Thursday, November 10, 2011

KAULI YA MWENYEKITI WA CHADEMA JUU YA SAKATA LA MAANDAMANO ARUSHA
Mwenyekiti wa CHADEMA. Mh. Freeman Aikaeli Mbowe(MB)


Ndugu zangu waandishi wa habari, nitazungumza kwa kifupi sana mambo machache ambayo nafikiri ni ya msingi kwa mstakabali wa taifa hili. Nimepata taarifa kwamba Jeshi la Polisi linanitafuta na taarifa imetolewa jana na Kaimu Kamanda wa Polisi wa Arusha kwamba mimi nilikimbia katika mkesha ambao tuliutangaza katika Viwanja vya National Milling (NMC).

Upotoshaji wa Polisi

Huu ni upotoshaji wa makusudi wa Jeshi la Polisi kutoa taarifa za uongo. Sikukimbia Polisi, sikukimbia National Milling, wala sitakimbia wananchi pale tunapodai haki na madai hayo ya haki yakawa ya madai ya msingi.

Ni kweli polisi walipovamia eneo la tukio, binafsi sikuwepo kwa wakati ule. Na nilikuwa sipo katika eneo hilo kwa sababu ya ratiba zetu wenyewe za ndani za namna ya kupanga mikakati mingine ya kufanya na maandalizi mengine muhimu ambayo nilistahili kufanya na nisingeweza kufanya nikiwa katika eneo la tukio.

Lakini niliporejea katika eneo la tukio baada ya shughuli maalum niliyokwenda kufanya, ndiyo nikakuta purukurushani lile limeshaendelea na watu wameshakamatwa. Kw hiyo eti nimekimbia sijakimbia, na wala siwezi kukimbia, sijifichi na wala siwezi kujificha. Mimi ni kiongozi ninayejiamini, siwezi kukimbia polisi wala siwezi kuogopa magereza.

Tatizo la msingi la Arusha na mkakati wa ugandamizaji haki za wananchi

La pili ambalo ningependa Watanzania wanielewe ni kwamba, kumekuwa na mikakati ya muda mrefu ya sana ya kudhalilisha CHADEMA na hususan viongozi wake ili kupunguza imani ya wananchi kwa viongozi wa CHADEMA.

Na kumekuwa na propaganda kutaka kuonesha kuwa CHADEMA ni chama cha matatizo, ni chama kinachochochea vurugu na kwa misingi hiyo, vyombo vya dola vimekuwa vikitumika kuinyima haki CHADEMA, kunyima haki wabunge wa upinzani na kwa hiyo kuwanyima Watanzania wa kawaida haki.

Kumekuwa na double standards katika utoaji haki ndani ya taifa hili. Na kwa muda mrefu tumekuwa tukilalamika lakini serikali imekuwa kiziwi. Matatizo yote yanayotokea Arusha…na narudia…matatizo yote yanayotokea Arusha, chimbuko lake ni uchaguzi wa Meya uliofanyika Novemba mwaka jana. Mwaka jana mpaka leo ni mwaka mzima umepita lakini serikali imeshindwa kumaliza tatizo la dogo mno kwa sababu tu kutatua tatizo lile ni kukibana Chama Cha Mapinduzi.

Kwa maana yake tumekuwa tuna-deal na matokeo ya kosa la msingi, lakini kosa (lenyewe) la misngi halitatuliwi. Serikali inakuwa bubu. Inaachia uongozi wa Mkoa wa Arusha na vyombo vya dola viendelee kuibana CHADEMA, viendelee kuiumiza Chadema, ili kuharibu reputation ya CHADEMA.

Tumelalamika mpaka, nimezungumza na Waziri Mkuu Pinda na Waziri Mkuu akamweleza Msjaili wa Vyama vya Siasa aunde timu ya pande zote mbili, kwa CHADEMA na Chama Cha Mapinduzi, tukae kwenye meza tuzungumze wote.

Tume imeundwa…aaah, Msajili wa Vyama vya Siasa, akaviandikia vyama, CHADEMA tumepeleka majina ya wajumbe wa tume hiyo , Chama Cha Mapinduzi hatujui mpaka leo kama wamepeleka. Mpaka leo hakuna mazungumzo yaliyofanyika, hakuna kikao kilichokaa, hatujui taarifa yoyote, wala hatujapewa taarifa yoyote.

Hivyo tunaona huu ni mkakati wa msingi kabisa wa kunyima haki kwa wananchi wa Arusha.

Sasa ndugu zangu mimi juzi katika Uwanja wa Arusha, nilitangaza kabisa kwamba tumechoka kufanya siasaza kudhalilisha, tumechoka kufanya siasa za kupuuzwa, mimi kama Mbunge, mimi kama Mwenyekiti, mimi kama Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, naweza kuzungumza na Waziri Mkuu jambo, tukaweka misingi watu wakazungumze, wenzetu hawataki kuzungumza, wanaendelea kuvunja sheria, wanaendelea kubebwa na polisi, wanaendelea kubebwa na vyombo vya usalama.

Hali hii ya kufanya siasa za namna hii za upinzani tumechoka nazo, kwa sababu tumeona hazina tija kwa wananchi na wala hazitaweza kuleta mabadiliko ya kweli katika taifa hili.

Sasa katika resistance za kisiasa kuna kitu kinaitwa Civil disobedience, civil disobedience ni pale ambapo wanaharakati wanalazimika kuchukua hatua na wakijua kuwa zina madhara yanayoweza kupatikana kutokana na hatua hizo ili kufikisha ujumbe kwa wahusika.

Kwa kweli tumedhalilishwa kiasi kikubwa mno, tunaendelea kudhalilishwa na tutaendelea kudhalilishwa kwa sababu wamedhamiria kufanya hivyo.

Na Mkuu wa Mkoa mpya, aliyeletwa Arusha huyu bwana anaitwa Magesa, ameletwa hapa kwa minajili hiyo. Na Magesa anatoa vitisho kwa kauli za kuwatisha watu na wanaharakati wasidai haki zao za misngi.

Mkuu wa Mkoa Magesa ni mwajiri wa serikali, lakini anakuja Arusha, Magesa anajipa mamalka ya kutaka kutisha kila mtu na kwamba yeye ni mkuu wa mkoa, who is mkuu wa mkoakatika mazingira ambayo amepewa kazi na mtu mmoja na Rais Kikwete.

Kwamba yeye anaweza kuja hapa, akatoa maagizo kwamba eti ni Kamati ya Ulinzi na Usalama imekaa na kuamua hatukai mchezo na Arusha! Anaijua vipi Arusha, amechaguliwa kwa kura ngapi Arusha, Magesa huyu…anamtisha nani Magesa!

Bunduki na mabomu si suluhisho bali mazungumzo kwa ajili ya haki.

Sasa viongozi kama hawa ambao wanapewa mamlaka makubwa, bila ridhaa ya wananchi ni rahisi sana kuwa wanatoa kauli zenye utata ambazo zinaweza zikaifanya hali ya Arusha ikawa tete, hali ya Arusha narudia tena, haitatuliwa kwa vitisho vya mkuu wa mkoa, hazitatuliwa kwa mahakama kuingiliwa na serikali. Itatuliwa kwa watu kukaa mezani na kuzungumza tatizo la misngi. Kuzungumza chimbuko la tatizo na kumaliza tatizo katika njia za kistaarabu na kiungwana.

Hili ndilo jambo linaweza kuhakikisha sustaibale peace, amani ya kudumu katika nchi yetu. Na CHADEMA tunalitaka hili.

Pamoja na na yote hayo, mimi nilikuja kumshawishi mbunge (Godbless Lema) atoke magerezakwa sababu niliamini kama Kiongozi wa Upinzani Bungeni, nilitaka wabunge wangu waende bungeni Dodoma wkafanye kazi. Tayari alishapeleka ujumbe, alistahili kwenda Dodoma akaendeleze kazi ya uwakilishi wa wananchi.

Katika kazi ile, polisi walitupatia ushirikiano mzuri, nao wakimtaka atoke magereza na tulielewa dhamana ilikuwa iko wazi.

Ile dhamana haikuwahi kufungwa. Lakini maamuzi yaliyofanyika ambayo tunaamini ni kwa shinikizo la Mkuu wa Mkoa, mahakama ilikataa kutoa removal order, wakisingizia kuwa hawakuvunja sheria yoyote. Tunaamini katika sheria, tunaheshimu sheria, lakini tunaamini zaidi katika busara, yaani wisdom katika kufanya maamuzi ya kiuongozi.

Nilichukua hatua ile si kwa sababu ya ishara ya uoga. Nilichukua hatua ile kwa sababu ya jambo moja la msingi, kwamba tuisaidie Arusha. Arusha iwe na amani. Maneno haya nimezungumza na Waziri Mkuu, maneno haya nimeazungumza na mawaziri kadhaa, maneno hayo nimezungumza na IGP Mwema. Kwamba tusiendeleze ubabe Arusha, tusi-politicize matatizo ya msingi ya Arusha.

Mahakamani-NMC

Mahakama imekataa…fine mahakama imekataa…wananchi walikuwa wanamsubiri mbunge wao, Polisi walikuwa na mabomu, polisi walikuwa na bunduki, mahakama ilikuwa na mahakama na ina mamlaka ya kisheria, wananchi wamejaa pale mahali (getini), walishindwa kuwaondoa wale wananchi.

Wameshindwa kuwaondoa wala wananchi, pale…pale…pale, pale mahakamani, nimekuja pale mimi, nimekuta polisi na vifaa vyao vipo, mahakama ipo, majaji wako ndani, watumisihi wa mahakama wako ndani, mahakimu wako ndani, wananchi wameziba geti wanataka mbunge wao.

Katika mazingira yale, polisi wnaniomba mimi niwasaidie kutawanya watu. Nashangaa kwa ninihawakutumia bunduki ambazo wanazo nyingi na mabomu ambayo wanayo mengi kuwatawanya watu hawa. Lakini mimi niliona si vyema Watanzania tukavuruga utamaduni wa kazi zetu za mahakama.

Kwa hiyo nilikuwa na courage na confidence ya kuweza kusimama kuwaambia vijana, wale wanachama walokuwa wanamtaka mbunge wao atoke kwamba nitakwenda kutoa ujumbe wa maamuzi ya mahakama katika Viwanja vya National Milling (NMC).

Katika mazingira hayo, hakukuwa na njia yoyote ungeweza ukawaondoa wale wananchi pale bila kuondoka kwa kutembea nao. Sasa mimi nikatembea nao kuwapeleka katika eneo la mkutano na tukazungumze katika mkutano ule uliokuwa na maelfu ya wananchi. Hakuumizwa pake, hakuumizwa panya.

Sasa tunaambiwa viongozi wa CHADEMA, wakiwemo wabunge, akiwemo Mwenyekiti, akiwemo Katibu Mkuu, wameandamana bila vibali, sasa unajiuliza haw watu wana busara gani! Tumeandamana wao kwa sababu walishindwa kuwaondoa wananchi wale na wakaniomba niwasaidie kuwaondoa wananchi wale. Sasa busara zangu zinakanipeleka kuwa hawa watu lazima niwaondoe kwa miguu katika maeneo hayo.

Badala ya kunipongeza na kunishukuru, wanalalamika kuwa nimevunja sheria, huu…huu mimi naweza kuuita ni wendawazimu.

Nakwenda polisi, daima nitakuwa mstari wa mbele

Sasa mimi nakwenda polisi. Nakwenda polisi mimi na ningependa kuwahikishia polisi, napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu, siogopi polisi, siogopi magereza, simwogopi mtu yeyote, naogopa kweli na ninamwogopa Mungu.

Nitafanya maamuzi magumu. Nitafanya maamuzi magumu ndani ya mahahakama hii leo, kwa sababu kuna tabia inajengeka kufikiri sisi ni waoga. Kwamba sisi tunawadanganya wananchi waingie katika mtego, lakini viongozi tunakimbia.

Ndiyo sura ambayo polisi wanajaribu kuionesha for a long time kuwa Mbowe amekimbia, Mbowe ametoroka, tutamkamata. Nikimbie niende wapi, mimi mwakilishi wa watu, sikupewa kazi na Kikwete na sitegemei kupewa kazi na kiongozi yeyote katika nchi hii.

Nitapewa kazi na wananchi watakapoona ninafaa kupewa nafasi Fulani.
Mimi kama Kiongozi Mkuu wa chama hiki, siwezi kuwa mstari wa nyuma. Nitakuwa mstari wa mbele katika kila hatua, bila woga wala bila ajizi, kutetea haki ya nchi hii. Oppression katia nchi hii imezidi.

Ukandamizaji katika nchi hii umezidi. Unyanyasaji katika nchi hii umezidi. Na nilisema pale uwanjani siku ile kuwa Chama Cha Mapinduzi kinaringa kwa sababu kina polisi, kina ringa kwa sababu kina Usalama wa Taifa, hakijali kuwa hakina nguvu ya umma , SISI TUNA NGUVU YA UMMA.

Kwa hiyo mimi napenda kumalizia kwa kuwaambia ndugu zangu wana habari kwamba, nakwenda mahakamani…nakwenda polisi, wana…sijui mimi wananitafutia nini. Na hawa polisi wanasema wananitafuta Mbowe, mimi Mbowe nina simu, simu yangu iko on, iko hii, iko on simu yangu, sijafunga hata wakati mmoja. Hajanipigia polisi. Mimi nina maofisi kila mahali, nina ofisi ya mkoa hapa Arusha, tuna ofisi ya wilaya. Hakuna mtu aliyetutafuta, hakuna…

Waseme kiongozi gani mmoja wa chama ameambiwa akamtafute Mbowe Mwenyekiti, aje aripoti polisi! Press conference ya polisi imefanyika mchana saa nane kwenda saa tisa na ndiyo waka-release kwamba wanamtafuta Mbowe. Lakini hawajanipigia simu. Juzi wakati wana matatiozo ya polisi, ya mahakama, walinitafuta kwenye simu, lakini jana hawanitafuti, wanasubiri, wanasema Mbowe hapatikani, amejificha. Najificha kwa sababu ya nani!

Sasa mimi nawaambia nakwenda polisi mwenyewe, si kwa sababu ya eti naogopa, eti nakwenda kujisalimisha, nijisalimishe kwani naogopa nini. Nimetoroka wapi, kwa sababu hata tukio lenyewe walipokuwa wanakamata watu sikuwepo mimi uwanjani. Lakini wengine wanasema Mbowe alikuwepo, ametoroka na gari lake, akakimbia. Mimi Mbowe nikimbie! Hivi wanamjua Mbowe, wanamsikia Mbowe?

Sasa ndugu zangu mimi nakwenda mahakamani, maamuzi magumu yatafanyika. Nawatakia heri sana Watanzania katika kudai haki za nchi hii.

Asanteni sana.

No comments: