Saturday, July 9, 2011

WANA CCM FUNGENI MIDOMO YENU


Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

SUALA hili nilipata kulijadili huko nyuma, lakini nimeamua kulirudia tena ili kukumbusha kwamba wana CCM waliowachagua wabunge wa CCM na kuwarudisha madarakani na wale waliomrudisha Rais kutoka CCM, wamepoteza haki ya kulalamikia utendaji wa serikali kwa miaka mitano ijayo.

Ninavyosema hivi nina maana ya kwamba walipoamua kuwarudisha watu wale wale, wenye sera zile zile kutoka chama kile kile, walikuwa wamekubali matokeo yale yale.

Leo hii tunaanza kuwasikia wanasiasa wa CCM, wanachama na mashabiki ambao nao hujitokeza kwa namna moja kushangaa na kulalamikia serikali. Kuanzia masuala ya elimu na utekelezaji wa miradi mbalimbali, tunawasikia kwenye vyombo vya habari, na hasa kule Bungeni wakielezea mapungufu mbalimbali.

Mfano mzuri wa yote ni suala la upungufu wa nishati ya umeme nchini. Imetokea (tena inashangaza) baadhi ya wabunge wa CCM na viongozi wake wanamlaumu sana Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja; huku wengine wakizungumza kwa “ukali na uchungu” wakitaka awajibishwe. Wengine wanambebesha mzigo wa lawama za tatizo la umeme nchini; eti “ameshindwa kutatua tatizo la umeme”. Kweli?

Ndugu zangu, sote tunajua kuwa kwa miaka 50 tumekuwa chini ya utawala wa chama kimoja. Ni chama hicho kimoja ndicho kimetunga sera, sheria na kusimamia utekeleza wa sera hizo na sheria mbalimbali ambazo ZOTE zimepitishwa na wabunge wa CCM.

Sote tunajua vizuri kabisa mabadiliko ya kiuchumi na ongezeko la watu siyo vitu ambavyo vimeshushwa toka mbinguni mwaka jana!

Tatizo la umeme Tanzania halikuanza na Kikwete wala halijaanza chini ya Waziri Ngeleja. Lilikuwepo akiwepo Karamagi, lilikuwepo alipokuwepo Msabaha na lilikuwepo alipokuwepo Kikwete! Kama hamuamini someni bajeti za wizara hiyo kwa miaka 20 iliyopita mtakutana na hoja zile zile, mipango ile ile na ahadi zile zile! Kumlaumu Ngeleja ni jaribio dhaifu la kukwepa kupeleka lawama kunakohusika.

Kwa miaka 20 ya utawala wa Mwinyi na Mkapa, hakukuwa na uwezekaji mkubwa katika sekta ya nishati zaidi ya kuliingiza taifa katika mzigo wa mikataba mibovu ya nishati ambayo hadi leo inaligharimu taifa. Ngeleja hakuliingiza taifa kwenye mikataba hiyo. Au mmesahau aliyekuwa waziri wa Nishati na Madini wakati huo alikuwa nani? Au niwakumbushe wana CCM kuwa ndiye waliyempitisha baadaye kuwa mgombea wao wa Urais na sasa ni rais?

Lakini hata yeye hatuwezi kumbebesha lawama! Lawama zinaangukia Chama Cha Mapinduzi; kwani ndicho ambacho kinatunga sera za nchi, ndicho ambacho kinatunga sheria na ndicho ambacho kimeunda serikali! Sasa iweje wamlalamikie Ngeleja kama sio jaribio la kuficha ukweli?

Wengine wanasema eti “mikabata ilikuwa na vipengele vibovu”! Kweli? Hivi vipengele vibovu tumekuja kuvigundua leo? Hivi vipengele vibovu ndio tumejua ubovu wake lini? Baada ya IPTL? Songas? Richmond? Dowans? Au lini hasa? Na tulipogundua vipengele vibovu tulisema nini?

Nitawakumbusha tulichosema. Akiwa katika mojawapo ya ziara zake huko Scandinavia, Rais Kikwete aliutangazia ulimwengu kuwa kwenye masuala ya mikataba hatuna “wataalamu wenye uwezo”! Naam, Rais wa nchi ametuambia kuwa hatuna wataalamu wenye uwezo!

Kweli? Sasa na mababu zetu waliosainishwa mikataba mibovu na kina Karl Peters na wenzake wao wangesema nini?

Leo hii, serikali hii hii imeanza kuruhusu kupangisha ardhi yetu kwa kisingizio cha “kupunguza tatizo la chakula” kwa mashirika, na makampuni makubwa ya kikabaila - mmeuliza vipengele vya mikataba hiyo vikoje? Hivi mmeangalia vipengele vya mikataba ya utafutaji madini? Mnataka tumlaumu Ngeleja?

Hivi mnajua ni kwa nini hata ardhi hatukutaka kuiweka kuwa ni ya mtu binafsi, lakini leo chini ya ma-genius wetu wa CCM ardhi yetu (baada ya madini, wanyama n.k) inaanza kubinafsishwa kinyemela kwa makampuni makubwa ya “kilimo cha mazao ya mimea ya mafuta”!

Tumeambia kuwa miwa, mihogo, mahindi n.k vinaweza kutoa mafuta ya dizeli kwa kutumia kwenye magari n.k; nasi tumerukia kwa furaha, na sasa tunataka kujisifia kuwa tumepiga hatua? Hivi huko Marekani mbona kuna maeneo mengi tu ya kilimo; kwa nini wasilime huko?

Baadhi ya mikataba (na siku nikifyatua tutaiweka hadharani) imewapa wawekezaji hawa wa kimataifa maeneo ya ardhi kwa ajili ya kulima mazao ya chakula - kwa ajili ya nchi zao! Tuko tayari kuwahamisha wananchi wetu na kunyang’anya maeneo ya vijiji kwa “mikataba” ili kuwapatia watu hawa! Halafu hao wana CCM kwenye hivyo vijiji watakapopata njaa ndio wanakuwa wa kwanza kulia “serikali itukumbuke!”

Watanzania walipewa nafasi ya kusahihisha makosa ya miaka 25 ya uongozi wa CCM hii ya Mwinyi, Mkapa na Kikwete. Hawakutaka kusahahihisha makosa hayo, wakataka kuendelea na kile walichokizoea. Na wengine katika woga wa kutishwa na wengine wakakubali kuuza haki yao kama Watanzania ili wasilete mabadiliko kwa sababu mabadiliko yangemuondoa au kuwaondoa watu wanaowapenda.

Sasa leo hii tunapoanza ngwe hii kuelekea 2015 kuna watu wamepoteza haki ya kulalamikia serikali. Hatutaki kusikia watu wa Dar es Salaam wanalalamikia misongamano ya magari, umeme, wala maji machafu, au nyumba zao zikiungua walalamikie “kikosi cha fire” au vyovyote vile.

Watu wa Dar es Salam walipewa nafasi ya kubadilisha utawala wao, lakini hawakutaka na badala yake wakakumbatia kile walichokizoea kwa miaka 50 na kwa hilo wakapoteza haki ya kulalamika.

Wana CCM wote na wananchi wote wengine walioirudisha Serikali ya CCM madarakani wamepoteza haki ya kulalamika. Sasa hivi inabidi wabakie kuimbiana nyimbo za “anameremeta… anameremeta” hadi 2015.

Ukifika mwaka huo, Watanzania watapewa tena nafasi ya kubadilisha maisha yao; wakikataa na kutaka kuendelea na watu wale wale, wenye sera zile zile zilioshindwa, wasije kuleta malalamiko yale yale!

Haiwezekani watu timamu wapande miiba halafu wakae pembeni wamefunga na kuomba wanategemea uote mchicha! Haiwezekani watu wale wale, wengine wasome, wamwagilie matuta ya miiba halafu wao na watoto wao wapeane ahadi kuwa tukijitahidi kumwagilia na kuweka mbolea, basi, mchicha utatokea! Hatutaki miiba ikikua watu hawa hawa wasimame na kuanza “ooh mbona tulimwagia na kuomba sana na kufunga ili uje mchicha!”

Ukipanda miiba utavuna miiba, ukipanda mchicha utavuna mchina. Kile ulichopanda, ndicho utakachovuna. Ukivuna usichopanda usilalamike. Ukiona wenzako wanapanda mchicha, na wewe changamka!


RAIA MWEMA.

No comments: