Thursday, October 13, 2011

HURUMA YA RAIS KWA WALIOMUUA IMRAN KOMBE YAZUA MJADALA

UAMUZI wa Rais Jakaya Kikwete kuwapunguzia adhabu, polisi wawili waliohukumiwa kunyongwa baada ya kupatikana na hatia ya kumuua aliyekuwa Mkurugenzi wa Idara ya Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Imran Kombe, umezua mjadala mzito miongoni mwa watu wa kada tofauti katika jamii.

Wasomi, wanasiasa, wanaharakati na wadau mbalimbali waliozungumza na gazeti hili kwa njia tofauti jana, walitoa maoni yanayopingana; baadhi yao waliupinga na wengine kuunga mkono.

Wakati wanaoupinga wanasema Rais hakutenda haki kwa kuwa kuna wafungwa wengi magerezani wanaohitaji huruma yake, wakati wanaomunga mkono wanamshauri aweke wazi vigezo anavyotumia kutekeleza mpango huo ili kuondoa manung'uniko ya watu.

Mawakili kadhaa mjini Moshi mkoani Kilimanjaro, walisema jana kuwa, mazingira ya tukio hilo la mauaji ya Kombe, yanaweza kumshawishi Rais kuchukua uamuzi aliouchukua, lakini kwa siku za usoni ni vyema vigezo vya misamaha hiyo vikawekwa wazi na kufahamika.

“Unajua kiini cha mauaji yale kama ushahidi ulivyokuwa ni 'mistaken identity' (kumfananisha mtu ambaye siye) ni tofauti na mauaji ya makusudi. Mimi nafikiri kwa msingi huo, uamuzi wa Rais ni sahihi,”alisema wakili Peter Shayo.

Kombe aliuawa kwa kupigwa risasi nne kifuani Juni 30, 1996 baada ya polisi waliokuwa wakisaka gari aina ya Nissan Patrol, mali ya W. Ladwa, kumfananisha na mtuhumiwa sugu wa wizi wa magari maarufu kama White.

Wakili Shayo ambaye ni miongoni mwa mawakili wa kwanza baada ya Uhuru, alisema mazingira ya tukio hilo ni kuwa polisi hao walikuwa wakisaka mwizi wa gari pamoja na gari ambapo njiani walikutana na gari linaloshabihiana na wanalolitafuta.

“Sasa kama ni kweli hayo ndiyo mazingira yaliyojitokeza katika tukio hilo, mimi naamini uamuzi wa Rais ya kupunguza ile adhabu na kuwa mauaji ya bila kukusudia, yanaweza kuwa sahihi,”alisema Shayo.

Wakili huyo alisema mazingira ya tukio la mauaji ya Kombe ni tofauti na mauaji ambayo mtu anamuua baba yake na kukata kichwa kisha kwenda kukiuza… akisema ukimsamehe mtu wa aina hii, kelele zitapigwa nchi nzima.

Hata hivyo, wanasheria wengine waliohojiwa na Mwananchi jana walisema japokuwa mamlaka hayo ya Rais yapo kikatiba, ni vyema kukawapo vigezo vya misamaha, vinginevyo wasaidizi wake wanaweza kutumia misamaha hiyo vibaya.

Kauli za wanaharakati

Kwa upande wake, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) kilipongeza hatua hiyo, kikieleza kuwa jambo hilo ni zuri kwa Serikali kutotekeleza adhabu ya kifo.

Mkurugenzi Mkuu wa LHRC, Francis Kiwanga alisema; “Tunampongeza kwa hatua hiyo kwa sababu Serikali inaelekea kusikia kilio chetu cha muda mrefu, siku zote tumekuwa tukitaka adhabu hii ifutwe.”
Hata hivyo, Kiwanga alisema kuwa, haitoshi kuachiliwa huru kwa watu hao wawili pekee, huku kukiwa na mamia wengine wamekaa gerezani kwa muda mrefu wakisubiri utekelezaji adhabu ya kifo.

“Ingawa tunamshukuru Rais kwa kuanza kusikia kilio chetu cha muda mrefu, tunataka iwekwe katika sheria kabisa kuwa, watu waliohukumiwa kifo, hukumu zao zibadilike na kuwa za kawaida,” alisema Kiwanga.
Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa Rais ametimiza wajibu wake kwa mujibu wa katiba na kwamba kilichobaki sasa ni nafasi ya wanaharakati kuhakikisha adhabu hiyo inafutwa kwenye vitabu vya sheria.

Alieleza kwamba, hatua ya kuandikwa kwa katiba mpya, ni moja ya nafasi nzuri zitakazowezesha kufutwa kwa adhabu hiyo.Mkurugenzo wa Mtendaji wa Kituo cha Taarifa kwa Wananchi (TCIB) Deus Kibamba alisema hatua ya kuwaachia watu wawili tu kati ya mamia inazusha maswali mengi.

“Mtu atajiuliza ni kwa nini hao wawili tu ndiyo wametoka, ni vigezo gani vilitumika kuwachagua wao tu?” alisema Kibamba.Alisema kuwa, hali hiyo ni matokeo ya Rais kuwa na madaraka makubwa kupita kiasi, yanayompa nafasi ya kupindua maamuzi yaliyotolewa na Mahakama.Hata hivyo, alisema hatua hiyo ni ushindi kwa wanaharakati wa haki za binadamu ambao kwa muda mrefu sasa wamekuwa wakipinga adhabu hiyo.

Wananchi wengine
Mwenyekiti wa DP, Mchungaji Christopher Mtikila alisema anashangwa na uamuzi wa Rais kubatilisha hukumu ya kifo kwa askari polisi aliosema walimuua kwa makusudi Mkurugenzi huyo wa zamani wa Usalama wa Taifa, Luteni Jenerali Kombe.

Akizungumza na Mwananchi, Mtikila alisema kuwa hajui ni kwa misingi gani Rais Kikwete alitoa uamuzi huo.
“Ninachojua nafasi aliyopewa Rais ya kutoa msamaha kwa wafungwa kwa mujibu wa katiba ni kufanya hivyo kwa ajili ya manufaa ya Taifa. Sasa, sijui hapa Taifa limenufaika na nini kuuawa kwa Kombe?,”alihoji Mtikila.

Alisema hatua ya Rais inaonyesha ni jinsi gani nchi isivyo na utawala wa sheria na isivyojali katiba ya nchi, inayosema kuwa, kila mmoja ana haki mbele ya sheria na Serikali kupitia katiba yake italinda na kuziheshimu haki za raia na kuwahakikisha ulinzi na usalama.

Kwa upande mwingine, wananchi wa kawaida nao wamekuwa na maoni tofauti kuhusu uamuzi wa Rais Kikwete kuwaachia huru polisi hao aliohukumiwa adhabu ya kifo mwaka 1998.Kupitia mtandao wa gazeti hili wananchi hao wameeleza kusikitishwa na uamuzi huo, huku wengine wakitaka Rais Kikwete kuangalia wahukumiwa wa aina hiyo wenye umri mkubwa, ili awaachie huru.

Askari walioachiwa ni Koplo Juma Mswa na Konstebo Mataba Matiku, ambao walikuwa gerezani takriban kwa miaka 16, wamechiwa huru kufuatia huruma ya Rais Jakaya Kikwete ambaye alipunguza adhabu hiyo ya kifo, kuwa kifungo cha miaka miwili jela.

Katika maoni yake mmoja wa wananchi hao ameeleza kuwa msamiati wa 'kupunguza' umetumika vibaya kwani katika hali ya kawaida adhabu imeondolewa na siyo kupunguzwa.

Alieleza kuwa adhabu kwa askari hao ingekuwa imepunguzwa iwapo ingebadilishwa kuwa kifungo cha maisha.

Madaraka ya Rais
Madaraka ya Rais ya kumsamehe mtu yeyote aliyepatikana na hatia, yamo katika Ibara ya 15 (1) (c) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2008.

Ibara hiyo inatamka, ”bila kuathiri masharti mengineyo yaliyomo katika Ibara hii ,Rais anaweza kutenda lolote ikiwamo kuibadilisha adhabu yeyote aliyopewa mtu yeyote kwa kosa lolote ili iwe adhabu tahafifu”.

Akizungumza na Mwananchi juzi, mmoja wa askari hao walioachiwa huru Matiku Mataba alisema walitoka gerezani Mei mwaka huu walikokuwa wakisubiri kutekelezwa kwa adhabu yao ya kunyongwa baada ya Rais kuwaonea huruma na kuwapunguzia adhabu.

Baada ya polisi hao kupatikana na kuhukumiwa adhabu ya kifo kwa kile Jaji Buxton Chipeta alichosema, “Uzembe wa hali ya juu”, mjane wa Kombe, Roselyne Kombe alifungua kesi ya madai dhidi ya Serikali.

Tangu Rais Kikwete aingie madarakani 2005, hajawahi kusaini hukumu yeyote ya kifo kama ilivyokuwa kwa mtangulizi wake, Benjamin Mkapa na hadi sasa zaidi ya watu 500 wanasubiri kunyongwa.

Habari imeandikwa na Daniel Mjema, Moshi, Boniface Meena, Joseph Zablon na Fredy Azzah, Dar

MAONI YA WASOMAJI KUTOKA MWANANCHI

MSOMAJI WA KWANZA

Kikwete hata kama umepewa mamlaka kikatiba ya kutoa msamaha ila hapa hujatenda haki hususani kwa familia ya marehemu Lt.General Imran Kombe kwani kuwaachia polisi hao huru ni dhulma na ipo siku utahukumiwa kwa dhambi hii uluyoifanya dhidi ya Lt.Gen.Kombe.Hao hawkustahili msamaha wowote ule kwani ni wauwaji wa makusudi kwa sababu Lt.Gen.Kombe alitii amri zote walizompa sasa ilikuaje wamuue tena kwa kisingizio eti wamemfananisha na jambazi?Hii nchi Kikwete unaipeleka wapi?Wapo wengi wanaosubiria huruma zako za msamaha ila sio hawa polisi waliomuua Lt.Gen.Kombe kwa makusudi kabisa ila pia kwa kuwaachia huru hii inatudhihirishi a ya kuwa Lt.Gen.Imran Kombe aliuwawa ndio maana umeamua kuwaachia huru hao wauwaji.Kaa ukijua dhambi hii ipo siku utakuja kuilipa wewe Rais Kikwete iwe duniani,kaburin i au akhera utailipa tu kwani haki ya mtu mbele ya Mungu haidhulumuwi.Watanzania wote kwa pamoja tuupinge uovu huu alioufanya mkuu wetu wa nchi dhidi ya Lt.Gen.Imran Kombe.

MSOMAJI WA PILI

Lt Gen Imran Hussein Kombe alipigwa risasi tarehe 30/06/96 na Polisi wawili ikwa ni wiki moja tu baada ya Kuvuliwa wadhifa wa Mkurugenzi wa Usalama Taifa na Serikali.Ukweli ni kuwa Serikali ndiyo Imetayarisha KIFO chake kwa sababu aliwaingilia Vigogo wa Serkali ni kama vile Mzee SOKOINE alivyo uliwa: Hii ni tabia ya Serikali ya Tanzania na Kikwete Kuwaachia Uhuru wale Polisi walio muua Lt General Imran Hussein ni kitendo chaAibu kwa Nchi nzima.Serikali ina Kesi ya Kujibu kwa Wananchi wote wa Tanzania,Sina Imani na Serikali ya Tanzania. Kwanini kabla ya Polisi kumpiga risasi wasimkamate Lt Gen Imran na Kumpeleka katika kituo cha Usalama na Kumhakikisha ya kuwa yeye ni jambazi au Sio.Ukweli hawo Polisi walipewa Amri na Viongozi wa Serikali kupitia kwa Viongozi wao wa Polisi Kumpiga risasi na baadaye kusema ATI walimfananisha na Mtu mwingine Hii HADITHI HATA ukimwambia [NENO BAYA] atacheka. Serikali Inajuwa UKWELI na Iwache Kutudanganya sisi Raia kama Wendawazimu. MYONGE MNYONGENI HAKI YAKE MPENI. Lt Gen Imran Hussein alikuwa ni Mwanajeshi mwenye Hekima kubwa na ni Hasara kubwa kwa Taifa letu Kumkosa mwanajeshi kama yeye.MUNGU AMREHEMU NA AMWEKE MAHALI PEMA PEPONI.AMIIN.

MSOMAJI WA TATU

Kuna siku hayo yote yatajulikana baada kupata mageuzi kama wenzetu Kenya na Zambia
Enyi wakubwa eleweni kuwa kila lenye mwanzo lina mwisho jaman tubuni gharika laja

MSOMAJI WA NNE

Hili ni tatizo la Katiba iliyozeeka, inayompa rais mamlaka juu ya kila kitu hata kuingilia uhuru wa Mahakama. Je "balance of power" ipo wap? Je tunayo demokrasia? Tunataka KATIBA MPYA!!!! itakayoamuru mambo ya kisheria (kutoa misamaha kwa wafungwa) ifanywe na mahakama.

MSOMAJI WA TANO
Ni tatizo la katiba yetu, tuibadili tuyaondoe haya madaraka makubwa ya rais.
Jaji mwenye uzoefu na kuijua vyema sheria anawahukumu wahalifu kifo, rais (asiye mataalamu wa sheria) anabatilisha huo uamuzi. Usiniambie rais ana wasaidizi wanaoijua sheria maana kla siku tunasikia hao wasaidizi wa rais ndiyo wanaompotosha!!
HAPA NI KATIBA MPYA, KATIBA MPYA, KATIBA MPYA TU!!!! Itakayofutilia mbali adhabu ya kifo na kuondoa madaraka ya rais kuingilia mamlaka ya Mahakama

MSOMAJI WA SITA

mimi nimesikitishwa sana kwa kuachiwa hao police. Hiyo inadhihirisha kwamba hapa duniani hakuna haki. Kiukweli kombe aliuawa na ccm.

MSOMAJI WA SABA

Ajabu ni kwamba hawa Polisi walishindwa kumjuwa kiongozi mkubwa wa Jeshi letu ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Usalama Taifa wa Serikali yetu,Laa hapa palikuwa na mchezo mchafu, kwani Lt Gen Imran alikuwa na Dereva wake,itakuwaje Polisi walipomwona tu bila hata kumkamata na kumhuji waanze kumpiga risasi kama sio njama za Serikali??? Jee haki ya Kiongozi wetu Lt Gen Imraan iko wapi??? na kwanini Rais Kikwete awaachilie Uhuru hususan hawa Mapolisi,Ambapo kuna wafungwa wengi katika jela zetu wamehukumiwa kifo kwa kusingiziwa kesi na Jeshi la Polisi wa Tanzania na hakuna Kiongozi anayewajali hao masikini ambao wanataabika katika jela zetu HAKI IKO WAPI????
KWA HISANI YA MWANANCHI

No comments: