Wednesday, October 12, 2011

KUELEKEA MIAKA 50 YA UHURU WA TANGANYIKANa Mohamed Said

Historia ya kudai uhuru wa Tanganyika bado haijaandikwa kwa ukamilifu wake sasa miaka 50 toka nchi ijitawale. Kwa kuwa haijaandikwa Tanganyika imebakia kuwa nchi isiyokuwa na mashujaa wake ukaichia shujaa mmoja Julius Kambarage Nyerere. Historia nzima ya TANU na juhudi za kuikomboa Tanganyika kutoka kwenye ukoloni unazunguka kwake yeye peke yake. Kuna uvumi kuwa waliokuwa madarakani wanaogopa historia hii kwa kuwa imejaa mchango wa Waislam na wana hofu kuwa endapo mashujaa hawa Waislam wataenziwa huenda hata mustakbali wa nchi ukabadilika. Katika hofu hii nchi imebakia katika kutojitambua na kuwatambua mashujaa walioikomboa Tanganyika kutoka makucha ya Waingereza. Viongozi wakubwa na wanachama wa mwanzo katika TANU walitoka Rufiji kasha wakafuatia wanachama wa mwanzo Dar es Salaam katika mitaa ya Gerezani na Kariakoo ikafuatia.

Naikumbuka Gerezani kama vile ilikuwa jana. Kuanzia mitaaa yake hadi nyumba zilizokuwapo pale pamoja na wakazi wake ambao kwangu mimi walikuwa baba, mama, shangazi zangu na wajomba ukiachilia watoto wa rika langu tuliokua tukicheza pamoja wengi wao wameshatangulia mbele ya haki wengine katika umri mdogo sana na wengine katika utu uzima. Lakini sote tulishuhudia harakati za kupigania uhuru wa Tanganyika na tukauona uhuru wenyewe sisi tukiwa kizazi cha mwisho kuzaliwa ndani ya minyororo ya ukoloni. Mitaa ya Gerazani takriban yote ilikuwa ni barabara za vumbi tupu lakini mchanga kama mchanga uliopo pwani. Ingawa hadi sasa hali ni kama ile iliyokuwa miaka ile mchanga hauonekani tena na mahali pale kuna udongo wa tope mvua zikinyesha kitu ambacho hakikuwapo hapa zamani.

Kwa sisi watoto ule mchanga kwetu ilikuwa afueni maana tuliweza kucheza tukakimbizana bila ya madhara ya kuumia sana endapo mmoja wetu ataanguka. Mchezo tuliokuwa tukiupenda sana ulikuwa mpira wenyewe tukiita”chandimu” na nyakati za usiku tukicheza mchezo wa kujificha. Mtaa wetu ulikuwa unaitwa Kipata Street. Jina hili wengi hawalijui asili yake lakini ni moja ya vijiji ambavyo “mvumbuzi” David Livingstone alivipitia katika safari zake Nyasaland.

Mtaa wa mbele ya Kipata ni mtaa maarufu wa Kitchwele Street sasa unaitwa Mtaa wa Uhuru. Hakuna ajuaye hili neno “Kitchwele” nini maana yake. Lakini mtaa huu umepata heshima kubwa kwa kubadilishwa jina na kuitwa “Uhuru” Tanganyika ilipojikomboa kutoka ukoloni wa Waingereza tarehe 9 Desemba 1961. Nyuma wa Kipata Street ulikuwa mtaa wa Kirk Street sasa unaitwa Mtaa wa Lindi. Asili ya jina la Kirk ni Consular John Kirk aliyekuwa akitazama maslahi ya Waingereza Zanzibar. Sasa wazee wetu walikuwa hawawezi kulitamka jina hilo kama litakiwavyo badala yake wakawa wanasema “Kiriki” jina lililodumu hadi mtaa ulipobadilishwa jina na kuitwa Mtaa wa Lindi. Nakimkumbuka kibao chake cha mtaa kiliandikwa kwa wino mweupe kwenye kibao cheusi “Kirk Street.” Nyuma ya Kirk Street ulikuwa mtaa wa Somali na nyuma ya Somali kulikuwa “Kiungani Street.” Asili ya jina hili ni Kiungani Zanzibar ambako Universities’ Mission to Central Africa (UMCA) ilijenga kanisa lake la kwanza pwani ya Afrika Mashariki katika miaka 1800.

Sasa tuingie katika mitaa ya kukatisha. New Street ndiyo ilikuwa inatengeanisha Gerezani na Uwanja wa Mnazi Mmoja, kisha inafuatia mtaa wa Livingstone, Sikukuu, Swahili, Nyamwezi, Congo na mwisho Msimbazi. Kisha kulikuwa na mitaa miwili midogo, Somali Kipande na Mbaruku. Kwa wakati ule kwa ajili ya udogo wangu ilikuwa shida sana kupambanua kuwa majina ya mitaa hiyo ya “Kipata,” “Kirk,” “Livingstone” na “Kiungani” ilikuwa ni kiashiria kuwa Tanganyika ilikuwa chini ya ukoloni wa Waingereza. Kwa Waingereza majina hayo yalikuwa yanawakumbusha mashujaa wao akina David Livingstone, Morton Stanley na ushawishi wao katika sehemu ambazo Waingereza walituma watu wao ama kuja “kuzivumbua” au kutawala. Juu ya hayo Gerezani ilijipambanua na mitaa mingine ya Dar es Salaam kwa kuwa na wapigania uhuru wengi waliokuja kutoa mchango mkubwa katika TANU. Lakini kwa bahati mbaya sana kwa hao wazalendo wote mchango wao haujathaminiwa wala hakuna leo mtu anaewafahamu au kuwakumbuka. Sasa hebu tuanze matembezi ya nyumba kwa nyumba kuzipitia nyumba walokuwa wakiishi wazalendo wapigania uhuru wa Tanganyika ili tuwakumbuke na tueleze yale waliyofanya wakati wa kupigania uhuru wa Tanganyika.

Tuanze Kipata Street inapoanza Gerezani. Kipata Street inaanzia kule Msimbazi.Pale kulikuwa na nyumba ya Abdallah Salum Matimbwa akifanya kazi Relwe. Nyumba yenyewe ya asili leo haipo. Mtoto wa MZee Abdallah Salum Matimbwa, Salum Matimbwa amejenga ghorofa. TANU ilipoanzishwa Abdallah Salum Matimbwa alikuwa mmoja wa wanachama wake wa mwanzo mwanzo lakini kwa kuwa wakati ule kudai uhuru lilikuwa jambo la hatari na yeye alikuwa mwajiriwa alijiunga TANU na kuwa mwanachama kwa siri. Halikadhalika alikuwa mwanachama wa Zaramo Union chama cha kikabila kikiendeshwa na Max Mbwana. Vyama hivi vya kikabila Waingereza wakivipenda sana kwa kuwa viliwasaidia katika ile njama yao wa “wabague uwatawale” Salum Matimbwa anaingia katika historia ya ukombozi wa Tanganyika si tu kama mwanachawa wa awali waliojiunga na TANU kabla ya 1958 bali kama mmoja wa wazalendo waliochanga fedha kuanzisha Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Fikrra ya kuanzisha Chuo Kikuu inasemekana ilianza na Nyerere akiwa na Dossa.

Ilkuwa kawaida ya Dossa baada ya mikutano ya TANU pale Mnazi Mmoja kumchukua Nyerere na gari lake kumrudisha Pugu. Njia ya zamani kwenda Pugu ilikuwa inapita hapo kilipo Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. Sasa ilikuwa kiza kimeingia na walitaka kutoka nje ya gari kuangalia mandhari ya Dar es Salaam maana kutokea pale mji ulikuwa unapendeza sana kwa taa zilizokuwa zikiwaka barabarani. Nyerere alimwambia Dossa, “Dossa tukipata uhuru wetu hapa lazima tujenge Chuo Kikuu.” Hili wazo lilifanyiwa kazi na wananchi wakahamasishwa kuchangia ujenzi wa Chuo hicho. Fedha zilichangwa na Chuo kikajengwa pale New Street kwenye kiwanja cha John Rupia alichokitoa kuwapa TANU. Hapo ndipo kilipoanza Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam. (Chuo hiki sasa ni Chuo Cha Watu Wazima).Abdallah Salum alikuwa mmoja wa wachangiaji wa chuo hicho na mwanae Salum Matimbwa hadi leo amehifadhi stakabadhi ya malipo y ash. 50.00 stakabadhi ambayo ina saini ya Joseph Nyerere. Wazee hawa walikuwa wazalendo wa kweli kabisa. Baada ya uhuru kupatikana mwaka wa 1961 na zilipokuwa zikianzishwa harakati za ushirika Abdallah Salum Matimbwa alitoa lori lake Commer Fargo DSY 435 kama mtaji kuingiza katika Coast Region Transport Company (CORETCO). Pamojanae katika kuanzisha CORETCO walikuwa wazee wengine kama Sharia Bofu na nduguye Ibrahim Bofu, Salum Kambi, Juma Mzee na wengineo.

Unateremka sasa Kipata unaelekea Mnazi Mmoja. Kipata kona na Congo kulikuwa na nyumba ya Ibrahim Hamisi mmoja wa waasisi wa African Association mwaka 1929. Huyu alikuwa Mnubi kutoka Darfur. Baba yake alikuwa askari wa Kinubi walokuja Tanganyika na Kamanda wa Kijerumani Harmine von Wissman kuja kuwasaidia Wajerumani katika vita yao dhidi ya wazalendo wa Tanganyika akina Bushiri bin Harith wa Pangani na Chifu Mkwawa kutoka Kalenga. Ibrahim Hamisi akifanya kazi Government Press kama “composer.” Wajerumani walikuwa wajanja na wepesi katika kulipa fadhila. Waliwasomesha vizuri sana watoto wa askari wao waliowaleta Tanganyika kuja kuwasaidia kutawala. Kwa njia hii waliweza kujenga tabaka la wageni lililokuwa juu kupita wenyeji wa Dar es Salaam, Wazaramo, Wamashomvi nk. Hali hii kwa kiasi Fulani ilileta migogoro baina Wamanyema, Wazulu na Wanubi kwa upande mmoja ambao walionekana kama “watu wa kuja” na wenyeji wazawa wa Dar es Salaam kwa upande mwingine.

Kwa wakati ule kazi ya “composer” ilikuwa kazi yenye hadhi kwa Mwafrika na ilihitaji mtu aliyesoma. Ibrahim Hamisi alikuwa mmoja wa waasisi wa Al Jamiatul Islamiyya fi Tanganyika chama cha Waislam kilichoanzishwa mwaka 1933 na kikajenga shule Al Jamiatul School New Street kona na Stanley Street ambayo jengo lake lipo hadi leo Mtaa wa Lumumba na Max Mbwana. Uongozi wa Al Jamiatul Islamiyya ndani yake mlikuwa na Waarabu, Wanubi, Wazulu, Wamanyema, Wazaramo na makabila mengine ya pwani na mara nyingi Wazulu na Wanubi ndiyo wakishika uongozi. Na hii ilipata kujaleta mgogoro mkubwa mwaka 1940 kiasi cha kufunga shule kwa muda hadi Gavana akaingia kati kusuluhisha. Hii Ilikuwa katika Ali Aljamiatul Islamiyya lakini hata katika African Association mambo yalikuwa hivyo hivyo. Mwaka wa 1933 kulitokea ugomvi uliosababisha secretary Kleist Sykes ajiweke pembeni katika chama hadi alipoombwa na Mzee bin Sudi aliyekuwa president ndipo aliporejea tena katika chama. Mzee Bin Sudi alikuwa Mmanyema. Hizi ndizo zililiwa siasa za wakati ule.

Mbele ya Kipata Street ukishapita Swahili Street unafika nyumba ya Hassan Machakaomo. Kizazi kingine cha wageni kutoka nje ya mipaka ya Tanganyika. Hassan Machakaomo ni mtoto wa Machakaomo Mzulu askari mamluki kama walivyokuwa Wanubi. Wazee wake waliletwa Tanganyika na lile jeshi mamluki la Harmine von Wissman. Hassan Machakaomo alijulikana zaidi kama kiongozi wa Young Africans Football Club katika miaka ya 1950 na harakati za kudai uhuru zilipoanza mwaka 1954 Young Africans, “Yanga” kama ilivyokuwa inajulikana ilijinasibisha moja kwa moja na bila ya kificho na TANU. Si mbali na nyumba hiyo kwa mkono wa kulia Kipata kona na Sikukuu ilikuwa nyumba ya Clement Mohamed Mtamila ambaye katika miaka ya mwisho ya 1940 ndiye alikuwa katibu wa TAA baada ya African Association kubadilisha jina na kuitwa TAA. Hapa itabidi tusimame kidogo.


Itaendelea...

MWANANCHI.
SHUKRAN: M.M MWANAKIJIJI

No comments: