Thursday, October 27, 2011

HADITHI HADITHI : MTEGO WA PANYA
MTEGO WA PANYA, KUINGIA WALIOMO NA WASIOKUWAMO
.


Palikuwa na mtu na mkewe. Ndani ya nyumba yao walikuwamo panya wengi sana, wakiharibu vitu, na kutoboa makanda yam tama. Hata Yule bwana wa nyumba akatafuta mtego akaenda ghalani akatega. Hatima akapita panya akauona ule mtego akatambua kuwa mtego huu ametegewa yeye. Akapita Jogoo. Panya akamwambia jogoo, Wewe mwenzangu mkubwa kuliko mimi, hufanyi jamala ukaupiga teke huu mtego ufyatuke? Jogoo akamwambia, mtego huu umetegewa wewe, mimi haunihusu kitu. Panya akanena, Kweli, lakini nauona umekaa vibaya wasije wakaingia waliomo na wasiokuwamo. Jogoo akanena, Najuaje? Akaenda zake. Mara akapita mbuzi. Panya akamwambia mbuzi, Bwana mdogo, hufanyi taratibu ukaufyatua huu mtego, na mimi nikapata riziki? Mbuzi akambambia, Mimi na mtego tu wapi? Mtego ule umetegewa weye unayeharibu vitu vya watu, mimi chakula changu majani. Panya akanena, kweli huu ni mtego wa panya, lakini tena ni mtego wa kuingia waliomo na wasiokuwamo. Akanena, Mimi sijui hayo, akaondoka akaenda zake.

Hatima akapita ng’ombe. Panya akamwambia, Eee Bwana mkubwa, tafadhali ukafyatue huu mtego, na mimi nikapata riziki, tena nauona umekaa vibaya, wasije wakaingia waliomo na wasiokuwamo. Ng’ombe akanena, Hayo ni mambo yako wewe unayetoboa makanda ya watu: mimi nakula majani, na mtama wapendapo kunipa. Sina haja ya kujishughulisha na mambo yasiyonihusu. Akaondoka akaenda zake. Na panya naye akaenda zake akawahubiri wenziwe kuwa ghalani kuna mtego wasiende. Mara akapita nyoka naye anawinda panya, akapanda juu ya mtego akanaswa. Yule mwenye nyumba aliposikia mtego ukifyatuka, akachukua fimbo akaenda ghalani. Mkewe akamwambia, Bwana , huchukui taa? Alipoufikia mtego, akapiga kwa ile fimbo yake , Yule nyoka akamwuma. Yule bwana akasema, Ah! Kaniuma ati! Mkewe akaleta taa kumulika, akasema, si panya, bwana, ni nyoka.

Yule bwana akawa hoi hoi tena, maumivu yamemshika. Huku na huku, wakaitwa jamaa zake, wasidiriki kuja wote, akafa. Basi wakaja watu wachache usiku kuwalaza wafiwa, akachukuliwa jogoo akachinjwa, kitoweo cha wale watu waliolala. Siku ya pili wakaja watu wengi kulala matanga. Akachukuliwa mbuzi akachinjwa, kitoweo cha watu wa matangani. Hata siku ya kusoma khitma, akachukuliwa ng’ombe akachinjwa. Maneno ya panya yakatimia, mtego wa panya, lakini wakaingia waliomo na wasiokuwamo.

No comments: