Wednesday, November 16, 2011

KAMISHNA CHAGONJA AMEPATA WAPI MAMLAKA YA KUSITISHA MAANDAMANO?Elias Msuya


HIVI karibuni jeshi la Polisi nchini limepiga marufuku maandamano ya Chadema na CCM yaliyokuwa yafanyike nchi nzima na Dar es Salaam, baada ya kugundua kuwapo mwelekeo wa uvunjifu wa amani.

Wakati ya Chadema yalikuwa yamepangwa kufanyika nchi nzima kupinga walichokiita uonevu dhidi ya viongozi wao kitaifa, ya CCM yalikuwa yafanyike Dar es Salaam pekee kulaani ilichokiita hatua ya Chadema kudharau mamlaka ya Mahakama nchini.

Wanajeshi wa J.KT na J.W.T.Z wakiwapiga wafanyabiashara ndogondogo wa Mwanjelwa waliokuwa wakiandamana kudai haki yao mkoani mbeya hivi karibuni

Kamishna wa Operesheni na Mafunzo wa Polisi,Paul Chagonja, alisema kuwa wamezuia mikutano na maandamano hayo ya Chadema kwa kuwa taarifa za kiintelijensia walizopata zimebaini kuwa mbali na kuvunja amani, pia Polisi haina taarifa ya shughuli hizo.

Marufuku ya Chagonja imekuja ikiwa ni siku chache tangu Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kupiga marufuku maandamano ya wanaharakati waliotaka kuandamana kupinga malipo ya Dowans, akidai kuwapo kwa tishio la mashambulizi ya Al-Shabaab.

Matukio haya yanatoa picha halisi ya hofu ya serikali dhidi ya nguvu ya wananchi na vyama vya siasa. Hofu hiyo ilidhihirishwa na kauli ya Waziri Mkuu Pinda, bungeni hivi karibuni, pale alipokuwa akitoa maelezo ya tukio la Arusha.

Askari wa kikosi cha kutuliza ghasia wakimnyanyasa kijinsia mwanafunzi wa CHUO KIKUU DAR ES SALAAM. Kwa kupitisha mikono sehemu za siri na kumshika makalio wakati wanafunzi hao walipokuwa wakitoa malalamiko yao kuhusu nyongeza ya mikopo


Hofu hii inakuja ikiwa ni miaka 19 tangu Tanzania iruhusu mfumo wa vyama vingi. Ni kama vile mfumo wa vyama vingi uliruhusiwa tu kwa shingo upande.
Baada ya kuridhia mfumo huo, serikali ilipitisha sheria ya vyama vingi Na. 5 ya mwaka 1992. Sheria hiyo ndiyo inayotoa haki na wajibu wa vyama vya siasa nchini, ambao leo serikali inaupiga marufuku.

Kwa mfano katika sehemu ya pili ya sheria hiyo Ibara ya 4 (1) (a), inasema, Kila chama cha siasa kitakuwa na haki ya kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano kwa mujibu wa sheria ya Vyama vya Siasa.
Pamoja na haki hiyo, sheria hiyo inavipa wajibu vyama katika Ibara ya 5 (1) (e), Kufanya mikutano ya kisiasa na maandamano bila vurugu kwa mujibu wa sheria ya nchi”.
Sheria hizi zinakwenda sambamba na Katiba ya Jamhuri ya Muungano; ibara ya 8 (1) (a) inatoa madaraka kwa wananchi,
Wananchi ndio msingi wa mamlaka yote na serikali itapata madaraka na mamlaka yake yote kutoka kwa wananchi kwa mujibu wa Katiba hii.

Ibara ya 18 (a) inasema, Kila mtu anao uhuru wa kuwa na maoni na kueleza fikra zake.
Ibara ya 20 (1) inasema, Kila mtu anao uhuru wa kukutana na watu wengine kwa hiari yake na kwa amani, kuchanganyika, kushirikiana na watu wengine na kwa ajili hiyo kutoa mawazo yake hadharani na kuanzisha na kujiunga na vyama au mashirika yaliyoanzishwa kwa madhumuni ya kuhifadhi au kuendeleza imani au maslahi yake au maslahi mengineyo.

Hivyo ndivyo Katiba na Sheria ya Vyama vya siasa zinavyosema. Sasa Kamishna Chagonja amepata wapi mamlaka ya kusitisha maandamano nchi nzima?
Hivi Watanzania sasa tunaongozwa kijeshi kiasi ambacho hatutakiwi kusema chochote kilicho kinyume na serikali, hadi tupate ruhusa ya polisi?
Hata kama Chagonja alitumwa na Rais kutangaza hivyo, ajue kuwa huyo rais na viongozi wengine wamewekwa madarakani na wananchi wenyewe.

Sasa kuwazuia wananchi kutoa maoni yao kwa njia ya maandamano ni kukiuka haki za raia, ni uporaji wa mamlaka ya wananchi kikatiba. Jeshi la Polisi halitakiwi kuingilia haki za wananchi, bali linatakiwa kuwalinda ili watekeleze haki zao.
Kisingizio cha uvunjifu wa amani hakina mashiko kwasababu jeshi hilo ndilo linalopaswa kuepusha uvunjifu wa amani ili wananchi waandamane, wakutane na watoe maoni yao kikamilifu kwa mujibuwa Katiba.
Nadhani sasa jeshi la polisi linapaswa kuchukua uzoefu kwa nchi nyingine kama ilivyokuwa Misri. Mapema mwaka huu wananchi wa nchi hiyo walianza maandamano nchi nzima.

Awali jeshi la polisi nchini humo lilianza kukabiliana nao. Lakini baada ya kugundua wajibu wao, wakawaacha.
Baada ya miezi kadhaa, wananchi wakaungana na kukusanyika katika uwanja Tahrir mjini Cairo wakishinikiza aliyekuwa rais wao, Hosni Mubarak ajiuzulu na ndivyo ilivyokuwa.
Sina maana kwamba sasa Watanzania tuandamane ili tuung’oe utawala uliopo madarakani, ila ninasema kuwa wananchi wapewe nafasi ya kueleza hisia zao kama Katiba inavyosema.

Wananchi ndiyo wenye mamlaka ya mwisho kwa serikali yao. Wakiamua kuandamana kupitia vyama vyao, mashirika yao au vikundi vyao, waachwe tu, ndiyo haki yao Kikatiba.
Jeshi la Polisi halina mamlaka kisheria ya kusitisha maandamano ya wananchi. Huo ni ubabe na kupora madaraka ya wananchi kwa serikali yao.


MWANANCHI

No comments: