Thursday, June 2, 2011

TANU MAKINI ILIJIVUA GAMBA MARA MBILI CCM HAIWEZITULIJUA tangu mwanzo kwamba uamuzi wa vikao vya juu vya Chama cha Mapinduzi [CCM] juu ya chama hicho kutaka kujivua gamba [la maovu ya kijamii, kisiasa na kiuchumi], zilikuwa mbio za sakafuni. Tumebaini kwamba, uamuzi unaodaiwa kufikiwa haumaanishi kile tunachoambiwa; na kile tunachoambiwa hakimaanishi kuwa ndio uamuzi unaodaiwa kufikiwa, na hivyo kugeuza kila kitu kuwa “usanii” wa kisiasa.

Awali, tuliambiwa na kuaminishwa kwamba, Halmashauri Kuu ya CCM [NEC], iliwataka viongozi wa Chama, ngazi ya taifa, wanaotajwa katika kashfa kubwa kubwa za ufisadi wajipime ndani ya siku 90 na kuachia ngazi; vinginevyo Chama kitawang’atua kwa nguvu, na kwamba wangeandikiwa barua hima kujulishwa uamuzi huo.

Lakini kauli ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa CCM, Bw. Wilson Mukama [ambaye wakati uamuzi huo ukifikiwa alikuwa hana cheo hicho], ni kinyume na tulivyoambiwa mwanzo. Yeye amesema, Chama hakijamtaja mtu, na hivyo hakuna aliyeandikiwa wala atakayeandikiwa barua kwa sababu [Chama] kina taratibu zake za kudhibiti wanachama wake.

Kauli ya Mukama inagongana na kauli ya Katibu wa Itikadi, Siasa na Uenezi wa Chama hicho, Nape Nnauye ambaye msimamo wake ni kwa yale yanayokanushwa na Katibu Mkuu wake. Lakini hata hivyo, tofauti na hapo mwanzo, sasa naye amenywea na kurudi kwenye msimamo wa bosi wake! Huu ni usanii na umamluki hatari wa kutaka kuzichezea akili za wananchi.

Tunaposhuhudia haya, hatuhitaji kuambiwa kwamba utekelezaji wa yaliyoazimiwa na NEC, yamepigwa ngwara kwa nguvu ya turufu nje ya vikao vya Chama hicho.

Hili lilijulikana mapema; kwa maana CCM ya sasa ina wenyewe wachache, wenye kauli turufu; tofauti na Chama cha kitaifa kilichotangulia cha “Tanganyika African National Union” [TANU], kilichokuwa Chama halisi cha ukombozi wa Mtanzania, na ambacho kiliweza kusimamia maamuzi yake bila kupindisha ukweli na utekelezaji wake. Kilitenda kazi kwa ukweli, uwazi na uaminifu mkubwa kwa wananchi; kilikuwa Chama cha watu, kiliwasemea na kuwatetea; na kwa sababu hiyo, nao wakakisemea, kukitetea na kukienzi.

Katika miaka 23 ya uhai wake [1954 – 1977], TANU kwa ujasiri mkubwa, kiliweza kujivua gamba mara mbili, na wananchi wakaona hivyo kwa macho yao, tofauti na ngonjera za sasa za CCM.

Mara ya kwanza ilikuwa mwaka 1967. Ilikuwa hivi: Kabla ya Azimio la Arusha, kuliibuka nchini tabaka la wanasiasa na watumishi wa umma [kama ilivyo sasa], lenye kujitajirisha na kujinufaisha kwa jasho la wananchi.

Tabaka hili lilitumia taasisi za fedha kujipatia mikopo na kujenga majumba ya kifahari ya kupangisha kwa balozi za nchi za nje na mabalozi. Walinunua magari ya kifahari, walikula na kusaza, walioa “vipusa” na kutaliki pia. Kwa sababu hii, waliitwa “Wabenzi”; kwa maana ya watu wenye kumiliki magari ya kifahari ambayo leo yanaitwa “Mashangingi”.

Wakati huo, kipato na maisha ya mwananchi wa kawaida yaliendelea kudidimia kwa kasi ya kutisha, kiasi cha kuonekana kwamba kumbe ilikuwa “afadhali wakati wa ukoloni”; na kwamba, kile kilichoitwa “uhuru” haukuwa uhuru ambao TANU iliwaahidi wananchi.

Miaka ya TANU, ishara za umma kukerwa na mwelekeo huo wa taifa zilianza kujionyesha kwa njia ya migomo ya wafanyakazi, maandamano na migomo ya wanafunzi vyuoni, ikiwa ni pamoja na ule mgomo wa 1966 wa wanavyuo kupinga kukatwa asilimia 60 ya mishahara yao kama mchango wao wa kujenga Taifa wakati na baada ya kutumikia Jeshi la Kujenga Taifa [JKT], ishara ambazo ni dhahiri tena leo kuashiria historia kujirudia.

Hivi leo, ingawa nembo ya CCM ni jembe kuwakilisha wakulima, na nyundo kuwakilisha wafanyakazi; lakini, tofauti na tafsiri za alama hizo, mkulima na mfanyakazi [masikini] hana chake kwa CCM [isipokuwa jasho lake na kura yake kuweka viongozi madarakani]; nafasi yake imechukuliwa na tabaka la wafanyabiashara, wawekezaji na wasomi wenye kuwakilisha ubepari uchwara nchini kufanya historia ya miaka ya kabla ya Azimio la Arusha kujirudia.

Kwa jinsi hii, hadhi ya TANU, kama ilivyo kwa CCM leo, ilishuka. Mwalimu Julius Kambarage Nyerere aliliona hili haraka, akalazimika kutangaza Azimio la Arusha kuzuia kuibuka na kushamiri kwa tabaka la vibepari uchwara nchini.

Kutangazwa kwa Azimio la Arusha, sambamba na “Miiko na Maadili ya Uongozi”, kulirejesha imani na matumaini ya wakulima na wafanyakazi kwa TANU na kukiunga mkono upya pamoja na Mwalimu Nyerere na Serikali yake. Huko ndiko kulikuwa kujivua gamba kwa TANU kwa ujasiri mkubwa, awamu ya kwanza.

Miaka ya 1967 – 1972 ilikuwa yenye heka heka na harakati tele. Kuingia madarakani kwa dikteta Idi Amin [1972], na baadaye kuvamiwa kwa nchi yetu mwaka 1978 na dikteta huyo, kulitoa changamoto kubwa kwa uongozi na wananchi kwa ujumla juu ya mustakabali wa usalama na ustawi wa nchi yetu.

Ahsante kwa umoja wa kitaifa ulioletwa na Azimio la Arusha, Mwongozo wa TANU na Maadili ya Uongozi; kwani wananchi walipambana kwa hali na mali katika umoja wao na kumshinda adui.

Fikiria; kama nduli Idi Amin angekuwa leo ndiyo anaivamia Tanzania, kama jamii yenye matabaka yanayoibuka haraka, kuyoyoma kwa uzalendo, umoja wa kitaifa na ubaguzi tele katika nyanja mbali mbali nchini; je, tungeweza kupigana kwa umoja kama tulivyopigana kwa umoja, wazee kwa vijana; wasomi kwa wasiosoma; wenye madaraka na wasio na madaraka? Uzalendo kama huu utatoka wapi leo wakati vigogo wengine wanadiriki hata kutaka tuwe na uraia wa nchi mbili?

Huo ulikuwa ni umoja uliojengeka kwa misingi ya usawa wa kijamii chini ya TANU makini, tofauti na “umoja” wa kilaghai wa sasa ambapo kila mmoja anaishi kinyang’au, kwa kunyofoa na kula kwa ukali wa meno yake.

CCM inapotangaza kujivua gamba, ijipime usafi wake kwa kuondoa matabaka yanayoibukia na kuzuia Watanzania kutenda kwa pamoja na hivyo kuzaa lugha ya “Wao na Sisi”.

Baada ya vita vya Idi Amin, Taifa letu liligubikwa [taratibu] na janga la rushwa, ingawa halikuwa kubwa kama rushwa ya sasa iliyoligubika Taifa letu. Kama ilivyokuwa hapo zama, na kama ilivyo leo, rushwa inapokithiri katika jamii, vyombo vyote vya dola, kama ilivyo kwa taasisi zinazosimamia uchumi na haki, hutuhumiwa; sheria na haki huuzwa, unafiki na kujipendekeza katika ngazi zote za uongozi hufanya wala rushwa na wanafiki kuishi na kula kwa jasho la wengine bila hofu ya kuwajibishwa.

Wakati huo, kwa watu wema na wa kawaida, maisha huwa magumu bila maelezo ya kuridhisha juu ya chanzo cha hali hiyo kwa sababu msingi wa maamuzi kisiasa na kisheria huporomoka; taasisi za kiuchumi huvunjika na watu hupoteza matumaini na imani juu ya uhalali wa Serikali kutawala.

Chama cha siasa, ambacho hapo mwanzo kilikuwa kimbilio la wanyonge katika kupata ufumbuzi wa matatizo yao hukosa mamlaka na hadhi ya kukubalika kwa sababu ya kuongozwa na watu “wachafu”. Hali hii ndimo ilimo CCM yangu ya sasa.

Ni katika mazingira kama haya kwamba, mwaka 1981, CCM [ya zamani] kwa kuongozwa na nguvu kani iliyorithi kutoka TANU [ambayo sasa imetiwa maji na mafisadi kufanya Chama kuwa rojorojo na legelege], iliamua kujivua gamba kwa mara ya pili.

Hadi kikao cha NEC cha Januari 9, 1987 hapakuwa na matumaini kwamba hali hiyo ingerekebika; nao uvunjifu wa maadili [law of the jungle], kama ulivyo sasa, wa kila mtu na lwake [bila hata kujali kwamba, sote tu watoto wa Mungu mmoja], ulishamiri.

Hapo, Chama, chini ya usimamizi thabiti wa Mwalimu Nyerere, kilijiuliza maswali magumu kabla ya kujivua gamba; maana, chama leo hakiwezi kudai kujivua gamba, kama hakijui aina na kiwango cha uchafu wa gamba kinalotaka kujivua. Je, CCM ya sasa inajua gamba inalotaka kujivua?. Kwa kauli za kisanii zinazotoka kwa viongozi leo, ni dhahiri CCM haijui inachotaka kujivua!

Kwanza, kiliona umuhimu wa kufufua matarajio ya watu, na kwamba kisingeweza kufanya hivyo katikati ya maswali magumu na tuhuma dhidi ya viongozi wake wabovu yakiendelea kuulizwa ngazi zote.

Na kisingeweza kufanya hivyo pia kama itikadi iliyokiongoza ilikuwa ni tafsiri ya kila mtu, na kama pasingekuwa na mijadala miongoni mwa viongozi wake yenye kufafanua ni nani [kiongozi] alikuwa kwa ajili ya watu na Ujamaa, na [kiongozi] yupi alikuwa akiwanyonya.

Pili, Chama kilibaini kwamba, vyombo vya Serikali na taasisi za kiuchumi, zisingeweza kufanya kazi ipasavyo, maadam watendaji wa taasisi hizo walijiona walikuwa na kinga dhidi ya kuwajibishwa kwa udhaifu na maovu yao, kama ambavyo viongozi wengi wanajiona leo, chini ya Chama na Serikali yake ya sasa.

Mwisho, kwamba, bila watu – Wafanyakazi mijini na wakulima vijijini kuruhusiwa kutumia haki yao ya kuhoji [na sio kuhoji tu kwa nidhamu kama ambavyo] Spika Makinda anataka iwe Bungeni] juu ya vitendo vya kiovu vya uongozi wao, pasingekuwa na uwezekano wa kupata viongozi wenye tija.

Hapakuwa na njia mbadala kwa hilo isipokuwa kuimarisha nguvu ya umma pekee dhidi ya hali hiyo ya kifisadi kuweza kukomeshwa, ili kwamba nguvu ya wananchi iliyodumazwa [na viongozi wabovu] iweze kutumika vyema kwa ujenzi wa Taifa.

Kwa njia hiyo ya Chama kujivua gamba, “safisha safisha” dhidi ya Chama na Serikali ilianza na hotuba ya mwaka mpya [1981] ya Mwalimu Nyerere, ambapo watendaji waandamizi wanane wa Serikali walifukuzwa kazi na wengine watatu kuteremshwa vyeo. Huo ulikuwa mwanzo tu wa kujivua gamba awamu ya pili. Na katika hotuba yake ya Mei Dei [1981], Mwalimu alisema, kazi ilikuwa inaendelea kitaifa na kuwaasa wananchi akisema:

“Tusaidiane kuwaanika hadharani mafisadi hawa – ni ninyi mnaoumia kwa matendo yao maovu; mnawafahamu kwa sababu mnawaona Maofisini, mitaani na katika biashara haramu. Msiwaogope, wasemeni”.

Ujasiri huo wa Mwalimu wa kuhamasisha umma uungane naye kufichua ufisadi, hauwezi kufikiwa au kuigwa na uongozi wetu leo kwa sababu, kwa kiwango fulani, wao wenyewe ni sehemu ya ufisadi huo.

Ndiyo maana tunashindwa kujizuia kuamini kwamba kelele zao za kujivua gamba ni kujaribu tu “kufunika kombe mwanaharamu apite”. Kilicho wazi hapa ni kwamba, ujasiri wa kizalendo, ambao viongozi wengi hawana, umezidiwa nguvu na ujasiri wa kifisadi na kuyumbisha Taifa.

Januari 14, 1981, Kamati Kuu [NEC] ya CCM ilikunjua makucha yake na kunasa wahanga wake wa kwanza. Hawa walikuwa ni Waziri wa Mawasiliano na Uchukuzi, Augustine Mwingira, na Meneja Mkuu wa Shirika la Ndege nchini [ATC], Lawrence Mmasi, waliotuhumiwa kukodi kwa ajili ya ATC, ndege mbovu kutoka kwa mfanyabiashara wa Kipalestina, George Hallack. Ndege hiyo baada ya kutua tu uwanja wa Dar es Salaam, ilifikwa na mauti, na gofu lake limebakia uwanjani hapo kwa zaidi ya miongo miwili.

Je, Serikali yetu ya leo imechukua hatua gani, kwa mfano, dhidi ya wale walionunua rada mbovu, mitambo mibovu ya umeme wa IPTL na ndege ya Rais? Kwa mwenendo huu, tuseme huku ndiko kujivua gamba kwa CCM na Serikali yake?

Wahanga wa pili walikuwa Mwenyekiti ambaye pia alikuwa Meneja Mkuu wa Benki ya Rasilimali [TIB], George Mbowe, na Mkurugenzi Mkuu wake, Gidion Tibesigwa. Hawa walituhumiwa kumuuzia kinyemela mfanyabiashara, Akberali Rajpar, meli ya mizigo – MV Jitegemee, kwa bei ya kutupa na kwa fedha za nchini badala ya fedha za kigeni. Meli hiyo iliuzwa kwa Sh. milioni 39 tu, lakini Rajpar alilipa Sh. milioni 14 tu na kuibatiza kwa kuipa jina la “Lord Rajpar”.

Kashfa hii inafanana na ile ya kuuzwa kwa Benki yetu ya Biashara ya Taifa [NBC] na mali zake kwa Kampuni ya Makaburu [ABSA] kwa bei ya kutupa ya 15bn/=, lakini wakalipa 12bn/= tu, ambapo hata hivyo, 12bn/= hizo zilizolipwa hazionekani katika vitabu vya Serikali na hakuna mtu aliyewajibishwa.

Kwa jinsi uuzaji wa MV Jitegemee ulivyofanyika katika mazingira machafu na ya kutatanisha, Rajpar na mfanyabiashara mwingine, Abdul Haji, walitiwa kizuizini Januari 10, 1981, kwa kile kilichoitwa “vitendo [rushwa] vinavyodhalilisha au kuhatarisha jina zuri la Tanzania machoni mwa mataifa”.

Zoezi hilo liliendelea kwenye Shirika la Vifaa vya Elimu [TES], ambapo Meneja Mkuu wake, Gervas Chilipweli na Meneja Kanda ya Dar es Salaam, John Lupalala pamoja na Mdhibiti Fedha wa Shirika hilo, Mujibur Rahman, waliachishwa kazi kwa ubadhirifu.

Baada ya hapo, kindumbwendumbwe kilitua kwa Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Abdulnuru Suleiman. Kilianza kwa malalamiko ya wananchi mbele ya Mwalimu, kwamba, uongozi wote wa mkoa huo na Mkuu wa Mkoa mwenyewe, walikuwa wala rushwa na wakamtaka Mwalimu aondoke na mtu wake huyo kwa kuwa alikuwa mzigo kwa wananchi.

Mwalimu hakuwapa wananchi hao jibu la papo kwa hapo lenye kueleweka; lakini haikupita wiki, Mkuu wa Mkoa huyo akawa amefukuzwa kazi “kama adhabu”.

Haya ni machache tu kati ya mengi ya kujivua gamba ambayo TANU na CCM ya Mwalimu Nyerere, viliweza kutekeleza kwa vitendo na kwa ujasiri mkubwa ili wananchi wajione kuwa ndio wenye mamlaka juu ya Chama na Serikali yao. Mazingira yaliyosababisha TANU na CCM ya Mwalimu kuchukua hatua hizo ndiyo hayo hayo yanayojirudia leo, tena kwa kasi ya kutisha.

Je, CCM ya leo inao ujasiri wa kujivua gamba mithili ya TANU na CCM ya Mwalimu, au inajaribu kufunika kombe tu mwanaharamu apite”, kwa maangamizi ya Taifa?

Je, kwa Taifa kugubikwa na ufisadi wa kutisha kiasi cha kiongozi wa nchi kukiri hilo [akifunga semina elekezi Mei 14, 2011], sasa tuelewe kwamba ujasiri wa kizalendo umezidiwa nguvu na ujasiri wa kifisadi kufanya Serikali ishindwe kukabili hali hiyo?

China imeendelea kwa sababu [Mwenyekiti] Mao Tse Tung hakuvumilia ufisadi; aliweza kuwaangamiza kwa kuwaua hadharani wahujumu wa sera za nchi [capitalist roaders], akiwamo mke wake, bila ya kuwaonea haya. Je, Mwenyekiti Jakaya Mrisho Kikwete, atahimili kishindo na mawimbi ya Chama kujivua gamba, au atarudi nyuma kuepuka ugonjwa wa moyo?

Yetu macho na masikio, kabla umma haujachoka na ngonjera za “Chama kujivua gamba”.

Simu:
0713-526972

Barua-pepe:


RAIA MWEMA

No comments: