Monday, October 17, 2011

KINA WARIOBA,MWINYI NA WAZEE WENGINE WANYAMAZE SASA; TAYARI TUNALIPIA HATIA YAO
Na M. M Mwanakijiji,

Kama kuna kitu kimeanza kunigusa pabaya katika fikra zangu ni kauli za mara kwa mara za wale wanaotajwa kuwa ni “viongozi wa zamani” wa taifa letu ambao hutoa kauli mbalimbali za kujaribu kuonesha kuwa nchi imefika pabaya. Kauli za hivi karibuni za aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Joseph Warioba na zile za aliyewahi kuwa Waziri na Mkuu wa Mkoa kwa muda mrefu na Mdhamini wa CCM Bw. Paul Kimiti zinanifanya nianze kuona kuwa kama taifa tunaanza kuchezewa akili na wale ambao waliwahi kuwa viongozi.

Lakini vile vile kauli za aliyekuwa Rais wa Tanzania Mzee Ally Hassan Mwinyi kuhusu masuala ya madawa ya kulevya na viongozi wa dini nazo zinanifanya niamini kabisa kuwa viongozi wetu hawa wa zamani wanaishi katika ulimwengu wa wale wanaokana. Yaani, wale ambao hawajakaa chini na kuangalia ni kwa jinsi gani maamuzi yao wao wenyewe ndio yamelifikisha taifa letu leo hii.

Wazee hawa wanapozungumza japo inaonekana kana kwamba ni katika “uzalendo” ukweli ni kwamba wanajaribu kujitenga na matendo na misimamo yao wakati walipokuwa madarakani. Ndugu zangu, leo hii tunalipia hatia yao. Wanayo hatia na wakati umefika waanze kukiri hatia hiyo na kuliomba taifa letu msamaha na wawajibike kwa kuanza kukaa kimya.

Tanzania tunayoiona leo hii na matatizo yake yote (ndani ya chama na serikali) na katika mfumo mzima wa utawala hayajashushwa kutoka kuzimu au kutumwa na mjumbe toka ahera madukani. Matatizo yetu mbalimbali yanahusiana moja kwa moja na maamuzi ya huko nyuma; maamuzi ambayo tukiyaangalia leo katika mwanga wa 20/20 tunaona kabisa kuwa yametokana na kushindwa kwa viongozi wetu na watendaji wetu mbalimbali waliopita.

Leo hii miji yetu inajengwa magorofa ya kila aina – wenyewe tunaita vikwangua anga – lakini miundo mbinu ya maji machafu, usafi, na usalama bado ikiwa duni. Lakini hili ni kwa sababu viongozi waliopita huko nyuma hawakuwa na maono ya kurithisha kizazi ambacho kingefuata mazingira bora ya utawala na utendaji. Waliandika mengi, walitoa hotuba nyingi na katika zama zao walionekana ni viongozi mahiri. Lakini leo hii tunalipia kushindwa kwao kuongoza.

Leo hii wanazungumza baada ya matukio ya aibu kule Igunga ambapo tumeona jinsi gani siasa yetu inazidi kudidimia si katika tofauti ya hoja na itikadi bali katika tofauti ya nani anataka nafasi gani na ataipata kwa nguvu gani. Mzee Warioba kwa mfano, hakusema lolote la kukaripia chama chake wala viongozi watendaji wakati mambo yanazidi kuharibika kule Igunga. Lakini leo baada ya uchaguzi anasimama na kutuambia kama kutuonya kuwa ati siasa zetu zimefika pabaya. Kweli?

Kweli siasa zetu hazikufika pabaya kule Tarime? Siasa zetu hazikufika pabaya pale watu walipopigwa na kujeruhiwa mikono mwa viombo vya dola kula Kiteto? Je kweli taifa letu halijafika pabaya pale tuliposhuhudia watu wanauawa Januari 5 mwaka huu kule Arusha? Mbona hawakusimama hawa “wazee” wetu na kuipa serikali yao hekima?

Leo kina Mzee Mwinyi wanatuambia kuwa viongozi wa dini wanahusika na madawa ya kulevya na kulileta taifa aibu na kuwafanya Watanzania wote waonekane wabwia unga au madalali wa madawa ya kulevya. Kweli? Viongozi wa dini wanapofikia kujihusisha na madawa ya kulevya namna hii na hadi kina mzee Mwinyi na Rais Kikwete wote wakajua tatizo liko wapi? Kwanini hawasemi udhaifu uliopo kwa watendaji wa vyombo ya usalama na usimamizi wa sheria? Kwanini hawasemi juu ya udhaifu wa usalama wetu wa taifa? Wanazungusha maneno na sasa wana hatia.

Ndugu zangu, hawa wazee tunaowaona leo hii ndio walikuwa vijana wenye nguvu, na matumaini ya taifa letu miaka hiyo. Mwishoni mwa miaka ya sitini ambapo wengi wa wahitimu wetu wa mwanzo wa vyuo vyetu katika Tanzania huru na iliyoungana wanaingia madarakani hawa ndio walikuwa tunu ya taifa letu. Tuliamini wakati huo kuwa “vijana ndio taifa la kesho”. Leo hii waliokuwa vijana enzi hizo na walioonekana kuwa ni tumaini tunaona jinsi gani tunavuna walichokipanda wao.

Na sisi kizazi cha leo tusipoangalia tutakuwa na hatia hiyo hiyo. Hatufikirii kurithisha watoto wetu, na watoto wa watoto wetu nchi iliyo bora, yenye neema, na nafasi sawa za kufanikiwa kwa kila Mtanzania. Leo hii tunashuhudia makundi ya yale wanaoitwa viongozi wakiendelea kuligawa taifa letu na wakiendesha wengine kampeni za chuki za kidini na kihali huku wakiamini kuwa kwa kufanya hivyo wanajinufaisha wao leo hii na sasa.

Sera zao na maamuzi yao yanafikiria “leo”. Wanafikiria jinsi gani leo wataweza kujenga majumba mazuri, kupata posho nono, na kuishi maisha ya afueni kule wale maskini kwa maelfu waliotawanyika katika taifa letu zuri na lipendezalo. Leo hii wanaendeleza kujitofautisha wao na wenzao katika chama na serikali yao katika kufanikiwa huku wakihumu kizazi kijacho kwa makosa yao.

Fikiria jinsi viongozi hawa hawa walivyokwisha kujitahidi kuuza urithi wetu na ule wa watoto wetu kwa mikataba ya ajabu ya madini na ardhi. Ni kweli wanajaribu kutatua tatizo la “sasa”. Lakini ni kana kwamba wamepigwa ukungu wa kutokuona jinsi gani maamuzi yao yatakuwa mzigo kwa watoto na watoto wa watoto wetu miaka hamsini ijayo kama vile leo hii sisi tunalipia maamuzi ya wale waliokuwa kwenye madaraka miaka hamsini iliyopita na ambao leo wanazungumza kana kwamba wao siyo sehemu ya historia yetu; kana kwamba wao hawakuwepo wakati maamuzi yakupitisha sheria mbovu au kulindana yalipokuwa yanafanyika!

Wao tayari wana hatia; na tusipoangalia leo hii tunaanza kuwaona kikundi kipya cha viongozi ambao nao watakutwa na hatia. Hatia ya kuwapora watoto wetu nafasi yao ya kufanikiwa. Tutakuwa na hatia ya kuiweka rehani kila nafasi ya wajukuu wetu kujenga taifa la kisasa. Tutakuwa na hatia ya kuikopa na kuipoteza ndoto ya Tanzania njema ambayo watoto wetu wangeistahili kuipata. Tutakuwa ndugu zangu – na hatia ya kukipora kizazi kijacho tunu pekee ya kufurahia matunda ya uhuru ambao mababu zao walipigania.

Na itakapofika miaka thelathini ijayo, na sisi tutaanza kutoa kauli za kama kina Mzee Warioba, kina Kimiti, kina Mwinyi na wengine kuwashangaa hao wa kizazi hicho wakati huo taifa letu litakapokuwa katika migongano mikubwa. Nikiyageuza maneno ya J.F. Kennedy kwa kizazi chake miaka karibu hamsini iliyopita – Tusijiulize tunataka kujifanyia nini sisi kizazi cha leo hii; tujiulize tunataka kukifanyia kizazi kijacho nini leo hii, sisi?

Makala hii imeandikwa na M. M. MwanaKijiji:
Baruapepe: mwanakijiji@klhnews.comFRANK MAKANGE BLOGLink

No comments: