Wednesday, October 19, 2011

UVCCM BADO INAFUKUTA

Na James Ole Millya,

Ndugu zangu, Wazee wangu na Wana-UVCCM wenzangu, wakati huu tukianzimisha miaka 12 ya Tanzania bila Baba wa Taifa letu, Mwalimu Julius K. Nyerere, ninaomba niwakumbushe baadhi ya maneno aliyowahi kuyasema wakati wa uhai wake akijaribu kuongelea siasa za Afrika na Wa-Afrika baada ya ukombozi wa Bara la Afrika toka mikononi mwa Wafaransa, Wareno, Waingereza na Wajerumani:

“…Ukoloni mambo leo ni aina ya ukoloni ambao ni mbaya hata kuzidi ukoloni mkongwe kwani tofauti ya aina hizi za ukoloni, ni kwamba ukoloni mambo leo unatawaliwa na watu wa kabila lako, wenye kuzungumza lugha yako, tamaduni na desturi kama yako na kwa maana hiyo basi, kushinda vita dhidi ya ukoloni mambo leo ni ngumu zaidi kwani unapigana vita na watu wanaokujua na wanaozijua mbinu zetu zote…”.

Ndugu wananchi, ninaomba kutoa wito kwa watanzania wote kwamba wakati huu tukimuenzi na kukumbuka kwa majonzi yale mema aliyotufundisha Mwl. Nyerere, Baba wa Taifa letu, wote kwa pamoja tuukatae ukoloni mambo leo kwa nguvu na akili zetu zote.

Uhuru wetu uliopiganiwa kwa gharama kubwa na wazee wetu hautakuwa na maana yoyote kama tutaendelea kutawaliwa vibaya na wale tuliowaamini na kuwapa dhamana ya kusimamia rasilimali zetu, kutuonyesha njia sahihi ya kupita kama taifa ili tupate maendeleo ya binafsi na ya jumla na kudumisha amani ya muda mrefu wa nchi yetu.

Ni jukumu la kila mwananchi wa Tanzania kuuliza na kupewa majibu yaliyo sahihi na wale wenye dhamana juu ya uendeshaji wa nchi yetu. Kwa kufanya hivyo hujavunja sheria au kanuni yeyote hata kama swali hilo au maswali hayo utayaelekeza kwa nani.

Ndugu zangu, Wazee wangu na Vijana wenzangu wa Arusha, kwanza kabisa ninawashukuru kwa kuja kuhakikisha juu ya usalama wangu na kufahamu yanayonisibu kwa kuwa mimi ni kijana wenu, na kiongozi wenu. Ninaomba niwatoe shaka kwamba, ninawahakikishia kwamba nipo Salama, Imara, na Madhubuti na hakuna baya ambalo Jeshi letu la Polisi walilonitendea.

Labda niwaeleze kwa ufupi kwamba nimeitwa kutoa maelezo juu ya kauli yangu niliyoitoa kwenye mkutano wa hadhara siku ya Jumatatu iliyopita ya tarehe 10/10/2011, lakini ni muhimu sana mfahamu kwamba sijayumba, na sintayumba kwani tuna safari ndefu ya kujenga Demokrasia ya kweli na Uhuru wa kweli wa mawazo na maoni, Uhuru wa utashi wa kisiasa, Uhuru wa kusimamia misingi na kanuni za Chama Chetu, Jumuiya yetu bila woga, wala kuyumbishwa na mtu yeyote hata akijaribu kutumia vyombo vya dola au taasisi binafsi ili nitoke kwenye hoja ya msingi ya kuhakikisha Tanzania huru inawezekana, Haki na Wajibu wangu kama Mwanachama na Kiongozi wa Jumuiya na Chama Inapatikana, Uhuru wangu na Ukombozi wa Fikra unapatikana.

Ninaomba niwahakikishie kwamba:

i) Kama kosa langu ni kusimamia HAKI ndani ya Jumuiya.

(ii) Kama kosa langu ni kujenga Jumuiya yangu na Chama Changu.

(iii) Kama kosa langu ni kukemea maovu ndani ya Chama Changu na Jumuiya yangu.

(iv) Kama kosa langu ni kukosoa upotovu wa maadili wa watoto wa viongozi wanaojitwika madaraka ya wazazi wao kinyume na taratibu na sheria za nchi yetu.

Nipo tayari kukumbana na adhabu yeyote kwani sipo tayari kuona Mkoa wangu, Nchi yangu inayumbishwa na mtu mmoja, au kikundi cha watu wachache kwa masilahi yao binafsi.

Aliyekuwa Rais wa Afrika ya Kusini, Mzee Nelson Mandela (Madiba) wakati wa hukumu dhidi yake na wenzake wakati wa kupigania uhuru wa nchi yake aliwahi kusema maneno haya:

“…it is an ideal for which and if need be I am ready to die for…”

Pili ndugu wananchi, ninaomba kwa unyenyekevu mkubwa nimshukuru Mhe. Benno Malisa, Kaimu Mwenyekiti wa UVCCM Taifa kwa kuja na kuhamasisha shughuli za CCM Mkoani kwetu na kwa kuendesha zoezi la ufunguzi wa mashina ya wakererketwa wa Umoja wa Vijana, wilaya ya Arusha mjini. Ninaomba pia kutoa shukrani zangu za dhati kwa hao wafuatao kwa kushiriki kikamilifu kwenye ufunguzi wa mashina tajwa:

1. Ndg. Jamal A. Kassim, Naibu Kati Mkuu wa UVCCM Zanzibar,

2. Ndg. Godlove, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Kilimanjaro

3. Ndg. Jonas Nkya, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Morogoro na

4. Ndg. Darabe, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Manyara

5. Ndg. John Nchimbi, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa

Ndugu wananchi, ninaomba kumshukuru Mhe. Maritine Shigella (MNEC), Katibu Mkuu wa UVCCM Taifa, Ndg. Mathayo Marwa, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Mara, Ndg. Hussein Bashe, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Ndg. Kamoga, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Tabora na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Sikonge Ndg. Fadhili Ngajillo, Mwenyekiti wa UVCCM Mkoa wa Iringa, na vijana wenzangu wengi, wazee wetu, na wana-CCM, na watanzania wenzangu walionitia moyo na kunifariji katika kipindi hiki kigumu cha majaribu katika kutetea HAKI na Demokrasia ya kweli nchini mwetu.

Ndugu wananchi wa Arusha, haki hufuatana na wajabu lakini Amani huletwa na HAKI. Niwaombe viongozi wetu wasikubali kutumia mamlaka kunyima watu haki zao kwani kwa kufanya hivyo ni kuhatarisha Amani na Utulivu wa muda mrefu wa nchi yetu.

Ninaomba kurudia kwa msisitizo mkubwa, kumuonya mtoto huyu wa kigogo ya kwamba kamwe hatutaruhusu, na hatutavumilia kwa nidhamu ya woga atumie mamlaka tuliyompa mzazi wake ili kutuvurugia jumuiya yetu ya Umoja wa Vijana au Nchi yetu.

Niwatie moyo wote waliotishwa, na msiogope kwani UKOMBOZI wa Fikra una gharama zake nazo ni kama hizi. Umefika wakati wa sisi sote kusema HAPANA kama tukiona haki zetu kama wanachama na wananchi zikikiukwa na mtu, au kikundi cha watu. HAKI haziwezi kupatikana kamwe kwa njia ya kuomba au kumpigia magoti kwa mtu fulani, HAKI Hupiganiwa.

Ndugu zangu wa Arusha na Vijana wenzangu, nani asiyejua kwamba, ‘Uongozi ni Dhamana?’ Na kwa mantiki hiyo basi, kwa kuwa mimi ni kiongozi wa vijana mkoa wetu wa Arusha, niwahakikishie ya kwamba, ninaheshimu sana dhamana mliyonipa na kama nilivyowaahidi siku zote, nitasimamia wajibu wangu kwa kufuata Misingi na Kanuni za Chama Chetu na Jumuiya yetu na kuweka masilahi ya Watanzania mbele bila kuogopa na kuyumbishwa na wale ambao wamekuwa wakiyumbisha ‘ku-remote control’ mkoa wetu wa Arusha kutokana na dhamana za wazazi wao.

Mkoa wa Arusha na Kanda ya Kaskazini

Ndugu wananchi wa Arusha na Watanzania wenzangu, ninaomba pia kutoa dukuduku langu juu ya mkoa wetu na Kanda yetu ya kaskazini na ninaomba kama nikikosea nisahihishwe lakini, nina kila sababu ya kuamini Mkoa huu

tunahujumiwa na kikundi kidogo cha watu wenye uchu wa madaraka na ambao wana nia ya kuhakikisha watanzania wanakosa haki ya kumchagua kiongozi wanayemtaka kwa nia ya kulinda masilahi yao binafsi ya sasa na ya baadaye. Kwanini nayasema haya;

a) Falsafa ya Kujivua Gamba na Tamko la Baraza la Vijana wa CCM Mkoa wa Pwani

Kwa bahati mbaya au nzuri, Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete ni mzaliwa wa Mkoa wa pwani. Lakini pia, mtoto wake ambaye ni Ridhiwani Kikwete ni mjumbe Mzito” kwenye baraza la vijana wa CCM mkoa wa Pwani.

Mnamo mapema mwaka huu, Baraza hili la Mkoa wa Pwani walitamka wazi kwamba:

“…Rais wa 2015, Kamwe hawezi kutokea Kanda ya Kaskazini na anayemjua Rais wa 2015, ni Rais Jakaya M. Kikwete…”. Mbali na kwamba hili ni tusi kubwa kwa watu wa kaskazini wenye haki yao kikatiba kuwania nafasi ya uongozi wa juu

wa nchi yetu, ni tusi pia kwa wapiga kura wa Tanzania wanaoamini katika demokrasia ya kuchagua na kuchaguliwa kwani, kwa matamshi haya mazito, ni dhahiri kuwa Rais wa 2015 ameshapangwa na kikundi kidogo cha watu na upigaji kura wa 2015 utakuwa ni usanii mtupu.

Mpaka leo hii, ninapatwa na butwaa na mshutuko mkubwa kwani hata baada ya Vijana hawa waliokosa adabu au walioagizwa kutamka maneno haya, IKULU haijaweza kukanusha na kusema, Mhe. Jakaya M. Kikwete hajatupangia au hatarajii kushinikiza kwa mabavu mtu wa kuiongoza Tanzania kwa nafasi ya Urais baada ya kipindi chake kuisha 2015.

Kwa tamko zito kama hilo, ninachela kusema na najua watanzania wengi wanaoipenda nchi hii wataamini kabisa kwamba, kunyanyaswa kwangu, kuonewa kwangu na kutishwa kupitia vyombo mbalimbali vya dola, pamoja na hata “Falsafa ya Kujivua Gamba yenye waasisi wake” kama ambavyo wengine walivyotuaminisha, ni mbinu madhubuti na endeleveu za kuwapunguza nguvu baadhi ya watu wenye ushawishi mkubwa ndani ya CCM ili mradi urais wa 2015 usitokee kanda ya Kaskazini.

Fununu zipo mtaani kwamba, wengine ni chambo tu lakini anayetafutwa ni mtu mmoja tu kwenye falsafa hii ya Kujivua Gamba. Imani yao ni kwamba, wakishamchafua huyu mmoja vya kutosha, basi itakuwa ni rahisi kuhakikisha wale wengine waliobaki wawe kwenye vyama vya upinzani au chama tawala mradi wanatokea kaskazini, wataweza kudhibitiwa ipasavyo ili mradi Urais wa 2015 usiweze kuja kwenye kanda hii. Ninaamini kabisa kwamba umefika wakati muafaka wa kupata kauli ya serikali juu ya swala hili hususan kutokana na kauli ya Vijana wa CCM Mkoa wa Pwani.

Ndugu wananchi, kwa mapana ya tafsiri ya maneno ya Vijana wa CCM pwani, maana yake, kwa namna yeyote, Rais wa Awamu ya Tano ameshajulikana na kwamba kwa vyovyote vile si wa kutoka kanda ya kaskazini iwe ni kwa Chama Tawala au Upinzani.

Kama maneno haya ya Vijana wa Pwani yana Baraka za IKULU ya Tanzania, Je demokrasia ipo wapi Tanzania? Ni maswali magumu yanayohitaji ufafanuzi wa kina kwani maneno na matamko vijana hawa wa CCM Mkoa wa Pwani si ya kuyapuuzwa.

Ninaomba nitaje mifano miwili inayoonyesha kuwa tayari baadhi ya watu ndani ya CCM na Serikali wana mpango madhubuti kuwazibiti watu fulani ili Urais wa 2015 uende kwa wale wanaojulikana na waliopangwa tayari na wakubwa pamoja na Vijana wa CCM wa Pwani.

Mgogoro wa James Millya (mimi) na Mary Chatanda.

Nilipojaribu kutetea maamuzi na msimamo wa Baraza langu la Vijana wa CCM Mkoa wa Arusha na kupinga kwa nguvu zote kuingiliwa na katibu wa Mkoa wa CCM Ndugu Marry Chatanda, niliitwa kwenye vikao vya maadili na viongozi wa kitaifa waliitwa kuja kuchunguza juu ya sakata zima lakini cha ajabu, baadhi ya Vijana waliojivika kilemba cha Vijana wa Arusha ndani ya CCM walipoamka na kumtusi na kumchafua kwa mfano Mhe. Edward Lowassa na wengine, CCM ilinyamaza kimya na mpaka hadi leo, Vijana hao hawakuitwa na kuonywa na CCM kama ilivyofanya kwangu mimi na vijana wenzangu tulioamua kutetea msimamo wetu wa Baraza la Vijana la Mkoa wa Arusha.

Uonevu huu mimi sintaukubali kamwe (Double Standards).

Ni mara ngapi majina ya watu mbalimbali yanatajwa kwenye majukwaa na polisi hawahangaiki kuitisha vyombo vya habari, au kuwatafuta wale waliowataja lakini kwasababu ni mimi ambaye inawezekana nimeshawekewa “red colour” kwenye system basi inabidi nifuatiliwe na kuhangaishwa kwa makusudi eti kwasababu nimetaja jina la mtoto wa kigogo.

Ninaomba kuonyesha wasiwasi wangu kwamba, hata wateule wa nafasi mbali ziwe za chama na serikali mkoani Arusha na Kanda ya Kaskazini, ni uteuzi wenye makusudi na malengo ya kutimiza azima ya 2015. Ninaomba kusahihishwa. Tutapambana mpaka uonevu huu uishe Tanzania. Hili pia sintakubaliana nalo.

b) Nape Nnauye, Katibu Mwenezi wa CCM (Kundi fulani linalowania Urais 2015)

Kijana huyu namfananisha na saratani ndani ya mwili. Hivyo sintakosea nikisema ni “Saratani na Janga kwa CCM”. Badala ya kueneza sera za CCM ameamua kueneza sera za upande mmoja na kujaribu kuutukana upande ambao hakubaliani nao kisiasa. Siamini kama anaeneza chochote kinachohusu au kitakachosaidia CCM kukubalika na wananchi na wana-CCM. Amekuwa vuvuzela la baadhi ya watu.

Kwa mazingira ya kawaida, Mtu hawezi kusema kwa madaha kwamba wilaya ya Kasulu pamejengwa zaidi kuliko wilaya ya Mpanda kama hujawahi kufika kwenye wilaya hizo mbili na kujionea. Kwa maana hiyo basi, Nape Nnauye anavyosema “Vijana Wanatumika”, yeye atuambie ametumika au anatumika na nani?

Historia ya kijana huyu inafahamika. Alifukuzwa na Baraza la Umoja wa Vijana wa CCM Taifa kwasababu ya upotoshaji wake wa dhamira njema ya Baraza hilo la Umoja wa Vijana. Vijana walishamkataa siku nyingi, tungeulizwa kwanini tumeshindwa kumvumilia.

Refa wa mchezo wowote lazima awe na anapaswa kuaminisha watu wote, au wachezaji wote kuwa yupo ‘neutral’, yaani hana upande wowote. Je ni kweli Saratani huyu wa CCM hashabikii upande fulani wa siasa za hapa nchini? Au ndiyo mikakati madhubuti ya 2015 yanatekelezwa? Hafai kuwa refa wa mchezo wa siasa ndani ya CCM, Hatoshi.

Na hata kama mkikaa kimya kwasababu mnamadaraka na mamlaka ya Nnape Nnauye kubaki hapo alipo, watanzania wanaona ukweli huo na fitina hizi, na dunia inajua ukweli huu. Kila jambo lina mwisho wake kwani hakuna marefu yasiyo na ncha.

Ushauri wangu kwa kijana mwenzangu Ridhiwani Kikwete

Kwa bahati mbaya au nzuri watu wengi kwenye nyanja mbalimbali wanakutaja hata kupitia mitandao mbalimbali na wanakutaja kwa mambo uliyoyafanya au mengine ambayo hukuyafanya. Ni vema utambue kwamba jamii ndicho kioo chetu sote hususani kwetu ambao tumepewa mamlaka ya kuwaongoza vijana na wana-CCM nchini mwetu. Lazima ujiulize maswali mazgumu na mazito kwa mfano, kuna watoto wangapi wa marais hapa nchini, kwanini natajwa mimi tu?.

Kuna uwezekano kuwa, waliyokuzunguka hawakuambii ukweli kwani wengine hawakupendi lakini kwasababu neema yaweze kupitia hata kwako kama vile vyeo, ajira, fursa za biashara na mengine mengi, hawakuambii ukweli

Tuacheni longolongo na kuwapotezea watanzania muda wao na kuwachanga kwa siasa za maji taka.

Mambo ya kuangalia ili turudishe heshima yetu iliyotukuka kwa muda mrefu ni kuwahudumia wananchi kwa moyo wetu wote. Kupunguza tatizo na changamoto za ajira kwa vijana wetu wanaohitimu vyuo mbalimbali na kukosa ajira. Kutoa mitaji kwa watanzania ili nao waweze kushindana kwenye soko huru la Afrika Mashariki, Afrika na dunia. Kuhakikisha watanzania wenye uwezo nao pia wanashiriki kusimamia miradi na rasilimali za nchi yao tofauti na kushikiliwa na wageni tu. Watanzania waone na waridhike kodi zao zinatumika ipasavyo.

Maisha yangu yapo Hatarini

Ndugu wananchi, Vijana wenzangu, nimeanza kuwa na wasiwasi na uhai wangu kwani tangu nitoe kauli yangu juu ya mtoto wa kigogo anayejaribu kuvuruga mkoa wetu, nimeanza kupokea ujumbe wa simu ya mkononi (sms) ikinitishia kuuawa. Nimeandika polisi jinsi ujumbe huo ulivyoandikwa. Ninaomba mniombee na tuombee nchi yetu ili UHURU wa Mawazo uweze kuheshimika na hatimaye Demokrasia ya kweli ipatikane. Nani aliye juu ya Sheria?

Kama ilivyokuwa kwa wapigania uhuru wengine kama kina stevin Biko, Patrice Lumumba, na wengine wengi, nami pia nipo tayari kuhakikisha mtanzania wa kawaida hanyanyaswi na haki zake za msingi zinazingatiwa na kuheshimiwa.

Nipo tayari kuiona Tanzania huru ikishamiri hata kama nitahitajika kufungwa, kuteswa ili mradi nisiyumbe katika imani yangu dhabiti kwamba, hakuna mtu yeyote aliye juu ya sheria ya nchi hii. Sisi sote tuna haki za msingi sawa bila kujali wewe ni mtoto wa mkulima, mfugaji, au kibosile!.

Siwezi kuvumilia kuona Tanzania ambayo haki za misingi za kibinaadamu, utawala wa sheria unawabagua watanzania kwa kuangalia familia waliyotoka.

Ndugu wananchi, msimamo wangu, ukweli wangu najua unaweza kusababisha hata wale wenye mamlaka kuingilia biashara zangu, lakini kwasababu sisi sote tupo hapa ninaomba tuhakikishe mamlaka tuliyokabidhi kwa baadhi ya watanzania wenzetu kwa niaba yetu sote, hayatumiwi kinyume na tulivyokusudia. Tuamkeni na tutetee HAKI ZETU.

HITIMISHO
Ndg zangu namalizia Kusema kuwa Nikiwa kiongozi wenu sitayumba wala kupoteza Muelekeo, Nitatimiza wajibu wangu.

Pia naomba nitumie nafasi hii kusema jambo moja:

KUNA watu ndani ya Chama ni GENGE LA WAHUNI Chini ya NAPE ambao wanatumia Mgongo wa 'Kuvua Gamba' kazi yao ni kupeleka majungu na uongo kwa MH RAIS na sasa wametengeneza SINEMA mpya kuwa kuna MPANGO wa KUMUONDOA RAIS katika nafasi ya Uenyekiti na mpaka Disemba asipowafukuza hao watu ambao GENGE HILO LA WAHUNI linawatuhumu basi Mwezi huo wa Disemba MH RAIS atakua ameondolewa katika nafasi ya uenyekiti.

Genge hilo linajitengenezea uhalali kwa kutunga uongo mwingi na wenye nia ya kutaka kumtisha MH Rais ili kufanikisha Mkakati wao wa kuivuruga CCM.

Niseme nikiwa mwana CCM na Kiongozi wa Jumuiya ya UVCCM, nimuhakikishie Mh RAIS sisi Vijana wa CCM ambao tuna FIKRA huru TUTAMLINDA kwa gharama yoyote bila woga, na nimuonye NAPE na genge lake la wahuni ambao wamekua wakitunga uongo kujihalalishia nafasi kuwa hatutamvumilia kuendelea kumpotosha RAIS na tuna uthibitisho juu ya mchezo wake huu, baada ya tukio letu la ARUSHA alienda kwa RAIS kumpelekea uongo huo. Namuonya aache ujinga huo.

No comments: