Thursday, September 29, 2011

IGUNGA WAKISAHIHISHA MAKOSA YAO TUTAWASAMEHE?Na M.M Mwanakijiji.


UAMUZI wa wapiga kura wa Igunga mwaka 1994 ndio uliotupatia Rostam. Ni uamuzi huo huo ndio uliotupatia Rostam mwaka 1995 na ni uamuzi ule ule ndio uliomrudisha tena mwaka 2000. Ni uamuzi wa wapiga kura wa Igunga mwaka 2005 uliomrudisha tena Rostam tena akiwa meneja wa kampeni ya Rais Kikwete. Naam, ni uamuzi wa wananchi wa Igunga uliomrudisha tena Rostam mwaka 2010 kwa ushindi wa zaidi ya asilimia 70. Ni wao wananchi wa Igunga waliolipatia taifa Rostam Aziz. Ni wao waliofanya kosa hili na kulirudia mara nne, tena kwa furaha.


Rostam alipoingia bungeni alikwenda na kupigania maslahi ya chama chake na ya biashara zake. Kwa kutumia migongo iliyopindika na nyuso zilizochoka za wana Igunga alikwenda bungeni na huko akajitengenezea mtandao wa watu wenye kuamini itikadi yake na matokeo yake ni kuwa siasa za Tanzania zikachafuliwa rasmi. Si kwa makosa ya Rostam peke yake tu, tukisema hivyo tutakuwa hatumtendei haki bali kwa kushirikiana na wabunge wengine na viongozi wengine wa CCM kututengenezea mfumo mbovu, dhalimu wa utawala.Ni mfumo huu ambao umeendelea kuligawa taifa kati ya wale walio nacho na wale wasiokuwa nacho, wale wenye madaraka na wale wasio na madaraka, wale wenye nguvu na wale walio dhaifu. Ni mfumo ambao RA (kama anavyojulikana na wengi) ameshiriki kuujenga.

Hakuna wakati wowote ambapo RA amewahi kusimama kuukosoa mfumo huu au hata kuonesha kuwa anajua madhara yake.
Tunaambiwa ni miongoni mwa wabunge wa chache ambao hawajawahi kuuliza maswali bungeni au hata kumbana waziri fulani. Alikataa bungeni kama mahali pa kufanyia biashara, kukutana na washirika mbalimbali, kukubaliana madili ya hapa na pale na hatimaye alipochoka aliweka manyanga chini na kulaani “siasa uchwara” za majitaka.


Lakini wakati wote huo alikuwepo mwana Igunga ambaye angeweza kutoa changamoto kwa Rostam na kuonesha uzalendo wa kupigania wananchi wake kwelikweli. Tangu mwaka 1994 mwana Igunga huyo alijionesha kuwa anata nia ya kuwatumia wananchi wa Igunga. Aliionesha nia hiyo hadi mwaka 2010 lakini mara zote hizo alikubali kukaa pembeni na kimya mbele ya RA. Huyu si mwingine bali ni Dk. Dalaly Kafumu. Dk. Kafumu alikubali kukaa pembeni – japo kwa manung’uniko – kumpisha RA. Hajawahi kusimama na kuwahimiza wananchi wake kumkataa RA kwa sababu ya mambo ambayo yalikuwa yanaendelea kitaifa. Aliamua kula njama ya ukimya akifurahia nafasi yake kwenye vyeo vya juu akiwa ni Kamishna wa Madini nchini.Kama kweli Kafumu alikuwa na nia ya kupigania masilahi ya watu wa Igunga angeweza kabisa kujitoa CCM na kusimama dhidi ya Rostam. Hakufanya hivyo. Kafumu angeweza kusema kuwa RA hajawa kichocheo cha maendeleo Igunga na amekuwa tatizo kwa taifa. Kwamba kuhusishwa kwake kwa kashfa mbalimbali kulikuwa kunaletea CCM sifa mbaya. Hakufanya hivyo. Kwanini? Kwa sababu wote wako chama kimoja na masilahi yao yamefungamana na yale ya chama.Ndiyo maana hadi leo Kafumu hajasimama kuzungumzia vita dhidi ya ufisadi au msimamo wake kuhusu wahusika wa kashfa za madini. Hajasimama kuonesha yuko upande upi katika vita ya magamba ndani ya chama chake. Na badala yake yeye kama baadhi ya viongozi wa CCM wameamua kuchukua ukimya ule ule ili wasijulikane wako upande gani. Kafumu aliamua kuipenda CCM na kazi yake zaidi kuliko kuwapigania wananchi wa Igunga. Kwa maneno mengine kama RA asingeamua kujiuzulu baada ya kuzidiwa na shinikizo la kisiasa Kafumu angeendelea kula bata kwenye ofisi yake huku akisubiri mwaka 2015 au 2020. Kweli huyu ni kiongozi ambaye Igunga wanamtaka?


Ndipo hapa basi wananchi wa Igunga wanapaswa kutambua. Kufanya kosa (mwaka 1994) si kosa. Kurudia kosa (1995) ni kosa, kulirudia kosa tena (2000) ni kosa kubwa.Lakini kulirudia kosa kubwa (2005, 2010) si kosa tena ni uzembe wa kufikiria. Iweje mtu analima kwa mtindo ule ule, na shamba lile lile na mavuno yanazidi kupungua na yeye anaendelea kulima vile vile akitarajia labda mambo yatabadilika? Kama nyumba imeanza kuwa na nyufa mwenye nyumba akiendelea kupiga magoti kuwa nyufa zisitokee ukuta ukianguka atalalamika kuwa “sala” zake hazikusikilizwa? Wananchi wa Igunga wanahitaji malaika gani atoke ahera madukani kuja kuwaambia kuwa wamefanya makosa vya kutosha?Lakini kinachonisumbua miye zaidi ni kuwa hivi wanapopiga kura hawajui matokeo yake kwa taifa? Hivi hadi leo hii wapo watu ambao wanafikiria kupiga kura ya mbunge ni swala la mahali tu? Wapo watu wanaotaka wananchi wa Igunga wapige kura kwa kuangalia masilahi ya Igunga peke yake. Haya ni makosa. Maamuzi ya Igunga yanaathari kubwa sana kwa taifa kama wakichagua vibaya.Tayari tunaona maamuzi yao yalivyogusa taifa kwa miaka hii karibu 18. Uamuzi wa wana Igunga utagusa taifa kwa namna nyingine tena.

Ni kwa sababu hiyo naamini kuwa wananchi wa Igunga wamepewa nafasi ya pekee ya kusahihisha makosa yao. Nafasi ya kutakafakari na kutambua kuwa ni maamuzi yao ndio ambayo yamechangia sana kuleta matatizo ya kisiasa nchini. Wazee, kina mama na vijana wa Igunga ambao walishabikia ubunge wa RA na ambao pasipo haya wala hisia ya hatia waling’ata alipowaambia anajiuzulu ndio hawa ambao waliweza kufurahia kidogo lakini kwa gharama kubwa sana kwa taifa.


Yawezekana kabisa kama wananchi wa Igunga wangechagua kwa umakini na kwa usahihi mwaka 1994 yawezekana kabisa kashfa za Richmond, EPA na Dowans zisingetikisa taifa hivi. Yawezekana kabisa kama wananchi wa Igunga wangefanya uchaguzi sahihi yawezekana hata utawala mzima uliopo madarakani sasa hivi usingekuwepo. Hivyo nafasi hii ni ya kihistoria kwa wana Igunga. Ni nafasi ambayo inahoji kama wametambua thamani yao na thamani ya utu wao. Ni nafasi ambayo inahoji kama wako tayari kufanya maamuzi ambayo matokeo yake wanayatarajia. Kwamba, wako tayari kuamua kubadilisha mwelekeo wa jimbo lao na mwelekeo wa Tanzania kwa kumchagua mgombea ambaye chama chake kinawakilisha mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini.Je, wanajua kuwa wanaposhika lile karatasi la kura ni kwamba wameushika utu wao mkononi mwao? Je, wanajua kuwa mpiga kura anaposhika karatasi ya kura ameshikilia njozi zake, matamanio yake, maisha ya watoto wake na taifa lake kwenye vidole vyake? Je, anajua anapopiga kura hiyo anapigia kura hatima ya maisha yake?Hivyo, siku ya Jumapili wananchi wa Igunga watakuwa wamepewa nafasi ya kuamua wanataka kufanya nini na utu wao. Wanaweza kuamua kuendelea na watu kutoka chama kile kile, chenye sera zile zile zilizoshindwa au wakaamua kuwa sehemu ya mabadiliko na hivyo kuweka historia ya aina yake mkoani Tabora ambako tangu zamani sana kilikuwa kiini cha fikra za mabadiliko. Wananchi wa Igunga watapewa nafasi ya kuamua wanataka kuuza utu wao kwa sababu wametishwa, kwa sababu wanaogopa au wako tayari kupigia kura yao kwa gharama yoyote ile?Njia pekee ni kuwa wananchi wa Igunga wanaitwa na historia kujitokeza mwa maelfu yao kupigia kura maisha yao. Wanaitwa kama ni malaika toka Mbinguni wajitokeze bila kujali kejeli, bila kujali maneno, bila hata kujali polisi na mitutu yao kuamua kutumia haki pekee ya uhuru wao ya kuamua kiongozi wanayemtaka. Wananchi wa Igunga wanaitwa kutokukaa nyumbani na kuombea wengine “wawachagulie” kiongozi wao. Ni witu mtakatifu, wito wa utu wao.Hivyo, kwetu sisi wengine tunawaita kuwa sehemu ya mabadiliko. Wafanye uamuzi ambao unaendana na matamanio ya wananchi wenzao. Lakini bado wana uhuru ule ule. Wakiamua wanaweza kurudia kosa lile lile mara ya tano! Hakuna tofauti kati ya Rostam na Kafumu. Hakuna. Wote wamelelewa na mfumo ule ule na mitazamo yao kuhusu Tanzania ni ile ile. Lakini wananchi wa Igunga wanaweza kabisa kuamua kurudia kosa hilo hilo, sisi tutawalaumu lakini hatuna jinsi bali kuheshimu uamuzi wao wa makosa.Lakini wakiamua kubadilika na kutuma ujumbe usio na utata kwa watawala kuwa Igunga ya sasa si ya 1994 au ya 2005 basi watakuwa wametuma ujumbe ambao unaweza hata kukisaidia CCM katika jitihada zake za kujivua gamba. Wakitumia haki hii kukataa geresha, vitisho, udini, na siasa za dharau wanaweza kujikuta wamefungua ukurasa mpya katika historia yao.Na wakisahihisha makosa yao hayo ambayo yameligharibu taifa hivi, na sisi wengine tutawasemehe. Wajitokeze kupiga kura, walinde kura zao zote zihesabiwe na wafurahie ushindi na kuwa tayari kuanza ngwe mpya ya siasa Igunga.Naomba nijisahihishe mimi mwenyewe kwanza. Nimesema kwa kirefu kuhusu “wananchi wa Igunga” na kuwa “wapiga kura wa Igunga” wasahihishe makosa yao. Ukweli ni kuwa watu pekee wanaotakiwa kusahihisha makosa haya ni wana CCM na mashabiki wa CCM waliompigia kura mgombea wa CCM na kuliletea matatizo taifa kwa karibu miaka 18. Hawa wajisahihishe na hapo ndio tutafikiria kuwasamehe.Kila la heri!

JAMII FORUMS

1 comment:

nyahbingi worrior. said...

Habari za siku.
Kama mwanablogu kutoka Tanzania,nakuomba kushiriki kuchangia Mchakato wa KUFUFUA JUMUWATA(Jumuiya ya Wanablogu Tanzania).

Tafadhali naomba ufungue hii kurasa ya
http://blogutanzania.blogspot.com/
kisha upendekeze jinsi ya kufufua JUMUWATA.
Ahsante
Luiham Ringo.