Tuesday, November 15, 2011

CHADEMA, NCCR MAGEUZI WACHAFUA HALI YA HEWA BUNGENIWATOKA NJE KUSUSIA MUSWADA WA MABADILIKO KATIBA, SPIKA ASEMA MUSWADA UNAPOTOSHWA


Neville Meena, Dodoma na Raymond Kaminyoge, Dar

WABUNGE wa Chadema na NCCR-Mageuzi jana walilitikisa Bunge baada ya kuungana kutoka nje ya ukumbi kupinga kile walichodai kuwa ni Spika wa Bunge, Anne Makinda kuwadharau kwa kuwanyima haki zao kwa mujibu wa kanuni.Wakati wabunge hao wakitoka bungeni kugomea muswada huo, Chama cha Majaji Wastaafu Tanzania (Tarja), kimetoa tamko kupinga hadidu za rejea za tume itakayoratibu mchakato wa kuundwa kwa Katiba Mpya kutolewa na Rais.

Licha ya Spika Makinda kuukingia kifua muswada huo katika utangulizi wake kabla ya kuruhusu uwasilishaji wa hoja kwa pande zote akisema ulifuata kanuni za Bunge, haikusaidia kwani muda mfupi baada ya Waziri Kivuli wa Katiba na Sheria, Tundu Lissu kutoa maoni ya Kambi ya Upinzani, wabunge hao waliamua kuondoka.

Muswada huo wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011, ambao uliwasilishwa na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani umepata pia upinzani kutoka kwa wanaharakati nchini ambao wametishia kufanya maandamano nchi nzima endapo wabunge watauridhia.

Tamko la Mbowe
Baadaye wabunge hao wa Chadema na NCCR Mageuzi katika tamko lililotolewa na Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe walisema: “Hatutashiriki katika mchakato wote wa mjadala wa muswada huu hadi mwisho na kesho (leo) tutaeleza hatua nyingine tutakazochukua.”

Mbowe katika mkutano na waandishi wa habari uliohudhuriwa na Wabunge wa NCCR Mageuzi, David Kafulila (Kigoma Kusini) na Felix Mkosamali (Muhambwe) alisema wamelazimika kutoka nje kutokana na Spika Makinda kuonyesha upendeleo wa wazi kwa Serikali kabla ya hata muswada huo kuwasilishwa.

“Spika ameonyesha upendeleo wa wazi kabisa kwa Serikali hata kabla ya muswada huo kusomwa na waziri, katika hali hiyo haki haiwezi kutendekeza. Hatuwezi kuunga mkono kitu ambacho kinapingwa na wananchi kote nchini,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Shughuli nyingine za mkutano huu wa Bunge zilizobaki tutashiriki lakini hili la kujadili muswada huu hatuko tayari na lazima tupange utaratibu wa kuwafikishia wananchi.”

Alisema upendeleo wa Spika pia ulijitokeza wakati wabunge zaidi ya watatu wa upinzani walipoomba mwongozo na yeye kukataa wakati kanuni zinawaruhusu kufanya hivyo.

“Spika anasema eti sisi tunawapotezea muda. Kuomba mwongozo si kupoteza muda, kanuni zinaturuhusu, kwa hili ametutusi lazima atuheshimu na afahamu kwamba hata sisi tumechaguliwa na wananchi,” alisema Mbowe.
Wabunge waliokataliwa na Spika walipoomba mwongozo ni Mkosamali, John Shibuda wa Maswa Magharibi (Chadema) na John Mnyika (Chadema).

Hata hivyo, wabunge wengine wawili wa NCCR Mageuzi, Mosses Machali (Kasulu Mjini) na Agripina Buyogela (Kasulu Vijijini) hawakuhudhuria kikao hicho na badala yake walibaki ndani ya ukumbi wa Bunge.

Ilikuwaje?

Hali ilianza kubadilika wakati Waziri Kombani alipomaliza kuwasilisha muswada huo, kwani Mnyika alisimama na kusema: “Hoja kuahirisha mjadala,” lakini Spika alimpuuza na kumwita Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Pindi Chana kutoa maoni ya kamati yake.

Wakati huo, Mkosamali alisimama kuomba mwongozo wa Spika lakini pia alikataliwa na Spika akisema huo haukuwa wakati mwafaka wa kuomba mwongozo kwani muda ulikuwa hauruhusu.

Chana alipomaliza kusoma maoni ya kamati, Shibuda naye alisimama kuomba kuhusu utaratibu lakini Spika hakumpa fursa hiyo, hivyo kumwita Lissu ili atoe maoni ya Kambi ya Upinzani.

Baadaye Mnyika alisimama tena baada ya Lissu kuwasilisha maoni ya upinzani, lakini Spika alikataa kumpa nafasi, ndipo wabunge wa Chadema walipoinuka kutoka kwenye viti na kutoka nje.

Wakati wabunge hao wakitoka, Mkosamali alisimama akisema: “Kuhusu utaratibu,” lakini Spika alisema hakukuwa na nafasi ya kufanya hivyo na badala yake alimpa nafasi Mbunge wa Same Mashariki, Anne Kilango Malecela (CCM) kuanza kuchangia muswada huo.

Maoni ya Upinzani
Mapema akisoma maoni ya Kambi ya Upinzani kuhusu muswada huo, Lissu alimtuhumu Spika kwamba alikuwa akiingilia Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala kinyume cha Kanuni za Bunge.

“Spika umekuwa ukiingilia sana kamati kinyume cha kanuni za Bunge na zaidi ya hapo ulikataa ziara za kamati kwenda mikoani kukusanya maoni ya wananchi kuhusu muswada huu, hali hii haikubaliki,”alisema Lissu kauli ambayo aliirudia katika mkutano na waandishi wa habari.

Lissu alisema Spika pia alikiuka Kanuni za Bunge kwa kuongeza wajumbe watano kwenye Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala na kwamba kwa kufanya hivyo anaufanya mchakato wa sasa kuwa batili.

Alisema muswada huo ni batili kwani Serikali haikutekeleza agizo hata moja lililotolewa na Bunge kwani hata tafsiri ya muswada huo kwa Kiswahili iliwasilishwa mbele ya kamati wiki mbili zilizopita na kwamba wananchi hawakupata nafasi ya kuijadili.

“Muswada huu ni mpya, tofauti sana na ule ulioletwa hapa Aprili, hivyo kutokana na mabadiliko makubwa na kimsingi yaliyofanywa, ni dhahiri kwamba usomwe kwa mara ya kwanza ili wananchi wapate fursa ya kuujadili tena,” alisema Lissu.
Alisema mchakato wa katiba mpya unafanya makosa yaleyale ya kuendeleza mamlaka makubwa ya urais na kwamba hali hiyo inaiweka Katiba Mpya katika mikono ya Rais jambo ambali siyo sahihi.

“Kutokana na kasoro hii, ni dhahiri kwamba tutapata katiba ambayo inakidhi matakwa ya Rais, chama chake cha CCM na siyo katiba ya Watanzania, hatari ya uraisi wa kifalme kuendelea inaonekana pia hapa,” alisema Lissu.Maoni hayo pia kwa kiasi kikubwa yalichambua kasoro za ushirikishwaji wa Tanzania Visiwani katika mchakato huo na kwamba ili kuwa na msingi bora lazima kuwe na meza ya majadiliano ya kurejeshwa kwa Serikali ya Tanganyika.

Kafulila na Mkosamali
Wakizungumza kwenye mkutano wa wabunge wa Chadema, Kafulila alisema tangu mwazo hakukuwa na dhamira njema ya Spika kwani alionyesha upendeleo wa wazi kwa kuisemea Serikali.

“Kwa jambo la kitaifa kama hili, si sahihi kwa Spika kuonyesha upendeleo wa wazi, sasa kwa msimamo wangu sikuona kwa nini niendelee kukaa ndani hali kukiwa na ushahidi wa wazi kwamba demokrasia inakandamizwa,” alisema Kafulila na kuongeza:

“Nikiwa kwenye kamati, mambo mengi yalikuwa yakifanywa ndivyo sivyo, suala la madaraka makubwa ya Rais wenzetu hawako tayari kabisa kulifanyia kazi, sasa hali hii si ya kuvumilika hata kidogo, lazima tutetee maslahi ya nchi.”

Makinda na Kombani
Mapema akiwasilisha muswada huo, Waziri Kombani alichukua muda mrefu kueleza sababu za Serikali kuamua kusoma muswada huo mara ya pili, akiwajibu wanaharakati, wanazuoni na wanasheria waliokuwa wakitoa mwito kwamba usomwe kwa mara ya kwanza kutokana na kufanyiwa marekebisho mengi.

Mapema kabla ya Kombani kusoma maelezo ya muswada huo, Spika Makinda alitoa maelezo kuhusu kuzingatiwa kwa matakwa ya kanuni ambazo zinalazimisha muswada huo kusomwa kwa mara ya pili.

Wakati akiahirisha Bunge jana, Makinda alisema kilichotokea kwa wabunge waliotoka nje ni kutotaka kutii kanuni za Bunge ambazo uongozi wake unawajibika kuzisimamia.

Kuhusu madai ya kuingilia utendaji wa Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, alikiri kwamba aliwazuia wajumbe wa kamati hiyo siyo tu kwenda mikoani kukusanya maoni ya wananchi, lakini hata wale waliotaka kwenda nje ya nchi kwa lengo la kujifunza.
“Katiba ni ya kwetu wenyewe, mnakweda nje kufanya nini?”alihoji Spika.

Msimamo wa Majaji
Tarja kimekosoa baadhi ya vifungu katika muswada huo kikiwamo kile kinachosema hadidu za rejea za Tume ya Katiba zitatolewa na Rais. Kinataka zisiwe siri ya Rais kama ilivyoanishwa katika muswada huo, bali ziwekwe wazi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Mwenyekiti wa Tume ya Kuchambua Muswada iliyoundwa na Tarja, Jaji Mstaafu Hamisi Msumi.
“Hadidu za rejea za tume ndiyo roho ya Katiba kwa sababu ndizo zitakazoiongoza tume kutekeleza majukumu yake,” alisema Jaji Msumi alipozungumza na waandishi wa habari.


MWANANCHI

No comments: