Tuesday, July 26, 2011

KIGOGO UVCCM JELA MIAKA 36

Link
Joyce Joliga na Kwirinus Mapunda, Songea

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Ruvuma, imemhukumu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), ambaye pia ni Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Mbinga Magharibi, John Komba, kutumikia kifungo cha miaka 36 jela baada ya kupatikana na hatia ya wizi wa Sh 80 milioni.

Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Baptista Mhelela, alisema jana alipokuwa akisoma hukumu hiyo kuwa ameridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi 24 kwamba, Benedict Ngwenya, alitenda kosa hilo la kuiibia Kampuni ya DAE Ltd.

Kwa mujibu wa Hakimu Mhelela, Mahakama hiyo bila shaka yoyote, imeridhika na ushahidi huo na kwamba imemtia hatiani mshitakiwa Ngwenya ambaye pia ni diwani wa Kata ya Mpepai katika Wilaya ya Mbinga.

Alifafanua kwamba mshitakiwa alikuwa akikabiliwa na makosa 13, lakini kosa moja kati ya hayo ambalo ni la kughushi kwa maandishi alishinda. Alisema ametiwa hatiani kwa makosa mengine 12 yaliyobaki.

Awali, Mwanasheria wa Serikali, Mwegole Shabani, alidai mahakamani hapo kuwa mshitakiwa Ngwenya alitenda makosa hayo mwaka 2008 kwa nyakati tofauti akiwa anafanya kazi kama mhasibu katika kampuni hiyo ya DAE LtD.

Shabani alisema mshitakiwa alizichukua fedha hizo kwa lengo la kwenda kugawa kwenye mitambo inayokoboa kahawa mbichi ambapo hata hivyo, hakuzifikisha sehemu husika.

Alisema baada ya kutenda kosa hilo, aliacha kazi bila kukabidhi ofisi kwa mwajiri wake, jambo ambalo lilimfanya mwajiri huyo kumtilia shaka na kumtaka mkaguzi wa mahesabu wa ndani kufanya ukaguzi ndipo alipobaini upotevu wa fedha hizo.

MWANANCHI

No comments: