Monday, October 31, 2011

FFU WASAMBARATISHA SHEREHE YA KUSIMIKA MANGI MARANGU

Daniel Mjema, Moshi

POLISI wa Kutuliza Ghasia (FFU), wamesambaratisha sherehe ya kumpongeza mfanyabiashara mashuhuri, Frank Marelle, kwa kuteuliwa kwake kuwa kiongozi wa kimila (Mangi) wa Wachaga wa Marangu.Kusambaratishwa kwa sherehe hiyo inayoelezwa ilikuwa ihudhuriwe na watu 3,000 wenyeji wa Marangu Moshi Vijijini, kulitokana na amri ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Kilimanjaro iliyotolewa Ijumaa.

Amri hiyo ilitolewa na Hakimu Mkazi, Ruth Mkisi, kufuatia maombi yaliyowasilishwa mahakamani hapo na wanaukoo wawili wa Marealle, William Mareale na Anitha Marealle.

Katika amri hiyo, Hakimu huyo alimwamuru Frank Marealle ambaye ndiye mjibu maombi, na mawakala wake kutofanya sherehe hiyo hadi hapo maombi ya msingi ya wanaukoo hao yatakaposikilizwa.

Hakimu huyo alimuamuru Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Mkoa (RCO) na Mkuu wa Polisi Wilaya ya Moshi (OCD), kutekeleza amri hiyo na kuhakikisha sherehe hizo hazifanyiki kama ilivyopangwa.
FFU wakiwa wamevalia mavazi rasmi yaliyosheheni mabomu ya machozi, walifika eneo zilipokuwa zifanyiwe sherehe hizo na kuamuru watu wote kutawanyika.

Wakati hayo yakifanyika, wananchi kutoka maeneo mbalimbali ya Marangu walikuwa wameanza kumiminika eneo la sherehe na kusababisha baadhi ya maduka eneo la Marangu Mtoni kufungwa.

Sherehe hizo zilizokuwa zifanyike juzi kuanzia asubuhi Hoteli ya Kitalii ya Kibo iliyopo Marangu, Wilaya ya Moshi Vijijini, zilikuwa zihudhuriwe na mamia ya wananchi wa vijiji vya Marangu atakakotawala Mangi huyo.
Mwenyekiti wa kamati iliyoundwa na ukoo wa Mareale, Dk Wilfred Marealle, alisema kuvunjwa kwa sherehe hizo kumewasababishia hasara kubwa kutokana na chakula kumwagwa.

“Polisi wametuzuia wanasema ni amri ya mahakama… nilikuwa nimealika wageni wangu 500 na hizi ni sherehe zetu, hivi mambo ya kimila yanawahusu nini?...hapa hatufanyi siasa tunadumisha mila zetu,” alisema.

Dk Mareale alisema polisi walipofika eneo la sherehe hiyo juzi, waliwaambia hakuna mkusanyiko wa zaidi ya watu watano unaoruhusiwa na kwamba, suala hilo watalihoji katika mahakama za juu na Bungeni.

Hivi karibuni vyombo vya habari vilimkariri mwenyekiti wa muda wa familia ya Chifu Marealle, Teddy Marealle, akisema wanaukoo wameamua mrithi wa kiti hicho awe mmoja wa watoto wa marehemu siyo ndugu.

Hata hivyo, Dk Marealle alisisitiza msimamo wa wanaukoo wa kuwataka wanaohoji uteuzi wa Frank kumrithi kiongozi huyo wa kimila, waache kuchanganya mila na siasa na uteuzi huo hauwezi kubatilishwa.

Mwenyekiti huyo aliwaonyesha waandishi wa habari muhtasari wa kikao cha matanga cha Desemba 4, 2006 kilichohudhuriwa na wanaukoo 41 na kusisitiza kikao hicho ndicho chenye mamlaka ya kuteua Mangi.


MWANANCHI

No comments: