Monday, September 12, 2011

MBEGU IKIOTA IKAMEA NA KUKOMAA ....TUTAKUJA KUULIZANA (HIVI ILIKUWAJE?)

Inashangaza kuona serikali inayoongozwa na viongozi wazandiki ikiacha chembechembe za mbegu mbaya ziendelee kuoteshwa na watu wao ilihali wao wamekaa kwenye mameza makubwa wakila kuku kwa mrija. Tanzania ya leo sio Tanzania ile ya Mwalimu Nyerere aghalabu Mwalimu aliweza kuijenga Tanzania kila pembe na kila sehemu alikijenga chama kisichojali udini, ukabila, ukanda, rangi, jinsia, cheo ama kasoro ya mtu. Kila kitu kiliendeshwa kwa ustaarabu na kila mtu alimweshimu mwenzake.

Leo hii watu kwa kigezo cha kisiasa wanajaribu kuleta maneno yenye kuchochea uvunjifu wa amani, mgawanyiko, ukabila, ukanda na udini. Hivi hawa viongozi wetu wamesahau yaliyotokea Rwanda mwaka 1994? Yaliyotokea Rwanda mwaka 1994 hayana tofauti na haya wanayotaka kuyapandikiza. Na swali la kuuliza leo katika nchi inayojiandaa kutimiza miaka 50 ya Uhuru wake ilihali watu walio wengi hawajui hatima zao huku kiwango cha aliyenacho kikizidi asiyenacho, ufisadi, umaskini wa kutisha, elimu duni, miundombinu duni, mapato yanayokusanywa kutotumika katika shughuli iliyolengwa na badala yake kwenda kwenye warsha na semina, majanga ya kutisha. Ni nani kati ya hawa ni mvunjifu wa amani. Serikali ama wananchi wa Kilimanjaro na Arusha kama hilo bango lilivyoandika?

Nchi ya Tanzania ni nchi ambayo iliyoongozwa kwa miiko. Ilikuwa ni kosa kubwa sana kumsikia mtu akimtusi mwenzake ati kwamba yeye ni mtu wa aina fulani. Lakini tangu kuanza kwa siasa uchwara tulianza kusikia mengi kuanzia "Magabacholi" na kuendelea ingawa katika miaka hiyo kulikuwa na misemo kama " Wa benzi" " Kabwela" " Bepari" "Kaburu" nk Misemo ambayo ilileta hamasa na kuwaamsha watu hisia zao ili kuepukana na maovu na ufisadi pamoja na unyonyaji.
Leo hii tunawaona watu wameweka ati bango likiwakashifu watu wa Arusha na Kilimanjaro na viongozi wa serikali wengi wao wa chama tawala chama kikongwe kilichokitia Tanzania umaskini wa kutisha wakiwa wakichekelea. Ndio ni lazima tuseme ukweli Chama Tawala ndicho kilichotusababishia haya yote pamoja na mengi kwa kuwa na serikali legelege yenye kupisha mianya ya majanga mengi kutokea huku wao wakitumia vyombo vyao vya habari kuupotosha ukweli ilihali uhalisia unajulikana rejea majanga mbalimbali mfano Ajali ya MV Bukoba, Ajali ya Treni ya mwaka 2002 iliyotokea Msagali Dodoma, Ajali ya mabomu mbagala, Ajali ya mabomu gongolamboto na hii ajali ya juzi ya meli kule Zanzibar. Wao watajifanya kwenda kimbelembele baada ya kuona viongozi wa serikali wameenda kimsingi wamegeuka kuwa makasuku wa serikali misingi na maadili ya taaluma haipo tena. Hii inawezekana inatokana na njaa zao za kusaka noti na mkate wa kila siku kwa kujipendekeza kwao ama inaweza ikawa kutokana na woga wa maisha yao.

Lakini kitu cha kujiuliza hawa Wananchi wa Kilimanjaro na Arusha wamewakosea nini hawa waliokuja na kibango chao uchwara na kusema ati kama ni fujo zenu pelekeni Arusha na Kilimanjaro wana maana gani? Ama wananchi na wakazi wa Kilimanjaro wamewakosea nini ama tuwe wawazi kabisa ina maana kwamba huko Kilimanjaro na Arusha hakuna Wanyamwezi na makabila mengine? Hili ni suala la kukemea na sio la kufumbia macho. Itakuja kufikia wakati tutaanza kukatana wenyewe kwa wenyewe halafu tukishamalizana tunaanza kukaa pembeni na kujiuliza. Hivi ilikuwaje?

Hii nchi sio ya wachaga sio ya wamakua sio ya wakwere sio ya wandendeuli n.k Hii ni nchi ya Watanzania. Kigezo cha kumsema mtu na ukabila wake ati alipendelewa kwenye elimu ama anapata nafasi serikalini ni uchochezi na kielelezo tosha cha uongozi kushindwa kazi ama dhamana aliyopewa. Ukimwona mtu anakwambia hivyo mpige mawe. Halafu umuulize wewe tulipokupa dhamana ulifanya nini kuleta maendeleo? Ukishindwa kazi usilete visingizio. Mbegu ya ukabila na ukanda na udini ndiyo iliyoleta maafa makubwa kule Biafra nchini Nigeria miaka ya sitini na wahanga wengi ni wale ambao hawakuwa na hatia wengi wao watoto na wanawake. Yote hii ni mbegu za chuki zinazopandikizwa na wanasiasa wetu.

Sina haja ya kuendelea zaidi isipokuwa naweza kusema kwamba ili tuendelee ni lazima tukubali ushindani na kamwe visingizio visiwe hoja ya kushindwa kwetu. Leo hii wakenya wanaweza wakajivuna kwa maendeleo na utendaji mzuri wa serikali yao ingawa kasoro hazizuiliki na wameweza kuutawala uchumi wa Afrika Mashariki. Lakini unaweza ukawasikia viongozi wetu aaaah! Wakenya Oooh! Wakenya visingizio kibao na kuanza kupandikiza chuki. Ama unaweza kusikia Ooooh Wabara wanafaidi Muungano Sisi hatufaidi visingizio kibao. Halafu yakitokea tunaanza kuulizana tena . HIVI ILIKUWAJE?

1 comment:

Mujahiduuna Mujahid said...

NI BORA UKANYAMAZA AU KUULIZA KAMA HUJUI MAMBO HUYO NYERERE UNAYEMTUMIA KAMA REFERENCE NDIYE ALIYETUFIKISHA HAPA! sema upewe data!