Monday, November 14, 2011

JUKWAA LA KATIBA LAWATEGA WABUNGE
Raymond Kaminyoge


JUKWAA la Katiba Tanzania, limetangaza kufanya maandamano nchi nzima ikiwa wabunge watapitisha Muswada wa Sheria ya Katiba wa mwaka 2011.Muswada huo unaotarajiwa kuwasilishwa bungeni leo kwa mara ya pili, umepingwa vikali na makundi ya kijamii ambayo yanataka uwasilishwe kwa mara ya kwanza.

Tayari muswada huo umeibua mvutano kati ya baadhi ya wabunge na Serikali, baada ya wawakilishi hao kutaka usomwe kwa mara ya kwanza.Jana Jukwaa la Katiba lilizidi kuongeza shinikizo likisema endapo muswada huo utawasilishwa kwa mara ya kwanza, utatoa fursa kwa wananchi kutoa maoni yao katika muswada huo tofauti na ukisomwa kwa mara ya pili.

Akihitimisha kongamano la kujadili Muswada wa Katiba Mpya lililofanyika Dar es Salaam jana, Mwenyekiti wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Deus Kibamba alisema: “Tumewaomba wabunge wasiupitishe muswada huu kwa mara ya pili kwa kuwa wananchi hawajatoa maoni yao, wakiupitisha tutatafuta nguvu ya umma.”

Alisema maandamano ya kudai Katiba yatakayoandaliwa, hakuna chombo chochote cha ulinzi kitakachoweza kuyazuia kwa sababu wananchi watakuwa wanadai haki yao.“Katiba Mpya itakayopatikana kwa mtindo huo wa ubabaishaji itaendelea kulalamikiwa na wananchi kama inavyolalamikiwa ile ya mwaka 1977,” alisema Kibamba.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta), Hezron Kaaya alisema wabunge wakiupitisha muswada huo, Tucta itaupinga kwa nguvu zote.“Msidhani Tucta tuko kimya, muswada huu hauelezi nafasi ya mfanyakazi katika nchi hii, tupewe muda tutoe maoni yetu vinginevyo tutaupinga,” alisema.

Alisema kwa kawaida viongozi hawawezi kuipenda Katiba Mpya wakati ya zamani ndiyo yenye manufaa kwao... “Tutawashangaa wabunge kama watapitisha muswada huu, ni lazima wasome alama za nyakati wananchi wamebadilika wanafahamu haki zao.”

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Josephat Kanywanyi alisema Katiba ni mali ya wananchi wanyonge. Alisema muswada huo unatakiwa kusomwa kwa mara ya kwanza ili wananchi waweze kutoa maoni yao.

Alisema ukiwasilishwa bungeni kwa mara ya pili, watakaoujadili watakuwa wabunge pekee yao na si wananchi.
Alisema muswada huo una upungufu mkubwa ukiwamo Rais kupewa madaraka makubwa ambayo ni kama kuteua Tume ya Katiba, Kuunda Bunge la Katiba na kutoa hadidu za rejea.

“Haya ni madaraka makubwa mno kwa Rais ambayo yanahitaji marekebisho kwa makundi mbalimbali ya kijamii kutoa maoni yao,” alisema Profesa Kanywanyi.

Mwakilishi wa Shirikisho la Vyama vya Walemavu Tanzania (Shivyawata), Maria Chale alisema muswada huo umewatenga walemavu: “Kwani watu wenye ulemavu siyo Watanzania? Iweje mtutenge, tutaelewaje kilichoandikwa wakati hakijawekwa katika lugha ya wasioona?”

Mjumbe wa Jukwaa la Katiba Tanzania, Christina Kamili alisema muswada huo umechapishwa katika Gazeti la Serikali Oktoba 14, mwaka huu... “Huu ni muda mfupi kwa wananchi kuweza kufahamu kilichopo, wabunge wawawakilishe wananchi katika suala hili, watapata heshima kubwa.”

Mwanaharakati, Renatus Mkinga alisema suala la muswada wa Katiba lisifanywe siri kama viongozi wanavyofanya kwenye mikataba ya madini.
“ Viongozi hawa wa ajabu sana... kila jambo wanadhani ni siri, hii siyo mikataba ya madini, Katiba ni mali ya wananchi waachieni waitolee maoni,” alisema Mkinga.

Alisema wabunge wafahamu kuwa wanapocheza na Katiba ambayo ni mali ya wananchi wanacheza na nguvu ya umma.“Huwezi kuwadanganya Watanzania wa sasa, wanafahamu kuwa viongozi wetu hawana nia ya dhati ya kuwapatia Katiba Mpya,” alisema.

Mwenyekiti wa Tadea, John Chipaka alitofautiana na washiriki wengine kwa kuhoji ni lini Jukwaa la Katiba Tanzania lilipeleka maoni yake kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala.

“Tusije tukawa tunazungumza hapa na mambo yanaishia hapa ni lini mlipeleka maoni yenu kwenye kamati?” alihoji Chipaka.Kauli hiyo kinzani ya mwanasiasa huyo wa siku nyingi ilisababisha mzozo na jazba miongoni mwa washiriki wa kongamano hilo waliompinga kabla hata hajamaliza kutoa maoni yake.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Ananilea Nkya alisema Katiba mpya ni lango wananchi kuingilia katika maisha yenye matumaini.


MWANANCHI

No comments: