Tuesday, July 12, 2011

WABUNGE WAHOJI UFISADI WIZARA YA AFYALeon Bahati, Dodoma


WABUNGE wamehoji ufisadi wa Sh5.5bilioni unaodaiwa kufanyika katika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa vipindi viwili mfululizo, ambavyo ni kati ya mwaka 2008/09 na 2009/10.Lucha ya kugundulika ufisadi huo, wabunge hao walidai kwamba, hadi sasa haifahamiki ni hatua gani zilizochukuliwa dhidi ya wahusika.

Fedha hizo zinadaiwa kutumika vibaya kwa kulipa mishahara hewa, malipo ya masurufu yasiyo na nyaraka stahili, ununuzi wa vifaa na mali bila nyaraka zinazotakiwa kisheria pamoja na mapokezi ya vifaa visivyo maelezo.

Tuhuma dhidi ya Wizara ya Afya zilitolewa bungeni na Kambi ya Upinzani kupitia kwa msemaji wake wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Antony Mbassa, alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi yake kuhusu makadirio ya bajeti ya Wizara hiyo.

Kwa mujibu wa Dk Mbassa ambaye pia ni Mbunge wa Biharamulo Magharibi (Chadema), mwaka 2008/09 ripoti ya Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), wizara hiyo ililipa mishahara hewa Sh17.7 milioni na kwamba tatizo hilo liliongezeka mwaka uliofuata 2009/10 ambao ripoti ilibainisha malipo ya mishahara hewa yanayofikia Sh83.8 milioni.

"Kama taarifa ya CAG ilifikishwa wizarani na kufanyiwa kazi, kwanini mambo yaliyotiliwa mkazo katika hoja za mkaguzi mwaka 2008/09 ndizo hizo hizo zilizojitokeza katika ukaguzi wa mwaka 2009/10?," alihoji Dk Mbassa na kuitaka Serikali ieleze hatua ilizochukua dhidi ya ubadhirifu huo.

Dk Antony alisema kinachoshangaza ni makosa hayo kujirudia kila mwaka, huku serikali ikiaa kimya bila kuwachukulia hatua zinazostahili wahusika.Alisema mwaka 2008/09 mbali na kulipa mishara hewa pia kulikuwa na malipo yenye shaka ya masurufu yanayofia Sh312.8 milioni na malipo yasiyo na nyaraka ya Sh157 milioni.

"Mwaka uliofuata 2009/10 wakaongeza kasi ya ubadhilifu kwa mishahara hewa kufikia Sh83.8 milioni, malipo yenye nyaraka pungufu Sh598 milioni, malipo kwa vifungu visivyohusika Sh3.4 bilioni, ununuzi wa vifaa visivyo na nyaraka 13.5 milioni, mapokezi ya vifaa visivyo na maelezo Sh20 milioni na madeni yasiyotarajiwaSh802 milioni,” alisema.

Watumishi hewa
Dk Mbassa alilaumuuwekaji mbaya wa kumbukumbu zinazowahusu wafanyakazi, jambo ambalo linasababisha watu wenye tabia za kifisadi kutumia mwanya huo kufuja kodi za Watanzania.Alisema Serikali inaweza kuondokana na tatizo hilo kwa kutumia mfumo wa raslimali watu kutoka kwenye Kitengo cha Ajira (Human Resources-Geographical Information System).

Kadhalika Dk Mbassa aliitaka wizara ya afya kuto taarifa zinazohusu maendeleo ya utafiti wa chanjo ya ukimwi, ambayo ulifanyika nchini kimya kimya kwa nyakati tofauti.Waziri kivuli huyo alisema moja ya majukumu ya wizara ni kuwapa wananchi taarifa zinazohusu maendeleo ya shughuli za afya nchini."Mpaka sasa wananchi wangependa kujua hali ya utafiti wa chanjo ya ukimwi uliyofanyika kwa baadhi ya makundi ya watu. Wangetaka kujua maendeleo yake yako je na hatua gani zinaendelea kufanyika ili kufanikisha mpango huu," alihoji Dk Mbassa.

Bajaji kubeba wagonjwa
Kambi ya upinzani bungeni pia, imepinga mpango wa serikali wa kutumia Sh5 bilioni kwa ajili ya kununua magari ya kubebea wagonjwa ya matairi matatu zipatazo 420.

Dk Mbassa alisema magari hayo yanazotarajiwa kutumika kwenye vituo vya afya vya vijijini, hayatakuwa na maana kwa sababu njia nyingi hazipitiki kwa kipindi chote cha mwaka.

Mipango ya Serikali
Wakati huohuo, Serikali imesema katika kipindi cha mwaka 2011/12, wizara itafuatilia mwenendo wa na viashiria vya milipuko ya magonjwa na kudhibiti milipuko.

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Hussen Mponda, alisema wizara itaandaa mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya mbu waenezao malaria katika kata zote 90 za mkoa wa Dares Salaam na kuendeleza katika mikoa mingine.

Akiwasilisha makadirio ya bajeti ya wizara yake bungeni jana, Waziri Mponda alisema Serikali itaanzisha mpango wa kutoa dawa za kuzuia kifua kikuu kwa watu waishio na VVU katika vituo 18 vilivyoteuliwa nchini na kununua mashine 150 za kupima CD4 na kuzisambaza katika vituo vya kutolea huduma za afya nchini.

"Pia wizara kwa kushirikiana na wadau itasambaza vifaa vya uzazi (delivery packs) 100,000 kwa wanawake wajawazito," alifafanua waziri.

Hospitali ya Taifa Muhimbili
Waziri alisema katika mwaka huo, Muhimbili itakamilisha ujenzi wa kituo cha Tiba na Mafunzo ya Upasuaji wa Moyo na kuanzisha Kitengo cha Uchunguzi wa Maradhi ya Mfumo wa Chakula.

"Vilevile, hospitali itakamilisha maabara ya kutengenezea vifaa vya usikivu kwa ajili ya kusaidia watu wenye ulemavu wa kusikia. Hospitali hiyo pia itaanzisha tiba ya mazoezi ya kuongea kwa wagonjwa wenye matatizo ya kuongea," alifafanua Waziri.

Mponda alisema Taasisi ya Mifupa (MOI), itaanza ujenzi wa awamu ya tatu ya hospitali hiyo huku Taasisi ya Saratani Ocean Road ikitarajiwa kutoa mafunzo ya uchunguzi wa saratani kwa wataalamu wa afya katika hospitali za rufaa za mikoa na kuendeleza ujenzi wa jengo lenye uwezo wa kulaza wagonjwa 170.

Kwa mujibu wa Dk Mponda, kila mkoa utatakiwa kupanga bajeti za kuendeleza hospitali za rufaa za mikoa ili kutoa huduma za afya za jumla na huduma za ubingwa.


"Wizara inaunga mkono juhudi hizo hasa kwa mikoa ambayo inaendelea na kazi za ujenzi, upanuzi kama mkoa wa Singida, Mara, Manyara na mengine ambako maandalizi ya dawa,vifaa na watumishi yatafanywa na wizara.

Kamati ya Bunge
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii, Dk Faustine Nugulile (Kigamboni-CCM), alisema Serikali kuu inachangia utendaji hafifu wa Bohari ya Dawa (MSD), ambayo wajibu wake ni kununua na kusambaza dawa kwenye hospitali, vituo vya afya na zahanati za serikali kote nchini.

Mara kwa mara MSD imekuwa ikilaumiwa kutokana na kushindwa kununua dawa kwa wakati, kusambaza kwa wakati pamoja na kushindwa kuzipatia uhakika wa dawa na vifaa vya afya.
Dk Ndugulile alisema Serikali inadaiwa na MSD Sh46 bilioni, ambazo zilizopangwa kwenye bajeti, lakini hazikutolewa kama ilivyotakiwa katika kipindi cha miaka mitano.

"Deni la Serikali kwa MSD linathiri utendaji, hiovyo tunaiomba iwapatie haraka," alisema Dk Ndugulile.
Ili kuisaidia MCD kutekeleza wajibu wake inavyopaswa, Dk Ndugulile alisema ni vyema halmashauri zote nchini zipeleke maombi ya dawa mapema iwezekanavyo, ikizingatia kuwa uagizaji wa dawa unachukua miezi tisa hadi kununuliwa na kuletwa nchini.

Ingawa Dk Ndugulile aliitetea MSD, kambi ya upinzani iliishutumu kwa kuagiza dawa ambazo huisha muda wake zikiwa hazijasambazwa hivyo kusababisha hasara kwa serikali.

licha ya dawa kuisha muda wake zikiwa ghalani, Dk Mbassa alizema MSD imeisababishia Serikali hasara ya Sh100 milioni kutokana na kutoa huduma za dawa kwa vituo vya afya hewa 45.Alisema kambi ya upinzani inashangazwa na hali hiyo hasa ikizingatiwa kuwa wananchi wengi masikini hasa waishio vijijini wanakufa kutokana na kukosa dawa na fedha kidogo zinazotengwa na Serikali zinaishia kwenye mikono ya wajanja.


MWANANCHI

No comments: