Thursday, August 25, 2011

DOLA YAMBANA MWANDISHI WA GAZETI LA MWANANCHIMWANDISHI wa habari anayeandikia gazeti la Mwananchi kutokea Arusha, Mussa Juma, ameanza kuandamwa na serikali na sasa uraia wake umeanza kuhojiwa huku yeye akihusisha hatua hizo na msimamo wake katika kazi zake.

Habari zilizothibitishwa na vyombo vya dola zimeeleza kwamba Mussa amekua akifuatiliwa kwa muda mrefu sasa kabla ya kuitwa na kuhojiwa rasmi na vyombo vya dola akituhumiwa kuwa uraia wake una utata.

Mbali ya kuandika habari za uchunguzi na zile za kisiasa, Mussa amekua mstari wa mbele katika kuwaunganisha waandishi wa habari mkoani Arusha na mikoa jirani ya Manyara na Kilimanjaro, lakini pia amekua kiungo na waandishi wageni wanaotembelea Arusha.

Imeelezwa moja ya sababu zilizochochea kuandamwa kwake ni mgogoro wa kisiasa katika Manispaa ya Arusha ambao Mussa amekua na msimamo usioyumba katika kuandika taarifa za mgogoro huo.

Juma aliyejipambanua kutoegemea upande wowote katika uandishi wake alisema amekuwa akikwaruzana mara kwa mara na viongozi wa serikali wasiopendezwa na habari hizo ambao walimtumia ujumbe kumtaka ajihadhari kwani serikali ina mikono mirefu ikiamua itamshughulikia.

“Baada ya kuripoti kwa kina utata katika tukio la uchaguzi wa Meya na vurugu zilizosababishwa na maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), mapema mwaka huu, nilianza kuandamwa na baadhi ya watendaji wa Idara ya Usalama wa Taifa ambao walinionya niache kuandika habari za matukio hayo la sivyo ‘nitakiona’,” alisema Mussa Juma.

Alisema awali mmoja wa maafisa wa ngazi ya juu wa Idara ya Usalama wa Taifa Kanda ya Kaskazini (jina linahifadhiwa kwa sasa) alituma mmoja wa waandishi wa habari mkongwe mjini Arusha Mwanaidi Mkwizu kumuonya Mussa asiendelee kuandika habari za mgogoro wa umeya kwa usalama wake kwani akiendelea yangemkuta makubwa.

“Baada ya kupokea ujumbe huo, nilimpigia simu afisa huyo ambaye alikiri kumtuma mwandishi huyo huku akidai alifanya hivyo kwa nia njema ya kunionya na kunihurumia kwa mabaya yaliyokuwa mbele yangu iwapo ningekaidi ushauri huo. Kwa ajili ya ushahidi nilirekodi mazungumzo yangu yote na afisa huyo,” alisema Mussa Juma

Alisema pamoja na tukio la umeya, afisa huyo pia alimtuhumu kuishambulia na kuiumbua serikali katika tukio la mgogoro wa jamii ya Wamaasai wa eneo la Lololiondo wilayani Ngorongoro na kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Oterllo Business Co-oparation (OBC) na pia mgogoro wa Mashamba ya NAFCO wilayani Hanang.

Kilele cha vitisho na ujumbe alizotumiwa kilifika juzi baada ya maafisa wa Idara ya uhamiaji mkoani Arusha kufika ofisi za gazeti hili kumtafuta Musa na walipomkosa waliamua kumpigia simu yake ya kiganjani wakimtaka kufika ofisini kwao siku inayofuata, Agosti 23, mwaka huu, saa 3 asubuhi bila kumweleza sababu za wito huo.

Akiwa ameongozana na wakili wake, Shilinde Ngalula na mmoja wa wafanyakazi wa Mwananchi mkoani Arusha Peter Saramba, Mussa alifika ofisi za uhamiaji na kutakiwa kutoa maelezo lakini Ofisa huyo wa uhamiaji alikataa kufanya mahojiano wakati mwanasheria na mfanyakazi huyo ya mwananchi yupo, jambo lililozua mgogoro uliodumu saa mbili.

Hata hivyo baada ya mashauriano baina ya Mussa Juma na wakili huyo, ambaye ni mkuu wa Kituo cha Sheria na Haki za Binaadamu mkoa wa Arusha, walikubaliana watoke nje ya ofisi na ndipo mahojiano yalianza na Mussa Juma kuandika maelezo.

Maelezo ya uraia wake kwa kujaza fomu maalumu kuonyesha jina lake, jina la wazazi wake, ndugu zake na mahali walipozaliwa.

Maelezo hayo yaliandikwa mbele ya mkuu wa upelelezi wa Idara ya uhamiaji mkoa wa Arusha, Embrosy Mwanguku ambaye baada ya kuyapitia alimruhusu kuondoka kwa maelezo kuwa akihitajika ataitwa.

Afisa huyo, hata hivyo,wakati akichukuwa maelezo ya Mussa Juma, alikiri kumfahamu kama rafiki yake kwa muda mrefu lakini anachofanya ni kutekeleza maagizo ya ngazi za juu.

“Mimi na Mussa hatuna matatizo, tunafahamiana muda mrefu na hatuna matatizo na ndio sababu suala hili tangu mwezi wa kwanza tumekuwa tukifuatilia ili tumhoji tukaambiwa yupo Samunge tukamsubiri hadi amerudi”alisema Mwanguku.

Wakati mwandishi aliyetumwa kumfikishia ujumbe juma alikiri alipozungumza jana kwa njia ya simu, Ofisa anayetuhumiwa kuhusika katika tukio hilo hakuweza kupatikana jana baada ya kutokuwepo ofisini kwake na hata simu yake ya kiganjani ilikuwa haipatikana. Juhudi za kumtafuta zinaendelea ili kuthibitisha iwapo hatua hii ya sasa dhidi ya Mussa Juma ni utekelezaji wa onyo lake.

Akizungumza mara baada ya kuhojiwa Mussa Juma alisema anaamini uhamiaji wametumwa na wakubwa zao kumfuatilia kutokana na masuala ya kisasa na utekelezaji wa kazi zake za uandishi.

“Sasa naweza kusema maisha yangu yapo hatarini kwani kuna mengi yametokea tangu uchaguzi mkuu na hata kabla ambayo yanatokana na vitisho ya dola lakini naamini nilichokuwa nafanya na ambacho ntaendelea kufanya kuwa sawa na sikiuki maadili ya uandishi wa habari,”alisema Mussa Juma.

Alisema kama vyombo vya dola vinaona kuwa uandishi wake na mwenendo ya gazeti la Mwananchi si sahihi kuna taratibu za kufuata ili madai yao yafanyiwe kazi.

“Nimekuwa mwandishi kwa zaidi ya miaka 15 sasa sijawahi kushitakiwa kwa kuandika habari zozote za uchochezi au kupotosha sasa nashangaa vitisho dhidi yangu,” alisema Mussa Juma.


FIKRA PEVU

No comments: