Friday, August 12, 2011

MFALME JUHA NI NANI HASA KATIKA TANZANIA YA WASIOIJUA?Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

WENGI wetu tunafahamu kisa cha Mfalme Juha. Ni miongoni mwa visa vya zamani vinavyojulikana katika lugha mbalimbali zaidi ya 100 duniani. Ni simulizi inayohusu Mfalme ambaye alikuwa anajali sana jinsi anavyoonekana kwa watu, mwenye kupenda makuu na ambaye alikuwa tayari kupata kila anachokitaka.

Mfalme huyo, katika kujiremba zaidi, akaamua kuajiri mafundi cherehani wawili ambao walimuahidi kumshonea vazi la kisasa, la ajabu na ambalo “material” au kitambaa chake ni cha ajabu, na hakiwezi kuonekana kwa mtu yeyote yule asiyestahili nafasi ile au mtu ambaye ni juha mkubwa.

Mafundi cherehani hao walitumia muda mrefu kuchukua vipimo mbalimbali vya mwili na mara moja wakaanza kuonekana wakifanya kazi ya kutengeneza nguo ile au vazi lile la ajabu. Watu waliwaona wakikata nguo kwa mikasi wakigeuza geuza kitambaa kisichoonekana na wakati ulipofika wakaanza kukishona asubuhi hadi jioni kwenye cherehani zao.

Walipomaliza kazi yao hiyo ngumu, wakaenda kwa heshima zote kumvisha mfalme vazi lake lile la ajabu. Baada ya kuhakikisha Mfalme amevua nguo zake zote wakamvisha vazi lake lisiloonekana kwa watu wajinga, majuha na wale wasiostahili nafasi kuu.

Kwa vile mfalme hakutaka aonekane juha, akaanza kusifia anavyoonekana na mafundi wakimsifia vile vile alivyopendeza. Wasaidizi wake nao walimsifia kuwa nguo hiyo ‘ya ajabu isiyoonekana’ ilikuwa imemkaa vizuri, na yeye kwa mbwembwe alijizungusha zungusha kwa mikogo.

Kwa vile nguo aliyovaa ilikuwa ni ya “ajabu na isiyoonekana” ikabidi ioneshwe hadharani katika gwaride ambapo Mfalme alivaa vazi hilo na kupitishwa kwenye gari la wazi likokotwalo na farasi.

Kwa vile alikuwa ni mfalme katili vile vile, kila aliyemuona alilisifia “vazi hilo” ili asije akaonekana ndiye juha au mtu asiyestahili, hivyo wasomi, wanasayansi na wanasiasa wote walijikuta wanamsifia Mfalme katika “vazi lake la ajabu lisiloonekana”.

Ilikuwa katika mtaa mmoja ambapo Mfalme alikuwa anapita na vazi lake hilo; huku watu wamejipanga mistari wakimsifia ndipo mtoto mmoja mdogo alishtuka na kupiga kelele: “Mfalme hajavaa nguo, yu uchi!!” na kurudia kelele hizo; huku akiangusha kicheko na ndipo Mfalme akashtuka na watu wakaanza kucheka na ikabidi akimbizwe kuondolewa soni yake.

Kutokana na simulizi hiyo, mfano umekuwa ukitungwa katika mazingira mbalimbali ambayo inahusiana na kusema ukweli kwa watawala au kwa watu wengine bila hofu ya kutaka kujipendekeza. Yaani kuwa na ujasiri wa kuwaambia watu wasiotaka kuambiwa kuwa “hawajavaa nguo”; licha ya wao wenyewe kuaminishwa kuwa wamevaa nguo nzuri na za kupendeza.

Tunao waishio kama Mfalme Juha

Katika siasa zetu nchini, sasa hivi kuna watu ambao wanaishi kama Mfalme Juha. Wanapenda kusifiwa, na kwa kila namna hujipitisha ili kutafuta sifa zaidi na huridhika na sifa hata kama ni sifa za kijinga.

Lipo kundi kubwa la watu ambalo linavalishwa, kila kukicha, vazi lisiloonekana na ambalo wanaambiwa linawapendeza, na wao wenyewe badala ya kuhoji mantiki ya vazi kama hilo au hata uhalisia wake, hujiangalia kwa kioo na kujikuta wako watupu lakini hawataki kuukubali ukweli ulio mbele ya macho yao, na hivyo hugeuka na kujisifia kuwa “nguo imewakaa”.

Ndugu zangu, kwa muda mrefu mfano huu wa Mfalme Juha umewahusu watawala wetu mara kwa mara au baadhi ya watawala hao, na maandishi ya watu mbalimbali yamekuwa yakitudokeza kuwa watawala wanahitaji kuambiwa ukweli kwamba “hawajavaa nguo” ili hatimaye waweze kujihifadhi utupu wao.

Hata hivyo, naomba nipendekeze kwako mpendwa msomaji kuwa leo hii Mfalme Juha katika Tanzania siyo watawala tena; bali ni watawaliwa. Ni sisi Watanzania ambao tumeamua kufumba macho kwa ukweli uliopo mbele yetu na kuishi katika sifa za kijinga na uongo; huku tukijionesha kuwa tunastahili sifa hizo.

Tumegeuzwa kama ma-supamodo

Tumegeuzwa kama ma- supamodo ambao hutembea kwenye jukwaa kwa mbwembwe; huku wakiamini kuwa wamevaa mavazi mazuri kupita kiasi kumbe wako watupu; huku alama za makovu, na vilema vyao vya miili vikiwekwa peupe! Angalau wale wenye kuvaa bikini hujihifadhi sehemu fulani fulani lakini hawa wengine hutembea wakiwa watupu.

Tumekubali kulishwa sifa za kijinga kutoka kwa mafundi cherehani wetu ambao wanatumia nafasi zao kutulaghai. Mafundi cherehani hawa wa maneno – a.k.a wanasiasa husimama kwa mbwembwe na kutuambia “nchi yetu imejaliwa kila utajiri’, wengine husimama na kutuambia “Tanzania imebarikiwa sana na imependelewa sana duniani”.

Katika ulevi wetu wa sifa za kijinga tunakenua meno na kuchekelea kwa sababu tunaamini tunaambiwa ukweli, na hivyo huanza kutembea kwenye magari yakokotwayo na farasi wa mbinu za kisiasa tujikipitisha kwa mbwembwe kuwa “tumevaa nguo safi, ya ajabu isiyoonekana”.

Ukiwasikiliza kwa mfano kule Bungeni au ukipitia vitabu vyao vya mipango ya maendeleo unaweza ukaamini kabisa kuwa Tanzania inaweza kuwa pepo au tayari ni pepo. Nakumbuka mmoja wa wanasiasa aliyewahi kutuhubiria “Tanzania inapaa”, na akashangiliwa! Na wapo ambao kwa kweli wanaamini kabisa kuwa Tanzania imepaa na imepiga hatua ya haraka ya maendeleo ya kuazimwa.

Tunafurahia sifa za kijinga

Lakini ni sisi Watanzania ambao tunafurahia sifa hizi za kijinga, na wenyewe tunasifiana kwa sifa za kijinga - yaani zisizo na ukweli. Huwa naangalia mijadala kwenye baadhi ya vipindi kwenye luninga, na naona vijana wanavyozungumza kwa hamasa kuhusu “Tanzania imebarikiwa sana” na kuwa “tuna utajiri mwingi!”

Ukweli ambao watu hawataki kuuzungumza kwa wazi ni kuwa tuko watupu! Tumevuliwa nguo za utu wetu, tumedharaulishwa mbele ya jamii na ukweli ni kwamba pasipo kuamua kujihifadhi siku moja watoto wetu watasimama na kutuambia ukweli.

Fikiria! Wakati baadhi ya watu wanakwepa uzito na ubaya wa ufisadi nchini na kujaribu kutufanya tuone kuwa ni “jambo la kawaida” ukweli ni kuwa ufisadi ndilo tatizo kubwa kwenye maendeleo yetu kuliko kitu kingine chochote.

Kama tukikubali taarifa mbalimbali zinazoonesha kuwa tumepoteza karibu dola bilioni 10 katika miaka kumi kwa ufisadi (zaidi ya Sh. trilioni ), na bado hatujakasirika, ni wazi kuwa tunaamini tumevaa kitambaa kisichoonekana!

Fikiria! Wakati sisi wengine tumepigia makelele bodi ya mikopo ya elimu ya juu kuwa ni taasisi mbovu na iliyohitaji kuvunjwa miaka kadhaa huko nyuma leo tunaambiwa ati imeshindwa kurudisha mikopo ya karibu Sh. bilioni 100. Na hawachelewi kutuambia kuwa katika kipindi kijacho watatoa mikopo mingine mingi!

Hadi leo hii hakuna uchunguzi wa maana umewahi kufanyika kwenye bodi hiyo na wahusika wake licha ya madai mazito ambayo sisi wengine tuliweka hadi vielelezo vyake miaka minne hivi iliyopita. Bado wanaendelea kutuambia kuwa “mfalme amevaa vazi lisiloonekana!”

Fikiria! Wakazi wa Dar wanaishi katika mkoa tajiri kuliko yote Tanzania, wenye nafasi lukuki za mafanikio na unaochangia kiasi kikubwa sana katika kodi Tanzania kuliko mkoa mwingine wowote. Mkoa ambao una wasomi wengi, una uharaka wa taarifa na habari kuliko mkoa mwingine wowote ule! Lakini ni hawa hawa wanaishi katika madimbwi ya matope, umeme wa shida, kipindupindu, hospitali za kupokea wafu nk! Lakini watu hawa hawa wanakaa chini na kuambiwa na wanasiasa kuwa “Dar ni jiji zuri la kisasa” na wao hucheka na kushangilia!

Hata kuuzwa UDA kifisadi hakutukasirishi?

Fikiria! Sakata la uuzwaji wa UDA shirika la umma. Skandali hiyo nayo bado haijawaudhi watu wa Dar! Watu wamekaa pembeni wakisubiri kuona nani anashinda kati ya kina Iddi Simba , Kisena na Masaburi.

Walio matajiri na wenye uwezo hawataki kufikiria kuwa kuboreshwa kwa usafiri wa umma kutapunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa magari mabovu na yasiyo ya lazima.

Ukienda kuishi au kufanya kazi jiji la New York, Marekani (kwa mfano), huhitaji gari lako binafsi! Unaweza kuishi miaka nenda rudi bila kuwa na hitaji la gari; kwani usafiri wa umma umeboreshwa – na mabasi yao ya UDA yanamilikiwa na Umma kwenye jiji la Ubepari uliokubuhu! Wanatumia sera hiyo ya mali ya umma ili kuujenga Ubepari!

Fikiria kuwa katika jiji la Dar ukizungumzia kurudisha shirika la UDA mikononi mwa Umma na kuliunganisha na DART – taasisi nyingine ya Umma hawatachelewa kuja na kutuimbia wimbo wa “sera zetu ni za soko na hivyo serikali haitaki kujihusisha na biashara”.

Hawajui kwamba usafiri wa umma si biashara; bali ni huduma ya lazima. Hata hivyo, wakazi wa Dar hawawezi hata kuuliza hilo; hawawezi kuuliza kwa nini London, Berlin, Paris, Copenhagen ambazo ziko kwenye nchi za kibepari wana usafiri unaomilikiwa na Umma na kutegemewa na Umma, lakini sisi ka-nchi ambako hata Ubepari wenyewe tumeshauvurunda, tunashindwa kuwa na usafiri wa Umma?

Jawabu liko wazi, watu wa Dar wameshalewa sifa za kijinga kuwa “Dar tambarareeee” na kuwa “maisha ya Dar ni bora zaidi”, na hivyo wamevaa vazi lisiloonekana.

Ukweli huu unawahusu Watanzania wengine vile vile. Kila mahali ambako kuna upungufu wa kila namna na mahali ambapo tungeweza kufanya vizuri zaidi kujenga majiji ya kisasa, tunaambiwa kuwa mambo siyo mabaya sana, na hivyo tunageuka kimikogo na kujirembua; huku tunapigwapigwa picha.

Hivyo, mtu anajitahidi kununua nguo nzuri za kutokea na anapendeza kweli, lakini pale mtaani kwake maji machafu yamezagaa, choo hakiko salama, na usalama wenyewe wa kunyemelea!

Vijana nao wamebweteka

Vijana wa Dar ambao tungetegemea ndio wawe wanaamka na kutamani mambo makubwa na kushiriki kubadilisha maisha yao na kuanza kuvisha nguo jamii yao ili isiiabike, wamebakia kufukuzia ndoto ya kuwa nyota wa bongo fleva au kufukuzia nyama choma na siku mbili tatu kusikia ni super star gani mwingine kutoka majuu anakuja kuwapa burudani katika umaskini wa fedheha zao; huku wakilindwa na vyombo vya dola!

Ndugu zangu, tuna uamuzi wa kufanya kama mtu mmoja mmoja au kama jamii. Je tutaendelea kusifiwa kuwa mambo ni mazuri, na hivyo tusijiangalie kama tuko watupu au la?

Je tutaendelea kupuuzia changamoto zilizoko wazi katika elimu na mashule yetu kwa sababu watawala wanatuambia “tumejenga UDOM na sasa tunajenga Chuo cha Mandela” wakati bado kuna maelfu ya watoto wanaishi na kusoma katika mazingira hatarishi na yenye kuuweka rehani utu wao?

Ni kwa kiasi gani Watanzania wataendelea kuchekelea kauli za kilaghai za baadhi ya wanasiasa ambazo zinawapamba katika umaskini wao?

Yaani; mtu amevaa nguo anapendeza na kakaa juu ya kifusi cha uchafu. Anakuja mwanasiasa na kuanza kumsifia kwa jinsi alivyovaa jeans ya kupendeza, wanja mzuri, midomo iliyotiwa lipstick na manukato yake mazuri. Na yeye anajigeuza kwa mikogo juu ya shimo la taka?

Au ni kwa kiasi gani Watanzania, wake kwa waume, watakuwa wanazungumzia “mafanikio” wakati matatizo yao bado yako dhahiri. Je tunahitaji watoto waje kutuambia kuwa Taifa zima halijavaa nguo ndio tushtuke? Siyo kwamba tutakuwa tumeshachelewa; kwani aibu yetu itakuwa imeshawekwa wazi?


RAIA MWEMA

No comments: