Wednesday, October 19, 2011

KUELEKEA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKA -4

Mohamed Said


Sasa inasemekana wakizaliwa watoto Wajerumani ndiyo walikuwa wakitoa majina kwa watoto hao na majina waliyowapa ni ya Kijerumani ndiyo kukawa na Kleist, Thomas, Schneider, Mashado na mengineyo. Lakini wakiondoka tu palepale baba zao wakawa wanatoa majina ya Kiislam kwa kuwa wao walikuwa Waislam hawakupenda sana watoto wao wajulikane kwa majina ya Kikristo. Kwa mfano Kleist jina lake ni Abdallah, Shneider jina lake ni Abdillah na Mashado jina lake ni Ramadhani. Hadi leo kwenye kaburi la Kleist pale Makaburi ya Kisutu jina lake limeandikwa: “Kleist Abdallah Sykes.” Haieleweki kwa nini yeye hakupenda kujinasibu na jina lake la asili “Mbuwane” au “Abdallah” na kwa nini watoto wa Plantan kwa jina lao la asili la “Mohosh” ambae huko kwao Kwalikunyi Mozambique alikuwa chifu wa Kizulu. Sasa zaidi ya miaka mia moja ukoo wa Sykes umevuma na kujulikana katika siasa na biashara kwa jina hilo la Kijerumani na hadi leo ukoo wa Plantan ambao uko Mission Quarter, Mtaa wa Masasi ni katika koo maarufu sana Dar es Salaam nao wanajulikana kama akina Plantan.

Kleist alisoma shule ya Kijerumani na shule yenyewe ndiyo hii sasa Ocean Road Hospital. Alisoma hadi darasa la sita na alipomaliza shule hapo alikuwa anasema Kijerumani, anajua short hand (hati mkato) na kupiga taipu. Huu ulikuwa ujuzi mkubwa sana kwa Mwafrika kuwa nao wakati ule. Lakini alipomaliza shule Wajerumani hawakumwacha afanye kazi ofisini walimtia katika jeshi na Vita Vya Kwanza vilipoanza mwaka 1914 Kleist na ndugu yake Scheneider Plantan walijikuta wakielekea Tanga kupambana na majeshi ya Kiingereza. Mkuu wa majeshi ya Kijerumani alikuwa Von Lettow Voberk na Kleist ndiye alikuwa Aide De Camp wake. Cheo kizito sana wakati ule kwa Mwafrika kukibeba. Baada ya vita na kushindwa kwa Wajerumani baadhi ya askari wa Kizulu walikimbia na kamanda wao Vorbeck na kuingia Mozambique. Wazulu waliobaki Tanganyika walikuwa wamepwelewa.

Kleist alikuwa mateka wa vita na alipoachiwa alianza kujifunza Kiingereza na hakutaka tena kujiunga na jeshi. Habari za Kleist ni nyingi sana na mengi katika maisha yake aliandika kwa mkono wake mwenyewe. Mwaka 1969 mjukuu wake, Daisy Sykes Buruku kwa msaada wa msaada wa baba yake, Abdulwahid Sykes na akiwa chini ya Profesa John Illife wa Chuo Kikuu Cha Cambridge wakati ule, Iliffe akisomesha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam na Disy akiwa mwanafunzi wake alikujakuandika upya maisha ya babu yake “Kleist Sykes The Townsman” katika kitabu “Modern Tanzanians” kilichohaririwa na John Illife. Katika kitabu hicho Kleist anatoka kama mwanasiasa makini na muasisi wa harakati za kudai uhuru wa Tanganyika. Kleist alifanya mengi Dar es Salaam, alijenga shule Al JAmiatul Muslim School, jengo la TAA ambamo TANU ilikuja asisiwa mwaka 1954, alikuwa katika baraza la Munispal Council, memba wa Dar es Salaam Maulid Committee, alikuwa kiongozi wa chama cha Wafanyakazi wa Relwe, alikuwa mfanya biashara mkubwa na mwanachama wa Chamber of Commerce Mwafrika pekee katika chamber.

Kleist aliwanunulia vyombo vya muziki wanae wakati huo vijana wadogo baada ya Abdulwahid na Ally kurudi vitani Burma mwaka 1945 walipokwenda kupigana kama askari katika KAR. Wanae pamoja na vijana wenzao wa mjini kama Matesa, Said Kastiko, Msikinya (huyu alikuwa ametokea Afrika ya Kusini), Dome Okochi Budohi na nduguye akiitwa Martin (hawa walikuwa wanatoka Kenya) wote hawa wakaanzisha bendi iliyojulikana kama “Skylarks.” Baadae walibadili jina na kujiita “The Blackbirds” Kleist mwenyewe akiwa patron wa bendi na akihudhuria maonyesho ya bendi hiyo. Kulikuwa na bendi kama hiyo siku zile Johannesburg ikiitwa “Skylarks.” Hili ni kundi ambalo Miriam Makeba wakati huo msichana mdogo alikuwa akiimba. Bendi hii ikaja tena baadae kubadili jina na kuitwa “Merry Makers.” Bendi hii ilipendwa sana na vijana wa mjini wa wakati ule hasa kwa kuwa wao walipiga ile mitindo ya Ulaya kama Waltz, Foxtrot, Quick Step nk. Bendi hii ikipiga nyimbo zilizokuwa maarufu wakati wa Vita Vya Pili Vya Dunia na maiaka ya 1950 mwanzoni si Tanganyika tu bali hata Ulaya na Marekani kama “More,” “Chacanuga Chouchou,” “Siboney,” “Siboney,” “Fly Me to The Moon,” “Perfidia” na nyinginezo, nyimbo ambazo zilipewa umaarufu na wanamuziki wakubwa wa Amerika na Uingereza kama Glenn Miller, Louis Armstrong, Charlie Parker, Benny Goodman, Andrew Sisters na wengineo.

Vijana hawa walikuwa wakipendwa sana hata Zanzibar ambako wakipiga Victoria Garden na kule mashabiki wao walikuwa akina Ahmed Rashad Ali (huyu alikujakuwa mtangazaji maarufu sana na mwanapropaganda mahiri katika Radio Afrika Huru kutoka Cairo wakati wa kupigania uhuru) nduguye Prince Sudi, Abdillah Masud maarufu kwa jina la “Smuts,” (huyu alikuwa vitani Burma pamoja na akina Sykes), Mkubwa Mohamed Mashangama maarufu kama “Bwana Mkubwa Shoto” (jina hili la “Shoto” alilipata kwa kuwa alikua mcheza mpira maarufu na akipiga mashuti makali kwa mguu wake wa kushoto), na jamaa wengi. Kleist alipenda kukaa meza ya pembeni pale Arnatuoglo Hall nadhifu katika suti yake akitingisha mguu sawa na midundo iliyokuwa ikiporomoshwa na watoto wake na rafiki zao, picha ya King George ikiwa inamkodolea macho kwa juu ilipokuwa imetundikwa katika ukumbi ule. Baada ya kifo cha King George, ikatundikwa picha ya Queen Elizabeth ambayo hata sisi tuliikuta pale Arnautoglo katika miaka ya 1950 mwishoni. Hebu tusimame kidogo hapa.

Vijana hawa walipotoka utotoni na kuwa watu wazima na wakaanza siasa misingi hii waiyoijenga katika urafiki wao wa utotoni uliwasaidia sana katika harakati. Aman Thani mmoja wa viogozi wa Hizbu au (Zanzibar Nationalist Party) anasema ilikuwa Abdulwahid Sykes na Dossa Aziz ndiyo walikuja na Nyerere Zanzibar kumjulisha kwa Karume. Historia bado haijaweka wazi mchango wa hawa watu watatu katika kuundwa kwa Afro-Shirazi Party lakini Issa Nassoro Ismaily amepata kusema kuwa Abdulwahid alipata kumweleza masikitiko yake kwa yale yalipotokea Zanzibar baada ya mapinduzi na akasema kuwa hapendi yeye kuzungumza suala lile kwa kuwa anahisi litavunja udugu baina yao. Halikadhalika Ali Mwinyi Tambwe hakupenda kabisa anasibishwe na mapinduzi yaliyotokea Zanzibar lau kama yeye alikuwa mmoja wa watu wa ndani katika kupanga mipango ile. Tuendelee.

Leo hii ukiangalia picha za wakati ule za bendi hii jinsi walivyokuwa wamevaa suti zao na “bow - tie” na ukiangalia zile ala za muziki pamoja na piano unaweza ukakosea ukadhani hiyo ni bendi ya Count Bessy, Louis Armstrong au Charlie Parker wa Marekani. (Kipindi hiki kiliibua vipaji, Hamza Aziz, mtoto wa Aziz Ally mmoja wa matajiri wakubwa Waafrika Dar es Salaam na rafiki wa Kleist alikuwa akiimba nyimbo za Nat King Cole na yeye mwenyewe alikuwa akijiita Nat Nat King Cole). Harakati za kudai uhuru zilipoanza mwaka 1954 Hamza Aziz alikuwa katika jeshi la polisi la kikoloni na kaka yake Dossa Aziz alikuwa mstari wa mbele na Nyerere katika TANU. Inasemekana TANU wakimtumia sana Hamza kupata siri za wakoloni. Sasa njoo angalia picha za mama zetu na mitindo ya nywele na magauni waliyovaa na mikanda mipana mithili ya wanawake wa Kizungu. Hapo wapo Arnatouglo Hall wakicheza mziki wa The Skylarks. Mama zetu waliokuwa ehe kidogo walikuwa wanavaa na glovu nyeupe kama wanawake waKizungu.

Nikiwa mtoto mdogo sana nina kumbukumbu ya party moja nyumbani kwetu Kipata Street na nyimbo ambazo zikipendwa sana wakati ule zilikuwa za Septet Habanero kutoka Cuba. Katika waliohudhuria party ile nina kumbukumbu ya Dome Okochi Budohi aliyekuja kuwa mmoja wa wanachama wa mwanzo wa TANU na mtu aliyekuwa inasemekana kiungo kati ya TAA na KAU ya Jomo Kenyatta. Okochi Budohi kadi yake ya tano ni nambari sita. Budohi na mwanachama mwingine wa TANU Patrick Aoko walikamatwa mara tu hali ya hatari ilipotangazwa Kenya baada ya mapambano kati ya Wakikuyu na Waingereza kupamba moto. Msako huu na kamata kamata ilokwenda pamojanayo ilipewa jina “Operation Anvil” na Waingereza. Kundi zima la viongozi wa Kenya kama Kenyatta, Bildad Kaggia, Paul Ngei, Kungu Karumba na wengine waliwekwa kizuizini sehemu moja Kenya ijulikanayo kama Manyati. Wakenya hawa wanachama wa TANU walitiwa mbaroni na kurudishwa Kenya chini ya ulinzi mkali wakiwa wamefungwa minyororo. Leo hii hakuna anaejua kuwa TANU ilikuwa na wanachama na viongozi Wakenya ndani yake toka enzi za TAA. Dome Budohi licha ya kuwa alikuwa mmoja katika vijana wa Skylarks vilevile alicheza senema na Kawawa iitwayo “Mgeni Mwema.”

Turejee kwa Kleist. Hapakuwa na mfano wa Kleist katika mji wa Dar es Salaam. Kleist alikuwa na kinyozi wake tena Muhindi akija mnyoa ndevu na nywele nyumbani. Kleist alikuwa anakwenda kazini kwa baskeli kitu nadra katika miaka ile na aliwanunulia wanae baskeli ndogo za kupanda kitu ambacho Mwafrika wa kawaida hakumudu. Kleist akiwashangaza wengi kwani alikuwa akila juu ya meza na wanae. Utamaduni wa wakati ule ulikuwa watu kula chini juu ya mkeka au jamvi. Wenzake wakimuona Kleist akiishi kama Mzungu. Vilevile wakati wote yeye alikuwa kavaa suti, hata anapokwenda msikiti kwake kusali pale Kipata. Msikiti huu upo hadi leo. Nyumba aliyoacha Kleist sasa haipo na mtoto wake, Ally Sykes amejenga nyumba ya gorofa tano pale. Nyumba hii ndimo alimozaliwa Ally na Abbas na ina historia kubwa kabisa kama ilivyokuwa historia za maisha ya wanae katika historia ya TANU na kudai uhuru wa Tanganyika.

Hatuwezi kuelezana yote hapa.

ITAENDELEA...

No comments: