Friday, October 28, 2011

HADITHI HADITHI: KISA CHA MAJUHA WATATU


KISA CHA MAJUHA WATATU

(MAANA YA MAJUHA NI WATU WAPUMBAVU)

Hapo zamani paliondokea mtu, akaenda kutembea akafika njiani akawakuta watu watatu wamekaa kitako, Yule mtu akawaamkia, Salaam aleikum ! Majuha. Wakaitikia, Aleikum salaam. Yule mtu akapita akaenda zake.

Wale majuha huku nyuma wakabishana, wao kwa wao, mmoja akasema, salaam hizi ni zangu mimi! Wa pili akasema, Juha ni mimi! Wa tatu akasema vilevile. Basi wakawa katika hali ya kubishana; mmoja akasema, sisi hatuna haja ya kubishana kutwa maana Yule mtu bado kufika mbali, twende tukamwulize, katika sisi watu watatu, Juha ni nani? Wakakubali wakaenda wote huku wanapiga kelele za kumwita Yule mtu, Ee Bwana weee, simama! Ee Bwana, simama! Yule mtu akawaza, Nimefanya nini huku nyuma nilipowapita wale watu? Akasimama.

Hata walipomfikia karibu mmoja wao akasema, Ati! Bwana, ile salaam uliyotoa si yangu mimi? Juha si mimi? Wa pili akamwuliza vile vile, Je! Ile salaam si yangu! Juha si mimi? Wa tatu akauliza, Juha si mimi, Bwana?

Yule mtu akawaza rohoni mwake ya kuwa nitawauliza watu hawa. Akamwuliza Yule mmoja, Lete habari za Ujuha kweli! Akasema, Bwana mimi ni juha kweli:-

Jana nalikwenda sokoni, nikaenda nikanuua nyama, nikampelekea mke wangu akapika, kabla nyama haijaisha kuiva bado, Yule mke wangu akatoka, akaenda kuomba chumvi. Huku nyuma nikatwaa vipande viwili vya nyama nikatia mdomoni nikatafuna, kabla sijameza, mke wangu akaja nami kutafuna nikaona haya, ile nyama nikaitia katika shavu moja likajaa fututuu, mke wangu aliporejea akaniona ni hali ile, akasema, Alhamdu Lillahi Rabbi-l-alamina, Mwenyezi Mungu ni Mkubwa. Mara hii natoka kwenda omba chumvi , naja ndani mume wangu amevimba shavu! Bahati! Lete uma na moto, akaleta ule uma, ukawashwa moto nikachomwa katika shavu, nikaona shavu hili linaungua, nikageuza nyama katika shavu la pili, nalo likachomwa, nikaona sina mahali pa kugeuzia tena nikaitema ile nyama, nikaiangusha pale chini pu! Mke wangu akaniambia, Ah! Mume wangu, mke ni mkeo, nyama ni nyama yako, umefanya upumbavu kama huu, hata nimekutia vidonda katika mashavu? Je! Bwana, wasemaje mimi si Juha? Akasema, Kweli Juha ni wewe. Naam.

Yule wa pili akasema, Bwana, Juha ni mimi. Jana nilikwenda sokoni nikanunua nyama, na mchele na nazi, na bizari na kuni pia nikaja nikampa mke wangu akapika akaisha. Na mji huu una amri, ikifika saa nne milango hufungwa, lakini ikifika saa nne kama hukufunga mlango hukamatwa ukalazwa korokoroni, asubuhi huzungushwa mji mzima kasha hupelekwa pwani kuchinjwa.

Basi nyumbani petu tumekaa hata ikapita saa nne bado hatujafunga mlango, wala chakula hakijapakuliwa. Nikamwambia mke wangu, Pakua chakula! Akapakua akaisha akaweka juu ya meza, tukitaka kula nikamwambia mke wangu, Tusile, nchi hii ina amri nawe unaijua, basi kafunge mlango kwanza tuje tule; mke wangu akaniambia, Kafunge wewe, nikamwambia, Kafunge wewe, akaniambia, kafunge wewe. Nikamwambia mke wangu, Hatuna haja ya kubishana, basi tukae vivi hivi tu, na chakula tusile, atakaye kula, na akafunge mlango. Basi tukakaa mimi na mke wangu kimya tukatazamana tu.

Tukakaa hata akaja punda mle nyumbani, akala mtama hata ukaisha, punda akatoka, hapana asemaye, atakayesema na akafunge mlango. Akaja mbwa akaingia nyumbani, akaramba vyombo vyote akaja pale mezani akala ule wali wote, sahani akazivunja akaenda zake, hapana asemaye kama mbwa amekula wali! Atakaye sema na akafunge mlango.

Tukakaa, hata saa saba akaja askari, akatuuliza, Sababu gani hamkufunga mlango? Tusiseme, tukanyamaza; askari akatuchukua, akatupeleka korokoroni hata asubuhi tukapelekwa kwa Sultani. Sultani akasema, wazungusheni mji mzima kasha mkawachinje.Mimi na mke wangu tukazungushwa mji mzima hatusemi, hata tulipofika karibu na ile nyumba yetu, mke wangu akasema, Mume wangu, si ile nyumba yetu mbona twaipita? Mimi nikamzomea mke wangu, Woooo! Mke wangu amesema, Eeeeee Wooooo, Mke wangu amesema! Yule askari akasema, Ah! Watu hawa wana nini? Sultani ameniambia niwazungushe, nikifika pwani niwachinje, sasa wanasema hivi: watu hawa nitawarudisha kwa Sultani. Askari akaturudisha, akamweleza Sultani, Sultani akatuuliza, nasi tukamjibu, akatupa ruhusa tukarudi kwetu nyumbani. Je ! Waonaje, wali wangu, mke wangu, nyumba yangu ikataka kuniua, Je Bwana mimi si Juha? Akamwambia, wewe Juha zaidi ya Yule wa kwanza.

W a tatu akasema, Bwana, Juha ni mimi, mimi jino langu liliniuma, nikauliza, Humu mjini hapana mganga wa jino? Nikaambiwa, Yupo hapa Ali. Nikaenda kwa Ali nikamwambia, Jino langu laniuma, unajua kutoa jino? Akasema, Najua. Nikamwuliza, Ela unatoa kwa pesa ngapi? Akaniambia, Nusu rupia tu. Nami nina nusu rupia yangu ya dhahabu, kwa reale tano. Nikampa akanitoa jino moja.

Nikarudi nyumbani kwangu, mke wangu akaniuliza, umekwishatolewa jino? Nikamwambia, Nimekwisha kutolewa. Akaniuliza, Umempa nini fungule? Nikamwambia, Ile robo yangu ya reale tano. Akaniambia , Ah! Mume wangu, wenzio watolewa jino moja kwa robo ya mapesa, pesa 32, wewe umetolewa jino moja, umetoa rupia 10.

Nikarudi kwa Ali, nikamwambia, Kumbe! Wenzangu unawatoa jino moja kwa pesa 32 mimi umenitoa jino moja kwa reale zangu 5, basi afadhali unitoe yote! Ali akanitoa yote nikarudi nyumbani. Mke wangu akaniuliza umepata rupia zako? Nikamwambia , Ohoooo; na miye nimemkopa, akaniuliza, kwa nini? Nikamwambia amenitoa meno yote kwa robo moja ya dhahabu, je , waonaje mke wangu, sikumkopa Ali!

Mke wangu akaniambia, Ndiyo wewe Juha. Je! Bwana, mimi si Juha?

Yule mtu akamwambia, Ah! Wewe Juha sana, hata salamu zile ni zako wewe. Wakarudi wakiambiana huyu ameshinda wenziwe kwa Ujuha.

No comments: