Thursday, June 23, 2011

TATIZO SIYO POSHO YA VIKAO NI MFUMO MZIMA WA MISHAHARA
Na Lula Wa Ndali Mwana Nzela

MJADALA wa posho za vikao kwa wabunge na watumishi wote serikalini unagusia dalili tu ya tatizo na haugusi tatizo lenyewe.

Ukifuatilia sana unaweza kabisa kuamini kuwa tatizo ni posho za vikao na kuwa posho za vikao zikiondolewa tu basi tatizo la posho litakuwa limeondoka na watu wote tutaishi kwa furaha baada ya hapo.

Ndugu zangu, mjadala wa posho umekuja wakati muafaka lakini umeambatana na kutokuwa wa kweli moja kwa moja wa nini hasa tatizo. Posho za vikao ni tatizo moja tu katika suala zima la posho. Bila kuangalia suala zima tutajaribu kutatua dalili moja tu ya tatizo.

Ni sawasawa na watu ambao wamegundua kuwa ndoo yao wanayochotea maji inavuja na wakaona tundu kubwa na mara moja wote wakakubaliana kuwa ni lazima kuliziba tundu hilo. Kama wote wakikubaliana kuwa tatizo ni tundu hilo kubwa na kuwa hakuna tundu jingine au sehemu nyingine ambayo ndoo inavuja basi hilo litakuwa ni jambo la maana.

Lakini kama wakiamua kwa makusudi kutoangalia matundu mengine yaliyo pembeni ya tundu hilo kubwa basi watakuwa ni wazugaji wakubwa kama wataimba wimbo wa “tuzibe tundu kubwa” na wakaamua kuliziba lakini yale mengine wakayaacha. Maji yataacha kuvuja kwenye tundu kubwa lakini hatuwezi kusema ndoo itaacha kuvuja! Posho za vikao ni tundu kubwa lakini kwa hakika siyo tundu pekee na kuliziba hilo huku mengine tunafikiria tutayaziba vipi hakuondoi ukweli kuwa ndoo yetu inavuja.

Aina za Posho

Wafanyakazi wa Tanzania (hasa kwenye ajira ya Serikali) wanazo posho za aina mbalimbali. Aina hizo za posho pia zinapatikana kwenye ajira binafsi vile vile kwa namna tofauti tofauti.

Katika ya mlundikano wa posho naweza kuzigawa posho kubwa na posho ndogo ndogo kwa maana ya zipi zinaoenakana mara nyingi zaidi na ambazo zinatumiwa kwa fedha nyingi na zipi ambazo zinatokea mara chache – labda bila kutoa fedha nyingi kwa wakati mmoja.

Posho ya Kujitokeza a.k.a posho ya vikao (sitting allowance)

Kwa kweli kama nilivyoiita hii si posho ya “vikao” kama wengi wanavyoiita au kwa Kiingereza sitting allowance. Haihusiani na mtu kushiriki kikao au hata kukaa kwenye kikao chote! Inahusiana na mtu kujitokeza pale panapofanyika kikao. Tungeweza hata kuziita ni posho za kuwapo (presence allowance).

Zinapoitwa posho za kikao zinamfanya mtu aamini kuwa zinamtaka mlipwa posho ahudhurie kikao toka mwanzo hadi mwisho! La hasha. Mtu anaweza akaenda mahali ambapo pana kikao akaweka sahihi jini lake kuwa alitokea, akapiga soga soga kidogo na kutoa udhuru au kuondoka bila kuaga na posho yake bado atapata! Hili ni kweli kuanzia Bungeni hadi kwenye maofisi yetu mbalimbali. Ndiyo maana naiita hii appearance allowance!

Kwa wabunge kwa mfano, wanalipwa shilingi 150,000 (posho ya kikao na ya kujikimu) kwa siku wanapokuwa kwenye vikao vyao Bungeni. Nimesema kwa siku. Mwalimu wa shule ya msingi Tanzania analipwa mshahara wa wastani wa shilingi 167,000 hivi kwa mwezi. Nimesema kwa mwezi. Mwalimu wa Sekondari mwenye diploma kama shilingi 203,000 wakati wenye shahada shilingi 360,000 kwa mwezi.

Labda niliweke hili lionekane vizuri. Mwalimu mwenye shahada atahitaji kufanya kazi kwa karibu miezi 12 ili kupata kiasi ambacho mbunge mmoja atakusanya kwa mwezi mmoja wa kikao cha bajeti kinachoendelea.

Labda sijaeleweka nilinyambue kwa mbele zaidi. Posho watakazolipwa wabunge 360 kwa mwezi mmoja zinatosha kuwalipa walimu wenye shahada zaidi ya 4000 mshahara wao wa mwezi mmoja!

Kumbuka sijazungumzia mishahara ya wabunge ni posho za aina mbili tu.

Posho ya kujikimu (living/subsistence allowance)

Posho hii hulipwa kwa ajili ya matumizi madogomadogo ya kila siku. Kimsingi posho hii iliingizwa ili kuweka nyongeza katika mshahara wa mtu ili kumfanya awe na maisha ya unafuu. Posho hii uwepo wake unajengwa kutokana na kutambua kuwa mshahara wa mtu haumtoshi! Hivyo, wapo watu wanaongezewa posho kidogo ya “kujikimu” ili kuinua pato lao.

Watumishi mbalimbali hupewa hizi posho za kujikimu kama sehemu ya nyongeza yao ya mishahara. Wabunge wanadai posho hizi mbili zinawasaidia kutatua matatizo “madogo madogo” ya wananchi wao. Nitawaachia wengine wafikirie maana ya hilo.

Posho ya Siku a.k.a per diem

Mojawapo ya posho maarufu sana kwa watumishi mbalimbali nchini ni hii ya “kwa siku”. Neno ‘per diem” linatoka kwenye Kilatini likimaanisha “kwa siku” au kwa “kila siku”.

Jinsi inavyotumika siku hizi inahusiana hasa na malipo ambayo mtu anapatiwa kwa kuwa nje ya kituo chake cha kazi kwa ajili ya chakula na usafiri. Hii ndiyo maana hasa ya posho hii. Hata hivyo, katika sehemu nyingi posho hii imekuwa ni sawa kabisa na posho ya vikao au mikutano.

Kwa mfano, waandishi wa habari wanapoitwa kwenda kwenye tukio fulani ambapo kiongozi atazungumza na waandishi wa habari wanatarajia kuwa kutakuwepo na bahasha za per diem. Hili ni kweli hata kwa baadhi ya watendaji ambao wanatoka eneo moja la mji au mahali ambapo pamo ndani ya eneo lao la kazi kwenda kushughulikia jambo fulani na huko aliko anatarajia kulipwa per diem. Ukiniuliza mimi nadharia yangu ni kuwa kati ya posho hizo mbili za kwanza (ya kikao na ya kujikimu) hakuna posho inayotumiwa vibaya zaidi kama hii ya per diem.

Sababu kubwa ya kutumiwa vibaya kwa mtindo huu ni kukosekana kwa utaratibu wa wazi wa kujua gharama za maisha katika miji yetu zikoje na hivyo karibu taasisi mbalimbali (za umma na binafsi) zina viwango tofauti vya per diem ndani ya mji mmoja. Kwa mfano, kama mkutano unafanyika Bagamoyo na taasisi mbalimbali zinaenda kufanyia mkutano huko je viwango vyao viko sawa vya per diem? Utakuta vina tofauti wakati mwingine tofauti yenyewe inatisha kweli kweli.

Nchi kama Marekani ina utaratibu wa per diem lakini kuna taasisi ambayo imeweka viwango vya malipo ambavyo vinatumiwa na taasisi binafsi na mtu hawezi katika mazingira ya kawaida kulipa zaidi ya hapo au chini ya hapo kwani ni kama standard rate.

Tena Wamarekani wameweka utaratibu kwamba ili mtu apewe per diem ni lazima shughuli yake iwe umbali wa zaidi ya kilomita 100 kutoka eneo lake la ajira ambapo analipia kodi na ihusishe kulala huko. Hii ina maana mahali ambapo mtu anaenda na kurudi siku hiyo hiyo na haendi zaidi ya umbali huo mtu halipwi per diem! Embu Tanzania ijaribu hilo tuone watu wakavyolia!

Unaweza kutembelea tovuti ya http://www.gsa.gov ya Marekani na kuangalia per diem rates tena wao wamefika mbali na kuweka posho hata kuhusiana na nchi mbalimbali ambazo zinasaidia watendaji wao wanaposafiri kwenda nje ya nchi.

Kwa mfano, Dar-es-Salaam na Zanzibar kiwango cha juu cha per diem ni dola 273 kwa siku na maeneo mengine ya Tanzania (bila kujali ni kijiji au jiji) ni dola 187 kwa siku! Kwa kulinganisha tu Kigali, 275 USD; Nairobi, 410 USD; Kampala, 310USD; na Lilongwe, 243 USD.

Mfumo kama huu unatumiwa hapa nchini katika baadhi ya taasisi hizi kimataifa lakini sijui ni kwa kiasi gani viwango vinalingana au kila taasisi ina viwango vyake. Nitakuwa tayari kusahihishwa.

Je, Tanzania ina utaratibu wowote wa kujua wastani wa per diems katika maeneo mbalimbali nchini ni kiasi gani? Mwajiri wa Tanzania akitaka kupanga kiwango cha per diems anaangalia nini au wapi? Je, mfanyakazi anapopangiwa kwenda kwa siku huko Kigoma analipwa karibu sawa na mfanyakazi mwingine ambaye naye anaenda Kigoma wakati huo huo na eneo lile au kuna tofauti kubwa kati yao?

Unaweza kuona kuwa kwa namna moja au nyingine hizo tulizozingumza hapo juu (posho ya kikao na ile ya kujikimu) zinaangukia kwenye hii hii tunayoita per diem na kwa kweli inapaswa kuwa hivyo. Lakini wakati mwingine inatofautishwa na baadhi ya watu ili kuweza kuweka utaratibu wa mtu kujipatia fedha nyingine ya ziada.

Wengine wanaita per diem kama malipo ya ziada tu ya usumbufu kwa watu na haihusiani na mtu kusafiri, kulala au usumbufu mwingine. Nakumbuka tukio moja mapema mwaka huu (bila ya shaka kati ya mengi) ambapo waandishi walienda kuripoti tukio moja kubwa tu la kitaifa (alikuja jamaa mmoja na kuita waandishi wa habari) na baada ya mwisho wa mkutano hakukuwa na bahasha zozote za per diem baadhi ya waandishi walikuwa wamekwazwa na walisikika wakilalamika pembeni.

Posho za Safari (travel allowance) na moving/transportation allowance

Posho hizi nazo ni maarufu sana na kwenye nchi nyingine kama Marekani hapo juu ni sehemu ya per diem. Lakini katika baadhi ya taasisi zetu (sijui kama zote) pamoja na
per diem mtu anaweza kujikuta anapewa pia posho ya safari!

Posho ya Nyumba (housing allowance)

Kama inavyoonekana posho ya nyumba hutolewa kwa mtumishi kumsaidia kumudu gharama za makazi. Mara nyingi posho hizi huwa sehemu ya mshahara na hulipwa kwa kila mwezi. Viwango vya posho ya nyumba sijui kama vinaendana na hali halisi ya soko la nyumba nchini au watu wanajipangia kwa kadiri wanavyojisikia.

Nitatoa mfano maarufu; aliyekuwa mkurugenzi wa TANROADS alikuwa analipwa posho ya nyumba dola 2200 kwa mwezi hiyo ikiwa ni juu ya mshahara wa dola 8500! Kwa wale msiojua TANROADS ni taasisi ya Serikali.

Matokeo ya Posho hizi

Nimechagua posho hizo chache kuonyesha tu kidogo na sijagusa kabisa zile posho ndogondogo ambazo nazo ukizijumuisha unaweza kuona mirija iliyowekwa na mabepari mamboleo katika migongo iliyopindika na kukauka ya walipa kodi wa Tanzania.

Hatujagusia posho za simu, umeme na maji! Ukiweka posho na marupurupu mengine unaweza kufikia hitimisho kuwa hakuna watendaji ambao wamedekezwa wakadeka kama wale wa Tanzania.

Tunaposikia kelele za watu kutetea posho mbalimbali na kudai kuwa ni muhimu sana tunasikia kauli ambazo tulizisikia karibu miaka hamsini iliyopita pale Azimio la Arusha lilipotangazwa. Tunakumbuka wengine tulipoimba “mabepari walia, kukatiwa mirija”. Leo hii suala la posho litakuwa ni ugomvi kati ya watawala na watawaliwa, huku watawala wakijaribu kutafuta sababu ya kuhalalisha kwanini posho hizo nyingi ziendelee kulipwa.

Lakini hawataki kuangalia gharama kubwa ambayo posho hii imetuingiza kwenye taifa. Mwaka 2008/2009 posho peke yake zilitengewa shilingi bilioni 509 kwa mwaka. Bajeti hii ambayo itapitishwa na wabunge wa CCM imetenga karibu shilingi trilioni moja kwa ajili ya posho na marupurupu.

Ndugu zangu huu ni wizi kwa jina la “mastahili”. Ni wizi ambao unafanywa na watu waliopita mwaka jana wakililia tuwape kura ili watuongoze. Ni wizi ambao hauna jina jingine zaidi ya uporaji wa fedha za Watanzania.

Kinachoudhi zaidi ni kuwa ni wakulima wa Tanzania ambao hawana pa kulalamikia. Wakulima wa kawaida wanapata posho gani? Kuna posho ya mazao? Kuna posho ya kusafirisha nafaka? Kuna posho ya jua kali? Hawana posho hata moja! Lakini kuna kikundi cha magenius kwenye Chama Tawala na Upinzani ambao wanaamini “wanastahili” posho hizo.

Hivi wastaafu wetu, kina Sarakikya, wanapewa posho yoyote ya kuinua zaidi hali zao ngumu - vipi posho ya utumishi wa muda mrefu kwa wastaafu wetu? Bila ya shaka hakuna mbunge anayeweza kuwazungumzia kwani wabunge hawana wasiwasi wa maisha yao baada ya kustaafu!

Tufanye nini?

Ukiondoa hili la kufuta posho za vikao jambo ambalo kwangu naona ni geresha ya wanasiasa tu kwani haigusi kiini cha tatizo, ni lazima mfumo mzima wa posho na marupurupu ufumuliwe na kuundwa upya kuweka mkazo katika kuboresha mishahara. Kama lengo ni kumuongezea malipo mtumishi basi ipo haja ya kuangalia hata namna mishaahara inavyolipwa.

 • Kabla hatujaenda mahali popote ni lazima kwanza wale wote wanaoidai Serikali walipwe. Serikali haiwezi kuendelea kukopa watumishi wake na kuwafanya watu wafanye kazi kwa mkopo wa nguvu kazi, huu unaitwa unyonyaji.

  Sitaki Serikali iwanyonye watumishi hasa wale wanaoanza kazi au wale ambao wamepata uhamisho na wanasubiri mishahara yao ya kwanza. Mishahara yote ni lazima ilipwe kwanza kwani hayo ni madai ya msingi; asiwepo mtumishi katika Serikali ya Tanzania ambaye anadai mshahara wake. Mshahara si hisani au wema wa Serikali, ni deni ambalo mfanyakazi anadai na kwa mujibu wa Katiba kila anayefanya kazi anastahili kulipwa ujira wa haki.

 • Posho zote za sasa zifutwe na tubakie na posho ya aina moja tu. Yaani, ibakie per diem ambayo itawekewa utaratibu mzuri wa kuhakikisha kuwa inatolewa kwa yule anayestahili, kwa mahali panapostahili na kwa viwango vinavyostahili.

  Mtu anayefanya kazi mkoani kwake au ndani ya maili kadhaa za mkoa wake na anaenda mahali ambapo hahitaji kulala (akilala bila kibali anajigharimia mwenyewe) atalipwa kiasi fulani.

  Tunaweza kujifunza kwa Wamarekani kwani mfumo wao umeondoa kabisa suala la kuzidisha malipo ya per diem. Tuweke kipimo cha per diem, kwa mfano, kwa mwaka mtumishi hatakiwi kuwa nje ya mji wake na kupata per diem zisizozidi kiasi fulani. Pamoja na hilo taasisi za Serikali zinahitaji kuwa na ofisi ambazo zinasimamia mambo ya usafiri (travel arrangement) na hivyo kusimamia watendaji wanaposafiri tiketi na malazi yanakuwa yameshaandaliwa ili kuondoa mtindo wa mtu kwenda kwenye hoteli na kutaka risiti iandikwe kiasi tofauti na bei halisi ili aweze kurudishiwa fedha!

 • Posho za nyumba na chakula zifutwe. Hivi ukishampa mtu posho ya nyumba na chakula, mtu huyo anatumia mshahara wake kwa vitu gani? Mshahara lengo lake ni kumpatia mtu fedha ya kuishi na ni kutoka humo anatakiwa apange chakula anatumia kiasi gani, nyumba atapanga wapi n.k.

  Sasa hivi kutokana na mtindo wa posho watu wameweza kupanga na kuishi kwenye nyumba wasizo na uwezo nao, simu za bei mbaya na gharama nyingine ambazo katika mshahara wao hawawezi kweli kuzimudu.

  Ni kutokana na hilo basi utaona huwezi tu kuondoa posho bila kuinua mshahara kwa kiasi fulani, hivyo, mishahara iongezwe kwa kiwango cha posho zitakazofutwa na mtu aamue mwenyewe ataishi wapi, atapanga nyumba gani.

 • Mtindo wa mishara kila mwisho wa mwezi umepitwa na wakati na kwa muda mrefu nimelizungumzia hili na nashangaa kwanini CHADEMA ambao waliliahidi kwenye Ilani yao hawajalisukumiza ili lianze kufanyiwakazi.

  Ndugu zangu rushwa nyingi ndogondogo zinatokana na mahitaji ya kila siku ya mtu. Mtu hawezi kukaa mwezi mzima kusubiri shiling laki mbili! Ni mfumo wa kijinga (na ninamaanisha hili, situkani) na ni mfumo ambao kuuendeleza ni kuendeleza rushwa za kijinga.

  Tuwe na mfumo wa mishahara wa aina tatu; watendaji wengi wa ngazi za chini ambao ni asilimia kubwa walipwe kila wiki, watendaji wa ngazi ya kati walipwe kila ndani ya wiki mbili na watendaji wakuu wa taasisi walipwe mishahara ya mwezi. Mtindo huu utafuta kabisa rushwa za kwenye madirisha ya huduma au barabarani.

 • Tuache kulipa kwa mtindo wa kima cha chini cha jumla ya mwezi na badala yake tuwe na kima cha chini kwa mujibu wa saa na huo ndio msingi wa waajiri kupanga mishahara yao kufuatana na soko la ajira, mahitaji ya kiuchumi n.k.

  Kama mtu anafanya kazi saa nane kwa siku kwa siku tano za wiki basi atafanya kazi saa 40 na kwa mwezi atafanya saa 160. Kwenye kima cha chini cha shilingi 135,000 mfanyakazi wa Tanzania analipwa shilingi 843.75 kwa saa. Kama dola moja ni sawa Sh. 1545, basi shilingi 843.73 ni sawa na dola 0.55 hivi yaani senti hamsini na tano za Kimarekani. Ndivyo tulivyoweka kima cha chini cha Watanzania.

  Mbunge wa Tanzania anayepokea sawa na dola 7000 kwa mwezi anapata kwa saa dola 43! Kwanini mtu wa chini asiamue kupokea kitu kidogo kila saa? Ndiyo maana naweza kuita rushwa hii ndogondogo kuwa ni posho ya rushwa! Hata wale watumishi wa kati wanaopokea kama dola 2500 kwa mwezi utakuta kuwa wanapokea kama dola 15 kwa saa. Jamani, kama watu wengine wamehalalisha kujilipa mamilioni ya fedha kwa sababu wanastahili; hawa wanaolipwa kiduchu hivi watalaumiwa kweli kwa kupokea rushwa ndogo ndogo. Matokeo yake hata rushwa siku hizi nayo imepanda dau!! Kima cha chini cha rushwa nacho kimepanda.

  Tupandishe mishahara, tubadili mfumo wa malipo na watu waanze kulipwa kwa saa wanayofanya kazi.

Yapo pia mawazo mengine mengi lakini kwa leo nadhani haya yanatosha nitawaacha wengine wafikirie jinsi gani tutawanyang’anya wezi wetu fedha zetu.

Kama kweli watu wanataka kubana matumizi na kuleta nidhamu ya fedha, mfumo mzima wa posho ufumuliwe kuanzia anazopata Raia Jakaya Kikwete hadi mfagizi wa ofisi! Hapo ndipo tutaanza kujua nani kweli anataka mabadiliko. Nje ya hapo wanaoshangilia wanafurahia gunia la mbuzi.RAIA MWEMA

No comments: