Tuesday, August 9, 2011

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI 9/08/2011 BUNGE KUCHUNGUZA UFISADI UDA


Ndugu Wanahabari, Suala la Ubinafsishaji wa Shirika la UDA limeibua hisia kali miongoni mwa Wabunge, vyombo vya habari na wananchi kwa ujumla. Suala hili limekuwa tata na kuzusha kila aina ya maneno. Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma imeona ipo haja ya msingi ya suala hili kuchunguzwa kwa kina na mhimili wa Bunge.

Kwa hiyo, imemuandikia barua Spika wa Bunge, ikimuomba aridhie mapendekezo ya wabunge watakaoundakamati ndogo ya Bunge chini ya Kamati hii ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma, ili ichunguze sakata zima la uuzwaji wa Shirika la UDA.

Uchunguzi huu umependekezwa kufuatia hisia kwamba taratibu za kuuza Shirika hili pamoja na mali zake hazikuzingatia Sheria za nchi na hivyo kupelekea Taifa kuwa katika hatari ya kupoteza mali.

Kwa mujibu wa Kanuni za Bunge Toleo la mwaka 2007, nyongeza ya sita kifungu cha 13(e),Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma ina jukumu la kufuatilia ‘Utekelezaji wa Sera ya Ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma’ na kanuni ya 13(d) ‘kufanya tathmini ya ufanisi wa Mashirika ya Umma’. Ili kutekeleza majukumu haya, Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma imemuomba Mhe. Spika aridhie kuundwa kwa kamati ndogo ili kufanya uchunguzi wa suala la Shirika la UDA.

Hadidu Rejea

Hadidu rejea za Kamati ndogo ya uchunguzi inayopendekezwa ni kama ifuatavyo:

i. Kuchunguza kama katika zoezi la kubinafsisha Shirika la UDA taratibu zote za Sheria zilifuatwa.

ii. Kuchunguza kama Ofisi ya Msajili wa Hazina na Shirika Hodhi la Mashirika ya Umma (CHC) walitimiza wajibu wao ipasavyo katika zoezi zima la ubinafsishaji wa Shirika la UDA.

iii. Kuchunguza kama Bodi ya Shirika la UDA ilifuata sheria na kanuni katika kuuza hisa zilizouzwa za Shirika la UDA na kama walikuwa na mamlaka ya kufanya hivyo bila kuhusisha wana hisa. Pia kuchunguza nafasi ya Bodi kwa umoja wake na mjumbe mmoja mmoja wa Bodi katika zoezi zima husika.

iv. Kuchunguza nafasi (role) ya wana hisa (Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam na Serikali) katika zoezi zima la kuuzwa kwa hisa (unalloted shares) za UDA kwa Kampuni ya Simon Group.

v. Kuwaita mbele ya Kamati wadau wote wa suala la UDA hususani Bodi ya UDA iliyokuwepo, Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la UDA, Mmiliki wa Kampuni ya Simon Group ltd,Msajili wa Hazina, Mkurugenzi Mkuu wa CHC, Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na mtu mwingine yeyote yule itakavyoonekana inafaa.

vi. Kufanya tathmini ya Shirika la UDA katika mazingira ya sasa ya biashara ya usafirishaji Jijini Dar es Salaam.

vii. Kutoa Mapendekezo ya hatua za kuchukua dhidi ya watakaobainika kuwa na makosa katika zoezi zima la Ubinafsishaji wa Shirika la UDA.

viii. Kupendekeza namna bora ya kuendesha Shirika la UDA.

Ukomo

Kwa kuwa mamlaka nyingine za Uchunguzi zinaendelea na uchunguzi wake, Kamati hiyo ya Bunge itajikita katika maeneo yaliyoainishwa hapo juu tu na haitahusika na suala kama la rushwa au Mahesabu ambayo yanashughulikiwa na TAKUKURU na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali.

Isipokuwa Kamati inaweza kuhitaji msaada wa Taasisi hizi katika kutimiza wajibu wake wa uchunguzi wa kibunge. Bunge, kwa namna yoyote ile, halitazuiwa kuendelea na uchunguzi wake wakati Serikali (Executive) ikitimiza wajibu wake. Izingatiwe kuwa uchunguzi huu pia unahusisha Taasisi za Serikali zenye mamlaka ya masuala ya Ubinafsishaji na utunzaji wa Mali ya Umma (hivyo Serikali pia inachunguzwa).

Muda wa Uchunguzi

Nimependekeza kuwa uchunguzi huu uchukue jumla ya Siku 14 (kumi na nne tu) na kuwasilisha taarifa yake kwa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma na kisha kwa Spika ambaye ataelekeza hatua zitakazofuatia.

Wajumbe wa Kamati Ndogo ya Uchunguzi.

Kwa kuwa Uchunguzi huu unahusisha mambo mengi, nimependekeza kamati hiyo ndogo ihusishe Wabunge wengine katika uchunguzi huu badala ya wajumbe wa Kamati ya Mashirika ya Umma peke yake.

Wajumbe wafuatao wanapendekezwa kuunda Kamati ndogo.

1. Mhe. Murtaza Mangungu, Kilwa Kaskazini (Kamati ya POAC) – Mwenyekiti

2. Mhe. Esther Bulaya, Viti Maalum (Kamati ya POAC)

3. Mhe. Amina Mwidau, Viti Maalumu (Kamati ya POAC)

4. Mhe. David Kafulila, Kigoma Kusini (Kamati ya LAAC)

5. Mhe. Angellah Kairuki, Viti Maalumu (Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala)

6. Mhe. Herbert Mtangi, Muheza (Kamati ya Miundombinu)

7. Mhe. John Mnyika, Ubungo (Mwakilishi Wabunge wa Dar es Salaam)

Katibu wa Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma na Katibu wa Kamati ya Sheria ndogo wanapendekezwa kuwa Makatibu wa Kamati ndogo ya Uchunguzi wa Ubinafsishaji wa Shirika la UDA.

Ni matarajio yangu na ya wenzangu kuwa Spika wa Bunge, Mhe.Anne Makinda ataridhia kuundwa kwa Kamati hiyo, ili Bunge liweze kuchukua wajibu wake wa kiuchunguzi na wa kuisimamia Serikali. Ninaamini, uchunguzi huo ndio utakaokata mzizi wa fitina kuhusu nani amehusika na achukuliwe hatua gani zichukuliwe kwa maslahi ya Wakazi wa Jiji la Dar es

Salaam na Taifa zima kwa ujumla.

Nashukuru kwa kunisikiliza.

Kabwe Zuberi Zitto (Mbunge)

Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma

No comments: