe. Mtazamo huu unadumu hadi leo.

Na katika kutekeleza hilo, Katiba ilitungwa kwa lengo la kuweka madarakani mtawala mwenye nguvu za imla, kwanza kuonyesha kwamba Watanganyika sasa walikuwa huru kuweza kuendesha mambo yao wenyewe.

Pili, ilikuwa ni kuwezesha Serikali kuingilia kikamilifu (na bila ya kuhojiwa) katika maisha ya kijamii na kiuchumi ya wananchi ili kuharakisha maendeleo kwa imla ya kiutawala.

Maandalizi ya uchaguzi wa kwanza wa Rais asiyeambilika yalianza Juni 18, 1962 kwa kuandikisha wapiga kura 1,800,000 katika majimbo 50 ya uchaguzi.

Wagombea walikuwa wawili – Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Rais wa Chama cha TANU, na Zuberi Mtemvu, Rais wa Chama cha African National Congress – ANC.

Uchaguzi ulifanyika Novemba mosi, 1962 ambapo Mtemvu alishindwa vibaya kwa kupata kura 21,276 na Mwalimu Nyerere alipata kura 1,127,978.

Kuanzia hapo Katiba ya nchi imekuwa ikiandikwa au kurekebishwa kukiwa na uwepo wa Mwalimu Nyerere vichwani mwa waandishi wa Katiba. Hali haijabadilika. Katiba yetu (ibara ya 63) inamfanya Rais kuwa sehemu ya Bunge la nchi kama njia ya kudhibiti demokrasia, kinyume cha dhana ya mgawanyo wa madaraka.

Ingawa mamlaka yote ya kutunga sheria yamo mikononi mwa Bunge (ibara 64), lakini muswada wa sheria hauwezi kuwa sheria mpaka utiwe sahihi na Rais. Hakuna muda maalumu aliopewa kwa ajili hiyo. Hivyo anaweza kukalia muswada kwa muda wowote atakavyo, kana kwamba Rais yuko juu ya wananchi kupitia Bunge.

Endapo atakataa kutia sahihi muswada asioutaka, na Bunge likashikilia msimamo wake juu ya muswada huo, Rais ana uwezo wa kulivunja Bunge na kuitisha uchaguzi mpya.

Haya ni madaraka makubwa mno kwa Rais dhidi ya wawakilishi wa wananchi. Inamaanisha kwamba ingawa Bunge laweza kupitisha muswada wa sheria, ukweli Rais ndiye anayetunga sheria kwa sababu ana hiari ya kukataa muswada wa Bunge. Rais anapogeuka kuwa mtunga sheria, Bunge lifanye kazi gani?

Ili kulinda hadhi ya ukuu wa Bunge linalowasilisha wananchi, ni vyema Bunge likadhibiti bajeti yake, tume ya utumishi na uwezo wa kupitisha miswada kuwa sheria inapotiwa sahihi Spika ahusike badala ya Rais.

Kama ilivyokuwa kwenye Katiba ya Jamhuri (1962) kwa Rais kuongoza nchi atakavyo na kuwa halazimiki kupokea ushauri wa mtu yeyote; Katiba ya sasa (ibara 37) bado inampa ridhaa hiyo, na hawezi kuhojiwa au kushitakiwa kwa vitendo vyovyote alivyofanya akiwa Rais na baada ya hapo (Ibara 46).

Pengine ni kwa sababu hii kumekuwa na vitendo visivyoendana na maadili ya taifa kwenye Ikulu yetu bila ya woga, vilivyomfanya Baba wa Taifa apige kelele kwa kusema “Ikulu ni mahali patakatifu, panatakiwa paheshimiwe” na akaonya pia kwamba, pasigeuzwe pango la wafanyabiashara na walanguzi.

Rais ndiye anayeteua Jaji Mkuu na Majaji (wanaosimamia mhimili wa Mahakama), Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na viongozi wengine. Kitendo cha kuteua kinamaanisha kwamba wateule hao wanawajibika kwake. Na kwa sababu hiyo mhimili wa kulinda haki (Mahakama) unawajibika kwa Rais.

Hii inakwenda kinyume cha dhana nzima ya mgawanyo wa madaraka na ya utawala wa sheria kwa ujumla, kwa Rais kudhibiti Bunge na Mahakama na watendaji wake.

Ili dhana ya utawala bora ifanye kazi vizuri, kuna haja kwa Rais kupunguziwa madaraka haya, badala yake iundwe tume mahususi kushughulikia ajira na utendaji kazi wa watumishi wa ngazi za juu serikalini, na kwamba ajira hizo zithibitishwe na Bunge.

Rais ateue mawaziri kwa kushauriana na Waziri Mkuu na mawaziri hao wathibitishwe na Kamati ya Bunge inayohusika na maadili ya uongozi, itakayokuwa na mamlaka pia ya kuhoji.

Waziri atakayeteuliwa asiwe mbunge na kama tayari atakuwa mbunge, atakiwe kuchagua moja kati ya ubunge na uwaziri, kwa sababu hawezi kutumikia mabwana wawili, yaani mhimili wa utawala na mhimili wa Bunge.

Uwaziri sio zawadi, wala si nafasi ya kubahatisha au ya majaribio kwa kusubiri “semina elekezi” huko Ngurdoto, kufundishwa namna ya kuongoza. Uteuzi ufanyike kwa makini na kwa kuongozwa na sifa, uwezo na uzoefu wa mtu kwa nafasi ya uongozi anayoteuliwa.

Uhuru na demokrasia si lelemama, bali “uhuru”, kama alivyosema Baba wa Taifa, “ni kazi”.


RAIA MWEMA

No comments: