Tuesday, November 8, 2011

DPP 'LEGELEGE' KIKWAZO CHA UTAWALA BORA
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

NIMEDOKEZA katika makala mbili za awali kuwa ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini ni ofisi ambayo ina umuhimu wa kipekee katika kusimamia sheria.

Nilielezea kuwa ni miongoni mwa ofisi za Kikatiba ambazo Rais hana uchaguzi nazo na wala hakuna mtu mwingine anayeweza kuziingilia utendaji wake. Nilienda mbali na kudai kuwa hakuna mamlaka nyingine yoyote inayoweza kuingilia utendaji kazi wa ofisi hiyo kwa mujibu wa Katiba Ibara ya 59B.

Pamoja na yote mazuri ambayo nimeyasema kuhusu madaraka na mamlaka ya ofisi hii, ukweli mwingine ambao nataka niuangalie ni kuwa ofisi hii inakabiliwa na changamoto kubwa ambazo zinaifanya kushindwa kwa kiwango kikubwa kutimiza majukumu yake ya Kikatiba.

Ni muhimu kuelewa kuwa kama zilivyo ofisi nyingine za Kikatiba ofisi hii ina uzito mkubwa sana katika suala zima la usimamiaji wa sheria na utii wa sheria.

Labda kuweza kulielewa hili zaidi nina uhakika hadi hivi sasa mpendwa msomaji utakuwa umeelewa zaidi ofisi ya DPP, nitumie jambo moja ambalo wengi mtakuwa mmeliona likisemwa kwenye vyombo vyetu vya habari. Hili ni suala la “utii wa sheria bila shurti”.

Yaani, kuna kampeni inayoendeshwa ya kuwafanya watu waone umuhimu wa kutii sheria bila kushurutishwa. Nadharia hii ni nzuri lakini ni mojawapo ya nadharia potofu kabisa ambazo inahitaji kukataliwa.

Mwanadamu kwa asili yake si mtii wa mamlaka. Tumeumbwa kuwa huru na kuishi kama watu huru. Lakini mazingira na watu katika maisha yetu wamekuwa wakiweka vikwazo mbalimbali aidha, kwa ajili ya kutulinda au kwa ajili ya kuwalinda wengine tusiwadhuru.

Hivyo, mtoto atajikuta anawekewa mahali pa kuchezea, ataambiwa muda wa kurudi nyumbani, atawekewa vikwazo mbalimbali. Baadaye mtoto huyo akijua kusudio jema la wazazi ataanza kutii yeye mwenyewe bila kulazimishwa.

Lakini anafanya hivyo kwa sababu anatambua kuwa ile mipaka ambayo imewekwa katika maisha yake inamtaka aitii kama anataka aishi kwa amani yeye mwenyewe na wenzake.

Lakini si watoto wote hukua wakaendelea kuheshimu mipaka ile. Wengine wakishafika balehe huanza kuasi na kuwa kinyume na mipaka yote inayowekwa kwa sababu – wameumbwa kuwa huru. Watataka kutumia uhuru wao na juhudi zozote za kuwalazimisha kutii zitakutana na pingamizi kubwa sana na wakati mwingine huishia katika madhara kwa mtoto – ya kimwili na hata kimaadili.

Katika nchi ya kidemokrasia hata hivyo utii wa sheria hauji kwa hiari. Unakuja kwa wananchi kutambua kuwa hakuna uchaguzi mwingine bali kutii sheria na kwamba wasipotii sheria basi wao wanaweza kujikuta katika matatizo bila kujali majina yao, vyeo vyao, nafasi zao, au hadhi zao katika jamii. Wazo hili la kwamba utii wa sheria ni wa lazima na kwamba kila mtu analazimishwa kuitii sheria hiyo ndio kitu kinachoitwa “utawala wa sheria”

Sasa, katika nchi kama ya kwetu ambayo imeweka vyombo mbalimbali vya kuhakikisha utii wa sheria ndipo tunapokutana na ofisi ya DPP. Kama nilivyoonesha mwanzoni kuwa ofisi hii imewekwa kwa ajili ya kuhakikisha kuwa maslahi ya umma yanazingatiwa katika mambo yote yanayofanywa.

Yaani, sheria inatakiwa kutumika kuilinda jamii (umma) na ndio maana ofisi hii inaitwa ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya/wa Umma. Hata hivyo, kwa bahati mbaya sana (naweza kusema kwa makusudi) ofisi hii haijapewa heshima na hadhi inayostahili kinyume cha lengo la Ibara ya 59B ya Katiba yetu.

Ofisi hii si huru

Kinyume cha matakwa ya Katiba kuwa ofisi ya DPP inatakiwa iwe huru kwa mtindo uliopo sasa ofisi hii bado haijawa huru inavyostahili na kwa bahati mbaya sana watu ambao wangepigania uhuru wake wanaonekana hawana muda wa kufanya hivyo.

Ofisi hii iko chini ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Na kwa kadiri ninavyoelewa hadi hivi sasa mwajiri katika ofisi hii ni Naibu Mwanasheria Mkuu ambaye pia ndiye Mhasibu Mkuu (kwamba Naibu Mwanasheria Mkuu ni sawa na Katibu Mkuu wa Wizara).

Hii ina maana ya kwamba ajira katika ofisi ya DPP zinasimamiwa na AAG. Siyo tu ajira hata bajeti inasimamiwa na AAG. Sasa kama ni hivi tunaweza vipi kuoanisha hilo na kile ambacho Katiba inasema kuwa chapaswa kuwa yaani uhuru wa DPP chini ya Ibara ya 59B(4)? Ni wazi kwamba kama DPP hawezi hata kupanga bajeti ya ofisi yake, je, anaweza kweli kuwa huru kutimiza wajibu wake wa Kikatiba?

Lakini kukosekana kwa uhuru huu kunaenda mbele zaidi. Kutoka na vyanzo vyangu mbalimbali ni kuwa DPP hana ofisi zake anazomiliki, karibu katika kanda zote DPP anapangisha. Hili ni lazima litushitue kidogo wale tunaopenda “utawala wa sheria”. Ofisi ya TAKUKURU inapatiwa fedha kuliko ofisi ya DPP!

Lakini ni ofisi ya DPP inayoamua kesi zote, zipi ziendelee na zipi zisiendelee na inaweza kutupilia mbali kazi yote ya uchunguzi iliyofanywa na TAKUKURU. Sasa nani ambaye yuko juu ya mwenzake hapo? Ni wazi ni DPP.

TAKUKURU hata hivyo ina ofisi zake! Leo hii tunaona majengo ya Jeshi la Polisi yakipambwa vizuri na kufunguliwa kila mahali lakini polisi na uchunguzi wao wote mwishowe kesi zao zinategemea huruma ya DPP.

Lakini DPP huyo huyo hana ofisi hata moja – niko tayari kusahihishwa. Yaani, DPP anapangisha wakati vyombo vingi vilivyo chini yake vinatengewa bajeti za kujenga majumba na vitendea kazi lukuki wakati wao ma-DPP wakiendelea kusota.

Hapa mtu anaweza hata kuwaonea huruma wale Polisi walioamua kuingia ofisi ya DPP badala ya kuendelea na upolisi wao wakiamini kuwa wanaitwa kutumikia nchi yao kwa namna nyingine, lakini sasa hivi wanajikuta wanasota tu.

Je, tunaweza kweli kuona sheria zinasimamiwa vilivyo bila ofisi ya DPP kupewa uwezo na nafasi yake inayostahili? Tunaweza vipi kulilia ofisi za TAKUKURU zipewe majengo mapya na ofisi za kisasa lakini DPP aendelee kupanga halafu tufikiria kuwa yuko huru?

Iweje TAKUKURU ambayo siyo ofisi ya Kikatiba iwe inapewa upendeleo huo wakati ofisi ya DPP ionekane kama kipandikizi kwenye ofisi ya Mwanasheria Mkuu?

Je umefika wakati kweli – kama nilivyoonesha wiki iliyopita – wa kuondoa ofisi ya DPP na kuiweka huru kabisa na AG ili isimamie maslahi ya umma? Je, kuiondoa ofisi hii mikononi mwa AGC kutasababisha ofisi hii ianze kupewa heshima na hadhi inayostahili?

Binafsi ninaamini kuna namna moja tu ya kufanya ofisi ya DPP iheshimike na watu wajue uzito wake na hili lote linamtegemea Eliezer Feleshi – DPP wa sasa.

Kama nilivyosema katika makala ya awali Bw. Feleshi anasimama kushtakiwa kwa sababu licha ya kujua madaraka makubwa aliyonayo, amekubali kuwekwa nyuma na kufanywa asiye na nafasi. Si mpiganaji wa kupigania uhuru wa ofisi yake hata kwa kujiuzulu.

Anaweza vipi kuendelea kuonekana – yeye na walio chini yake – kama watumishi tu wa ofisi nyingine wakati Katiba imewapa na kuwahakikishia uhuru mkubwa?

Inawezekana vipi aendelee kuwa chini ya AAG na watumishi wake wawe hivyo hivyo na bado akajiita ni DPP chini ya Ibara ya 59B? Ninaamini ameshindwa kupigania nafasi na maslahi ya ofisi yake na matokeo yake ameijengea msingi mbaya sana ofisi hii.

Hata hivyo akipenda anaweza kujiokoa na kuacha jina lake katika historia. Hii itatokea endapo ataweza kuhakikisha kuwa ofisi yake inakuwa na jengo lake nje ya AG na zaidi kuacha kupanga kama ilivyo sasa hapo Sukari House.

Inashangaza hata ofisi za Kanda za Dar-es-Salaam nao wanapanga na hakuna watu wenye kupigania ofisi hii ipatiwe fedha za kujenga ofisi zake – Makao Mkuu na zile za kanda? Jibu la kuwa “hatuna fedha” ni jibu la kuwavutia watoto!

Hivi majuzi tu tumeambiwa kuwa Serikali yetu imenunua jengo la karibu dola milioni 25 huko Marekani (New York) kwa ajili ya shughuli zake za kibalozi – na labda kupangisha vile vile. Je kiasi hicho kingeweza kutosha majengo mangapi hapa Tanzania kwa ajili ya DPP?

Kama yale majumba ya Benki Kuu yalitumia karibu dola milioni tatu ni wazi kuwa kiasi hicho cha dola kingeweza kufanya maajabu nchini. Lakini nani anafikiria hilo? Nina uhakika mkubwa tu ikitolewa hoja ya kujenga Makao Makuu ya DPP na ofisi za Kanda jibu litakalokuja ni kuwa “serikali haina pesa”.

DPP afanye nini?

Kama hatojiuzulu kwa kushindwa kazi yake kama nilivyoanisha makala za nyuma, Feleshi na walio chini yake wana wajibu mmoja tu wa kufanya ili waheshimike.

Waoneshe kuwa wao wana madaraka ya kusimamia sheria za nchi hii na wafanye hivyo pasipo hofu, woga, upendeleo wala ubaguzi wa aina yoyote ile. Watanzania wengi hawajui nafasi yao na hivyo ni vigumu hata watu kuwapigania.

Na ni vigumu zaidi kupata watu wanaowaunga mkono hasa kama wanaonekana kufanya kazi kama waoga na wasio na weledi au wasiojua majukumu yao.

Nje ya hapo, Watanzania tupiganie uje uongozi mwingine kutoka chama kingine ambao utaweza kutumia rasilimali zetu na uwezo wetu kuweza kujenga na kuitumia ofisi ya DPP vizuri ili kuhakikisha kuwa utawala wa sheria siyo tu unakuwa ni kitu cha kunuiwa bali unaonekana kweli kweli.

Kwani hadi hivi sasa sioni kama kuna mbunge yeyote ambaye anaweza kuona umuhimu wa kuipatia nakuiwezesha ofisi hii ili kweli iwe ni ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Umma.RAIA MWEMA

No comments: