Monday, July 4, 2011

SHIBUDA AZIDI KUKALIWA KOONIMh Shibuda akichangia Bungeni.

MAMBO yanazidi kuwa magumu kwa mbunge wa Maswa Magharibi (Chadema), John Shibuda kufuatia Kambi ya Upinzani Bungeni kuanza rasmi mchakato wa kuchukulia hatua mbunge huyo kutokana na kile kinachodaiwa kuwa ni kuisaliti kambi hiyo.Shibuda ambaye alijiunga na Chadema akitokea CCM wakati wa harakati za uchaguzi mkuu uliopita, leo atakabidhiwa barua rasmi inayomtaka ajieleze kwanini aliwasaliti wakati akichangia hotuba ya makadirio ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu bungeni, kabla ya kuchukuliwa hatua za kinidhamu.

Tuhuma zinazomkabili Shibuda ni kutoa matamshi yanayopinga na msimamo wa kambi yake inayoongozwa na Chadema pale alipowapiga vijembe wabunge wanaopinga posho zinazotolewa kwa wabunge na watumishi wengine wa umma nchini.

Akizungumza na Mwananchi, Mnadhimu Mkuu wa kambi hiyo, Tundu Lissu alisema kitendo Shibuda kupingana msimamo wa kambi ya upinzani ambao ni kukataa kulipwa posho za vikao, kimewadhalilisha na kwamba lazima muhusika (Shibuda) atoe maelezo kabla ya hatua zaidi kuchukuliwa dhidi yake.

"Kutokana na tukio la kudhalilisha uamuzi ya vikao vya kambi, kuna aina mbili za kumchukulia hatua Shibuda, kwanza ni kwa upande wa kambi ya upinzani na pili kumshitaki Chadema,”alisema Lissu na kuongeza:

“Mbunge anapokiuka uamuzi ya kambi anastahili kuchukuliwa hatua za kinidhamu na kupewa adhabu, na adhabu kubwa anayoweza kupewa na kambi hii kwa kanuni zetu ni kumtenga katika kambi na kumtangaza hadharani kuwa huyu ametengwa na kambi kwasababu amefanya makosa kadhaa".

"Mimi kama kiongozi wa nidhamu katika kambi hii kesho (leo) nitamuandikia barua ya kumtaka ajieleze ni kwanini amekaidi msimamo wa kambi katika suala la posho alipokuwa akichangia mjadala wa bajeti ya Ofisi ya waziri Mkuu, bungeni, ambalo sisi kama kambi ya upinzani tulikubaliana wote kukataa posho hizo,"alifafanua Lissu.

Kwa mujibu wa Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki, Shibuda mbali na kosa hilo, pia amekuwa akitoa matamshi ya kudhalilisha kambi ya upinzani na Chadema, pamoja na kuwadhalilisha viongozi wao.

Kushtakiwa Kamati Kuu
Lissu alisema baada ya kumuita Shibuda na kumuadhibu, kambi ya upinzani itawasilisha malalamiko katika vikao vikuu vya chama hicho, ili kuvipa ya nafasi ya kujadili suala hilo na kuchukua hatua.

"Katiba ya Chadema imeweka miongozo ya viongozi na wanachama na kwa yoyote atakayeivunja anastahili kuadhibiwa, sisi kama kambi ya upinzani bungeni, tutapeleka malalamiko yetu katika mkutano wa kamati kuu ya Chadema ili chama kione kama haya matamshi aliyoyatoa Shibuda hayakiuki hiyo miiko ya chama chetu,"alisema na kuongeza:

"Tukumbuke kwamba hii haitakuwa mara ya kwanza kwa Shibuda kushtakiwa katika kamati hiyo, alishaadhibiwa kwa kutoshiriki kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akihutubia Bunge mjini Dodoma, ambapo yeye na wenzake ambao hawakushiriki walipewa onyo kali na kutakiwa kuwaomba radhi wabunge wenzao walioshiliki katika tukio hilo, wenzake walifanya hivyo, lakini Shibuda hadi leo hajawahi kuomba radhi".

"Tutaiomba Kamati Kuu suala hili lilishughulikie kwa umakini sana na waangalie matukio yake ya nyuma hili adhabu watakayotoa hiwe staiki na kubwa, na adhabu kubwa ya chama ni kufukuzwa tu,"alifafanua Lissu.

Lissu alisema madai kwamba Kiongozi wa Kambi hiyo, Freeman Mbowe na Naibu wake, Zitto Kabwe waliwalazimisha wabunge wa Chadema kukataa posho kwa kuwatisha kufukuzwa ubunge ikiwa watapingana, siyo ya kweli na kwamba ni ya kupikwa.

"Si kweli kwamba wabunge wa Chadema wametishwa, kufukuzwa iwapo hawataunga mkono kukataa posho, suala hili lilizua mjadala mrefu kwenye vikao vyetu na ilikuwa lazima iwe hivyo, lakini baadaye wote tulikubaliana kwasababu ulikuwa ni msimamo wa chama na tukasema ndio utakuwa msimamo wetu bungeni," alisema Lissu.

Alisema wanataka kuondoa utamaduni wa posho katika malipo ya utumishi wa umma nchini kwasababu unaangamiza uchumi wa taifa na kufanya watumishi wa umma kutowajibika ipasavyo kwani wanafanya kazi ya kukimbilia vikao kila mahala ili walipwe posho.

Kauli ya Zitto
Naye Naibu Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Zitto alisema msimamo wa kumfukuza Shibuda upo pale pale kwani kambi hiyo wala Chadema hawawezi kumuacha mbunge anayekiuka sera na kuwadhalilisha viongozi hadharani.

"Shibuda hatafukuzwa kinyemela, lazima taratibu zifuatwe kwa Mnadhimu Mkuu wa kambi yetu kumuandikia barua ya kumueleza makosa yake na yeye kupata fursa yakujibu shutuma hizo, pili ataitwa katika Kamati Kuu ya chama chetu (Chadema) nao watatoa uamuzi wao,"alisema Zitto na kuongeza:

“ Chadema si chama cha kihuni kwamba tutakurupuka ni lazima haki itendeke na mimi sipendi mtu aonewe, Shibuda atapata haki zake zote kama mwananchama. Mbunge yeyote wa Chadema anapaswa kujua akienda kinyume na sera ya chama atafukuzwa”.

Alisema suala la posho lipo kwenye Ilani ya uchaguzi wa 2010 kwahiyo ni sera, na kwamba anayepinga atafukuzwa tu na kwamba Chadema wataanza na Shibuda.

Zitto alisema "Shibuda anajua mie humtetea sana, lakini anapokwenda kinyume na sera ya chama tutamfukuza, aniite majina yoyote tu akienda kinyume na sera nitakuwa wa kwanza kumfukuza".

"Kuna masuala ya nidhamu kwenye bunge na wabunge wa chama fulani inaitwa’ three line whip, masuala ya msimamo wa kitendaji mfano tulipokaidi kwenda bungeni kutoka nje ya ukumbi wakati Rais Jakaya Kikwete alipokuwa akihutubia bunge (walk out), haya ni ya kawaida na hayana adhabu kali, lakini likiwa la sera adhabu ni kufukuzwa, Shibuda asipapalike," alisema Zitto.

Wabunge Chadema wanena

Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa aliwaomba wananchi wampuuze Shibuda kwa kauli zake kuwa wabunge wa Chadema wamelazimishwa na viongozi wao kukataa posho za vikao.

"Shibuda anataka umarufu mrahisi tu, Mbowe na Zitto hawezi kutuburuza wote 46 wa Chadema kwenye suala la posho, kwa kauli moja wabunge tulikubaliana swala hili na yeye hakuwepo kwenye vikao, nadhani ana tatizo".

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema alisema hakuna hoja hata moja waliyowahii kulazimishwa na viongozi wa kambi ya upinzani bali wabunge wote hujadiliana jambo kwa pamoja kwa kushindana kwa hoja.

"Huyu mwenzetu Shibuda amekuwa akikiuka maagizo mengi ya vikao na kujitetea kuwa hakuwepo katika vikao, sisi hatuitani katika vikao kwa barua bwana, tunatumiana ujumbe mfupi wa maandishi wa simu au kumuomba Spika, Naibu Spika au Mwenyekiti wa Bunge yoyote kati yao anayeongoza bunge siku hiyo kututangazia bungeni," alisema.

Msimamo wa Shibuda
Wakati hayo yakiendelea, jana Shibuda amenukuliwa na gazeti moja litolewalo kila siku (siyo Mwananchi) akisema kwamba haogopi kufukuzwa katika Chadema na kwamba ataendelea kusimamia ukweli siku zote.

Shibuda alinukuliwa na gazeti hilo akiwataka viongozi wa juu wa Chadema akiwemo Mbowe na Zitto kumwomba radhi kwa kile alichodai kwamba ni kumchafulia jina, huku akiahidi kwamba ataanika maovu ya viongozi hao.

Shibuda ni mwanasiasa ambaye alipokuwa CCM aliwahi kuzua mtafaruku ndani ya chama hicho na hata kuzuiwa kwake kugombea katika uchaguzi wa mwaka jana kunatokana na kutofautina na waliokuwa viongozi wake wa chama mkoani na Taifani.


MWANANCHI

No comments: