Thursday, October 20, 2011

OCCUPY DAR INAKUJA HIYO


“Ndiyo tumekibinafsisha (Kiwanda cha Sigara) na hii ndiyo sera mpya ya kuleta manufaa Tanzania! Hii ndiyo mbinu mpya imegunduliwa? Ujamaa mpya huo! Huo ni unyang’anyi tu wa mali yetu wote.Hili ni jambo la upumbavu. Katika masuala ya uchumi wa nchi, lazima tufanye tofauti baina ya kujitajirisha wachache na kuleta manufaa ya watu wengi. Sasa, sera hii itazaa mamilionea sasa hivi na sio baadaye, lakini watakuwa mamilionea watano. Hata hivyo, wakati huo huo, pia itazaa masikini na Tanzania itakuwa na masikini wengi sana… Sasa taabu yetu, wala si Tanzania peke yake kuna vi inchi vingi, ni kwamba viongozi wetu hawakatai. Wanakubali tu. Lakini sisi ni madodoki? Dodoki ulitumbukize katika maji, hata yenye takataka, linazoa tu!” Julius K. Nyerere, Uwanja wa Sokoine Mei Mosi 1995


IMETOSHA!

Sisi 1% ya Watanzania ambao tumeathirika na tunaendelea kuathirika na mfumo mbaya utawala ambao unaendekeza matajiri wakubwa na wawekezaji wa kigeni tunasema ‘imetosha’. Tunasema ‘imetosha’ kwa sababu tunabebeshwa mzigo usiobebeka huku tukilazimishwa kwenda ambako sisi hatupaswi kwenda huku maisha yetu yakiendelea kufanywa duni zaidi na zaidi. Tumetengeneza “mamilionea watano” lakini “maskini wengi sana”.


Tunachokitaka:


TATIZO LA NISHATI YA UMEME HALIELEZEKI, HALIONDOKI NA HAWAWAJIBIKI
– Tunataka Waziri wa Nishati na Naibu wake wajiuzulu kama kuwajibika kisiasa kwa kushindwa kulipatia taifa sera na uongozi unaostahili kukabiliana na tatizo hilo ambalo limekuwa ni mzigo wa kudumu mabegani mwa wafanyabiashara wadogo, maskini na wafanyakazi nchini!


TUNAKATAA MALIPO YA BILIONI 111 KWENDA DOWANS – Kama viongozi wetu waliweza kudai fedha za rada ambazo ni bilioni karibu 60 hivi na wakazing’ang’ania tunataka watuoneshe kuwa hawako tayari maskini wa Tanzani walipie uzembe na kutokuwajibika kwa watu wengine. Tunakataa kubebeshwa mzigo wa ufisadi wa viongozi wetu waliovumiliwa walipoliingiza taifa kwenye mkataba wa Richmond na wakaa kimya uliporithishwa kwa Dowans. Tunatakaa fedha za walipa kodi wa Tanzania kulipia ufisadi kwa kutumia kisingizio cha “hukumu halali ya mahakama”! Wakilipa na wao walipe!


SERIKALI ISITISHE UKODISHAJI WA MAENEO MAKUBWA YA ARDHI KWA WAGENI – Kutokana na ukosefu wa sera bora ya kusimamia ardhi taifa letu limejikuta likiwa miongoni mwa maeneo yanayokimbiliwa na makampuni makubwa ya kimataifa ambayo yana lengo la kukodisha ardhi kwa ajili ya kulima mazao ya nishati ya mafuta au chakula kwa ajili ya kulisha viwanda vya kwao. Bila sera itakayolinda ardhi yetu kwa ajili ya vizazi vijavyo tunaona jinsi 1% wanavyohukumu kizazi kijacho kwa kugawa ardhi yetu sisi 99% kwenda wageni kwa miaka 99! Tunataka kusitikishwa kwa mipango hiyo hadi sera itakayolinda maslahi yetu itakapowekwa na kukubalika nasi.
WAHUSIKA WALIOHUSIKA NA DOWANS NA RADA WAKAMATWE – Tunataka wahusika wote waliohusika na mikataba ya Dowans na Rada na kulisababishia taifa hasara kubwa ambayo inalipwa na maskini wa Tanzania na u kosefu wa fedha za kutosha kufadhili elimu ya juu au kupatia wadogo na watoto wetu madarasa mazuri yenye utu wa kibinadamu wakamatwe na wafikishwe mahakamani.Uwe ni mwanzo wa vita dhidi ya watendaji na wafanyabiashara wanaohujumu taifa hili na hivyo kuhujumu haki ya urithi wa kizazi kijacho.

KUVUNJWA KWA BODI YA MIKOPO YA ELIMU YA JUU
– chombo hiki kimekuwa chanzo kikubwa cha matatizo ya elimu ya juu nchini na wakati umefika kivunjwe na kibadilishwe na mamlaka ambayo itakuwa na uwezo, weledi na uwazi wa kutambua kuwa elimu ya juu ni injini ya maendeleo ya haraka ya jamii yoyote.

TUNATAKA MABADILIKO JESHI LA POLISI
– Jeshi la Polisi linahitaji mabadilko makubwa ili liweze kuondolewa na mfumo ambao ni wa kisiasa. Hatutaki tuwe na hofu na polisi wetu; kukosekana huduma ya haraka na ya kisasa ya kipolisi kunafanya wananchi wengi kukata tamaa na utawala wa sheria. Mauaji ya wananchi mikononi mwa polisi katika mazingira tata hayakubaliki tena na hasa mauaji ambayo yanatokea kwa wananchi na kushindwa kwa polisi kuwakamata wahalifu kwa muda muafaka.

TUNATAKAA AJIRA ZA UNDUGU NAKUJUANA
- Mfumo wa ajira licha ya kwamba kinadharia unatakiwa uwe usio na upendeleo wa aina yoyote ukweli wake ni kuwa bila kujuana ni vigumu kupata kazi za maana au zinazoendana na elimu na uwezo wa mtu. Matokeo yake mfumo wetu wa ajira hautoi nafasi sawa kwa Watanzania wasio na ndugu au jamaa kwenye viti vya juu kupata nafasi za kazi. Tunataka tuhakikishiwe kuwa jambo hilo linashughulikiwa (siyo linaangaliwa) ili kuondoka na undugu (undugunization a.k.a nepotism)

NANI ANAITWA KU-OCCUPY DAR?

- Wanafunzi wote waliohitimu masomo yao lakini wakiwa hawana ajira kutokana na hali mbaya ya uchumi duniani au kukosa watu wa kuwafanyia ‘connection’ au ambao wamekataa kuuza utu wao kwa kutoa rushwa ili wapate ajira!
- Vijana wote ambao wamejikuta wakiishi maisha ya kuombaomba, kujishikiza hapa na pale huku wakiwa na uwezo wa kujiendeleza kielimu na kikazi lakini kutokana na mfumo mbaya wa utawala wamejikuta wakiishi maisha ya kubangaiza hapa na pale na kuwa mzigo kwa watu wengine
- Watu wote ambao wamechoshwa na vitendo vya ufisadi uliokithiri na hasa namna ambapo mafisadi wa kila aina wanaonekana wakitamba mitaani, huku wakitumia fedha zao kunyanyasa wale 1%!
- Wale wote ambao wamechoshwa na kuanza kutishwa na sera za uuzaji wa ardhi yetu kwa wageni na kusababisha eneo kubwa la ardhi yetu kuanza kumegwa na kupewa wageni huku wananchi walioishi kwenye maeneo hayo mbalimbali aidha wakihamishwa kwa nguvu au kukataliwa haki ya ardhi (right to land) kwa kujipatia maisha yao.
- Wale wote ambao wamejikuta wakilazimika kufanya vitendo vya kujipatia kipato kwa kutumia njia za mkato kutokana na nafasi zao kwa vile mfumo uliopo umefanya maisha kuwa magumu sana huku kipato cha 99% kikiwa chini kulinganisha na mapato ya kufuru yanayopatwa na mashirika, makampuni makubwa na matajiri wanaounda 1%!
- Wale wote ambao wanaamini sauti zao kuhusu masuala mbalimbali ya kimaisha yanayowahusu wao hayajasikilizwa na watawala waliopo.


MAENEO GANI YATAKALIWA (OCCUPIED AREAS)
Kwa vile lengo la kukalia (occupy) maeneo haya ni kutuma ujumbe wa kuwa tumechoshwa na hali iliyopo (status quo) maeneo mbalimbali ya kimkakati yamechaguliwa ili yaweze kukaliwa na wananchi waliochoshwa na mfumo wenye kufanikisha na kuendekeza 1%. Ikumbukwe kuwa huu ni mwamko wa amani, siyo maandamano wala mgongano na watawala ni mwamko ambao umeanzia Marekani baada ya wafanyakazi na vijana kuchoshwa na mfumo mbovu wa utawala uliowafanya wao kuwa maskini zaidi; mwamko huu sasa umeenea kwenye nchi mbalimbali na wakati umefika na sisi Watanzania kutambua kuwa tuna haki ya kutoa sauti zetu kwa njia ya amani bila kujali siasa za vyama na maslahi ya watu mbalimbali.

- Eneo lote la Bustani ya Mnazi Mmoja (ENEO KUU la OD)

- Eneo la Bustani ya Posta ya Zamani
- Eneo jingine lolote la umma ambalo ni rahisi wananchi kuweza kukutana na kulikalia kwa amani.

VITU VYA KULETA

Kila mtu atajihudumia yeye mwenyewe hivyo ni vizuri kuhakikisha unavyo vitu vya kukusaidia kukaa chini katika hali ya usafi na usalama – mikeka, mahema madogo, kanga vinaruhusiwa. Kwa wale wenye vipaji na biashara mbalimbali kutoa huduma wanakaribishwa vile vile.


VITU VISIVYORUHUSIWA
Haitaruhusiwa kuleta au kuwa na silaha ya aina yoyote ile kwani mwamko huu ni wa amani. Hairuhusiwi kuleta vitu vyovyote vya kulevya (vileo au madawa) kwani katika mazingira ya vileo ni rahisi watu kupoteza uwezo wa kujitawala na kuvunja amani. Usilete alama za chama chochote cha siasa kwani huu si mwamko wa vyama vya kisiasa bali mwamko wa wananchi waliochoshwa!

KUJIANDAA NA VYOMBO VYA DOLA

Kwa vile huu ni mwamko wa amani, KILA ANAYEKUJA ajiandae kukwamatwa bila kupinga. Kwa hiyo, endapo polisi watalazimisha kutuondoa kwa nguvu hakuna kupingana nao wala kujibizana nao bali kuacha wao watuondoe kwa nguvu. Hii ndio maana ya PEACEFUL CIVIL DISOBEDIENCE. Kosa kubwa katika mazingira halo itakuwa ni “kuzurura” au “kukaidi amri ya polisi”. Tukisimama pamoja hawana jela za kutosha kufunga vijana wote wa DAR wala magereza ya kuwaweka watu wote waliochoshwa na mfumo uliopo!Kama hauko tayari kukamatwa kwa kutoa sauti yako USIJE!

UKIMYA WETU UMEFIKIA MWISHO - HATA PUNDA AKIZIDIWA HUGOMA NA MASKINI HANA CHA KUPOTEZA ISIPOKUWA UTU WAKE!


by
The Occupier

Kwa taarifa zaidi ingia hapa

No comments: