Friday, October 14, 2011

MIAKA 12 BAADA YA MWALIMU
Na Baraka Mfunguo,

UTANGULIZI

Leo tunaadhimisha miaka 12 baada ya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aghalabu wapo wale ambao roho zao zinawauma wanapoona taifa linapozizima kwa kumkumbuka Mwalimu na wapo wale ambao ndio sisi wengi wetu tunaoamini kwamba Mwalimu alikuwa hazina kubwa katika taifa hili na historia inavyoelekea inaniashiria kwamba hatutaweza kumpata kiongozi aliyekuwa na haiba ya kipekee kama yeye. Labda Mwenyezi MUNGU ashushe rehema yake atuletee mkombozi mwingine na tuombe Mungu atupe hekima tusimsulubishe kama wanavyosulubishwa wengine kwa shinikizo la mabeberu kwa kigezo cha kutetea demokrasia ili hali wakihalalisha uharamia wao.

Nitajikita zaidi katika misingi mikuu ya Azimio la Arusha nayo ni falsafa nzima ya Ujamaa na Kujitegemea pamoja na matokeo yake nayo ni Utaifishwaji wa njia kuu za uchumi , Vijiji vya Ujamaa changamoto zake nikihusisha na muelekeo wa Tanganyika katika kusheherekea miaka 50 ya uhuru

Kama inavoelezwa na wachambuzi wengi, misingi ya Azimio la Arusha ilijikita zaidi katika umiliki wa njia kuu za Uchumi pamoja na Uchumi wenyewe mikononi mwa wananchi ili kujenge jamii yenye usawa, jamii yenye kuheshimiana pamoja na kuthamini utu wa mtu. Azimio la Arusha la mwaka 1967 lilikuja kama mbadala wa kuwawezesha wananchi wengi kupata fursa mbalimbali katika ujenzi wan chi yao na ninaweza kusema katika nyakati zile watu walikuwa wana uzalendo na utaifa wa kweli. Yote hii ilitokana na miongozo na misimamo madhubuti aliyokuwa nayo mwalimu.

Katika hayo kuna falsafa ya Ujamaa na Kujitegemea ambayo ilijikita katika misingi ya utu pamoja na utamaduni wa Mwafrika hususan Mtanzania iliyojikita katika familia na maisha ya kidugu kwa ujumla. Watanzania wote tuliitana ndugu mchaga kwa mzaramo….Mhaya kwa Mjita……Mngoni kwa mhehe…..Mmakonde kwa Mmwera na hata endapo kutatokea mtu yeyote ambaye hana asili ya kitanzania ama kwa rangi yake au vinginevyo, madhali ni Mtanzania, alikuwa ndugu na alipata fursa ambayo waliipata watanzania wengine. Hivyo basi twaweza kusema kwamba sera ya Ujamaa ilikuwa ni moja ya mwongozo mkubwa ambao ulilenga katika kutuletea maendeleo katika misingi ya Uhuru, Umoja na Usawa. Kwa mujibu wa Mwalimu, alisema ni muhimu kuwapo na usawa kwani hiyo ndiyo njia ya pekee ya kuwawezesha watu kushirikiana na kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi. Ni vyema kukawa na uhuru kwa sababu mtu hawezi kuhudumiwa na jamii . Kila mtu ilimlazimu afanye kazi ili kupata ujira halali. Na ni lazima jamiii iwe na umoja utakao wawezesha wananchi kuishi kwa amani kufanya kazi kwa pamoja na pia usalama wa uhakika wa watu pamoja na mali zao.

SERA YA UTAIFISHWAJI WA NJIA KUU ZA UCHUMI NA CHANGAMOTO ZAKE

Sera ya utaifishaji wa mali ililenga katika kukuza uchumi wan chi. Ikumbukwe kwamba moja ya sababu iliyochochea vuguvugu la kudai uhuru lilikuwa ni kutokuwa na usawa katika umilikaji wa njia kuu za uchumi baina wa Waafrika na Wakoloni. Kwa kiasi kikubwa Wakoloni walitugawa kwa madaraja kutokana na rangi ya ngozi zetu na hata katika fursa mbalimbali ilikuwa hivyo hivyo. Kutokana na sera ya utaifishwaji wa mali masuala yote ya kiuchumi yalikuwa yamegawanywa katika makundi matatu mosi yale ambayo yalisimamiwa moja kwa moja na serikali ama nchi, pili yale ambayo serikali ilikuwa na umiliki mkubwa wa mtaji wa uwekezaji na tatu asasi binafsi ambazo zingweza kuwekeza kwa kuishirikisha ama pasipo kuishirikisha nchi katika umiliki wa mtaji wa uwekezaji Baada ya kutangazwa kwa Azimio la Arusha Mwalimu Nyerere alitangaza moja kwa moja kutaifishwa kwa mali ikijumuisha mabenki yote, viwanda vikubwa, viwanda vya usindikaji vilivyotokana na Kilimo. Sehemu ya sekta ya Biashara ilitaifishwa pamoja na umiliki wa asilimia sitini wa uzalishaji wa kilimo cha mkonge (Arkaide 1973:37). Mpaka mwisho wa mwaka 1967 Serikali ilikuwa imeshamiliki njia zote kuu za uchumi.

Changamoto iliyojitokeza ilikuwa ni kukubalika kwa sera ya utaifishaji wa njia kuu za uchumi kwenda mikononi mwa serikali kimataifa. Kulikuwa na mkanganyiko mkubwa wa baadhi ya nchi katika kuukubali ama kuukataa mkakati huu. Kwa mfano nchi zote za Kiskandinavia ziliufurahiaa mkakati huu na kuuona kuwa wa manufaa kwa nchi wakati mataifa mengine ya magharibi hayakuufurahia mpango huu na mataifa hayo ndiyo viranja wakuu wa uchumi huria. Kwa mfano banki kubwa maarufu za Uingereza kama vile Barclays, Standard, National na Grindleys hazikutoa ushirikiano na lengo lao kuu ilikuwa ni kuhakikisha mashirika ya umma pamoja na mabenki yanakufa. Hili liliendana sanjari na kuwaondoa wafanyakazi wao pamoja na kuwapa masharti na maelekezo ambayo yalilenga kabisa kushusha ari na kiu ya watanzania katika kuumiliki uchumi wao ikiambatana na kauli za kejeli kuhusiana na mauzo ya nje ya mazao ya chakula na biashara yananyozlishwa nchini. Lengo lao kuu lilikuwa ni kuhakikisha sera hii haifanikiwi kwani kufanikiwa kwake kungeweza kuzishawishi nchi nyingine za kiafrika kuiga hususan Kenya na Uganda ambazo zilikuwa zinafuata mfumo wa kibepari. (Coulson, 1985:41)

Pamoja na kwamba katika Azimio la Arusha kulikuwa na sera ya kutaifisha njia kuu za uchumi na kumilikiwa na wananchi, Asilimia kubwa ya Asasi zilizotaifishwa na kuwa za serikali ziliingia ubia na kampuni za nje ambazo zilikuwa wamiliki wa awali kabla ya kutaifishwa kwa mfano Kampuni kubwa ya kimataifa ya ushauri kwenye masuala ya Uongozi na uendeshaji ya Mckinsey ilipatiwa mkataba wa kusimamia na kuratibu usimamizi wa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), Shirika la Mkonge, Shirika la Bandari la Afrika Mashariki (Loxley na Saul, 1975:72). Ni kutokana na sababu hizi wachambuzi wengi wanasema kwamba, pamoja na kuwa na sera ya kutaifisha njia kuu za uchumi kwenda mikononi mwa wananchi kufanyika, maamuzi bado yalibaki mikononi mwa wageni . Shivji anatanabaisha kwamba , mchakato wa kutaifisha njia kuu za uchumi haukuipatia serikali/wananchi fursa ya kumiliki njia kuu za uchumi na wala kufanikiwa kuzuia muingiliano wa mtaji wa makampuni makubwa ya nje katika sera ya uchumi na siasa ya Tanzania (Shivji 1973)

Viashiria vya awali kuhusu maendeleo baada ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi kwenda mikononi mwa wananchi ulikuwa chanya . Moja ya Malengo ya kutaifisha njia kuu za uchumi yalikuwa kuhakikisha mtaji unaozalishwa ndani ya nchi ni wa kutosha kwa matumizi ya wananchi kwa kupunguza kiwango cha mtaji kinachosafirishwa nje ya nchi. Na hii ilisaidia kupunguza mfumo tegemezi wa kifedha wan chi dhidi ya asasi kubwa za mikopo za kidunia mathalan IMF. Benki ya Tanzania ilifanikiwa kudhibiti na kusimamia hifadhi ya hazina ya Taifa dhidi ya pesa ya Mwingereza ya Sterling pound na kujihakikishia kutoshuka thamani ya shilingi ya Tanzania jambo ambalo lisingewezekana kabla ya Azimio la Arusha la mwaka 1967 (Nnoli 1978 :213).

Kiashiria kingine kikubwa cha mafanikio cha sera hii ya Utaifishwaji wa njia kuu za uchumi kilikuwa ni kuongezeka kwa ukusanyaji na udhibiti wa rasilimali za ndani ambapo mwaka 1964 kiwango cha mtaji kilikuwa ni Asilimia 15% ya GDP mwaka 1969 iliongezeka kwenda asilimia 20% na kupaa mpaka asilimia 26% mwaka 1970. Mafanikio mengine yalikuwa ni kuongezeka kwa mapato ya nchi yaliyotokana kwa sekta ya viwanda pekee kutoka shilingi milioni 81.9 mwaka 1968 mpaka shilingi milioni 134.5 mwaka 1969 (The United Republic of Tanzania, 1970:16)

Hata hivyo kulikuwa na changamoto za msingi na za wazi kabisa ambazo zilibainika wazi wakati sera hii ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi ikiwa inatumika Serikali haikuweza kusimamia na kuimarisha umiliki wake wa njia kuu za uchumi kwa kujenga uchumi imara wa kujitegemea hususan katika sekta ya viwanda kama inavyobainishwa na mtafiti Dianne Bolton (1985:154) katika utafiti wake uliohusiana na utaifishwaji wa sekta ya viwanda uliotokana na zao la mkonge Tanzania. Bolton anahitimisha kwa kusema “dhana ya utaifishwaji kama inavoainishwa kwenye uzalishaji wa zao la mkonge ina mkanganyiko mkubwa hususan katika kuelekea katika sera ya Ujamaa na kujitegemea.” Hii ilitokana na sekta hiyo haikuwa na uwezo ya kuratibu kusimamia kwa ufanisi na weledi njia za uzalishaji na jamii. Masuala kama ya urasimu na usimamizi kutoka serikali kuu iliongeza mwanya mkubwa wa rushwa pamoja na upotevu wa rasilimali ( Bolton,1985:156).

Mpaka mwaka 1975 ilikuwa wazi kwa watunga sera kwamba maendeleo yote ya ndani na nje ya nchi ambayo msingi wake ulijikita katika utaifishwaji wa njia kuu za uchumi hayatoi suluhisho bora juu ya mustkabali wa maendeleo ya nchi wala njia sahihi za kujenga uchumi imara , ulio bora na unaojitegemea. Baadhi ya wachambuzi na watafiti wanatanabaisha kwamba suala la utaifishwaji wa njia kuu za uchumi umezaa kundi Fulani la watu ambao wanatumia mtaji wa serikali na wananchi wake kwa namna na uelekeo ambao ni wa kibepari. (Shivji 1974, 85-90).

Ni miaka 12 sasa baada ya mwalimu kututoka na hali inajidhihirisha wazi kwamba tabaka lile ambalo lilitokana ama na matunda ya sera ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi mara baada ya kubinafsishwa kwa njia kuu hizo wamegeuka na kuwa mabepari na matajiri wa kutisha. Wale ambao walikuwa wakituimbia nyimbo za ujamaa na wale ambao walikuwa wanajifanya wakisema “zidumu fikra za mwenyekiti wa CCM” Na ndio maana ukiuliza unaambiwa “una wivu wa kike” ama “ Songombingo” na maneno kama hayo.

Ni ndani ya CCM ambako kuna uozo mwingi na asilimia kubwa ya walio ndani yake walimsaliti mwalimu kwa kutofanya na kusimamia misingi iliyowekwa. Tujiulize ikiwa CCM imeshindwa kusimamia mashirika yake tu kwa mfano SUKITA na mengineyo itaweza kuisimamia serikali ipi katika kuelekea miaka 50 ya uhuru wa nchi? Matokeo yake baadhi ya viongozi ndani ya chama hicho wamemgeuza mwalimu kama mtaji wao wa kisiasa katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

SERA YA UJAMAA VIJIJINI

Dhamira kubwa ya ujamaa vijijini ililenga katika maendeleo vijijini, upatikanaji wa huduma za kijamii pamoja na dhamira ya kujitegemea. Kilimo kilikuwa ndio uti wa mgongo na mbadala wa utegemezi wa mitaji ya fedha za nje ililenga kubeba dhana ya uwekezaji katika elimu iliyoambatana na mitazamo ya kisiasa iliyolenga maendeleo vijijini. Kuwepo kwa vijiji vya ujamaa. Kimsingi kujenga mtazamo wa kwamba maendeleo hayapo mjini isipokuwa vijijini. Binafsi nakumbuka wimbo maarufu miaka hiyo wa “GEZAULOLE” ama kipindi maalum katika RTD miaka hiyo uliokuwa na kiashiria cha wimbo wa “Vijiji vya ujamaaa sote tunajitegemea….Mwalimu kasema tujenge vijiji vya Ujamaa……. ndipo tutakapo jiendeleza…(kibwagizo).Siasa ya Ujamaa ndio lengo letu Watanzania sote tuwe pamoja “tungo za nyimbo hizi zilihamasisha watu waende vijijini wakajiendeleze na kilimo. Wakati sera ya utaifishwaji wa njia kuu za uchumi ulijikita katika sekta ya viwanda na sekta za kifedha, suala la maendeleo vijijini ndilo lililokuwa lengo kuu la ujamaa. Kulingana na sera ya Ujamaa Vijijini. Lengo kuu la kuanzisha vijiji vya ujamaa lilikuwa ni kuleta mabadiliko katika jamii ya vijijini na kujenga uchumi imara utakaoishirikisha jamii ambao kwao wananchi wote kwa rika zote wataishi pamoja kwa furaha na kufaidi matunda yake.(Nyerere,1968:337). Sera ya ujamaa vijijini ilijikita katika maendeleo vijijini ambapo watu wataishi pamoja , watazalisha pamoja na kuwa na ushirika wa pamoja na kuweza kupata huduma muhimu za kijamii kuliko kuishi kwa mbalimbali. Dhana ya “Umoja ni nguvu..utengano ni udhaifu na kidole kimoja hakivunji chawa “ zimejikita hapa. Mashamba pamoja na uzalishaji vilikuwa ndani ya vikundi vya ushirika badala ya mtu mmoja mmoja. Mwalimu alihalalisha sera ya Vijiji vy a ujamaa kulingana na utamaduni na mila za Kiafrika za ujima na usawa.

Pamoja na mafanikio hayo ya mwanzo na mapokeleo yake kutoka kwa wananchi, sera ya ujamaa vijijini ilikumbana na vikwazo na changamoto nyingi. Hii ilitokana na watu kutokubaliana na sera hii ya Ujamaa vijijini na kutokutoa ushirikiano wa kwenda kuanzisha vijiji vipya vya Ujamaa hasa kwa vijana wale waliotimiza umri wa miaka 18. Hii ilitokana na kupanda kwa gharama ya vifaa vya kilimo pamoja na pembejeo ambazo serikali iliwajibika kuvitoa kwa vijiji vya ujamaa. Matokeo yake ushawishi wa kutumia nguvu kuwafanya watu waende katika vijiji vya ujamaa ilikuwa ikitumika. Njia ambayo serikali ilikuja kuilaumu na kuahidi kutoitumia tena. Kwa mfano mnamo mwaka wa 1970 mwanzoni mwa “OPERESHENI RUFIJI” lengo kuu lilikuwa ni kuwaondoa wananchi waliopo pembezoni mwa kingo na bonde la mtu Rufiji kwenda katika maeneo ya ukanda wa juu na kwenda kuanzisha vijiji huko. Na serikali iliazimia kutumia nguvu endapo ingelazimu. Kulikuwa na “OPERESHENI DODOMA” ambayo iliazimia kuwaondoa wananchi wote mijini na kuwapeleka vijijini ambako serikali ilikuwa imeandaa vijiji maalum(Coulson,1975:55). Mwaka 1972 Operesheni kadha wa kadha zilianzishwa zikiwa na malengo hayo hayo mfano Kigoma na Chunya lakini matokeo wake wananchi wazawa hawakutoa ushirikiano wa kutosha wakihofia kupokonywa ardhi yao na wageni. Mwishoni mwa mwaka 1973 baada ya operesheni nyingi pamoja na matumizi ya kijeshi hatimaye Mwalimu aliipitia upya sera ya Ujamaa vijijini kulingana na hali halisi na kuweka msimamo wa kuwa mtu aweze kuishi katika kijiji cha Ujamaa walau kwa miaka mitatu. Hata katika kipindi hiki ilijulikana wazi kabisa kwamba sera ya vijiji vya Ujamaa imefeli na mpaka mwaka 1975 ikawa imewekwa kando.

Suala la kutokufanikiwa kwa sera ya vijiji vya Ujamaa limekuwa na maelezo tofauti kulingana na watafiti tofauti. Mojawapo ilikuwa ni hatua za mwanzo za utafiti juu ya usimamizi na uendeshaji wa zoezi zima la Sera ya Ujamaa Vijijini lilivyokuwa ambalo lilifanywa na kundi la watafiti waliobobea wa CHUO KIKUU CHA DAR ES SALAAM (Proctor, 1975) Mwingine alikuwa ni Goran Hyden aliyegusia zaidi katika kudorora kwa maendeleo ya kilimo pamoja na kilimo cha mkono (Hyden, 1980). Katika tafiti hizo wachambuzi wametoa sababu kuu tatu za kushindwa kwake.

Mosi Suala la kuanzishwa kwa vijiji vya Ujamaa halikuanzia chini. Yaani suala la vijiji vya ujamaa halikuanzishwa na wakulima isipokuwa ilikuwa ni wazo liliilotoka juu na hivyo liliikosa hamasa na msukumo kwa wakulima toka lilipoanza kufanyiwa kazi. Dhana hasi , mtazamo tofauti na sintofahamu ya wananchi kutokana na kuamininiana na kusababisha upinzani mkali. (Lofchie, 1978: 452)

Pili matumizi ya nguvu za kijeshi kwa wananchi kuhakikisha sera ya ujamaa vijijini inafanikiwa kwa kuhusisha kuwasafirisha wananchi kwa nguvu/kimabavu pamoja na vifungo vya muda mfupi vilivyotokana na malimbikizo ya kodi za maendeleo kwa mwananchi vilisababisha sera ya Ujamaa vijijini kutofanikiwa

Tatu , jitihada za kujenga vijiji vya Ujamaa zilikwamishwa na urasimu wa viongozi ambao waliyatumia madaraka yao vibaya hususan katika suala la ruzuku iliyokuwa inatolewa na serikali katika uanzishwaji wa vijiji vya ujamaa kutowafikia walengwa. Kama ingekuwa ni miaka hii ya leo tungeita “UFISADI WA VIONGOZI WA UMMA”. Wakulima walichukulia ruzuku wanayopewa na serikali kama mbadala wa kazi wanazofanya katika vijiji vya ujamaa mwanya uliotengenezwa na viongozi wa serikali. Na hili likapelekea wao kujiona kama bidhaa ya bure inayotumiwa na watawala kujinufaisha. Hali hii ilipelekea asilimia kubwa ya wakulima kuwa tegemezi serikalini badala ya kujitegemea kama mpango ulivyokuwa umepangwa awali.

Pengine picha mbaya ambayo ilikuja kujionesha kama vile ambavyo watafiti Issa Shivji (1974) na Raikes (1975) wanavyotanabaisha ni kuwapo kwa kundi la wakulima tajiri ambao wanatumia mwanya huo kuwarubuni watendaji wa vijiji na kuanza kuwatumia wanavijiji kwa maslahi yao binafsi na kundi hili walilita kama “Kulak Ujamaa”

Sera ya Ujamaa vijijini haikuweza kutoa majawabu ya msingi ya kumkomboa kiuchumi mkulima matokeo yake ni kuzaliwa kwa mtandao mpya tegemezi ambao unawafanya wakulima wanakuwa wazalishaji wakuu wa mazao ya chakula pamoja na mazao mengine na kuyasafirisha huku mlaji, mwamuzi mkuu wa bei na anayebuni sera akiwa ni mtu wa mjini. Mfumo huu wa unyonyaji ulirithiwa toka enzi za ukoloni na kwa sasa uchumi umekua huria umeota mizizi na kukomaa. Matokeo yake inajengeka dhana ya maendeleo na vitu vizuri vinatoka mjini ilihali mzalishaji mkuu anatokea kijijini

HITIMISHO

Kwa kuhitimisha naweza kusema Mwalimu aliweza kufanikiwa kwa kiasi kikubwa sana katika kusimamia uchumi wa serikali/nchi wakati wa Ujamaa kwa kuzingatia maslahi ya jamii kama vile huduma za jamii kutolewa bure kama vile matibabu, elimu n.k Leo hii Marekani twasikia kwamba Obama anataka kupitisha sera itakayowapa unafuu wananchi wake kupata matibabu nafuu hicho ni kiashiria tosha kwamba Mwalimu alikuwa anatupeleka katika uelekeo sahihi. Nchi isiyokuwa na migogoro iliyotokana na ukabila, udini ama rangi watu kuishi kwa amani upendo na utulivu pamoja na mshikamano wa kitaifa yote hayo ni matunda ya Mwalimu (Legum na Mmari, eds,1995;Pratt, 1999; Ishemo,2000)

Wako ambao wanamwona Mwalimu kama dikteta lakini mwalimu alilenga kujenga mifumo imara itakayoshirikisha wananchi wote katika njia kuu za uchumi , katika siasa na katika jamii kuanzia siku za mwazo wa uhuru wa nchi na mpaka katika kipindi cha mfumo wa vyama vingi. Swali ni je nchi wakati inatimiza miaka 50 ya uhuru na tokea mfumo wa vyama vingi uanze kuna mafanikio yoyote zaidi ya yale ya kumdanganya motto mdogo peremende kwa mabango makubwa ya kampuni za simu na makampuni ya pombe na matangazo ya kondomu ama mabadiliko katika umiliki wa mifumo ya kiteknolojia, umiiliki wa njia kuu za kiuchumi mikononi mwa wananchi, Utawala bora, huduma bora za jamii, serikali makini inayowajbika kwa wananchi wake, elimu bora kwa wote, fursa sawa kwa wote ama ni wimbo wa kisiasa majukwaani? SWALI LIKO KWAKO MWANANCHI.Mwalimu tutakuenzi na sera na utu wako vitarindima katika mioyo yetu daima. Na hao wenye dhamana wakuonapo na kuisikia sauti yako mioyo yao itapasuka kwa woga huku dhamira zao zikiwasuta.

No comments: