Monday, July 4, 2011

TOFAUTI ZAANZA KUJIANIKA UPINZANI
HALI ya mambo ndani ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), si shwari, baada ya Mbunge wa Maswa Magharibi, John Shibuda, kuwatolea uvivu viongozi wa juu wa chama hicho, akisema hatishiki na vitisho vinavyofanywa na viongozi hao.

Alisema kutokana na hali hiyo, yuko tayari kufukuzwa katika chama kwa kosa la kusema ukweli siku zote.
Hivi karibuni, Shibuda amedaiwa kwenda kinyume cha msimamo wa chama chake, kuhusiana na suala la posho za wabunge, kitendo ambacho kimemfanya aonekane muasi ndani ya chama na hivyo kuundiwa tume ya kumchunguza.


Akizungumza na MTANZANIA Jumapili mjini Dodoma jana, Shibuda alibeza shutuma hizo zilizoelekezwa kwake na kuwataka viongozi wa juu wa chama hicho kumwomba radhi kutokana na kumchafua.
Shibuda aliwataja viongozi hao ambao alidai wanamchafua kupitia vyombo vya habari kuwa ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe na Naibu Katibu Mkuu, Kabwe Zitto.

Hata hivyo Shibuda alisema mbali ya kuombwa radhi, pia atalazimika kuandaa mikutano ya hadhara yenye lengo la kuwaeleza wananchi tabia za viongozi hao.
“Natarajia kusafiri kwenda nje ya nchi kwa shughuli za kibunge, nitakaporudi, nitaitisha mikutano ya hadhara katika maeneo mbalimbali nchini kuwaeleza wananchi juu ya Zitto na Mbowe, ambao tayari wameshanishutumu kupitia vyombo vya habari.

“Mikutano hiyo nitaianzia jimboni kwangu mwishoni mwa mwezi huu, nitaweka wazi kila kitu kwa sababu wananchi ndio wenye chama na wana haki ya kujua nani anasema ukweli na nani anasema uongo.
“Hata hivyo, kabla mimi sijaenda kwa wananchi nawaruhusu wao waende kwa wananchi wakanishitaki, wakaeleze ubaya wangu ili mimi nitakapowaeleza wananchi basi wao ndio wapime wenyewe.

“Mimi nayajua mengi sana ya CHADEMA, kwa muda mfupi niliokaa katika chama hicho nimejionea mengi sana na nalazimika kusema kuwa alichokuwa akikisema Chacha Wangwe (marehemu) ni sawa kabisa na hakukosea kitu.

“Nakwambia sura ya CHADEMA ukiwa nje ya chama ni tofauti na sura ya CHADEMA ya ndani, ni tofauti kabisa kwa sababu yanayofanyika humo ni mambo ya ajabu sana.
“Mbowe anaendesha chama kibabe na anaungwa mkono na Zitto ambaye anaonekana kuwa na tabia ya ukuwadi na unafiki, mimi siwezi kunyamaza, siwezi kufumbia ukweli katika jambo ambalo naamini ni sahihi. Niliyosema nimeyasema na kama hayakuwafurahisha sitawaomba radhi na sina tabia ya kuomba radhi, kwani hata nilipokuwa CCM sikuwahi kuomba radhi.

“Lakini kwa kuwa wao ndio wamenikosea kwa kunichafua kupitia vyombo vya habari, basi nawataka waniombe radhi kwa waliyonizushia na pia nawataka wawaombe radhi Watanzania kwa kutowaambia ukweli,” alisema Shibuda.

Katika maelezo yake, Shibuda, ambaye alihamia CHADEMA mwaka jana akitokea CCM, baada ya kushindwa katika kura za Mahon, alisema pamoja na kwamba Mbowe na Zitto wanaamini wako sahihi, ukweli utabaki pale pale kwamba wanasiasa hao wanahatarisha demokrasia katika chama hicho.

“Hili suala la posho ambalo ndilo chanzo cha haya, nakwambia siyo msimamo wa chama kama wanavyowaambia Watanzania, huo ni uamuzi wao wawili tu kwa sababu katika vikao walikuwa wanawatisha wabunge na kuwatishia kwamba watawafukuza kama hawatakubali kukataa posho.

“Huwezi kuendesha chama kwa nguvu kwa sababu hizo posho ndicho kipozeo cha mbunge, kwani kama ng’ombe anayekamuliwa akikosa malisho ukimkamua ujue atatoa damu.
“Sasa kama ndivyo hivyo, wabunge wasipolipwa posho kazi zao watafanyaje, katika hili siwezi kunyamaza, nitaendelea kuheshimu uongozi kwa ajili ya kujenga ufanisi wa maslahi ya chama ya kutajirisha masikini dhidi ya vatu, cheo ni dhamana.

“Sitoona haya kukosoa tabia ya umimi na uyeye kwa mtu yeyote, sitahama CHADEMA kwa sababu sikutofautiana na chama bali nimetofautiana na watu wachache kutokana na kutoridhishwa na uongozi wao,” alisema.

Akimchambua Zitto, alisema anajifanya mzalendo machoni pa watu wakati tabia na matendo yake ni tofauti na anavyowaambia Watanzania.
“Zitto siyo mzalendo, namtaka aache tabia ya ukuwadi na kuunda uzandiki wa kufunika uwazi na ukweli kwa dhamira ya ubinafsi wa kujikweza kisirisiri ili apendwe na uongozi na kuidanganya jamii kwamba yeye ni mwadilifu.

“Zitto asigandamize haki za watu, wanaojua stahili zao kwa sababu yeye anajipamba ili asihitilafiane na kiongozi wake kwa masilahi yake binafsi, aache tabia ya kujifanya mzalendo wakati ni mnafiki anayetaka kujenga matarajio yake binafsi huku akificha ajenda ya siri ya umimi na uyeye.

“Ili kutambua tabia yake na mwenzake huyo ni sawa na mwenye kiatu ambaye ndiye anayejua jinsi kinavyomuumiza badala ya mtazamaji ambaye anafurahishwa na rangi ya kiatu, aache kabisa tabia hiyo awe wazi na asitafute umaarufu,” alisema.

Alisema kinachomgombanisha na wenzake ndani ya chama hicho ni tabia yake ya kupenda uwazi, wakati baadhi ya wenzake wanataka ukweli usielezwe kwa wananchi.
“Chuki iliyopo ni kwamba mimi Shibuda napinga chama kuwa kama kampuni ya kuingiza wanachama wa kutekeleza masilahi binafsi ili kudumisha ukabila, uyeye, umimi, uwao, umajimbo ambao umefichwa na msemo usemao siri ya mtungi aijuaye kata.

“Binafsi sitarudi nyuma, naahidi kulinda maslahi na kutetea shabaha ya CHADEMA kwa maslahi ya wananchi, nitaendelea kupingana na tabia ya kuwaonea watu kwa sababu wabunge maskini kama mimi tunapata fedha za kuwahudumia wananchi kwa kudunduliza fedha za mishahara na posho.

“Wabunge matajiri wao wana mapokeo ya hisa kutoka katika biashara zao binafsi, kwa hiyo ndondondo za mapato kutoka bungeni hawazihitaji, ndiyo maana wanawalazimisha wenzao wasiokuwa na kitu wafuate nyayo zao hata kama wanawaumiza,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, Shibuda alisema atahutubia mikutano ya hadhara wakati wowote mwishoni mwa mwezi huu baada ya kurejea nchini, ili kuweka wazi tabia za badhi ya viongozi wa chama hicho.
Juni 28 mwaka huu, akichangia bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya mwaka wa fedha 2011/2012, Shibuda aliitaka serikali iongeze posho za wabunge kutoka Sh 150,000 hadi Sh 500,000 kwa siku, kwa kuwa kiwango cha sasa hakitoshi.

Akijibu shutuma hizo, Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Freeman Mbowe, alisema hapendi malumbano kupitia biombo vya habari.
“Kamanda sipendi malumbano kwenye vyombo vya habari, tusubiri muda ukifika ukweli utajulikana tu,” alisema MboweMTANZANIA

No comments: