Friday, October 14, 2011

KUELEKEA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKA -3

Tumkumbuke Marehemu Mzee Kiyate Mshume


Dalali wa Samaki Kariakoo na Mfadhili wa TANU na NyerereMohamed Said

Napenda nieleze kisa hiki cha kusisimua cha marehemu Mshume Kiyate kama nilivyoelezwa na mzee wangu Ahmed Rashad Ali, kisa ambacho yeye alihadithiwa na Mwalimu Julius Nyerere kwa kinywa chake mwenyewe. Ahmed Rashad anasema siku aliyosikia kisa hiki yeye alikuwa pamoja na Dossa Aziz na Lucy Lameck. Ilikuwa mwaka wa 1965 siku ile mlowezi Ian Smith alipojitangazia uhuru kutoka kwa Waingereza.

Ahmed Rashad wakati ule alikuwa Katibu Mkuu Msaidizi Idara ya Habari na alikwenda nyumbani kwa Mwalimu Msasani ili apate kauli ya Mwalimu Nyerere na msimamo wa serikali kuhusu mgogoro wa Rhodesia. Walimkuta Mwalimu Nyerere nyumbani kwake katika maktaba yake anaandika. Ahmed Rashad anasema Nyerere aliwaeleza kuwa katika kutafakari mambo yaliyokuwa yakiendelea Rhodesia, Uingereza haitofanya lolote dhidi ya Ian Smith kwa kujitangazia uhuru wa maguvu. Ahmed Rashad alinieleza kuwa Mwalimu Nyerere alisema, “Hawa ni mtu na mjomba wake,” akikusudia kuwa Waingereza na walowezi wa Rhodesia walikuwa ndugu wa damu kwa hiyo Waingereza hawatatia jeshi pale kuwang’oa walowezi.

Baada ya Mwalimu Nyerere kumaliza kutoa msimamo wake wakawa sasa wamekaa wanapiga gumzo huku wakinywa vinywaji na Mwalimu alikuwa mtu hodari sana wa kustawisha baraza. Waliokuwa karibu na Nyerere wanamjua kwa sifa hii. Mwalimu Nyerere alianza kuhadithia kisa chake na Mshume Kiyate. Haifahamiki hasa ni lini Nyerere alijuana na Mzee Mshume lakini huenda ilikuwa hata kabla ya kuaisiswa kwa TANU siku zile za TAA Nyerere alipokuwa nakwenda ofisini kwa Abdulwahid Sykes pale Kariakoo sokoni ambako Abdulwahid alikuwa Market Master.

Mzee Mshume alikuwa ndiye dalali wa samaki soko la Kariakoo na alikuwa mzee aliyeheshimika sana mjini Dar es Salaam na baadae alikuja kuwa mmoja wa wazee katika Baraza la Wazee wa TANU. Nyerere alianza kukihadithia kisa chake na Mzee Mshume kwa kusema kuwa siku moja wakati wa kudai uhuru alikuwa anatoka nyumbani kwake Magomeni Majumba Sita kwa miguu kuelekea Kariakoo ili kupata mahitaji yake lakini katika safari hiyo mfukoni mwake alikuwa hana hata senti moja. Akiwa njiani karibu na sehemu inayoitwa Mwembe Togwa (hapa kwa leo ni pale Fire makutano na Morogoro Road na Barabara ya Umoja wa Mataifa)Mwalimu alikutana na Mzee Mshume Kiyate. Mwalimu Julius Nyerere akamfahamisha Mzee Mshume kuwa alikuwa anakwenda sokoni Kariakoo lakini hana fedha za kununulia mahitaji yake. Mzee Mshume Kiyate aliingiza mkono katika koti lake akatoa shilingi mia mbili na kumpa Nyerere. Ukitaka kujua thamani ya fedha hiyo kwa wakati ule, naitoshe kujua kwamba ilimgharimu mtu shilingi mia tano tu kujenga nyumba ya vyumba sita katika eneo la Kariakoo.

Mzee Mshume alifadhaishwa sana na hali ile ya Nyerere kuwa anahangaika na kuikimu familia yake na huku wamemtwisha mzigo wa kuendesha TANU. Kutokana na hali hii Mzee Mshume aliona itakuwa ni kumtaabisha Nyerere bila sababu ikiwa atakuwa anashughulika na kuwatafutia wanawe chakula na wakati huohuo akiwa na jukumu la kufanya kazi za TANU. Hapo ndipo Mzee Mshume alipojitolea kuihudumia nyumba ya Mwalimu Julius Nyerere. Kila asubuhi Landrover ya TANU inapiga breki Karikaoo sokoni pale na Mzee Mshume ananunua mahitaji yote ya siku anamkabidhi dreva wa TANU jina lake Said lakini watu wakampachika jina wakimwita TANU. Said TANU anachukua vitu vile anapeleka vile Magomeni Majumba Sita kwa Mama Maria. Mzee Mshume alifanya hivyo hadi uhuru ulipopatikana. Baada ya uhuru Mwalimu Nyerere sasa akiwa Waziri Mkuu alimwomba Mzee Mshume aache kumnunulia chakula lakini Mze Mshume alikataa na badala yake akamtafadhalisha Mwalimu Nyerere aendelee kupokea chakula chake na kile ambacho kinatolewa na serikali kwake yeye, kama mkuu wa nchi alimuomba Mwalimu awakirimu wageni wake. Mwalimu Julius Nyerere alikiita kisa hiki ‘the TANU spirit’ – yaani moyo wa TANU akieleza mapenzi na moyo waliokuwanao wana TANU wakati ule wa kudai uhuru.

Kisa hiki kwa mara ya kwanza kabisa kilihadithiwa hadharani na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kwa wakati ule marehemu Ditopile Mzuzuri Mkiwaona kada wa Chama Cha Mapinduzi. Ditopile alikieleza kisa hiki kama alivyokieleza Mwalimu Nyerere kwa Ahmed Rashad na Lucy Lameck kwa nia ya kuonyesha moyo wa TANU na mchango wa wazalendo katika kupigania uhuru wa Tanganyika. Kisa hiki kwa Dossa hakikuwa kipya. Dossa akimjua Nyerere nje ndani. Kwa bahati mbaya waandishi wa magazeti wakapotosha kisa kizima. Badala ya kutoa umuhimu kwa moyo wa ukarimu wa Mzee Mshume na kumueleza kama mzalendo aliyejitolea katika kupigania uhuru, magazeti yakageuza maneno ya Ditopile kuwa masimango dhidi ya Mwalimu Nyerere. Kwa ajili hii nafasi ambayo ingeliweza kutumiwa ili kueleza umuhimu wa Mzee Mshume na historia ya TANU ikapotezwa.

Tuendelee na Mzee Mshume na Mwalimu Nyerere. Tarehe 20 Januari 1964 wanajeshi waliasi ikabidi Nyerere aombe msaada kwa Waingereza waje kuwanyang’nya silaha askari. Baada ya uasi ule kuzimwa na jeshi la Kiingereza, TANU ilifanya mkutano mkubwa sana katika Viwanja vya Jangwani Dar es Salaam. Mzee Mshume kwa niaba ya wazee wa TANU alipanda jukwaani na kumvisha Nyerere kilemba kama ishara ya kumuunga mkono. Hakuna picha alioyopiga Nyerere kati ya mwaka 1955 na 1961 ambayo Mzee Mshume asiweko ndani yake. Mzee Mshume alikuwa mstari wa mbele katika harakati za uhuru na kumuunga mkono Nyerere kwa kila jambo kwa hali mali. Picha ya Mzee Mshume akimvisha Nyerere kilemba ilichapishwa katika magazeti mengi. Halikadhalika picha nyingine mashuhuri ya Mzee Mshume na Mwalimu Nyerere ni ile iliyopigwa Novemba 1962 wakati wa Uchaguzi Mkuu.Picha hiyo inamuonyesha Mzee Mshume akiwa amevaa koti, kanzu na kofia na huku amemshika Mwalimu Nyerere mkono akimsindikiza kupiga kura. Magazeti ya Chama na Serikali Uhuru na Daily News yamekuwa yakiitumia picha hii kila baada ya miaka mitano katika uchaguzi wa rais kama njia ya kuwahamasisha watu kupiga kura na kumchagua Mwalimu Julius Nyerere. Kwa bahati mbaya picha ile siku zote hutoka bila maelezo na kwa hiyo wengi hawafahamu yule mzee aliyefuatana na Mwalimu Julius Nyerere ni nani. Kadhalika si wengi wanaoufahamu mchango wa Mzee Mshume Kiyate katika kupigania uhuru wa Tanganyika kwa sababu Mwaka 1995 Jiji lilipoamua kubadilisha jina la mtaa aliokuwa akiishi Mshume Kiyate – yaani Mtaa wa Tandamti ili uitwe Mtaa wa Mshume Kiyate kama ishara ya kumuenzi na kuthamini mchango wake katika kupinga ukoloni, baadhi ya magazeti yalipinga kitendo hicho na hadi leo mtaa ule haujawekewa kibao kilicho na jina la Mshume Kiyate.

Hofu iliyotanda katika vyombo vya habari na kwa wengi wasiojua historia ya kupigania uhuru wa Tanganyika ilikuwa mbona majina ya mitaa yote yanapewa majina ya Waislamu? Lakini kubwa zaidi la kushangaza sana ni kuwa hata pale magazeti yalipokuwa yameingia katika malumbano ya kupinga majina yale mapya ya wazalendo katika mitaa kama vile Kleist Sykes, Max Mbwana, Mshume Kiyate, Tatu Bint Mzee, Omari Londo nk. Mwalimu Nyerere ambaye yeye ndiye akiwajua vyema mashujaa hawa alikuwa kimya. Katika mahojiano aliyofanyiwa Meya wa Dar es Salaam, Kitwana Selemani Kondo na Serah Dumba wa Radio Tanzania kuhusu mabadiliko ya majina ya mitaa, Mzee Kondo alisema hao wanaosema hawawajui hao walioenziwa kwa kupewa majina yao kupewa mitaa waulize watu hao walikuwa nani wataelezwa.

Mzee Mshume amekufa pweke Hospitali ya Muhimbili na katika maziko yake hawakuonekana wale waliokuja faidi matunda ya uhuru. Akiwa kitandani mgonjwa pale hospitali alisikika mara kadhaa akimwambia mwanae akiitwa Kiyate, ”Kiyate umewapa taarifa wenzangu (anawataja majina) kuwa mimi nimelazwa?” Mazishi ya Mzee Mshume yalifanyika mtaa wa Matumbi kwenye nyumba ya Sheikh Maguno aliyekuwa ndugu yake. Sheikh maguno ndiye alikuwa muadhini wa msikiti wa Shadhly kwa miaka 35. Mazishi ya Mshume Kiyate yalikuwa ya kawaida sana na wala hapakuwa na hotuba wala rambirambi. Kwa miaka mingi Mzee Mshume alipumzika kaburini kwake kwa amani hadi pale alipoenziwa na Kitwana Kondo kwa jina lake kupewa mtaa.


Itaendelea....

MWANANCHI

No comments: