Wednesday, June 29, 2011

MOTO WA KISIASA WAWASHWA BUNGENI

Kizitto Noya, Dodoma na Fidelis Butahe,Dar

KITI cha Spika wa Bunge, Anne Makinda jana kilitikiswa kufuatia malumbano makali baina ya wabunge hasa wa kambi ya upinzani walipokuwa wakichangia hotuba ya ofisi ya Waziri Mkuu, huku mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje akidai kuwa nchi imejaa “wezi wasiokuwa na hatia”.Kidhalika kikao hicho cha bunge jana, kilishuhudia malumbano makali baina ya Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema) na mwenyekiti wa Bunge, Sylivester Mabumba, ambayo yalitanguliwa na mvutano baina ya Spika, Anne Makinda na Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali.

Mvutano uliotokea kipindi cha bunge jioni, baina ya Mdee na Mabumba ulikwenda mbali kiasi kwamba Mdee alitoa matamshi makali kwa mwenyekiti huyo wa bunge akimwambia “….mwenyekiti ukiendesha mjadala huu kwa ushabiki, kiti kitakushinda”.

Malumbano hayo yalisababishwa na kauli za Mbunge wa CCM, Zarina Madabida kusema wanaopinga posho za wabunge (sitting allowance) wanataka chama chao kiwafidie fedha hizo, jambo ambalo lilisababisha Mdee, kusimama kuomba mwongozo.

Madabida alikuwa akichangia hotuba ya bajeti ya ofisi za Waziri Mkuu ya mwaka 2011/12 jana na bila kukitaja chama hicho alisema kama kina dhamira ya kweli ya kukataa posho hizo kwanini wabunge wake wanataka kufidiwa posho hizo na chama.

“Mwenyekiti hizi posho ni muhimu, mimi leo nikienda Dar es Salaam akinamama nakwenda kuwasaidia na hizi posho,” alisema Madabida.

Baada ya Madabida kumaliza kuchangia hotuba hiyo na kukaa chini, Mdee aliomba mwongozo wa mwenyekiti huku akitaja kanuni ya bunge inayomtaka mbunge asiseme uongo na endapo atasema jambo hilo atatakiwa alithibitishe.

Lakini kabla hajamaliza kukifafanua kifungu hicho, Mabumba alimtaka Mdee akae chini, lakini mbunge huyo kabla ya kukaa alisita kwa sekunde kadhaa kutii amri hiyo.

Mabumba alimweleza Mdee kwamba Madabida wakati akizungumza hakutaja chama chochote na endapo angekitaja chama hicho ndio angetakiwa kuthibitisha.

Baada ya ufafanuzi huo, Mdee alinyanyuka na kusema kwamba chama kinachopinga posho ni Chadema na NCCR-Mageuzi.

“Kwa implication, Mheshimiwa Madabida alikuwa anavilenga vyama hivi… Mwenyekiti usikikalie kiti kwa ushabiki, kitakushinda,” alisema Mdee.

Hata hivyo kabla hajaketi, ilisikika sauti ndani ya bunge ikisema “Jumamosi mligombea posho’’ hatua iliyomfanya Mdee kumtaka mwenyekiti huyo wa bunge kumlinda.

Pamoja na ombi hilo la Mdee, Mabumba hakuzungumza lolote juu ya hali hiyo badala yake alimtaka mbunge huyo kukaa chini huku akiwaita wachangiaji wengine wachangie hotuba hiyo ya bajeti ya ofisi ya waziri mkuu.

Machali na Spika
Mvutano baina ya Machali na Spika Makinda, ulitokea katika kipindi cha asubuhi, kufuatia mbunge huyo wa Kasulu Mjini kudai kuwa “…kuna mambo yanafanyika kihuni ndani ya serikali”.

Machali alisema mwaka uliopita zilitengwa zaidi ya Sh6 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya Kidawe-Kasulu kwa kiwango cha lami lakini, fedha hizo hazijawahi kutolewa na kwamba hata katika bajeti ya Wizara ya Ujenzi 2011/12 fedha hizo hazijatengwa.

“Kuendelea kuwaahidi wananchi wakati jambo lenyewe halijafanyika ni uhuni wa serikali.., inawafanyia uhuni watu wa Kigoma,”alisema Machali.

Kauli hiyo ilimfanya Spika Makinda kumtaka mbunge huyo kutumia lugha nzuri katika utoaji wa mchango wake na kuacha kutumia neno ‘uhuni’.

“Barabara inaanza kujengewa Nyakanazi.., Nyakanazi sio Kigoma. Hivi Kigoma tumewakosea nini, Rais Kikwete alisema barabara itajengwa, lakini leo mmezihamisha fedha hizo sehemu nyingine, kama sio uhuni ni nini,”alihoji Machali.

Kitendo cha Machali kurudia neno hilo kilimfanya Spika Makinda kumwonya tena mbunge huyo na kumweleza kuwa akitumia neno ‘uhuni’ anaweza asisikilizwe na anaowapelekea ujumbe huo.

Lakini Machali alionekana kutokubaliana na Spika kwa kujibu kuwa, “Hata Shelukindo alitumia neno ‘kijingajinga’ na alikuwa akitulenga sisi wapinzani, sasa sisi wapinzani tukitumia maneno ya ukali tutahukumiwa, spika tuwe na 'check and balance' (kuangalia usawa)”.

Machali alikuwa akifanya marejeo ya mchango wa Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shellukindo (CCM), ambaye wakati akichangia alisema kumekuwa na wabunge wanaoingiza hoja za kijingajinga bungeni.

Machali aliweka wazi kwamba wabunge ni kama wamejivua uwakilishi wa wananchi kwani wamekuwa mbogo dhidi ya hoja ya kufutwa kwa posho za vikao.

Mbunge huyo alisema maendeleo ya Tanzania hayalingani na umri wa miaka 50 ya Uhuru wake na kwamba wananchi wa Tanzania hawana amani, bali wana utulivu ulioambatana na nidhamu ya woga.

“Siwezi kukubali kuwa kuna amani, wakati watu wanawaza watapata wapi mlo, polisi wanaendeleza vitendo vya kuwapiga raia kama wakimbizi ndani ya nchi yao, Serikali inakaa kimya na kusema mamlaka husika ziachwe zifanye kazi yake,”alisema Machali.

Kauli ya Wenje
Naye Wenje aliungana na Machali akisema kuwa Tanzania haina amani bali wananchi wake wana nidhamu ya woga akihoji kwamba maana ya amani ni mtu kutangazwa kuwa ameshinda ubunge baada ya vurugu polisi kupiga mabomu ya machozi?.

“Hapa mtu akieleza ukweli au watu wakiandamana wataelezwa kuwa wanataka kuchafua amani, hii si kweli,”alisema Wenje na kuongeza:
“….. tutaandamana kwa sababu, maandamano ni lugha ya sauti isiyosikika na hata kesho tutaandamana tu,”.

Alisema kuwa baadhi ya ripoti ya Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) zinaonyesha kwa baadhi ya Halmashauri nchini zina hati chafu, lakini serikali haielezi wakurugenzi katika Halmashauri hizo wamechukuliwa hatua gani.

“Mimi nilitegemea Mkuchika (Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI) wakati akisoma makadirio na matumizi ya ofisi yake atasema wakurugenzi hawa amewafuta kazi, nchi ina matatizo mnasema ina amani, amani ipi sasa,” alisema Wenje.

Wenje ambaye ni mbunge wa Nyamagana alisema nchi imejaa wezi na inaendelea kuporwa lakini, serikali haionyeshi nia ya kuchukua hatua za kisheria dhidi ya wahusika. “Nchi imejaa innocent thieves (wezi wasio na hatia), lakini serikali haijali.

Mimi nilitegetemea wakati Waziri (Tamisemi) aliposema kuna halmashauri nne zimepata hati chafu, nilitegema asema tayari wakurugenzi wake tumewafukuza na zingine zenye kasoro, wakurugenzi wako under probation (chini ya uangalizi) na wakirudia hivyo miaka miwili waondoke. We must sack them!”alisisitiza.

Aliendelea,”ATCL is almost dead due to poor management, (imekufa kwa sababu ya uongozi mbovu). Nchi iko looted (imeporwa). Tulikuwa na Deepgreen Finance na sasa tuna issue (suala) la rada. Kwa nini hatuchukui hatua?”alihoji.

Wenje aliitaka serikali ichukue hatua za kisheria dhidi ya wahusika, akibainisha kuwa kuendelea kuwalea mafisadi na watu wasiowajibika, ni tatizo ambalo siku moja, litagharimu amani ya nchi.
Katika hatua nyingine mbunge huyo aliendeleza madai ya chama chake kutaka posho ifutwe akisema “kwenye suala la posho za vikao (Sitting allowance) haturudi nyuma, na as from tomorrow (kuanzia kesho), tunaomba mtuletee fomu mbili ili sisi (Chadema) tusisaini fomu ya posho hizo.”

Watanzania ndani ya Chupa
Mapema, Shellukindo aliwagutua wabunge pale aliposema Watanzania ni kama wako kwenye chupa hivyo kutofahamu chochote kinachoendelea katika nchi nyingine.

Shelukindo alisema, “ Ukiwachukua panzi ukawatumbukiza ndani ya chupa wataruka na kukosa chakula na baadaye wataanza kuumana, Tanzania tuko ndani ya chupa, nchi ina kila kitu, lakini Watanzania bado masikini, tumebaki kufanya siasa za kuchafuana.”

Alisema misaada mingi inayotolewa haiwafikii walengwa lakini, wabunge wamebaki kujadili hoja sizizo za msingi bungeni.

“Ajira kwa vijana hakuna, ndio maana wakiambiwa waandamane wanakubali, ukabila, udini, mauaji ya albino. Jamani Watanzania tumefungwa, tupo ndani ya chupa tumefungwa,” aliongeza.

Alisema Watanzania ili watoke ndani ya chupa, kila mtu anapaswa kutekeleza wajibu wake ikiwa ni pamoja na kumwomba Mungu, huku akitolea mfano nchi ya Rwanda ambayo ilikuwa katika vita, lakini kwa sasa imepiga hatua kimaendeleo.

Naye Mbunge wa Lindi Mjini Salum Barwany, alipendekeza serikali kuanzisha mjadala wa kitaifa ili watu wajadili matatizo yao na kuyatafutia ufumbuzi kwa kuwa serikali, inaonekana kushindwa.

Alisema serikali imeshindwa kutekeleza ahadi za rais anazozitoa maeneo mbalimbali nchini ikiwamo Lindi mjini na hili linawafanywa wananchi wakose imani naye na serikali yake.

Barwany ambaye alikuwa akizungumza kwa hisia kali bungeni, alisema kuwa kitendo cha serikali kutotekeleza ahadi hizo za rais ni kumdharau rais mwenyewe ambaye maagizo yake, ni zaidi ya sheria.

“Kauli ya rais ni ya thamani kuliko hata sheria. Sasa rais kaja Lindi na akatuahidi soko kuu bandari, maji, uwanja wa ndege wa Kimataifa, mashamba ya mkonge na mambo mengine kibao, lakini mpaka leo anapobakiza miaka mitatu, hakuna kinachofanyika,”alisema Barwany.

Alihoji “Ahadi za rais ziko wapi Lindi leo? Kama nyie serikali mnamdharau rais wananchi watafanya nini? Leo manung’uniko kila kona. Kuna haja ya kuwa na mjadala wa kitaifa na sio mipango isiyotekelezeka ya Kilimo Kwanza, ili watu wajadili namna ya kutatua matatizo yao.”


MWANANCHI

No comments: