Wednesday, July 27, 2011

TANZANIA SI NCHI YA KULIA NJAA KILA MWAKA

KWA miaka mingi sasa Serikali imekuwa ikiweka mipango ya kuondoa njaa nchini, ukiwamo makakati uliobuniwa hivi karibuni wa kuimarisha kilimo uliopewa jina la 'Kilimo Kwanza'.Lengo la mipango hiyo kwa ujumla wake ni kuhakikisha kuwa sekta ya kilimo inatoa mchango mkubwa katika pato la taifa na kumaliza tatizo la uhaba wa chakula nchini.

Juzi Waziri wa Kilimo na Chakula, Profesa Jumanne Maghembe, alisema bungeni kuwa katika kipindi cha mwaka 2011/12, taifa linategemea kujitosheleza kwa chakula kulingana na tathmini iliyofanywa na kuwa na ziada ya tani 1,311,404 .

Licha ya kusema kuwa kutakuwa na chakula cha ziada katika maeneo kadhaa, Waziri alikiri kuwa bei ya vyakula nchini iko juu kiasi cha kuwakatisha tamaa wahitaji na kwamba, hali hiyo linavuruga mipango ya Serikali katika kuwahudumia wananchi wake.

Hata hivyo, wakati Waziri akisema hayo yameripotiwa maeneo mengi nchini yenye uhaba wa chakula. Miongoni mwa maeneo hayo ni Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro, Namtumbo mkoani Mtwara na Ngorongoro Mkoa wa Arusha.

Iimeripotiwa kuwa katika maeneo hayo hali ya chakula ni mbaya sana na kwamba, watu wengi wanaweza kufa kwa njaa kama msaada wa chakula hautapelekwa haraka.

Kufuatia hali hiyo, tunalazimika kusema kwamba, mipango mibovu ya Serikali ndiyo imetufikisha hapa tulipo sasa.
Inasikitisha kuona kuwa, licha ya sekta ya kilimo kutegemewa na asilimia 80 ya Watanzania, lakini inachangia kiasi kidogo mno katika pato la taifa.

Kwa mfano katika mwaka wa fedha wa 2009/2010 sekta hiyo ilichangia asilimia 26 tu katika pato la taifa, huku ukuaji wa Sekta ya Kilimo ukiendelea kushuka kila mwaka.

Katika mwaka wa fedha wa 2008/2009, Sekta ya Kilimo ilikua kwa wastani wa asilimia 4.2 tu, wakati ongezeko la watu linakua kwa asilimia 2.9. Kasi hiyo ukuaji wa Sekta ya Kilimo hailingani na ongezeko la watu nchini. Hali hii inaonyesha kuwa kama hatua madhubuti hazitachukuliwa kuongeza uzalishaji na kudhibiti wa ongezeko la watu, uhaba wa chakuka utakuwa mkubwa na watu wengi watakufa kwa njaa.

Kijiografia Tanzania ina ardhi kubwa yenye rutuba, isiyotumika kabisa inayoweza kuzalisha chakula cha kuwatosha Watanzania wote na kingine kuuza nje ya nchi.

Kwa mfano, kama Bonde la Mto Kilombero na Rufiji lingetumiwa vyema kwa ajili ya kilimo, tunaamini kuwa lingeweza kuzalisha chakula cha kutosha nchi nzima na ziada.

Sisi tunajiuliza kwamba, kwa nini Watanzania tuendelee kulia njaa kila mwaka kama kila kitu tunacho? Kama mahindi yapo Rukwa, Mbeya, Rvuma na Iringa ambako wakulima hawana sehemu ya kuyahifadhi, kwa nini tulie njaa? Kwa nini Serikali isiwe na mpango wa kudumu wa kukusanya mahindi kutoka mikoa hiyo na kuyapeleka katika maeneo yaliyo na uhaba wa chakula?

Ni wazi kuwa tumekosa mipango thabiti ya kuhakikisha kuwa mahindi yanayozalishwa Mpanda mkoani Rukwa yanafika kwa urahisi Dar es Salaam, au Mtwara ambako yanahitajika.Tunadhani tatizo lipo kwa viongozi wa Serikali ambao wamekuwa wakiimba wimbo mzuri wa kuinua kilimo bila utekelezaji thabiti.

Tunasema hivyo kwa sababu, mkakati wa Kilimo Kwanza unavyoelezwa na viongozi majukwaani ni tofuati na jinsi Serikali inavyotekeleza kwa vitendo. Kama kweli Serikali imedhamiria kuwaondolea wananchi wake njaa ingeimarisha kilimo na kujenga masoko ya uhakika, sambamba na miundombinu ya barabara na utunzaji bora wa nafaka.

Tunaishauri Serikali kuwekeza zaidi katika kilimo kwa kuwawezesha wakulima wadogo kutoka katika kilimo cha jembe la mkono na power tiller kwa kuwakopeshe matrekta na pembejeo.

Si hivyo tu, kuna umuhimiwa wa Serikali kuzihamasisha halmashauri za wilaya na manispaa katika maeneo yenye uhaba wa chakula kujenga maghala na kununua nafaka na kuzisafirisha hadi katika maeneo yao ka ajili ya kuwauzia wananchi wao kwa bei nafuu.Mipango ni kutumia akikili, ubunifu, uwajibika, ukelezaji na usimamizi bora badala ya ngonjera zinazoibwa katika majukwaa ya siasa na viongozi wetu kila kukicha.


MWANANCHI

No comments: