Thursday, July 28, 2011

TULIPOONGOZWA KUMSHINDA IDI AMIN TULIKUWA NA VIONGOZI
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

NINAJIULIZA kama viongozi tulionao leo hii wangekuwepo wakati wa kile ambacho Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere alikiita “chokochoko za Idi Amin” kinatokea sijui wangefanya nini. Nimeangalia igizo la bungeni ambapo tuliaminishwa kuwa wabunge wameguswa sana na tatizo la nishati na kugundua kabisa kuwa kile nilichokiandika karibu miaka miwili iliyopita kwenye gazeti hili bado ni kweli. Kwamba tatizo la Tanzania siyo sera wala hela! Tatizo lake ni uongozi.

Wakati Idi Amin ameanza chokochoko zake tishio kubwa lilikuwa kwenye mikoa ya kanda ya ziwa hasa Kagera na Mwanza. Tangu alipoingia madarakani baada ya kumpindua Milton Obote mwaka 1972, Idi Amin alikuwa ana kitu kinamsumbua kuhusu Tanzania na ni wazi Nyerere naye alikuwa anasumbuliwa na uwepo wa Idi Amin kule Uganda. Lakini majaribio mbalimbali ya kuzungumza na kutumia vyombo mbalimbali vya kimataifa ikiwemo OAU (sasa AU) kutafuta suluhisho bado kulikuwa na “damu mbaya” kati ya viongozi hao wawili.

1978 vikosi vya Idi Amin viliingia na kuvuka mto Kagera na kufanya uharibifu mkubwa. Na hata viliporudi na kupongezwa na Idi Amin mwenyewe huku wakimkabidhi Bendera ya CCM. Yeye mwenyewe Idi Amin aliwahakikisha wapiganaji wake kuwa Tanzania ikimjibu basi vikosi vyake vingeweza kwenda na kuipiga Tanzania hadi “Dar-es-Salaam”!!!.

Nyerere hakuwa katika haraka ya vita. Pamoja na uchokozi huo walitaka Idi Amin akanushe madai ya eneo la Tanzania, aombe radhi na alipie uharibifu. Kama yangefanyika hayo labda vita ya Uganda isingetokea. Idi Amin hakufanya hivyo na matokeo yake ni ule Mkutano Diamond Jubilee ambapo Nyerere alitoa ile hotuba maarufu ya “Nia Tunayo”.

Alipoamua kulipeleka Taifa vitani hakuamua tu hivi hivi. Na uamuzi ulipochukuliwa ulifafanuliwa vizuri kwa wananchi, tulijua kwanini tunaenda vitani, na tulijua maana ya kwenda vitani. Kila kona ya nchi watu walihamasishwa kusaidia vita tushinde. Na kweli tulishinda na zaidi ya kushinda. Kulikuwa na gharama kubwa sana, lakini hakuna gharama kubwa kama kuamua kuachia sehemu ya nchi kwa adui. Tulikuwa tayari kufa - na wapiganaji wetu walikufa kwa ajili ya kulinda eneo la ardhi yetu. Hatukuwa tayari kuachilia hata nchi moja kwa Idi Amin.

Ndugu zangu, ule ulikuwa ni uongozi uliotambua kuwa heshima na hadhi ya taifa lolote ni pamoja na kuhakikisha kuwa adui hachezei mipaka yake. Lakini yote yalitegemea sana uongozi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Baba wa Taifa.

Muda wa kuzungumza ulipita, muda wa kamati na vikao ulipita, mazungumzo na hotuba za wanasiasa zilipita. Ulifika wakati Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama ambao alitumia madaraka yake ya kuamuru. Naam, kutangaza vita ni jukumu zito zaidi kuliko kushughulikia umeme. Nyerere alijua matokeo ya uamuzi wake - yaani kuwapeleka baadhi ya Watanzania kwenye vifo vyao. Hakuna uamuzi mgumu kwa Rais yeyote duniani kama kuingia vitani. Lakini Watanzania tulikuwa tayari kulipa gharama hiyo na tukailipa.

Najiuliza hawa wanasiasa wetu wa leo wangekuwa wakati ule si tungeichia hadi Mwanza mikononi mwa adui? Najiuliza kwa miaka zaidi ya kumi watu wale wale kwenye chama kilekile chenye sera zile zile wamekuwa wakizungumza kwa jazba Bungeni na nje ya Bunge kutuambia hali mbaya ya tatizo la nishati. Najiuliza hawa wangekaa na Idi Amin hadi wazeeke. Kuna wakati wa kuzungumza na wakati wa kutenda.

Nimeshangazwa sana na kusitikishwa na uamuzi wa kukwepa kufanya maamuzi magumu na sahihi. Kwa mara nyingine Bunge la CCM limefanya uamuzi salama wa kuahirisha kushughulikia tatizo na badala yake kujipanga kuja kuzungumza tena baada ya siku ishirini na moja. Idi Amin angekuwa anacheza nao hawa kama paka anavyocheza na panya aliyekufa.

Kwamba, tatizo la nishati aidha ni kubwa kama wanavyotaka tuamini, au siyo kubwa kama tunavyooneshwa kwenye luninga na mazungumzo ya wabunge Bungeni. Kama ni kubwa na lenye athari za maisha na uchumi wa Watanzania basi linastahili kushughulikiwa kwa uzito wake. Kama siyo zito hivyo na siyo baya kiasi hicho kuzungumza, kamati, vikao, mikutano, semina, maelezo, hotuba, mipango, na michango ya Wabunge iendelee hadi mwaka 2015 au 2020 au miaka hamsini baadaye.

Wabunge wenyewe wanajisifia kwa kurudisha Bajeti iangaliwe upya. Na kuna watu watataka wapewe pongezi ati kwa sababu Bunge limekataa bajeti ya Ngeleja. Kama kweli kwanini wasingepiga kura waikatae? Kwanini walikubali tu? Wabunge wengi walizungumza wakitaka Ngeleja kujiuzulu. Kwa maneno mengine Wabunge hawana imani na serikali yao. Kuilazimisha serikali kubadilisha bajeti yake ni kutokuwa na imani na serikali hiyo. Jamani, kama wabunge wanataka wangeweza kuifanyia marekebisho. Naelewa hilo ndilo lengo sasa. Na wapo watu ambao watashangilia baada ya siku ishirini na moja watakapounga “mkono hoja”.

Ndugu zangu, kama hivyo ndivyo tunataka kushughulikia tatizo la nishati sawa. Tusiliite “janga la taifa” wala tusiite “hali ya dharura”. Kwa sababu kama ni janga basi sisi ni miongoni mwa watu ambao hatujui kushughulikia majanga kabisa. Tunashughulia kama tatizo dogo. Janga linahitaji hatua kubwa zaidi ya kubadilisha bajeti. Hali ya dharura inahitaji zaidi ya vikao vya Bunge.

Ninachosema ni kuwa haiwezekani kuwa na Urais ni taasisi na suala la Rais kuwa safarini bado si sahihi. Si sahihi kusikia kwamba hata Makamu wa Rais hawawezi kuchukua hatua yoyote kwa sababu “Rais hayupo”. Idi Amin ndugu zangu angekuwa amejitangaza kuwa ni Mfalme wa Bukoba!

Tunahitaji viongozi wa vitendo wenye kuelewa uzito wa mambo. Kama wabunge wanataka tatizo la nishati litatuliwe kwa njia za dharura, wamtake Rais Kikwete ambaye ni Amiri Jeshi Mkuu - sijui watu wanadhania hicho ni cheo cha mapambo - atangaze hali ya hatari chini ya Ibara za Katiba. Na akishatangaza hali hiyo ya hatari atumie madaraka yake kama Rais.

Cha kushangaza wanalaumiwa wengine wote, isipokuwa mtu pekee ambaye akitaka kwa kalamu yake tu anaweza kuondoa tatizo la nishati nchini kama dharura ndani ya siku sitini tu. Hili liendane na kupiga marufuku wizara na idara za serikali kununua majenereta! Labda ndio wataelewa uzito wa tatizo lilivyo. Nyumba za mawaziri ziondolewe majenereta ya dharura! Labda ndio watajua uzito wake. Hivi mmewahi kuuliza majenereta ya idara na wizara huwa yananunuliwa wapi na kwa bei gani? Mtakimbia!

Kama Rais Kikwete anaona uzito wa kutumia madaraka yake aliyopewa kikatiba, na kama Bunge linaona haliwezi kumtaka Rais kutumia madaraka hayo kwa sababu wanaogopa kuonekana madikteta. Well, Rais na Bunge lake wakubali kuwapo kwa kiongozi na Bunge lililo tayari kutuingiza Vitani.

Wananchi wako nyuma ya uamuzi wenye maslahi kwao na kwa hili hakuna wa kumlaumu Rais atakapoamua kuwa ‘dikteta’ kuingiza taifa ‘vitani’ kuwanusuru wapiga kura wake ambao walipungua kutoka asilimia 82 (mwaka 2005) hadi 61.

Haya ya kumbwatukia Ngeleja, ni geresha tu; Mwenye kulipeleka taifa vitani siyo Waziri wa Ulinzi - ni Rais.


RAIA MWEMA

No comments: