Friday, October 14, 2011

NYERERE AMEONDOKA NA SERA YAKE YA UJAMAA


Elias Msuya


OKTOBA 14, mwaka huu, itakuwa ni miaka 12 tangu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere aiage dunia, lakini Watanzania wanazidi kuwa mbali kimawazo na kutokuendelea kuzienzi fikra zake, mipango na mikakati yake, labda pengine kwa sababu ya mabadiliko ya nyakati.
Katika utawala wake Mwalimu Nyerere aliasisi Azimio la Arusha ambalo kwalo alisisitiza sera ya Ujamaa na Kujitegemea.

Siasa ya Kujitegemea
Katika kitabu cha Azimio la Arusha, lililozinduliwa mwaka 1967, kuna ufafanuzi wa kina kuhusu sera ya Ujamaa na Kujitegemea.
Kinafafanua maana ya ujamaa kama sera kuwa ni imani na unapaswa kujengwa na watu wanaoamini na kufuata kanuni zake.
Muundo wa Ujamaa ni pamoja na kutokuwa na unyonyaji wala matabaka ya watu.

“Nchi yenye Ujamaa kamili ni nchi ya wafanyakazi, haina ubepari wala ukabaila. Haina tabaka mbili za watu, tabaka ya chini ya watu wanaoishi kwa kufanya kazi na tabaka ya juu ya watu wanaoishi kwa kufanyiwa kazi.

“Katika nchi ya Ujamaa kamili, mtu hanyonyi mtu, bali kila awezaye kufanya kazi hufanya kazi na kila mfanyakazi hupata pato la haki kwa kazi aifanyayo na wala mapato ya wafanyakazi mbalimbali hayapitani mno”.

Kuhusu njia kuu za uchumi, sera hiyo inasisitiza kuwa zinatakiwa kuwa chini ya wakulima na wafanyakazi.
“Namna pekee ya kujenga na kudumisha ujamaa, ni kuthibitisha kuwa njia zote za uchumi wa nchi yetu zinatawaliwa na kumilikiwa na wakulima na wafanyakazi kwa kutumia vyama vyao vya ushirika”.

Njia hizo za uchumi zinatajwa kuwa ni ardhi, misitu, madini, maji, mafuta na nguvu ya umeme, njia za habari, njia za usafirishaji, mabenki, bima, biashara na nchi za kigeni na biashara kwa jumla, viwanda vya chuma, mashine, silaha, magari, simenti, mbolea, nguo na kiwanda chochote kikubwa ambacho kinategemewa na sehemu kubwa ya watu katika kupata riziki zao au viwanda vingine, mashamba makubwa yanayotoa mazao ya lazima katika viwanda vikubwa.

Kuhusu demokrasia katika ujamaa, kitabu hicho kinaeleza kwamba umilikaji wa njia kuu za uchumi haukamilishi ujamaa, sharti serikali ichaguliwe na kuongozwa na wakulima na wafanyakazi wenyewe.

Msingi wa Siasa ya Kujitegemea
Msingi wa siasa ya kujitegemea ni ukombozi unaotokana na unyanyasaji wa wakoloni waliotutawala kwa muda mrefu.
“Tumeonewa kiasi cha kutosha, tumenyonywa kiasi cha kutosha na tumepuuzwa kiasi cha kutosha. Unyonge wetu ndiyo uliotufanya tuliofanya tuonewe, tunyonywe na kupuuzwa. Sasa tunataka mapinduzi ya kuondoa unyonge ili tusionewe wala tusipuuzwe tena” anasema Mwalimu Nyerere.

Fedha siyo msingi wa maendeleo
Hata hivyo Mwalimu Nyerere anasema silaha ya kupambana katika vita hiyo, siyo fedha kwani fedha siyo msingi wa maendeleo.
Kwa mujibu wa Nyerere, fedha zinaweza kupatikana kwa njia ya zawadi kutoka nchi tajiri au mikopo ambayo masharti yake kama vile muda wa kulipa, kima na faida.
Vile vile kuna rasilimali ya kibiashara (uwekezaji) ambapo watu au makampuni yanayotaka kuja nchini kuanzisha shughuli za uchumi kwa manufaa yao wenyewe.

“Ni jambo la kijinga kuchagua fedha kuwa ndiyo chombo chetu kikubwa cha maendeleo na hali tunajua kuwa nchi yetu ni masikini. Ni ujinga vile vile, kwa kweli ni ujinga zaidi tukidhani kuwa tunaweza kuondoa hali hii ya unyonge wetu kwa kutegemea fedha za kutoka nje badala ya fedha zetu wenyewe,” anasema Mwalimu Nyerere.

Anazitaja sababu mbili za ujinga huo akisema kwamba, kwanza hatutazipata fedha hizo kwakuwa hakuna nchi hata moja duniani ambayo iko tayari kutupa msaada au mikopo au kuja kujenga viwanda katika nchi yetu kwa kiasi cha kutuwezesha kutimiza shabaha zetu zote za maendeleo.
Vilevile anasema, nchi masikini ni nyingi sana duniani. Hata kama nchi tajiri zingekubali kuzisaidia bado msaada usingetosha.
“Njia ya kuzipata fedha za matahjiri ili zisaidie umma ni kuwatoza kodi wakipenda wasipende. Hata hivyo huwa hazitoshi, hata tukiwakamua vipi wananchi, masikini na matajiri, hatuwezi kupata fedha za kutosha kutimiza mipango yetu ya maendeleo,” anasema.

Misaada na mikopo inahatarisha uhuru wetu
Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, kujitawala ni kujitegemea na kujitawala huko hakuwezekani ikiwa taifa moja linategemea misaada na mikopo ya taifa jingine kwa maendeleo yake.

“Hata kama pangetokea taifa au mataifa ambayo yako tayari kutupa fedha zote tunazohitaji kuendesha mipango yetu ya maendeleo, isingekuwa sawa kupokea misaada hiyo bila kujiuliza matokeo yake yatakuwa nini kwa uhuru wetu na uzima wetu”.
Anaendelea kusema kuwa misaada ni chombo cha kuongeza misaada, lakini inaweza kuwa sumu ya maendeleo kama utapekelewa bila kujiuliza.
Kuhusu mikopo anasema ni bora kuliko misaada ya bure, lakini anasema nayo ina kikomo chake.

“Tunapokopa fedha, mlipaji ni Mtanzania na kama tulivyosema, Watanzania ni maskini. Kuwabebesha matu masikini mikopo ambayo inawazidi kimo si kuwasaidia bali ni kuwaumiza na hasa inapokuwa mikopo hiyo wanayotakiwa kuilipa haiwasaidii wao bali watu wachache”.
Tufanye nini ili tuendelee?

Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, maendeleo ya nchi huletwa na watu, siyo fedha. Fedha ni matokeo na siyo msingi wa maendeleo.
Anasema ili tuendelee tunahitaji viti vinne, yaani watu, ardhi, siasa safi na uongozi bora.
Kwa kuzingatia kuwa Tanzania ina eneo la ekari 362,000 na watu zaidi ya 40 milioni. Kwa idadi hiyo inatosha kabisa kupata nguvu kazi ya kuleta maendeleo.

Siasa safi na uongozi bora kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, ilitokana na sera ya ujamaa na kujitegemea iliyokuwa ikiaminiwa na TANU.
Ili kuyafikia maendeleo kupitia vitu hivyo vitatu, Mwalimu anatoa masharti mawili ambayo ni juhudi na maarifa katika kazi.


Misingi ya uongozi bora
Ili kuwadhibiti viongozi wa serikali kwa wakati huo, chama cha TANU kiliweka misingi ya uongozi bora ambapo, kiongozi wa TANu alipaswa kuwa mkulima au mfanyakazi na asishiriki katika jambo lolote la kibepari au la kikabaila.
Vilevile hakutakiwa kuwa na hisa katika makampuni yoyote. Pia asiwe mkurugenzi katika kampuni ya kikabaila ua kibepari, asiwe na mishahara miwili au zaidi na asiwe na nyumba ya kupangisha.

Azimio la Arusha limebaki historia
Kwa muda wote Mwalimu Nyerere alipokuwa madarakani aliamini katika Ujamaa na kujitegemea. Hata alipong’atuka mwaka 1985, aliendelea kuamini katika misingi hiyo, japo ilishaanza kuwekwa kando.

Hadi kufikia mwaka 1990, Azimio la Arusha lilitelekezwa kabisa na kuanzishwa kwa ‘Azimio la Zanzibar’ ambalo viongozi walilegeza masharti ya misingi ya uongozi hali inayoashiria kushuka kwa maadili ya viongozi wa umma na kuwepo kwa kashfa nyingi za ufisadi serikalini.
Hadi sasa Azimio la Arusha lililokuwa na sera ya ujamaa na kujitegemea limebaki kuwa kama tukio la kihistoria lisilokuwa na na umuhimu katika zama hizi.

Mwalimu Nyerere kabla ya kifo chake alilibaini hilo ambapo katika katika kitabu chake cha ‘Nyufa’ anaeleza jinsi viongozi wa CCM walivyokutana Zanzibar na kuliua Azimio la Arusha.

“Viongozi wetu walikutana Zanzibar wakaona Azimio la Arusha halifai. Wala hawakututangazia na hawakutuzungumzia kwamba tumekutana Zanzibar tumeona Azimio la Arusha halifai” anasema Nyerere katika kitabu hicho ukurasa wa 21 na 22.
Anaendela kusema,

“Walikuja kimya kimya, tukaona wanaanza kufanya mambo ambayo hayafanani na Azimio la Arusha. Wenye akili tukajua limekwisha hilo”.
Kwa mujibu wa Mwalimu Nyerere, Azimio hilo lilikuwa na miiko na hakuna serikali yoyote duniani isiyo na miiko.
Miiko hiyo inaelezwa katika sehemu ya tatu ya Azimio la Arusha, inapozungumzia umuhimu wa kuwa na viongozi bora.

“Wameacha miiko ya Azimio la Arusha, hawakuweka miiko mingine. Sasa ni holela tu, hovyo tu,” anasema Mwalimu Nyerere.

No comments: