Thursday, November 3, 2011

ATUHUMIWA KULAWITI WATOTO WA KIUMENora Damian,


MKAZI wa Lumo, Mkoa wa Dar es Salaam, Dotto Rajabu (38), amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya ya Temeke kwa tuhuma za kulawiti watoto watatu wa kiume.

Ilidaiwa mahakamani hapo na Mwendesha Mashtaka wa Polisi, Michael Kaniki, kuwa mshtakiwa alitenda makosa hayo kati ya Oktoba 10 na 23, mwaka huu.

Iliendelea kudaiwa kuwa kati ya tarehe hizo majira ya saa za usiku, mshtakiwa aliwalawiti watoto hao ambao wana umri kati ya miaka 14 na 18.

Mwendesha mashtaka alidai kuwa, mshtakiwa aliwalawiti watoto hao na kuwasababishia maumivu makali sehemu za haja kubwa.

Mshtakiwa alikana mashtaka yote na upande wa mashtaka ulipinga dhamana kwa madai kuwa, mshtakiwa ni mzoefu wa vitendo hivyo. Hakimu Mariam Mfanga aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 15, mwaka huu itakapotajwa tena.


MWANANCHI

No comments: