Thursday, October 20, 2011

RAIS AONJA SHUBIRI YA KUKATIKA KWA UMEME

Aziza Masoud

RAIS Jakaya Kikwete juzi usiku alionja adha ya kukatika kwa umeme alipokuwa akiendesha hafla ya kuchangia ujenzi wa kituo cha wanafunzi cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwenye ukumbi wa Mlimani City, Dar es Salaam. Tukio hilo lilitokea majira ya saa 5:43 usiku takriban saa nne tangu hafla hiyo ianze. Rais Kikwete alifika ukumbini hapo saa 2:33 muda mfupi akitanguliwa na viongozi wengine wa Serikali. Baadhi ya viongozi hao ni Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dk Shukuru Kawambwa, Waziri wa Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadiki. Kukatika huko kwa umeme, kuliwafanya wageni waliokuwapo ukumbini kuanza kupiga kelele za: “Ngeleja... Dowans... Ngeleja... Dowans... Ngeleja... Dowans.”

Rais Jakaya Kikwete akimkabidhi Mkurugenzi wa Masoko wa Benki ya CRDB Tully Mwambapa picha ya Mwalimu Julius Nyerere iliyonunuliwa na Benki hiyo kwa kiasi cha Sh.milioni 35,wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na Ofisi ya Rais kwa ajili ya kukusanya pesa za upanuzi wa Chuo kikuu cha Dar es Salaam juzi na kupatikana Sh.722 milion.Fidelis Felix


Tukio hilo lilidumu kwa dakika mbili kabla uongozi wa Mlimani City kuwasha genereta. Katika hafla hiyo, Rais Kikwete alichangisha Sh720 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho kinachotarajiwa kujengwa katika Kampasi ya Mlimani katika kumbukizi ya Miaka 50 ya Uhuru. Kituo hicho kitakuwa na maeneo ya kupumzika wanafunzi, hosteli, sehemu za michezo, maktaba, huduma za vyakula, benki, ofisi za serikali ya wanafunzi na kituo cha intaneti.

Akizungumza kabla ya uchangishaji huo, Rais Kikwete alisema lengo la kuchangisha fedha hizo za kujenga kituo cha wanafunzi ni kuboresha mahitaji ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ambayo kwa sasa yamekuwa changamoto kubwa inayosababisha wanafunzi kupata elimu katika mazingira magumu.

“Mara nyingi ukipita katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, unakuta wanafunzi wamezagaa katika maeneo mbalimbali na wengine chini ya miti. Hii yote inatokana na kukosa eneo maalumu la kujisomea na kupumzika mara wanapomaliza au kusubiri kuingia katika vipindi,” alisema Kikwete.

Alisema kutokana na ongezeko la watu na shughuli za kimaendeleo, chuo hicho kwa sasa kinakadiriwa kuchukua wanafunzi 20,000 kwa mwaka, tofauti na miaka ya nyuma kilipokuwa kinachukua wanafunzi 14,000. Alisema kutokana na hali hiyo, wahitimu wanapaswa kuchangia maendeleo ya chuo hicho kwa kuwapatia wanafunzi nafasi za malazi ambazo kwa sasa hazitoshi na kuwalazimu wengine kulala nje ya eneo la chuo.

Awali, Dk Kawambwa alisema kukutana kwa wanafunzi na wahitimu wa chuo hicho ni kuendeleza utamaduni unaotumika duniani kote wa kuchangia maendeleo ya shule au vyuo wanavyotoka. “Jambo tunalolifanya jioni hii lina maana kubwa, tunajenga utamaduni wenye manufaa katika nchi yetu kuendeleza elimu nchini kwa kuchangia maendeleo ya shule au chuo,” alisema.

Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Rwekaza Mukandala alisema kituo hicho kitagharamu Sh17bilioni na hatua ya kwanza ya kupata fedha za ujenzi huo ni kuandaa kampeni hizo za uhamasishaji na uchangiaji kutoka kwa wadau mbalimbali. “Hafla ya uzinduzi wa michango hiyo ilifanyika Januari 27 mwaka jana.

Iliwahusisha wanajumuiya ya chuo na wajumbe wa baraza la chuo na tulibahatika kupata Sh1.2bilioni, nyingi zikiwa ni ahadi za wafanyakazi,” alisema Profesa Mukandala. Alisema baada ya hafla hiyo, kulifanyika hafla nyingine Ikulu mwezi huohuo iliyokuwa ikiongozwa na Rais Jakaya Kikwete. Katika hafla hiyo jumla ya Sh1.5bilioni zilikusanywa.

Alisema hafla ya tatu ilikusanya Sh658 milioni za ambazo zilitolewa na Rais Yoweri Museveni wa Uganda ambaye naye ni muhitimu wa chuo hicho. Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Mkuu Mstaafu, Jaji Joseph Warioba aliwataka wahitimu waliosoma chuoni hapo kuwa mstari wa mbele kuchangia maendeleo yake.

Katika hafla hiyo Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) iliahidi kutoa Sh150 milioni, Hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro Sh130 milioni, Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF), Sh100 milioni, Mikumi Interprises Sh20 milioni, Benki ya NMB Sh20 milioni. Kampuni ya Sigara Tanzania (TCC) ilitoa Sh30 milioni, Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) Sh30 milioni, Mfuko wa Pensheni wa PSPF Sh20 milioni na Mnyika alitoa Sh2milioni na kuahidi kutoa Sh milioni moja kila mwaka kwa kipindi cha miaka mitano.

Benki ya CRDB ilinunua katika mnada wa kuchangisha fedha za ujenzi huo, picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere kwa Sh35milioni. Rais ndiye aliyeendesha mnada wa picha hiyo.MWANANCHI

No comments: