Thursday, October 13, 2011

KUELEKEA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKA -2Na Mohamed Said

Baada ya vita ya pili ya dunia vijana askari waliokuwa katika King’s Africa Rifles (KAR) 6th Batallion waliopigana Burma katika wengi wao wakiwa Dar es Salaam walianza kuwachachafya viongozi wazee waliokuwa wakiongoza TAA. Rais wa TAA wakati ule alikuwa Mwalimu Thomas Plantan mtoto wa Afande Plantan mkubwa wa askari mamluki wa Kizulu aliokuja Tanganyika na Harmine von Wissman. Afendi Plantan alikuwa ndiye kiongozi wa askari wa Kizulu na mkubwa wa Wazulu wote pale mjini. Afendi Plantan hakutoroka na Harmine von Wissman kurudi kwao Mozambique baada ya Vita ya Kwanza kumalizika na jeshi la Wajerumani kushindwa wakaoroka kukimbilia Mozambique kupata hifadhi. Afande Plantan alibaki Dar es Salaam na kuweka makazi yake Mtaa wa Masasi Mission Quarter Mtoto wa Affendi Plantan Thomas, akijulikana kwa jina lingine la Sauti alipata elimu nzuri katika shule ya Kijerumani akawa mwalimu wa shule. Thomas Plantan alistawi hadi kufikia kushika uongozi wa African Association.

Sababu ya uongozi huu wa wazee kuchachafwa ni kuwa vijana walikuwa wakiona chama hakina malengo ya kudai uhuru wa Tanganyika. Kwa hakika chama kilikuwa kimezorota sana. Mikutano ilikuwa haiitishwi na chama kilikuwa hakina fedha za kuweza kujiendesha. Hapa ndipo tunakutana na kijana Abdulwahid Sykes, mtoto wa Kleist Sykes, (Mzulu mwingine) yeye na kundi la vijana wenzake, Dossa Aziz, Hamza Mwapachu, Stephen Mhando, Dr Vedasto Kyaruzi na wengineo wakawa wanatafuta njia za kuingia katika uongozi wa TAA ili wadai uhuru wa Tanganyika. Tatizo lililowakabili ikawa wazee hawataki kuachia hatamu za uongozi wala kuitisha mkutano wa uchaguzi.

Thomas Plantan alikuwa muwindaji na alitumia muda wake mwingi porini kuwinda, hakuwa na muda na siasa za mjini. Hata miaka mingi baada ya kifo chake, bado kuta za nyumba yake Masasi Street, Mission Quarter zilipambwa na vichwa vya pofu na mbogo aliowaua porini. Hata hivyo walikuwapo wazee ambao ingawa walikuwa watu wazima lakini walikuwa wanataka kuona mabadiliko katika TAA. Mmoja wa wazee hawa alikuwa Schneider Plantan, mdogo wake Thomas Plantan. Katika mkutano ulipoitishwa Arnautoglo Hall mwaka 1950, Schneider alifanya vurugu mbele ya maofisa wa kikoloni kiasi ilibidi wazee wakubali kuitisha mkutano wa uchaguzi, lakini kabla ya uchaguzi kufanyika Abdulwahid Sykes na Hamza Mwapachu walivamia ofisi za TAA pale New Street na kuchukua uongozi kwa nguvu wakaitisha mkutano wa uchaguzi na Dr Vedasto Kyaruzi akachaguliwa President na Abdulwahid Sykes Secretary. Hii ilikuwa mwaka 1950.

Inasemekana harakati za kupanga mipango ya kufanya mapinduzi katika TAA ilikuwa ikipangwa Ilala Welfare Centre ambako Hamza Mwapachu alikuwa akifanya kazi kama Welfare Officer, mahali pengine ilikuwa Kariakoo Market ambako Abdulwaihd alikuwa Market Master. Tuachie hapa, tutakuja kuyazungumza haya huko mbele. Turudi kwenye nyumba ya Mzee Mtamila turudi kwa Nyerere. Nyerere aliambiwa na mwajiri wake achague moja siasa au kazi. Nyerere alilileta tatizo hilo kwa Clement Mtamila, Mwenyekiti wa Kamati Kuu ya TANU. Mtamila aliitisha mkutano wa kamati kuu nyumbani kwake mtaa wa Kipata na TANU ilijadili tatizo hilo. Miongoni mwa wajumbe wa kamati ile mbali na Rupia walikuwa Bibi Titi Mohamed na Bibi Tatu bint Mzee. Kamati Kuu ya TANU ilimshauri Nyerere ajiuzulu. Tafarani hii ilitokea wiki chache tu baada ya Nyerere kurudi kutoka Umoja wa Mataifa katika wiki za mwisho za mwezi Machi. Tarehe 23 Machi, 1955 Nyerere alijiuzulu ualimu.

Ilikuwa adhuhuri Nyerere alipokuja Dar es Salaam kutoka Pugu, akiwa si mwalimu wa shule tena. Inasemekana aliposhuka tu kwenye basi alikwenda moja kwa moja ofisini kwa Abdulwahid Kariakoo Market. Nyerere alikaa na Abdulwahid katika nyumba yake namba Mtaa wa Stanley na Abbas Sykes ndiye aliyeambiwa na kaka yake atoke chumbani kwake ampishe Nyerere. Abbas wakati ule alikuwa kijana mdogo. Baadaye kidogo Nyerere alirudi kijijini kwake huko Musoma.

Mtamila. Nyumba hii leo haipo, ilipokuwa nyumba ya Mzee Mtamila kuna gorofa na si watu wengi wanofahamu historia iliyopata kubebwa na nyumba ile. Leo hakuna anaewajua watu hawa wala historia haiwataji lakini walifanya kazi kubwa sana. Clement Mtamila hatajwi, Tatu Biti Mzee hatajwi wala Iddi Faizi Mafongo ndiye aliyefanikisha ukusanyaji wa fedha za TANU ziliotumiwa kumpeleka Nyerere Umoja wa Mataifa, New York. Watu wachache sana wanajua kuwa Sheikh Iddi Faizi Mafongo alichota fedha katika hazina ya Aljamitul Islamiyya kutunisha mfuko wa TANU ili Nyerere aende Umoja wa Mataifa kudai uhuru wa Tangnayika. Hili la kuchota fedha za Al Jamiatul Islamiyya halikuwa na shida yoyote kwani katibu wake alikuwa Ali Mwinyi Tambwe mmoja wa watu wa mwanzo kujiunga na TANU.

Licha ya hilo Abdulwahid na Ally walikuwa na sauti katika jumuia hiyo kwa kuwa ilianzishwa na baba yao na walisoma Al Jamiatul Islamiyya Muslim School. Akina Tatu bint Mzee, Bi Asha Ngoma, Bi Hawa Maftah, Bi Titi Mohamed, Mwalimu Sakina Arab na wanawake wengine wa mjini ndiyo waliotia nyimbo za Lelemama katika kwaya ya TANU nyimbo ambazo zilihamasisha watu kupita maelezo. Kuna nyimbo moja ilikuwa inaimbwa hivi:

“Muheshiwa nakumpenda sana,
Wallahi sina mwinginewe,
Insha Allah Mungu yupo,
Tanganyika tutajitawala”
Hii ndiyo ilikuwa nyimbo ya mwanzo ya lelemama kutiwa katika harakati za kudai uhuru na baada ya hapo zikaja nyingine nyingi lakini maarufu na inayofahamiza zaidi ni “Hongera Mwanangu.” Mzee Mtamila ameacha hazina kubwa sana ya picha za siku za mwanzo za harakati za kudai uhuru zikionyesha wana TANU katika mikutano ya mwanzo Mnazi Mmoja. Picha hizi zilipigwa na Mzee Shebe Mohamed Awadh ambae studio yake ilikuwa Livingstone Street si mbali na nyumbani kwa Mzee Mtamila.

Baadhi ya picha zikimuonyesha Mzee Mtamila, Bibi Titi Mohamed, John Rupia wakiwa wamekaa katika jukwaa huku Mwalimu Nyerere akihutubia wananchi. Studio ya Shebe ilikuwa Livingstone Street kona na Kipata unaelekea Kiungani mkono wa kushoto kulikuwa na nyumba ambamo kulikuwa studio ya Mzee Shebe. Mzee Shebe ndiye alikuwa mpiga picha wa mwanzo wa TANU na Nyerere na ameacha hazina kubwa ya historia ya TANU na Nyerere katika picha. Ukitaka kuijua historia ya TANU na matokeo yote kuanzia 1954 hadi uhuru ulipopatikana mwaka 1961 pitia picha za Mzee Shebe ambazo hivi sasa hazina hii imehifadhiwa na watoto wake mjini Dar es Salaam.

Ukivuka Kipata mbele unakutana na Livingstone Street, ukitazama mkono wa kulia kabla ya kufika New Street labda nyumba tatu kabla pale ndipo ilipokuwa nyumba ya Kleist Sykes, Mtoto wa Sykes Mbuwane, askari wa Kizulu aliyekufamaji Mto Ruaha akiwa anarudi vitani baada ya kumshinda Mkwawa. Hii ilikuwa mwaka wa 1898. Kuna kisa kitatokea miaka 56 baadae kati ya kizazi cha Mtwa Mkwawa na Sykes Mbuwane. Wajukuu wao watakuwa wamoja katika TANU kupambana na ukoloni. Nitakieleza kisa hicho kwa ufupi. Mwaka 1954 fuvu la Mkwawa liliporudishwa Kalenga Adam Sapi Mkwawa mjukuu wa Mtwa Mkwawa aliwaalika Abdulwahid Sykes mjukuu wa Sykes Mbuwane, adui wa babu yake na Dossa Aziz kuja katika sherehe ya kupokea fuvu lile. Ilikuwa pale Kalenga ndipo Abdulwahid alipomuingiza Adam Sapi katika TANU kwa siri na kumfanya awe mmoja wa machifu wa mwanzo kabisa kuiunga mkono TANU.

Wakati Chifu Adam Sapi anajiunga na TANU chama kilikuwa hakijamaliza hata mwezi moja katika uhai wake. Tutazieleza habari za Abdulwahid Sykes na ushawishi mkubwa aliokuwa nao katika TAA na baadae TANUna katika wanasiasa wa wakati ule pamoja na machifu tutakapofika kusanifu makazi yake pale Stanley Street kona na Sikukuu Street. (Baada ya uhuru mtaa huu ulikuja ulibadilishwa jina na kuitwa Aggrey) Ila ieleweke tu kuwa kwa wakati ule wa siku za mwanzo za harakati kuanzia enzi za TAA baadhi ya machifu hawakuitazama TAA na baadae TANU kwa jicho zuri sana. Hofu kuu na ndiyo hofu aliyokuwanayo mshirika wao Muingereza katika ule mfumo “indirect rule” wa Lord Lugard ni kuwa TANU imekuja kuwanyang’anya madaraka yao.

Sasa turejee kwenye nyumba ya Kleist Sykes hapo Kipata. Kwa hakika Kleist alikuwa mtu wa mipango na mjengaji wa mikakati si tu katika maisha yake binafsi bali hata katika kupeleka mbele maslahi ya Waafrika katika Tanganyika. Kleist alizaliwa Pangani mwaka 1894. Akiwa na umri mdogo wa miaka 25 alikuwa keshaasisi African Association mwaka 1929 na kufikia mwaka 1933 aliasisi Al Jamiatul Islamiyya Fi Tanganyika, hicho ni Kiarabu (maana yake kwa Kiswahili ni “Umoja wa Waislam wa Tanganyika”). Mwaka wa 1924 Dr Aggrey alikuja Tanganyika kama mjumbe katika kamisheni moja ya elimu kuchunguza hali ya elimu kwa Waafrika wa Tanganyika. Kwa wakati ule Dr Aggrey alikuwa mfano wa Mwafrika aliyeelimika sana. Alipokuwa Dar es Salaam Dr Aggrey alikutana na Kleist na katika mazungumzo Dr Aggrey alimshauri Kleist kuwa endapo Waafrika wanataka kupiga hatua ni lazima waunde umoja wao. Ilimchukua Kleist miaka mitano hadi kuja kufanikisha ushauri ule na kuunda African Association akiwa katibu muasisi.

African Association na Al JAmitul Islamiyya ndivyo vilivyokuja kuwa chimbuko la kuundwa kwa TANU kwa kutoa viongozi kama Abdulwahid na Ally Sykes, Ally Mwinyi Tambwe, Iddi Faizi Mafongo, Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Abdalla Iddi Chaurembo, Sheikh Suleiman Takadir na wengineo na wanachama wake wa mwanzo. Kleist alilelewa nyumba moja na Thomas, Schneider na Mashado Plantan baada ya kifo cha baba yake. Hapa ningependa kidogo kuwaeleza wasomaji asili ya majina haya ya Kikristo na yenye asili ya Kijerumani. Hawa watoto baba zao walikuwa askari katika jeshi la Wajerumani. Wajerumani baada ya kuituliza Tanganyika kwa mtutu wakaliita lile jeshi lao la mamluki wa Kinubi na Wazulu “Germany Constabulary.” Mkubwa wa jeshi hili alikuwa Afendi Plantan, baba yao Thomas, Schneider na Mashado.


Itaendelea...

MWANANCHI.

No comments: