Wednesday, November 2, 2011

HADITHI HADITHI: KISA CHA MAJUHA WAWILI WANAWAKE

KISA CHA MAJUHA WAWILI WANAWAKE

Paukwaaaaa………………..Pakawa

Kaondokea chenjegaa

Kajenga nyumba kakaa

Mwanangu mwana Siti

Kijino kama chikichi

Cha kujengea Kikuta

Na vilango vya kupita

Hapo zamani palikuwa na maskini katika mji mmoja, akaoa mke, akazaa naye mtoto mmoja mwanamke. Alikuwa na ng’ombe mmoja jike ndiyo rasilimali yake. Na kazi yake ni kulima makonde huko nje ya mji. Na kila siku wakati wa kuingia mjini huchukua mzigo wa majani ya ukoka ili chakula cha ng’ombe wake. Bibi na motto hubaki nyumbani.

Hata siku moja alipokuwa Yule mtoto ametimia miaka saba umri wake, aliota ndoto usiku. Na ndoto yake ilikuwa ameota kaolewa, tena kazaa mototo mwanamke mzuri sana. Asubuhi, baba yake akaamka akaenda kondeni kwake. Mtoto mwanamke alipoamka akaangua kilio akalia, Mama wee! Mama wee! Mtoto wangu yuko wapi? Hata mama mtu akasikia kilio, akaenda chumbani akamwuliza, Je, mwanangu walilia nini asubuhi yote hii? Mtoto akamwambia mama yake ya kuwa nimeota ndoto usiku mmenioza mume, kisha nikazaa mtoto mwanamke mzuri, sasa naamka simwoni, ndiyo maana nalia, umemchukua wewe mama? Akisema hivi huku analia. Mama mtu aliposikia habari ya mtoto aliyezaliwa usiku, na kumwona mwanawe analia, nay eye akaangua kilio akalia. Ikawa kelele moja kwa moja. Hata majirani mtaani wakasikia vilio wakaja nao kusikiliza kuna nini? Mama mtu akawaeleza watu mambo yote ya ndoto. Majirani wakacheka sana, wakanena, Haya mambo! . Hatujapata kuona sisi watu kulia kwa sababu ya ndoto. Lakini wale wenyewe wamekazana kulia.

Jirani mmoja mzee alipoona hawa ni wapumbavu, na kelele zinazidi, akataka kuwanyamazisha. Akaenda akamwambia Yule mama, Bibi hapana maana kukaa kitako ukilia, kama mtoto aliyezaliwa usiku amekufa, iliyobaki ni kuweka matanga na kuondoa. Lakini aliyekufa kwa kuwa ni mtoto mdogo, fanyeni chakula tu mpate kuondoa msiba. Yule mke wa maskini akasema, Hayo ni mashauri mazuri, lakini nitafanyaje na mume wangu hayupo, naye ndiye mwenye mashauri ya mapesa. Yule jirani akamwambia , Huna hata kikuku ukachinja? Akasema, Nyumbani hamna kitu ila ng’ombe wa bwana, naye ampenda sana. Akaambiwa, Utafanyaje basi, na wewe una sharti ya kuondoa msiba huu. Usipoondoa itakuwa uchimvi, utakufa wewe, au mume wako. Yule mwanamke aliposikia vile akafanyiza hofu, akaona afadhali nimchinje huyu ng’ombe maana sina kitu kingine. Akawaita watu akawaagiza wamchinje ng’ombe.

Watu wakachekelea sana, wakajua leo ndiyo kufaidi. Wakamchukua ng’ombe wakamchinja, wakamchuna upesi upesi. Wakatwaa mguu wakaenda wakabadili kwa mchele, wakatwaa nyama nyingine wakabadili mwa vitakataka vingine vya kupikia. Mara upishi ukasiamama, ukapikwa wali hata ikipata saa saba chakula tayari. Akaitwa mwalimu kuja kusoma khitma. Watu wengi wakaja kula chakula . Ikawa tena kila aliyesikia akaja, na wote waliokuwa wakija wakapata chakula. Hata habari ikaenea mji mzima kwa maskini kuna khitma, na wakisifu chakula kuwa kingi. Wakati huu wote, mume yuko shamba analima. Lakini habari za khitma nyumbani kwa maskini, kasikia kwa watu waliokuwa wakitoka mjini kwenda shamba, lakini hakutiamoyoni maana hali ya nyumbani kwake aijua mwenyewe. Akakaa hata saa zake za desturi akang’oa ukoka wake, akashika safari taratibu kwenda zake mjini. Wakati huu kule nyumbani kwake watu wamekwisha ondoka. Maskini akafika nyumbani kwake mkewe akamlaki juu kwa juu, karibu, bwana , karibu. Yule maskini kimya akaongoza njia moja kwa moja mpaka zizini, akatua mzigo wake, akafungua mzigo wake. Aingie ndani ya zizi ng’ombe hayumo! Akashangaa, Ng’ombe wangu yuko wapi? Mara mkewe akaja, akamwambia, Mume wangu, twende ndani nikakupe habari za mkasa ulionipata, nikueleze ng’ombe wako yuko wapi?. Yule maskini akasema siendi popote mpaka nimwone ng’ombe wangu kwanza. Mkewe akamwambia, Bwana, twende ndani nikakueleze, akanena, Nieleze papa hapa. Yule mkewe tena akaona hana budi kumweleza mambo yaliyopita. Akamweleza yote. Maskini aliposikia kuwa ng’ombe wake amechinjwa kwa ajili ya ndoto, akaduwaa, asijue la kutenda. Akaingia ndani akakaa kimya. Mkewe akamletea chakula asiweze kula.

Hata usiku Yule maskini akamwambia mkewe, waama tangu kuzaliwa sijapata kuona Juha kama wewe. Ilikwendaje wewe kusikiliza maneno ya ndoto, hata ukamchinja ng’ombe wangu kwa habari ya ndoto? Basi sasa nifanyizie mikate nataka nisafiri, niende mbali nikatafute mtu mwingine aliye Juha kama wewe. Nikimwona utakuwa mke wangu vivi hivi. La, sikumwona, nitakuacha. Asubuhi mkewe akamtengenezea mikate akafunga , akachukua na karatasi na bahasha na wino. Akaondoka akaenda zake msitu na nyika hata zikatimia siku saba, hata siku ya saba akafika katika mji mmoja mkubwa. Na yeye kwa kuwa alikuwa na mashauri yake moyoni, hakuingia mjini, akafikia katika kibanda cha kizee mmoja mwanamke. Yule mwanamke hakukasiri akamkaribisha, akamfanyizia chakula. Yule mgeni akauliza sana habari za mjini, na habari za wakubwa wa mji. Kizee mwanamke akamwambia, Je ! utakwenda mjini leo, au utalala hapa leo? Akanena, Ningependa nilale hapa, asubuhi niingie mjini. Yule kizee akamwambia, karibu, mwanangu, ipo nafasi tele hapa. Akapewa chumba cha pili katika kile kibanda chake. Yule mgeni akafurahi sana. Alipoingia chumbani, akafunga mlango wake. Akatoa karatasi zake, akakaa kitako akaandika barua zake, moja kwa Sultani, moja kwa Binti Sultani, moja kwa Waziri, moja kwa mke wa Waziri. Akazifunga katika bahasha, kila barua bahasha ya peke yake. Asubuhi akamwuliza Yule kizee nyumba za watu hawa aliowaandikia barua ziko wapi.. Yule kizee akanena, Nyumba za watu hawa wote ziko pwani forodhani, ila nyumba ya binti Sultani iko nje ya mji, si mbali kwa kutokea hapa. Akauliza namna ilivyokaa, na alama zake. Akaambiwa zote. Basi alipokwisha kupata habari zote alizotaka, akaaga, akasema, Kwa heri mama, sina budi kwenda mapema nikamwahi kila mtu nyumbani mwake niwape barua zao. Akaondoka akaenda akashika njia akaingia mjini. Akafika panapo ile nyumba ya Binti Sultani. Akataza,a huko na huko akaona tanuu imeelekea penye dirisha la Binti Sultani. Akachimba chini ya ile chokaa. Akangoja mpaka alipoona sasa ni saa tatu akajifukia pale penye chokaa. Kisha akaaza kuitutumua ile chokaa kwa kichwa chake, na huku anapiga kelele. Eee jamaa! Nifaeni mwenzenu, nisaidieni, natoka mbali mimi, shime jamaa. Mara akachungulia mtumishi dirishani, akaona chokaa inatutumka, na kichwa cha mtu kinatokeza. Akaenda akamwita bibi yake. Akamwambia Bibi, tazama chini, kitu gani kile? Akichungulia chini aona mtu anatokeza penye chokaa, na huku apiga kelele. Mara Binti Sultani akamwita mtumishi mwanamume, akamwambia, Uledi, nenda upesi ukamtazame mtu Yule ana nini? Mara Uledi akaend, akamwuliza, Nani wewe? Shetani au binadamu? Yule mgeni akasema, mimi ni mtu, lakini natoka ahera nimetumwa kuja kuleta barua za watu wa hapa mjini. Je! Sasa mimi niko wapi hapa? Yule Uledi akamwambia, Hii nyumba inayokukabili ni nyumba ya Binti Sultani. Yule mtu wa ahera akasema, Oh! Vema sana, maana ninayo barua yake hapa. Uledi akamshika mkono akatoka katika ile chokaa, akampeleka uani, akapewa maji akakoga, akapewa na chakula. Na wakati wa kula akistaajabu, Hivyo ndiyo chakula cha ulimwenguni siku hizi? Afanya kukisahau maana yeye atoka ahera. Alipokwisha wakampeleka juu kwa Bibi. Kufika tu Yule mtu akamwamkia bibi, akatoa barua akampa. Akamwambia, Barua yako hii yatoka ahera kwa mjomba wako, naye akusalimu sana pamoja na bwana.

Binti Sultani akafungua barua akasoma, nayo imeandikwa hivi:- Salaam mjomba, mimi huku ahera sijambo, na jamaa wote waliopo wazima ila mimi nina dhiki ya deni, nalikopa fedha za watu name sina cha kuwalipa. Basi tafadhali mpe huyu mtu niliyemtuma rupia elfeen aniletee nilipe deni za watu. Salaam. Wakatabahu. Mjomba wako. Yule binti Sultani aliposoma ile barua akasikitika sana, akaenda zake moja kwa moja mpaka chumbani akafungua bweta akatoa rupia elfeen ndani ya mifuko miwili. Akaenda kwenye sanduku la nguo akatoa kanzu ya hudhurungi safi, na kanzu ya meli meli iliyo safi, na kanzu ya doria iliyo safi. Akatoa na buraa Muskati moja, na kitambi cha debwani iliyo njema, na kofia nyeupe ya kazi nzuri. Akatwaa na vitu vingine vidogo vidogo kama miski, na haluudi. Akatafuta kileso kikubwa cha Hariri akafunga pamoja vitu hivi vyote. Kisha akaandika barua kwa mjomba wake wa ahera, akaandika hivi : Salaam mjomba, waama baada ya salaam barua yako imewasili. Nami nimefurajhi kuniletea huyu mtu wa kunipasha habari ya kuwa wewe mzima. Na vitu ulivyoagiza nimempa huyu mtu, nimempa fedha rupia elfeen, na nguo maana nasikia nguo adimu huko, Salaam. Mimi Binti Sultani. Akampa bahasha Yule mtu wa ahera, na barua hii, akamwambia, Mchukulie mjomba, mwambie bwana hukumkuta, ungepewa zaidi ya hivi.

Binti Sultani akamwambia, Je! Nikupe mtu akuchukulie mzigo? Yule maskini akenena, Itanilazimu kuchukua mwenyewe, maana ahera haendi mtu ila aliyekufa. Basi kwa heri, Bibi sina budi kwenda upesi maana jua linapanda, na sisi watu wa ahera jua linatudhuru. Yule mgeni alipotoka nje, akaona hana haja ya kuzidi kwenda mbele kupeleka barua zile nyingine . Akatazama huko na huko akaona mahali pana njia inapita vichakani, akachagua njia hii, akashika njia kwenda zake. Njiani akapita akisema kimoyomoyo, Ah! Kumbe majuha wapo wengi, nikadhani mke wangu tu! Kumbe hata katika watu wakubwa wamo majuha! Akaenda zake upesi upesi, akaviisha vile vichaka, akatokea katika mashamba. Alikuwa anakwenda hivi upesi upesi kwa kuwa alishuku kuwa anafuatwa. Alipofika mle mashambani akamkuta mzee mmoja analima. Akamwambia, Ee baba umepata habari za mjini leo? Yule baba akasema, La, sina habari. Akamwambia, kumezidi nini? Yule mtu wa ahera akanena, Imetoka amri kwa sultani, wafuatwe vizee vya shamba wote wauawe ili mhanga wa nyumba mpya ya Sultani inayojengwa. Basi mimi kwa hisani yangu napenda uvae hii kanzu yangu, na mimi unipe nguo zako za kulimia na jembe lako nilimie. Na wewe panda juu ya mnazi huu utazame njia ya mjini utaona mtu anakuja.

Sasa turudi kwa Binti Sultani. Baada ya kuondoka huyu mtu wa ahera, mara bwana mume wa Binti Sultani akarudi nyumbani. Akamkuta mkewe ana majonzi, Akamwuliza, Je! Bibi, una nini? Yule Bibi asijibu neno akatwaa ile barua akampa mumewe akaisoma. Alipokwisha soma, akamwuliza mkewe jinsi yalivyokwenda mambo haya. Mkewe akaeleza yote, jinsi alivyokuja mtu wa ahera akaleta barua hii, nay a kuwa amempa mjomba wake wa ahera haja aliyotaka, na zawadi nyingine. Yule mume akakasirika sana, akamwuliza mkewe, Wewe una wazimu? Sasa niambie huyu kaendea njia gani? Akamwambia, kapitia ile ya vichakani. Mara akaagiza atandikwe farasi, akavaa nguo zake joho na kilemba na upanga mkononi, akapanda farasi ili kumfuata huyu mwizi mkubwa. Lakini akamwambia mkewe, Fahamu mimi namfuata huyu mtu, maneno yake yakinielea, vema, utakuwa mke wangu, lakini ukiwa ni upuzi wako na wazimu, nitakuacha.

Akatoka akaenda zake shoti. Basi alipokuwa akienda mbio, Yule mtu wa shamba aliyepandishwa juu ya mnazi, akasema, Naona kivumbi kinatoka mjini, mtu anakuja mbio. Yule mjumbe wa ahera akasema, Je! Sikukuambia miye? Mara Yule mpanda farasi akafika pale, akamkuta Yule hasimu wake analima. Akamdhani huyu ni baba ya shamba tu. Akamwuliza, Hukumwona mtu anapita hapa na bahasha? Akamjibu, Sikumwona, bwana. Lakini tazama huko juu mnazini, kuna mtu; huyo ndiye aliyekuja kutoka huko mjini, alipofika hapa akapanda juu ya mnazi; nilipomwuliza akasema anaogopa. Basi sijui kama ndiye unayemtafuta. Yule bwana akamwuliza Yule mtu kuwa ajua kupanda mnazi. Yule akasema, La, bwana sijui. Yule Mwarabu akawa ameshikwa na uchungu, ataka kumwua Yule mtu aliye juu ya mnazi. Basi akabua nguo zake, kanzu na joho na kilemba na jamvia akampa Yule mgeni wa ahera amshikie pamoja na farasi, yeye akapanda juu ya mnazi. Alipokuwa akipanda akawa anasema, Utanitambua leo mwizi mkuu wee, leo kutoka yangu au yako. Na Yule aliye juu naye akaona maneno ya Yule mgeni wa ahera kuwa ya kweli. Akadhani huyu anakuja kuniua kwa habari ya amri iliyotoka. Basin aye akamwambia, Haya njoo name nikuonyeshe kazi kama sikukupiga kwa mundu wangu. Yule Mwarabu akawa anapanda tu, wala hatazami chini. Yule mjumbe wa ahera kule chini akatwaa bahasha yake akafunga juu ya farasi. Akatwaa na zile nguo za Mwarabu akazifunga juu ya farasi. Akatwaa na zile nguo za Mwarabu akazifunga juu ya farasi, kasha akampanda. Huyoooo! Akaenda zake. Yule mkulima aliye juu ya mnazi akamwambia Mwarabu, Ela tazama chini yuko wapi farasi wako? Akatehemu, kwenda juu hawezi, kushuka chini hawezi. Halafu akaona hana hila ila kushuka apate hakika ya maneno haya. Akamwambia Yule baba, Shuka chini tupate kuulizana vema. Yule kizee akakataa kushuka mpaka Mwarabu alipomwapia kuwa hatamwua. Basi wakashuka wote. Walipofika Mwarabu akamwambia, Nipe habari ya Yule habithi. Mkulima akampa habari zote tangu mwanzo, alivyokuja na alivyosema, kumtisha kwa mari ya mfalme iliyoko mjini. Hata ikajiri kubadilishana nguo nay eye kupanda juu ya mnazi hata kutokea yeye Mwarabu. Yule Mwarabu aliposikia kisa hiki mahali pa kukasirika akacheka sana. Na Yule mkulima akamwambia Mwarabu, Ela na mimi nieleze ilivyokwenda huko mjini. Mwarabu akamweleza habari zote za barua ya ahera, na vitu alivyopewa! Wote wawili wakakauka kwa vicheko.

Yule mkulima akamwuliza Mwarabu, Sasa ukienda nyumbani utakwenda semaje? Yule Mwarabu akasema, Sina la kusema ila nitakwenda kumwambia Bibi kama nimemkuta Yule mtu, name niliposikia habari za ahera moyo wangu ukaingia huzuni sana hata sikuweza kustahimili nikampa farasi wangu na nguo zangu zote awachukulie watu wa ahera. Je! Waonaje kizee? Kizee akasema , kweli maneno yako . Maana ukisema umenyang’anywa utachekwa sana.

Mwarabu akarudi mjini na kikoi chake chini na jambia lake mkononi. Kisha akafika kwa mkewe. Mkewe akamwuliza, Jinsi gani Bwana? Nguo zako na farasi vi wapi? Akamwambia, Kweli maneno yako, Bibi. Habari za ahera nilizozisikia kwa Yule mjumbe wa ahera zimenitia huzuni sana, hata nimempa farasi na vitu vyangu vyote kuongezea vile ulivyompa wewe. Basi sasa Bibi na tukae. Lakini pamoja na hayo akija mtu mwingine kutoka ahera usimpe kitu mpaka unishauri.

Sasa tumrejee Yule mjumbe wa ahera. Baada ya kupata farasi akamwendesha shoti akaenda mwendo wa siku chache kuliko alivyokuja maana sasa kapanda farasi. Akafika hata kwa mkewe, amechoka kwa mbio. Akamfungua farasi mzigo wake akamweka katika lile zizi la ng’ombe wake . Na mzigo akautia ndani. Alipokwisha pumzika na kula chakula, akamweleza mkewe mambo yote ya safari yake. Akamwonyesha na fedha. Akanena, Sasa na tukae kitako mke wangu, nimekwisha mwona aliye Juha kuliko wewe. Lakini pamoja na hayo ukitokea tena upuzi wa ndoto wajibu uningoje unieleze tufanye shauri pamoja wakakaa raha mustarehe.

No comments: